Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kilichonileta hapa sio uhaini ni vita vya kisiasa - Lissu

Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu imeahirishwa kwa muda hadi Jumatatu wiki ijayo atakapoendelea kujitetea mbele ya mahakama.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Eagan Salla, Abdalla Dzungu & Rashid Abdalla

  1. Kesi ya Lissu imeahirishwa kwa muda hadi jumatatu

    Kesi inayomkabili kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeahirishwa hadi Jumatatu saa tatu asubuhi, baada ya Lissu kuendelea kutoa ushahidi wake mahakamani.

    Baada ya kueleza msimamo wake kuhusu masuala ya uchaguzi na uzoefu wake wa kisheria, majaji walimweleza Lissu kuwa wanatumaini atakuwa amekamilisha ushahidi wake ifikapo Jumatatu.

    Hata hivyo, Lissu aliwaambia majaji kuwa hataweza kumaliza ushahidi wake katika muda huo.

    Kesi hiyo inaendelea baada ya mahakama kuu kuamua Tundu Lissu ana kesi ya kujibu.

    Soma Zaidi Hapa:

  2. Majaji wamejifunza kwangu sheria za uchaguzi - Lissu

    Lissu: Majaji ukiachia ushiriki huo vile vile nimeshiriki kwenye masuala ya uchaguzi kama wakili kwa wagombea au wabunge wa vyama tangu 2005 ningependa kuamini kwamba kwenye sheria za masuala ya uchaguzi ni mjuaji kuliko hata mawakili wengi wa nchi hii.

    Lissu: Majaji wa mahakama hii na hata ya rufaa naamini wamejifunzia kwangu kwasababu ninafahamu sheria za uchaguzi na sio kwa kujigamaba

    Lissu: Nje ya ujuzi wa hiyo sheria kuanzi mwaka 2021, mpaka wakati nakamatwa mwaka jana, nimefanya utafiti mkubwa sana kuhusu mfumo wetu mzima wa uchaguzi na jinsi ynavyofanya kazi tangu enzi za ukoloni kama is ingekuwa kusumbuliwa ukonga ningechapisha kitabu na masuala ya uchaguzi ya nchi hii na uchafu wake

    Lissu: Kwasababu ya ufahamu wote ya masuala ya uchaguzi nimekuwa mstari wa mbele kusimamia na kupigania mfumo mpya wa huo wa uchaguzi

    Lissu: Na hakuna hoja yoyote ya CHADEMA ya masuala ya uchaguzi ambayo hayajapitia kwenye mikono yangu.

    Soma Zaidi Hapa:

  3. Kukaa gerezani hakujapunguza heshima yangu, bali kumeiongeza - Lissu

    Lissu: Majaji ni muhimu pia iingie kwenye rekodi ya ushahidi pamoja na kukaa gerezani muda wote huo heshima yangu nchi hii na hata kwenye jumuiya ya Kimataifa haijapungua bali imeongezeka.

    Lissu: Majaji taasisi nyingi sana za Kimataifa, za kikanda na za kimataifa, ikiwemo umoja wa mataifa, Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya madola imesema haya mashtaka ni mashtaka ya kisiasa hakuna uhaini wala jinai yoyote ni siasa na yanadai niachiliwe huru bila masharti yoyote.

    Lissu: Baraza la haki la kimataifa lenye makazi yake nchini uswizi sio tu niachiliwe bila masharti yoyote lakini pia nilipwe fidia kwa usumbufu niliopata kwa wakati wote huo.

    Lissu: Majaji, ninaomba iingie kwenye ushahidi kwamba imesimamisha misaada kwa Tanzania kwasababu kesi hii, marekani imesimamisha millioni 700 dola kwasababu ya mashtaka haya.

    Lissu: Majaji kwasasa bunge la marekani linajadili muswada wa kuwekea serikali ya Tanzania vikwazo kwasababu ya mashtaka haya.

    Lissu: Majaji Dunia haiwezi kukupigania hivi kama wewe ni mtu wa hovyo hovyo, mhalifu, dunia inakupigania kwasababu wewe ni mtu wa heshima.

    Lissu: Majaji mashtaka yanahusu kauli niliyoitoa tarehe 3/4/2025 kuhusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

    Lissu: Majaji nilitaka kusema hivi mashtaka yanahusu uchaguzi nataka rekodi ya mahakama iseme kwamba nina uzoefu mkubwa sana kuhusiana na masuala ya uchaguzi ya Tanzania.

