Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mnyika Mahakamani: Si Lissu aliyesambaza video za mkutano wa watia nia

Mnyika aeleza majaji kuwa Lissu hakushiriki katika maandalizi ya mkutano wa Aprili 3 wala kuwaalika waandishi waliohudhuria.

Muhtasari

Moja kwa moja

Elizabeth Kazibure, Rashid Abdallah & Asha Juma

  1. Kutoka Tume ya Nyalali hadi Samia: Mnyika asimulia hotuba ya Lissu

    Lissu: Lengo la kualika waandishi wa habari kwa sehemu hiyo lilikuwa nini?

    Mnyika: Lengo lilikuwa kuwapa nafasi ya kuchukua habari na kuzifikisha kwa umma kuhusu madai yetu ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria ili kuwezesha uchaguzi huru na wa haki chini ya kaulimbiu ya No Reforms, No Election; bila ya mabadiliko hakuna uchaguzi.

    Lissu: Unaposema hotuba ya mwenyekiti ndiyo ilikuwa ndefu, unamaanisha nini?

    Mnyika: Katika muda wa masaa matatu, masaa mawili na zaidi alizungumza mwenyekiti wa chama.

    Lissu: Waeleze majaji hotuba hiyo ndefu ilihusu nini.

    Mnyika: Mwenyekiti alieleza historia ndefu ya madai ya kutaka haki kuanzia kabla na baada ya Tume ya Rais maarufu kama Tume ya Nyalali kati ya mwaka 1991 na 1992. Aliendelea kuzungumzia mabadiliko ya kikatiba na kisheria ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki yaliyokataliwa na serikali ya chama kimoja wakati huo, CCM.

    Lissu: Suala lingine nililolizungumzia?

    Mnyika: Alieleza madhara ya kutofanyika kwa mabadiliko hayo kuanzia uchaguzi wa mwaka 1995.

    Pia alieleza maoni ya tume nyingine zilizoundwa kushughulikia mambo ya kikatiba wakati wa uchaguzi. Alitaja Tume ya Kisanga, akataja Tume au Kamati ya Bomani, na akaeleza kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba kati ya mwaka 2011 hadi 2014, maarufu kama Tume ya Warioba, na jinsi CCM ilivyotumia wingi wake katika Bunge la Katiba kukwamisha mchakato huo.

    Pia alieleza madhara ya kukosekana kwa mabadiliko hayo kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, uchaguzi wa vijiji na vitongoji wa mwaka 2019, uamuzi wa Chadema kujitoa kwenye uchaguzi baada ya wagombea wengi wa Chadema kuondolewa kwenye uchaguzi, na yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo yeye alikuwa mgombea urais.

    Alieleza baadhi ya wagombea kuenguliwa kwa mapingamizi yasiyokuwa na msingi, na wale waliobaki kufungiwa kampeni. Pia alieleza kuwa siku ya kura mawakala wa Chadema waliondolewa vituoni katika maeneo mengi na kwamba kura ziliingizwa kwenye vituo vya kupigia kura zikiwa zimeshapigwa.

    Pia alieleza kuhusu hatua ambazo chama kilichukua baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 wakati huo mwenyekiti wa chama akiwa Freeman Mbowe, akidai mabadiliko ya kikatiba na tume huru ya uchaguzi. Alisema matokeo yake ni Mbowe kubambikizwa kesi ya ugaidi na kukaa rumande gerezani kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2022.

    Alieleza kuwa baada ya kesi hiyo kufutwa na Mbowe kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu mwaka 2022, ndipo mazungumzo kati ya Chadema na CCM pamoja na serikali yalipoanza.

    Akaeleza kuwa katika mazungumzo hayo upande wa Chadema uliwasilisha kwa mdomo na kwa maandishi mapendekezo ya maeneo ya marekebisho ya kikatiba ili kuwezesha uchaguzi huru na wa haki. Alisema baada ya mwaka mmoja wa mazungumzo, upande wa CCM na serikali ulijibu kwa mdomo kukataa mapendekezo yote ya marekebisho ya Katiba yaliyolenga kuwezesha uchaguzi huru na wa haki, na hatimaye mazungumzo yakavunjika.

    Lissu: Subiri, waeleze waheshimiwa majaji hayo mazungumzo na mapendekezo yalikuwa yanahusu uchaguzi gani?

