Lissu: Baada ya kushambuliwa kwa risasi
wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, nilikwenda uhamishoni. Nilinusurika
kuuawa na hatimaye nikakimbilia katika Ubalozi wa Ujerumani.
Tarehe 17 Februari 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa
katika ziara barani Ulaya kwa mkutano uliowakutanisha viongozi wa Umoja wa
Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU), nilipokea ujumbe kupitia watu wangu kwamba
alikuwa anataka kuonana nami.
Wakati huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alikuwa
gerezani kwa takribani miezi sita au saba akikabiliwa na kesi ya ugaidi.
Nilipopata
ujumbe huo, nilishauriana na viongozi wenzangu. Tuliona ilikuwa ni hatua nzuri,
hivyo nikaenda kukutana naye. Aliniambia alikuwa na nia ya kuyamaliza matatizo
yaliyokuwa yamejitokeza wakati wa utawala uliopita.
Nikamwambia
aanze kwa kumwachilia Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe, ndipo mazungumzo mengine
yaweze kuendelea. Pia nikasema tunahitaji kuzungumzia Katiba Mpya na Tume Huru
ya Uchaguzi. Alijibu kuwa alikuwa tayari kufanya mazungumzo hayo.
Aidha,
nilimweleza kuwa mimi, Godbless Lema na wengine tulikuwa tumekimbia nchi
kutokana na hofu ya usalama wetu, hivyo tulihitaji uhakikisho kwamba ilikuwa
salama kurejea nyumbani. Baadaye, alitangaza bungeni kuwa Watanzania waliokuwa
uhamishoni warejee nchini. Mbowe naye aliachiwa huru, jambo lililotupa faraja
ya kurudi nyumbani.
Tuliporejea,
tulipendekeza kuwa watu wote waliokuwa wamefunguliwa kesi ambazo tuliamini
zilikuwa na misingi ya kisiasa wafutiwe mashtaka, na baadhi ya kesi hizo
zilifutwa.
Baadaye
yakaanza mazungumzo kati ya CHADEMA na CCM. Tulipeleka mapendekezo mbalimbali
kuhusu Katiba Mpya, muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi na ratiba ya utekelezaji wa
mageuzi hayo.
Kwa upande
wetu, tulitaka mchakato wa Katiba Mpya ukamilike kabla ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025. Hata hivyo, tulianza kuona hakuna hatua za kutosha zilizokuwa
zinachukuliwa. Mara nyingi tuliwasilisha mapendekezo kwa maandishi lakini
majibu yalitolewa kwa njia ya mazungumzo badala ya maandishi rasmi.
Takribani
mwaka mmoja ulipita bila majibu rasmi ya maandishi kuhusu mapendekezo yetu.
Mwaka 2025,
tuliendelea kusisitiza kuwa majibu yatolewe kwa maandishi ili kuwe na uwazi
kuhusu mambo yaliyokubaliwa na yaliyokataliwa.
Tarehe 21
Mei 2025, tulipokea majibu ya maandishi yaliyokataa mapendekezo yetu yote.
Baada ya
hapo, tulikaa na kujiuliza maana ya maridhiano ikiwa hakuna makubaliano
yanayotekelezwa zaidi ya vikao vya mazungumzo. Tukafikia hitimisho kwamba ni
lazima kurejea kwa wananchi.
Tarehe 31
Mei 2025, tuliamua kama chama kuanzisha kampeni ya kuhamasisha madai ya Katiba
Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi. Tulizunguka nchi nzima kuzungumza na wananchi
kuhusu masuala hayo.
Kadiri joto
la kisiasa lilivyoongezeka, ndivyo madai ya kukamatwa kwa wanachama na viongozi
wa upinzani pamoja na kesi mbalimbali yalivyoendelea kujitokeza.
Hali hiyo iliendelea hadi uchaguzi wa serikali za mitaa na
vijiji wa Novemba 2024.
Ndani ya chama kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu kushiriki
au kutoshiriki uchaguzi huo kutokana na kutokuwepo kwa mageuzi yaliyokuwa
yanadaiwa. Hatimaye, CHADEMA iliamua kushiriki.
Lissu alidai kuwa uchaguzi huo ulisimamiwa na mfumo wa
utawala wa serikali kupitia TAMISEMI, huku watendaji mbalimbali wa uchaguzi
wakiwa ni wateule wa mamlaka ya serikali.
Pia alidai kuwa wagombea wengi wa upinzani walienguliwa
katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali ambayo, kwa mujibu wake, iliathiri
ushindani wa kisiasa katika uchaguzi huo.
Lissu alidai kuwa wagombea wengi wa upinzani walienguliwa
katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali ambayo, kwa mujibu wake, iliathiri
ushindani wa kisiasa katika uchaguzi huo.
Alisema waliopinga matokeo hayo walikumbana na nguvu za dola
katika maeneo mbalimbali, akidai kuwa watu kadhaa waliuawa Tarime.
Baada ya uchaguzi huo wa Novemba 28, wiki iliyofuata, tarehe
3 Desemba, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana kujadili hatua za kuchukua kufuatia
yaliyotokea katika uchaguzi na mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo nchini.