    Lissu: Nilipiga kura kwa Mara ya kwanza Oktoba 29 mwaka 1985 nikiwa na umri wa miaka 18 na kati ya mwaka huo na mwaka jana, nimeshiriki katika uchaguzi kama Mgombea au mpiga kura katika chaguzi zote ispokuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na maafa yale ya mwaka jana.

    Lissu: Majaji ukiachia ushiriki huo vile vile nimeshiriki kwenye masuala ya uchaguzi kama wakili kwa wagombea au wabunge wa vyama tangu 2005 ningependa kuamini kwamba kwenye sheria za masuala ya uchaguzi ni mjuaji kuliko hata mawakili wengi wa nchi hii.

  4. 'Kilichonileta hapa sio uhaini ni vita vya kisiasa' - Lissu

    Lissu: Majaji, nje ya ubunge nimewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika, kuanzia Machi 2017 hadi Septemba 7, 2017, niliposhambuliwa. Nilichaguliwa na mawakili kuwa rais wao. Na huyu ni rais wa mawakili wa nchi hii.

    Lissu: Nje ya uongozi wa mawakili wenzangu, hapa nilipo ni Makamu Mwenyekiti wa International Democrat Union, shirikisho linalounganisha vyama zaidi ya 80 vya kisiasa kote duniani. Ni muungano wa vyama kutoka Ulaya, Amerika Kaskazini na maeneo mengine, ikiwemo chama cha Republican cha Marekani.

    Lissu: Na mimi ni Makamu Mwenyekiti ninayewakilisha bara zima la Afrika. Majaji ni ushahidi wangu kwamba mimi ni mtu wa heshima, ninaye heshimika ndani ya nchi hii na Kimataifa. Na heshima niliyo nayo ni kwasababu ya msimamo wangu wa kupigania haki, demokrasia na utawala wa sheria na sio sababu nyingine. Majaji mwezi Mei 2011, nilipewa tuzo ya kutoka Chuo Kikuu cha Bridgecourt, jimbo la Connecticut nchini Marekani.

    Lissu: Majaji na sababu hiyo heshima hiyo ni muhimu kuiweka kwenye Mahakama. Chuo hicho kilisema tunakuzawadia kwasababu ya kusimamia haki za binadamu, mazingira, na demokrasia nchini Tanzania na katika bara la Afrika.

    Lissu: Majaji, mwezi Desemba 2020, nilitunukiwa tuzo nyingine ya heshima na IDU, iliyoitwa Bush Thatcher for Freedom. Tuzo hiyo ilipewa jina kwa heshima ya aliyekuwa Rais wa 41 wa Marekani, George H. W. Bush, na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Margaret Thatcher. Sababu ya kutunukiwa ilikuwa: “Tundu Lissu, umekuwa kielelezo cha msimamo thabiti wa kupigania haki, demokrasia na utawala bora katika nchi za Afrika.”

  5. Lissu aanza kujitetea mbele ya mahakama

    Majaji: Mashahidi wengine wanatakiwa kutoka nje hadi pale watakapoitwa. Wangekuwa washtakiwa wangebaki.

    Jaji Ndunguru: tuambie majina yako kamili

    Lissu: Naitwa Tundu Antiphas Lissu

    Jaji: Umri wako?

    Lissu: Umri wangu ni miaka 59

    Wakili wa mahakama kuu : Kiongozi wa kisiasa na mwenyekiti wa chama cha dini yako ni gani?

    Lissu: Dini yangu ni Mkatoliki wa Roman na nina apa mbele ya Mahakama hii kuwa ushahidi utakuwa wa ukweli, ukweli mtupu eh Mungu nisaidie.

    Lissu: Sehemu ya kwanza ya ushahidi wangu ni masuala yanayonihusu mimi mwenyewe kwasababu kosa ninalo shtakiwa nalo ni kubwa. Majaji kama ambavyo nimesema mimi ni kiongozi wa chama kilichoandikiswa rasmi kwa mujibu wa sheria za nchi hii. Nafasi yangu ya sasa ilikuwepo wakati matukio haya yanaendelea mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA.