    Mnyika: Yalikuwa yanahusu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

    Lissu: Waeleze majaji ushiriki wako katika mazungumzo hayo.

    Mnyika: Mimi nilikuwa miongoni mwa timu iliyokutana na Rais tarehe 22 Mei 2022. Katika kikao hicho, mapendekezo ya namna ya kukwamua na kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya yaliwasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa wakati huo, Freeman Mbowe.

    Lissu: Waeleze majaji kulikuwa na nini baadaye?

    Mnyika: Mapendekezo ya hoja nyingine kumi za mazungumzo, mojawapo ikiwa ni marekebisho ya kikatiba na kisheria ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki, yaliwasilishwa na mimi.

    Lissu: Uchaguzi huru wa mwaka gani?

    Mnyika: Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024. Mapendekezo hayo yalihusu kufanyika kwa marekebisho ya kuwezesha uchaguzi huru na wa haki tuliyoyaita Minimum Reforms.

    Lissu: Baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo, nini kiliendelea?

    Mnyika: Rais aliahidi kwamba mchakato wa mazungumzo utaendelea, na akaahidi kuunda timu ya watu watano ikiongozwa na Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM. Sisi kwa upande wetu, aliyekuwa mwenyekiti wetu pia aliahidi kuunda timu ya watu watano, na aliunda.

    Lissu: Mazungumzo hayo yaliendelea hadi lini?

    Mnyika: Mazungumzo yaliendelea hadi tulipojibiwa na upande wa pili kwamba marekebisho hayo yasubiri hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Hata yale tuliyoyaita Minimum Reforms, kama kuwa na tume huru ya uchaguzi, matokeo ya urais kupingwa mahakamani, maamuzi ya tume kufanyiwa mapitio, na tume kuwa na watumishi wake huru. Walieleza kuwa mradi yanagusa marekebisho ya Katiba, yasubiri mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

    Nzengeli: Waheshimiwa majaji, muda si rafiki na tumepokea maombi kutoka kwa watu wa usalama. Tunaomba tuishie hapo kutokana na muda.

    Jaji: Mshitakiwa, wewe umechoka?

    Lissu: Ombi linahusu masuala ya kiulinzi, sasa mimi siwezi kufahamu, lakini tukubali tu kwamba saa kumi na moja hii inatosha.

    Jaji: Tunaahirisha hadi siku ya Jumatatu saa tatu asubuhi.

  2. Mnyika Mahakamani: Hotuba ya Lissu ilijikita kwenye mabadiliko ya Katiba

    Lissu: Lengo la kualika waandishi wa habari hiyo sehemu ilikuwa ni nini?

    Mnyika: Lengo ni kuwapa nafasi ya kuchukua habari na kufikisha kwa umma, ambayo inahusu madai yetu ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria kuwezesha uchaguzi huru na wa haki chini ya kauli mbiu ya No Reforms, No Election; bila ya mabadiliko hakuna uchaguzi.

    Lissu: Unaposema hotuba ya mwenyekiti ndiyo ilikuwa ndefu unamaanisha nini?

    Mnyika: Katika muda wa saa tatu, saa mbili na zaidi alizungumza mwenyekiti wa chama.

    Lissu: Waeleze majaji hotuba hiyo ndefu ilihusu nini?

    Mnyika: Mwenyekiti alieleza historia ndefu ya madai ya kutaka haki kuanzia kabla na baada ya Tume ya Rais maarufu kama Tume ya Nyalali kati ya mwaka 1991-92.

    Aliendelea kuongea juu ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria kuwezesha uchaguzi huru na wa haki yaliyokataliwa na serikali ya chama kimoja wakati huo, CCM.

    Lissu: Swala jingine nililolizungumzia?

    Mnyika: Alieleza madhara ya kutofanyika kwa mabadiliko hayo kuanzia mwaka 1995 wakati wa uchaguzi.

    Pia akaeleza maoni ya tume nyingine zilizoundwa kushughulikia mambo ya kikatiba wakati wa uchaguzi. Akataja Tume ya Kisanga, akataja tume au kamati ya Bomani, akaeleza kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba kati ya mwaka 2011 mpaka 2014 maarufu kama Tume ya Warioba, na jinsi CCM ilivyokwamisha mchakato huo na kueleza madhara ya kukosekana kwa mabadiliko hayo kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, uchaguzi wa vijiji na vitongoji mwaka 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

  3. Mnyika Mahakamani: Si Lissu aliyesambaza video za mkutano wa watia nia

    Katuga: Mshtakiwa anamtilia maneno shahidi. Amuulize maswali in chief, waheshimiwa majaji. Inatakiwa itoke kwa shahidi.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, sasa hizi objection zinatupotezea muda. Ni leading question na si vinginevyo.

    Katuga: Waheshimiwa majaji, leading question imekuwa provided kwenye kifungu cha 159. Sasa shahidi yeye anatiliwa maneno na hizo ndiyo leading questions.

    Lissu: Sasa swali langu lina-lead namna gani? Mimi nilisoma LLB miaka 32 iliyopita. Mimi si mjuzi, waheshimiwa majaji. Swali langu ni sahihi, tunapotezana muda tu hapa.

    Jaji: Tuendelee.

    Lissu: Ahsante, Mheshimiwa.

    Lissu: Shahidi, inadaiwa kwamba mimi ndiye niliyesambaza video za mkutano huo.

    Mnyika: Hapana, hayo madai ni ya uongo. Tunaamini katika uhuru wa vyombo vya habari na mwanzo wa mkutano nilitangaza mkutano utakuwa na awamu mbili. Awamu ya kwanza waandishi wa habari watahusika, na baadaye vyombo vya habari vitaondoka kuendelea na watia nia wenyewe.

    Lissu: Waeleze majaji hiyo sehemu ya kwanza ambayo waandishi wa habari wangehusika nayo ni ipi.

    Mnyika: Kwa kadiri ya kumbukumbu zangu, zilitolewa hotuba fupi fupi na Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ally Ibrahim; Katibu Mkuu wa Chama, John Mnyika; Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Mzee Said; Makamu Mwenyekiti Bara, John Wegesa Heche; na Mwenyekiti Tundu Antipas Lissu, aliyetoa hotuba ndefu.

    Lissu: Ahsante, waheshimiwa majaji. Ninaomba health break ya dakika tano.

  4. Mahakamani: Mnyika akanusha Lissu kuhusika na mialiko ya waandishi wa habari

    Lissu: Sasa wakati wewe na Sekretarieti yako mnafanya yote haya, mwenyekiti alikuwa wapi?

    Mnyika: Mwenyekiti alikuwa kwenye mikutano ya Kanda ya Nyasa kwenye operesheni ya No Reforms, No Election.

    Lissu: Wafafanulie majaji, Kanda ya Nyasa ndiyo sehemu gani ya nchi hii?

    Mnyika: Waheshimiwa majaji, Kanda ya Nyasa inajumuisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa na Rukwa.

    Lissu: Waeleze majaji hiyo ziara ya mwenyekiti ilitumia muda gani?

    Mnyika: Nakumbuka ilianza tarehe 23 Machi hadi kabla ya tarehe 3 Aprili.

    Lissu: Waeleze majaji, wakati mnafanya maandalizi ya mkutano huo, kama mwenyekiti alishiriki kwa namna yoyote kwenye mkutano huo.

    Wakili wa Serikali: Tuna concern kidogo jinsi shahidi huyu anavyoongozwa. Tunaomba muongozaji akumbushwe kufuata kanuni.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, hili pingamizi ni la kitu gani? Taratibu ipi ambayo nimekiuka? Na kwa sababu haijasemwa, naomba niendelee.

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji ni namna gani mwenyekiti alivyoshiriki kwenye maandalizi ya mkutano huo wa tarehe 3 Aprili.

    Mnyika: Mwenyekiti wa chama hakushiriki kwa namna yoyote ile.

    Lissu: Waeleze majaji namna mwenyekiti alivyoshiriki kuwaalika watia nia au waandishi wa habari.

    Mnyika: Mwenyekiti hakushiriki kwa namna yoyote ile.

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji waandishi wa habari na vyombo vyao ambavyo unakumbuka vilihudhuria mkutano huo.

    Mnyika: Nakumbuka The Chanzo, Mwanzo TV na Jambo TV.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, naomba nipatiwe Exhibit D16. Shahidi apatiwe Exhibit D16, maelezo ya PW17.

    Lissu: Shahidi, kwenye hicho kielelezo naomba wasomee waheshimiwa majaji huyo shahidi wa Jambo TV alipataje taarifa za mkutano.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, naomba nipatiwe Exhibit D16. Shahidi apatiwe Exhibit D16, maelezo ya PW17.