    Lissu: Nimekuwa mwenyekiti wa CHADEMA tangu 22 Januari 2025. Nimekaa kwenye nafasi hiyo ya mwenyekiti wa chama kwa takriban wiki tano au sita ndipo nikakamatwa na kushtakiwa kwa kosa hili. Kwasasa nitasema Hilo maana yake ni nini. Kabla ya hapo nilishikilia nafasi yangu Makamu kwa upande wa Tanzania bara kwa miaka 5 tangu Disemba 2019 hadi Januari tarehe 22 2025 nilipochaguliwa kuwa mwenyekiti. Na kabla ya hapo nilikuwa mwanasheria mkuu wa CHADEMA na mjumbe wa kamati kuu yake ya chama kati ya mwaka 2010 hadi 2017.

    Lissu: Kwa uhakika ni tarehe 7 Septemba 2017. Hii tarehe ni muhimu kwa hapo baadaye. Kabla ya hapo nilikuwa mkurugezi wa Tiba na haki za binadamu wa CHADEMA tangu Julai 2004 nilipojiunga na chama hadi around Novemba 2011. Na nafasi hiyo ilinifanya kuwa aliyekuwa mwanachama wa kamati wamjumbe wasiokuwa na kura. Kwa ushahidi huu mimi nimekuwa katika uongozi wa CHADEMA katika Ngozi za juu kabisa takriban miaka 20.

    Lissu anaendelea kujiieleza mbele ya mahakama.

    Lissu: Nje ya uongozi wa chama niliousema vilevile nimeshikilia nafasi zingine za uongozi kama ifuatavyo: mwaka 2010 kwenye uchaguzi mkuu nilichaguliwa kuwa Mbunge katika bunge la jamhuri ya muunguano nikiwakilisha jumbo la singida mashariki Maarufu kama kumbi mashariki. Na nilichaguliwa kwa tiketi ya chadema. Nilichaguliwa kwenye nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 nilitumikia nafasi hiyo Juni 2019.

    Lissu: Ilikuwaje hadi nikaishia hapa? Narudi kwenye tarehe 7 Septemba 2017, nikiwa Dodoma kwenye vikao vya bunge nilifuatwa kutoka bungeni mpaka kwenye makaazi yangu rasmi na kushamhuliwa na risasi, risasi nyingi sana na watu ambao serikali ya Tanzania inawaita watu wasiojulikana.

    Lissu: Majaji, kufuatiwa shambulio nilikimbizwa hospitali ya Dodoma na siku hii hiyo kupelekewa nairobi Kenya ambapo nilikaa hospital hadi 6 January 2018. Baada ya hapo nilipelekwa ubelgiji kwaajili ya matibabu zaidi katika hospitali ya Chuo kikuu ya Leuven. Nilitibiwa katika hospitali hiyo hadi Januari 2022.

    Lissu: Tarehe 29 June 2019 aliyekuwa spika wa bunge ndugai marehemu alitangaza kunifuta ubunge kwasababu nilikuwa mtoro na sijaonekana takriban miaka miwili bungeni hiyo ndiyo sababu iliyopelekea nisimalize muhula wangu wa pili kama mbunge.

    Lissu: Na niongeze tu kuwa katika kesi hii licha ya kuwa mbunge nakuumizwa vibaya nikiwa kazini bunge na serikali ya Tanzania ilikataaa katakata kulipa gharama ya matibabu yangu. Sikupewa hata senti moja.

    Lissu: Vilevile nilikuwa Msemaji mkuu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa masuala ya katiba na sheria, muungano, pamoja na mwanasheria mkuu mwandamizi wa Mwanasheria Mkuu.

    Lissu: Majaji ningependa Mahakama irekodi kuwa nilifanya kazi yangu ya ubunge kwa heshima kubwa na umahiri. Majaji nilikuwa kipindi hicho hicho cha 2011-2015 nilikuwa mjumbe wa bunge maalum na katiba. Na kwa kipindi hicho bungeni niliongoza harakati za kupigania katiba mpya na mfumo huru wa uchaguzi. Kilicho nileta hapa sio uhaini ni mgogoro wa katiba mpya, ni vita vya kisiasa.

  6. Majaji kutoa uamuzi kuhusu mashahidi wa serikali

    Majaji: Kwa kuwa mashahidi 8-11 hawana pingamizi kulingana na kifungu cha 314 basi naomba tuendelee nao. Kwa hao mashahidi wengine nitaoa uamuzi wakati mwingine.