    Lissu: Shahidi, kwenye hicho kielelezo naomba wasomee waheshimiwa majaji huyo shahidi wa Jambo TV alipataje taarifa za mkutano.

    Mnyika: Anasoma sawa sawa na alivyoelekezwa juu ya PW17, alivyopata taarifa za mkutano huo kutoka kwa mkurugenzi wao, John Marwa.

    Lissu: Endelea.

    Mnyika: Anataja vyombo vingine vya habari.

    Lissu: Hivyo vyombo ulivyovisahau vilikuwepo?

    Katuga: Hii ni kinyume cha taratibu, waheshimiwa majaji. Shahidi anasomeshwa document ya mahakama halafu analazimishwa kusema kama anakumbuka.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, hiyo naiondoa.

    Lissu: Sasa shahidi, baada ya ushahidi huo ambao umeutoa mpaka hapo ulipofikia, hii tuhuma ya kwamba mimi ndiyo nilialika hao waliokuja kwenye huo mkutano, wewe unaionaje?

    Mnyika: Waheshimiwa majaji, hiyo ni tuhuma ya uongo. Ni tuhuma ya kubambikiza tu.

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, wakati mnatuma mwaliko kwa hawa waandishi wa habari, mlitoa maelekezo waje na nini?

    Mnyika: Hakukuwa na maelekezo yoyote waje na kitu gani.

    Lissu: Imetolewa ushahidi kwamba waandishi wa habari wa Jambo TV waliokuja waliagizwa waje na kamera na vitu vingine kama hivyo.

    Ubishani kidogo pande zote, Jaji anasema tuendelee.

    Lissu: Waeleze majaji iwapo kulikuwa na maelekezo juu ya namna ya kutumia vifaa vyao.

    Mnyika: Hakukuwa na maelekezo juu ya namna ya waandishi wa habari kutumia vifaa vyao katika tukio hilo.

    Lissu: Wafafanulie majaji utaratibu uliotumika kurusha matangazo ya huo mkutano.

    Mnyika: Ninachofahamu...

  5. Shahidi John Mnyika anatoa ushahidi wake

    Pande zote mbili ziko tayari kuendelea Lissu anamwita shahidi wake wa pili.

    Mnyika tayari amepanda kizimba cha shahidi anasubiri kiapo kwa mujibu wa imani yake.

    Jaji: Shahidi unaitwa nani

    Mnyika: John John Mnyika

    Jaji: Unafanya shughuli gani

    Mnyika: Katibu mkuu wa Chadema

    Jaji: Dini yako

    Mnyika: Mkristo

    Jaji: Utaapishwa kwa mujibu wa imani yako

    Myika anakula kiapo mbele ya mahakama tayari kutoa ushahidi

    Lissu: Shahidi naomba nikuongeze kwenye kutoa ushahidi wako naomba ujibu pole pole na kwa sauti

    Lissu: Umeshikilia nafasi hii ya katibu mkuu tangu lini?

    Mnyika: Tangu mwaka 2019 Lissu waeleze majaji kabla ya nafasi hiyo ulikuwa na nafasi nyingine ndani ya chama chako.

    Mnyika: Nilikua Mkurugenzi wa vijana taifa tangu mwaka 2003 Nafasi ambayo niliishikilia mpaka mwaka 2011 wakati nashikilia nafasi mwaka 2007 niliteuliwa kuwa mkurugenzi wa habari na uenezi nilikua nashika nafasi zote mbili ambazo nilizitumikia mwaka 2014

    Na wakati huohuo kati ya mwaka 2009 mpaka mwaka 2011 nilishikilia pia nafasi ya ukurugenzi wa mambo ya nje na mahusiano ya kimataifa Chadema Mwaka 2014 niliteuliwa kuwa naibu katibu mkuu chadema taifa hadi 2019 nilipochaguliwa kuwa katibu mkuu Nilikua pia mbunge.

    Lissu: Huko sijakupeleka bado nataka za chama kwanza

    Mnyika: Nilishakuwa mwenyekiti wa chama mkoa wa kinondoni kwa vipindi viwili.

    Lissu: Nafasi nyingine zaidi ya hizo..?

    Myika: Nilipokuwa Mbunge wa ubungo nilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa wabunge wa Chadema bungeni mwaka 2010 hadi 2015.

    Na nilikuwa Mbunge wa jimbo la kibamba kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2020.

    Lissu: Sasa shahidi nafasi ya katibu mkuu wa Chadema ni nafasi ya aina gani ndani ya chama.

    Mnyika: Chadema inaongozwa kwa misingi ya Chadema na nafasi ya katibu mkuu ni nafasi ya Mtendaji mkuu wa Chama ambaye ndiye mwenyekiti wa sekretarieti ya chama ambacho ndio chombo kinacho simamia chama hivyo Katibu Mkuu ndiye msimamizi wa rasilimali zote za chama na shughuli zote za chama.

    Lissu: Ukisikia jaji amesema mh ndio unaendelea hahahaha.

    Jaji: Tuendelee.

    Mnyika: Vilevile ndio msimamizi mkuu wa watumishi wote wa makao makuu ya chama na watendaji wake.

    Lissu: Ahsante, sasa shahidi naomba uwaeleze majaji kama chama chako huwa kinafanya mikutano na taratibu za kuandaa hiyo mikutano.

    Mnyika: Chama huwa kinafanya mikutano ya ndani ikiwemo vikao vya kikatiba ikiwemo mikutano ya hadhara kwa upande wa mikutano ya ndani ngazi husika ya kiutendaji ambayo ni sekretarieti inakaa kikao ngazi ya taifa chini ya katibu mkuu, kinafanya maamuzi ya kufanya kikao husika na utaratibu wa maandalizi yake.

    Lissu: Kwa vikao vya ndani kama nimekuelewa kazi ya kuandaa vikao ni kazi ya sekretarieti taifa ya Chama naomba waeleze majaji nani ni wajumbe wa hiyo sekretarieti

    Mnyika: Ni Katibu Mkuu, manaibu katibu wakuu wawili mmoja wa bara mwingine wa Zanzibar wakurugenzi wa kKurugenzi za Chama taifa, wataalamu, makatibu wa sekretarieti na makatibu wa mabaraza ya chama wakiongozwa na baraza la wazee, Baraza la wanawake (Bawacha) na Baraza la Vijana (Bavicha).

    Lissu: Hao ndio wajumbe wa sekretarieti ya chama taifa

    Mnyika: Ndio

    Lissu: Katika wajumbe wote uliowataja waeleze majaji kama mwenyekiti wa chama ni sehemu ya sekretarieti ya Chama taifa.

    Mnyika: Mwenyekiti sio sehemu ya sekretarieti taifa Lissu waeleze majaji kama mwenyekiti anashiriki kwenye hivyo vikao vya maandalizi.

    Mwenyekiti huwa hashiriki kwenye hivyo vikao

    Lissu: Leo tuko mahakamani sababu ya kesi ya uhaini inayonikabili mimi. Mimi niliitisha mkutano wa watia nia wa uchaguzi mkuu mwaka 2015, waeleze majaji kama unaufahamu huo mkutano wa Aprili tatu mwezi wa nne mwaka jana.

    Mnyika: Ninaufahamu huo mkutano sababu uliandaliwa kwa maelekezo yangu na sekretarieti ambayo ninaisimamia na ilifanya maandalizi chini ya usimamizi wangu na nikishiriki mkutano wewe

    Lissu: Waeleze majaji huo mkutano ulikuwa wa hadhara.

    Mnyika:Ulikuwa mkutano wa ndani.

    Lissu: Mkutano ulikuwa na lengo gani?

    Mnyika: Ulikuwa ni mkutano wa ndani wa kutaka kufanyika kwa azimio la kimageuzi ya kikatiba na kisheria na kuwezesha kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki chini ya kauli mbiu ya No reforms no Election ikimaanisha bila mabadiliko hakuna uchaguzi

    Lissu: Huo mkutano uliwahusu wakina nani?

    Mnyika: Mkutano uliwahusu wote waliokuwa na nia ya kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 maarufu kama watia nia 2025.

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama kuna watu wengine nje ya hao watia nia mliowashirikisha kwenye mkutano huo

    Mnyika: Tulialika viongozi wakuu wa chama na waandishi wa habari

    Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kusema ulialika viongozi wakuu wa chama mnaaanisha akina nani?

    Mnyika: Mwenyekiti wa chama taifa.