    Lissu: Naomba muda wa kuzungumza na mashahidi wangu maana sijakaa kuzungumza nao tangu November mwaka jana, naomba muda tushauriane alafu tuendelee. Sidhani kama tutachukua muda mrefu.

    Upande wa serikali: Tunaomba mapumziko, na kama itaridhia ihairishwe hadi Jumatatu.

    Lissu: Kwahiyo naunga mkono kupata mapumziko

    Majaji: Hata sisi tunaunga mkono tunaendelea na mapumziko.

    Majaji: Kwahiyo tutarudi mahakamani saa Tisa na nusu.

    Soma Zaidi Hapa:

  7. Kumuita Rais ni kumuita kwa ajili ya kumhoji - Upande wa serikali

    Upande wa Serikali: Kumuita Rais ni kumuita kwa ajili ya kumhoji kuhusu jambo alilofanya mfanyakazi wake kwa niaba yake.

    Majaji Kuhusiana na kuitwa kwa viongozi wengine wakuu wa Serikali, akiwemo Rais, Makamu wa Rais na Mkuu wa Jeshi, ushahidi wao unatokana na nafasi zao kama viongozi katika upelelezi. Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, kauli hizo zililenga kuvunja amani.

    Lissu: Hizo kauli zililenga kuvunja amani? Nilidhani zililenga kuitisha Serikali. Kwa mujibu wa sheria zetu, hayo ni makosa mawili tofauti na uhaini.

    Upande wa Serikali: Nilikuwa naelezea ushahidi uliotolewa na mashahidi. Kama mashahidi hao wanaonekana kuwa muhimu, hawawezi kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa na upande unaowaita.

    Badala yake, upande husika unaweza kuomba mashahidi hao waje kutoa ufafanuzi kuhusu jambo fulani, lakini hilo linapaswa kufanyika baada ya kufuata masharti ya Kifungu cha 314.

    Soma Zaidi:

  8. Mshtakiwa anatafuta huruma za majaji – Upande wa serikali

    Upande wa mwendesha mashtaka wa serikali katika kesi ya Tundu Lissu, umesema kuwa sheria haipo kwa ajili ya kumfurahisha mtu yeyote, wala haipo kwa ajili ya kufuata maombi au kulipendeza upande wowote.

    Kitendo cha kuililia mahakama kwa hoja za huruma si msingi wa mahakama kufanya maamuzi. Mahakama ipo kusimamia sheria. Mshtakiwa alipaswa kufuata sheria na vifungu tulivyovitaja. Badala yake, anaomba majaji wamuone huruma.

    Lissu amejibu kwa kusema, Kama nina sehemu yoyote nimesema, “Nionee huruma,” au nimewatisha majaji, basi nionyesheni rekodi. Napenda nimwambie wakili kwamba madai kwamba ninaitisha mahakama au naomba nihurumiwe, mimi sijayasema.”

    Upande wa Serikali: “Mahakama hii haiwezi kuita mashahidi kwa sababu ya hofu ya kuogopa serikali.” Sasa, maneno haya yana tafsiri gani? Kwa maoni yangu, yanalenga kuitisha mahakama yenu na kujenga hofu ili mahakama isifanye kazi yake ipasavyo. Hiyo ndiyo tafsiri yangu ya maneno hayo.

    Upande wa Serikali: Waheshimiwa Majaji, msikane maamuzi yenu wenyewe. Tumepitia rekodi zetu na hakuna jambo kama hilo alilolisema. Hakukuwa na hoja yoyote iliyohusu mashahidi hao. Alitaja majina hayo kama alivyotaja mambo mengine mbalimbali, ambayo yaliandikwa katika rekodi. Ndiyo maana tunasema kwamba anayasema haya yote kwa lengo la kuitisha Mahakama ili iwapatie huruma.

    Kwa hiyo, tunaendelea kusimamia msimamo wetu. Alipaswa kuwasilisha hoja yake kwa Mahakama ili Mahakama yenyewe iamue kama ina uwezo wa kuwaita mashahidi hao au la. Suala la kama Serikali ilitishika au haikutishika si jambo la msingi katika shauri hili.

    Upande wa serikali unaongozwa na wakili Nassoro Katuga.

    Soma Zaidi Hapa:

  9. Kama hamuwezi kutoa wito, hakutokuwa na haki katika kesi hii – Lissu

    Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ameiambia mahakama ikiwa haiwezi kutoa wito kwa mashahahidi aliowataka kutoka upande wa serikali kufika mahakamani basi hakutokuwa na haki katika kesi hiyo.

    “Kama kwenye kesi kubwa kama hii mahakama haiwezi kupeleka wito basi sijui itaonekanaje, lindeni haki yangu ili kuweka na haki katika kesi na uadilifu,” amesema Lissu.

    Lissu ameelza kuwa hakuna shauri lolote kwa mashahidi lisilo ruhusu kupelekewa wito na wengine wote wanawezwa kupelekewa wito. Ushahidi wao ni muhimu.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Lissu: Hakuna mtu anayeweza kutoa ushahidi kwa niaba ya Rais

    Katika juhudi za kusisitiza kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, apewe wito wa kufika mahakamani, kiongozi wa upinzani Tundu Lissu amesema hakuna utaratibu wa mtu kutoa ushahidi kwa niaba ya mtu mwingine.

    “Hoja hiyo haina msingi wowote kisheria. Kama ingekuwa kweli kwamba Rais hawezi kutoa ushahidi kwa sababu wafanyakazi wa serikali wameshatoa ushahidi, basi sheria ingesema hivyo. Lakini sheria haisemi hivyo,” ameeleza.

    Pia, Lissu amesema kuwa hoja kwamba Mkuu wa Ujasusi hawezi kutoa ushahidi haina msingi, akidai kuwa maafisa wa usalama wamewahi kutoa ushahidi katika kesi nyingine nchini Tanzania.

    “Akija Mkuu wa Usalama, ushahidi wake utakuwa mzuri kwa sababu yeye ndiye mkuu wa taasisi inayoshughulikia usalama,” amesema.

    Soma Zaidi Hapa:

  11. Lissu apinga hoja ya Rais kutoweza kuitwa mahakamani

    Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amekataa hoja kwamba Rais wa Tanzania hawezi kupelekewa wito wa kuhitajika mahakamani, akieleza kuwa anaweza kupelekewa wito usio wa moja kwa moja.

    Lissu amesema kwa upande wa Rais, wito unaweza kupelekwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Binafsi ili amsaidie mahakama kumfikishia Rais wito huo.

    Amesema ni kweli huwezi kumpelekea Rais moja kwa moja wito wa mahakama, bali unapaswa kupelekwa kupitia katibu wake. Lissu amekiri kuwa huwezi kumlazimisha Rais kufika mahakamani, lakini unaweza kumpelekea wito kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

    “Na Rais ndiye ataamua kuuheshimu wito huo au la,” amesema Lissu.

    Kuhusu Makamu wa Rais mstaafu na Waziri Mkuu mstaafu, amesema kuwa tayari wamestaafu na hivyo hawana hoja ya kwamba wanamsaidia Rais.

    Vilevile, Lissu ametoa hoja zake kuhusu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Ujasusi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkuu wa Majeshi, akisema wote wanaweza kuwa mashahidi.

    Lissu amesema hakuna mtu wala afisa yeyote ambaye hawezi kupelekewa wito, awe Rais, Makamu wa Rais mstaafu, Mkuu wa Majeshi au Mkuu wa Jeshi la Polisi.

    Amesema mahakama inaweza kutoa wito kwa Rais, ingawa haina uwezo wa kutoa hati ya kukamatwa dhidi yake.

    Hata hivyo, Makamu wa Rais mstaafu, Waziri Mkuu mstaafu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Majeshi na Mkuu wa Ujasusi wanaweza kupelekewa hata hati ya kukamatwa iwapo mazingira ya kisheria yataruhusu.

    Soma Zaidi Hapa:

  12. Mahakama haina mamlaka ya kumwita Rais Samia kutoa ushahidi – Mwinuka

    Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, Henry Mwinuka, amesema katika kesi ya Tundu Lissu kuna shahidi mmoja ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na masuala yanayomhusu Rais yanasimamiwa na Presidential Affairs Act, Sura ya 19.

    Mwinuka amesema kuwa, kwa mujibu wa sheria hiyo, mahakama haina uwezo wa kutoa wito wa kumtaka Rais kufika mahakamani kutoa ushahidi au kushiriki shughuli nyingine zozote za kimahakama.

    “Kwa upande mwingine, kifungu hicho kinaeleza msingi wa utoaji wa taarifa. Kwa kuzingatia kwamba mshtakiwa anahitaji kuwaita baadhi ya mashahidi, anaomba Mahakama hii itoe wito ili mashahidi hao waweze kufika mahakamani, kwa sababu anahitaji kuonana nao na kupata ushahidi unaohitajika ili aweze kujitetea,” amesema Mwinuka.

    Pia amesema kuwa kwa upande wa maafisa wa Tanzania Intelligence and Security Service (TISS), nafasi na majukumu yao ya kikazi yanawawekea mipaka katika kutoa taarifa kwa kuwa hawawezi kuweka hadharani kila kitu wanachokifahamu.

    “Kwa hiyo, hatuoni kama ni sahihi kuwalazimisha kutoa taarifa ambazo zinaweza kuwa na siri au taarifa nyeti wanazozifahamu kwa mujibu wa majukumu yao,” ameeleza.

    Aidha, amesema sheria hiyo imeweka masharti na adhabu kuhusu utunzaji na utoaji wa taarifa hizo.

    “Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuiingiza Mahakama hii katika mgogoro wa kisheria unaohusiana na taarifa ambazo, kwa mujibu wa sheria, zinapaswa kubaki kuwa siri,” amesema.

    Soma Zaidi Hapa:

  13. DPP yapinga baadhi ya mashahidi wa Lissu kuitwa mahakamani, akiwemo Rais Samia

    Upande wa mashtaka unaoongozwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) umeitaka mahakama kutowaita baadhi ya mashahidi katika kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kama mshitakiwa alivyowataja.

    Baada ya mahakama kumkuta Lissu na kesi ya kujibu, Mwenyekiti huyo wa CHADEMA ametoa orodha ya mashahidi kumi na mmoja ambao ameiomba mahakama iwaite kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

    Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imesema mashahidi namba 1 hadi 7 wasiruhusiwe kuja kutoa ushahidi.

    Mashahidi ambao DPP imetaka wasiitwe ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Philip Mpango, pamoja na Kassim Majaliwa aliyekuwa Waziri Mkuu.

    Wa nne ni Camillus Wambura, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania. Wa tano ni Jenerali John Mkunda, Mkuu wa Majeshi Tanzania. Shahidi wa sita ni Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS). Shahidi wa saba ni Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Kanali wa Polisi Ramadhani Kindai.

    Kuhusu mashahidi watatu wa awali, waendesha mashtaka wamesema hao ni viongozi wa serikali inayomtuhumu Lissu kwa kosa la kutishia Katiba ya nchi.

    DPP imeiomba mahakama iuone ushahidi wa mashahidi hawa saba kuwa si muhimu kwa sababu ushahidi wao umeshatolewa na mashahidi wa upande wa serikali ambao ni watumishi wa serikali.

    Soma Zaidi Hapa:

  14. Lissu: Nimezuiwa kukutana na mashahidi gerezani

    Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ametoa malalamiko mbele ya mahakama iliyomkuta na kesi ya kujibu katika tuhuma za uhaini, akisema baadhi ya viongozi wa chama chake aliowataja kuwa mashahidi wanazuiwa kumtembelea akiwa kizuizini.

    “Nimekuwa na matatizo makubwa ya haki ya mtu kukutana na mawakili wake na mashahidi wake. Hawa watu nimewataja kama mashahidi wanaotoka Chadema wamepigwa marufuku kunitembelea gerezani,” Lissu amesema.

    Lissu ameiomba mahakama itoe amri ili aweze kukutana na mashahidi wake.

    Soma Zaidi Hapa:

  15. Lissu aomba Samia na viongozi wakuu wa serikali kuwa mashahidi

    Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ameliambia jopo la majaji waliomkuta na kesi ya kujibu kuhusu tuhuma za uhaini kuwa atajitetea mwenyewe.

    Pia, Lissu amesema ataomba mashahidi wafuate, ambao ataiomba mahakama iwapelekee wito wa kuitwa. Amemtaja shahidi wa kwanza kuwa ni Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais wa Tanzania.

    Mwingine ni Philip Mpango, ambaye wakati wa matukio yanayolalamikiwa alikuwa mjumbe wa Baraza la Taifa na kiongozi namba mbili serikalini.

    Kassim Majaliwa, wakati matukio hayo yanatokea, alikuwa Waziri Mkuu na kiongozi anayesaidia serikali katika masuala ya usalama wa taifa.

    Lissu pia amemtaja shahidi wa nne, Camillus Wambura, ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania.

    Shahidi wa tano ni Jenerali John Jacob Mkunda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania.

    Shahidi wa sita ni Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).

    Shahidi wa saba ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ramadhani Kindai.

    Wengine ni John Mnyika, Katibu Mkuu wa CHADEMA, ambaye amesema ndiye mtendaji mkuu wa chama na anaweza kutoa ushahidi, kwani aliandaa mkutano huo na alikuwapo.

    Shahidi wa tisa ni Amani Sam Molugwa, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA.

    John Heche ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA.

    Mwingine ni Brenda Upia, shahidi wa kumi na mmoja, ambaye ndiye aliyewaalika watu wa Jambo TV kwenye mkutano huo.

    Soma Zaidi Hapa:

  16. Lissu ana kesi ya kujibu ya tuhuma za uhaini - Mahakama

    Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa uamuzi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na kumkuta ana kesi ya kujibu.

    Akisoma uamuzi huo, Jaji Ndunguru, anayeongoza jopo la majaji linalosikiliza shauri hilo, amesema baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka unaowakilishwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), mahakama imejiridhisha kuwa kuna ushahidi wa kutosha unaomfanya Lissu awe na kesi ya kujibu.

    Uamuzi huo unamaanisha kuwa kesi hiyo sasa inaingia katika hatua muhimu ambapo Tundu Lissu atapewa fursa ya kuwasilisha utetezi wake mbele ya mahakama.

    Katika hatua hiyo, upande wa utetezi unaweza kuwasilisha ushahidi pamoja na kuwaita mashahidi wake ili kujibu hoja na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

    Lissu alikamatwa mkoani Ruvuma kabla ya kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam, ambako alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa rasmi mashtaka yanayohusiana na uhaini pamoja na makosa mengine yanayodaiwa kuhusiana na kauli na shughuli zake za kisiasa.

    Upande wa mashtaka umekuwa ukidai kuwa baadhi ya kauli na matendo ya Lissu yalilenga kuzuia au kuvuruga mchakato wa uchaguzi mkuu na kuchochea uasi dhidi ya serikali. Madai hayo ndiyo ambayo yamekuwa msingi wa mashtaka yanayomkabili mwanasiasa huyo.

    Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya Tanzania kutokana na uzito wa mashtaka pamoja na nafasi ya Lissu katika siasa za Tanzania. Mwenendo wa kesi hiyo pia umeibua mjadala mkubwa kuhusu haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na namna sheria za uhaini zinavyotumika katika mazingira ya kisiasa.

    Jumuiya na taasisi mbalimbali za kimataifa zimeonyesha wasiwasi kuhusu mwenendo wa kesi hiyo na zimekuwa zikitoa wito wa kuhakikisha mchakato wa kisheria unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia haki za msingi za mshtakiwa.

    Baadhi yao wamekuwa wakitaka mamlaka kuhakikisha kuwa Lissu anapata dhamana, matibabu na mazingira yote muhimu ya kisheria yanayostahili, huku wengine wakitoa wito wa kuachiwa kwake.

    Hata hivyo, uamuzi wa mahakama kwamba Lissu ana kesi ya kujibu sio hukumu ya kuwa amepatikana na hatia. Ni hatua ya kisheria inayomaanisha kuwa mahakama imeona kuna msingi wa yeye kuitwa kutoa upande wake wa utetezi dhidi ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

    Kwa sasa, macho yanaelekezwa katika hatua inayofuata ya kesi hiyo, ambapo Tundu Lissu atapata nafasi ya kujibu mashtaka, kupinga ushahidi uliowasilishwa dhidi yake na kuwasilisha ushahidi wa upande wa utetezi.

  17. Maombi yakiendelea mahakamani

    Raia wanaotaka kuingia wanaambiwa mahakama imejaa.

  18. Kesi ya Lissu: Hali ilivyo ndani ya mahakama

    Kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa Chadema Tundu Lissu nchini Tanzania inatarajiwa kuamuliwa.

  19. Lissu: Ulinzi umeimarishwa nje na ndani ya mahakama

    Ulinzi umeimarishwa huku baadhi ya wafuasi wakizuiwa kuingia mahakamani.

    Raia wanaotaka kuingia wanaambiwa kuwa mahakama imejaa.