    Tundu Antipas Lissu, Makamo mwenyekiti Bara John Wegesa Heche, Makamo mwenyekiti Zanzibar Siad Mzee Said na viongozi wengine wakuu ambao ni sehemu ya manaibu wake.

    Lissu: Ahsante Katibu mkuu , Shahidi huo mkutano wa ndani ulifanyikia wapi?

    Mnyika: Mkutano ulifanyikia makao makuu ya chama mikocheni mtaa wa daima nyumba namba 31 kwenye ukumbi wa chama wa mikutano

    Lissu: Shahidi umesema vilevile mlialika waandishi wa habari na ni wa vyombo vipi kwa kumbukumbu zako?

    Mnyika: Kazi ya kualika waandishi wa habari ilifanywa na mkurugenzi wa mawasiliano wa Chama Brenda Jonas Rupia na nilielekeza itolewe taarifa kwa umma (Tangazo) ambalo lilitolewa tarehe 27 mwezi Machi ambalo lilialika waandishi wa habari na kuutarifu umma juu ya kikao hiki na ilisainiwa na Brenda Rupia.

  6. Lissu akamilisha ufafanuzi wa ushahidi wake

    Kielelezo cha D14. Detective Amani Michael ndiye afisa wa polisi kati ya hawa wote pekee aliyejaza maelezo kwa usahihi. Kila sehemu kuna saini yake katika kila ukurasa, na mwisho kuna saini ya afisa wa polisi aliyemchukua maelezo na kuyaandika. Huyu tu.

    Lissu: Niliulizwa na wakili wa Serikali, Nzengeli, "Hawa mashahidi wa Jamhuri unawaita wahalifu kwani walishahukumiwa?"

    Waheshimiwa majaji, watu ambao wamepanga kufanya uhalifu wakakamatwa kwa kupanga kufanya uhalifu, wakakiri mbele ya polisi kuwa wanapanga kufanya uhalifu, wakaja mahakamani wakaiambia mahakama, walio panga kufanya uhalifu. Ni ushahidi wangu kwamba hawa ni wahalifu.

    Nzengeli: Kweli ni ushahidi wake, lakini mimi nilimuuliza kati ya wewe na mahakama nani anaweza kusema wale ni wahalifu?

    Lissu: Waheshimiwa majaji, nimetoa ufafanuzi.

    Jaji: Tuendelee.

    Lissu: Naelekea kumaliza, waheshimiwa majaji.

    Kulikuwa na maswali niliyoulizwa juu ya omission na contradiction, na kwenye jibu langu moja wapo ni kwamba hizi omission ndio contradiction zenyewe. Sijui kama kwenye rekodi ipo sahihi.

    Jaji: Kwa swali lipi?

    Lissu: Basi niondoke hapo, waheshimiwa majaji. Kwa karatasi ambazo ninazo, waheshimiwa majaji, nimemaliza.

    Jaji: Na ndio msingi wa re-examination. Huwezi kuuliza na kufafanua kila kitu.

    "Lissu amemaliza kutoa ushahidi"

    Wakati Lissu ameomba mapumziko kidogo kesi iendelee saa nane. Akiwa anarudi kizimba cha mshitakiwa alisema "Uhuruni kunaendaje? Waambie nimewamiss."

  7. Mahakama yamzuia Lissu kutoa ufafanuzi zaidi kwenye Re-examination

    Lissu: Naomba washauri wangu wanisomee swali la mwisho, sikuliandika.

    Nzengeli: Naona utaratibu unakiukwa. Hao anaowaita washauri hawatambuliki na mahakama. Kama hakuandika, aiombe mahakama.

    Jaji: Naomba tuendelee.

    Lissu: Nimeulizwa kwamba nia ya kutenda kosa inathibitishwa na matendo? Nikajibu si kweli. Ufafanuzi wangu ni huu kwenye kesi za uhaini.

    Nzengeli: Swali niliuliza mwenyewe na sikuacha nafasi ya maelezo. Swali lilifungwa, kama atatoa maelezo itabidi turudi kwenye cross-examination.

    Lissu: Hili pingamizi ni la bure. Sasa anayeamua nifafanue ni wakili wa serikali au ni mimi?

    Jaji: Wote tunajua re-examination inajikita kwenye swali lililoulizwa na si zaidi.

    Lissu: Sawa, waheshimiwa majaji. Ufafanuzi wangu ni kwamba si kweli makosa yote nia inathibitishwa kwa matendo. Makosa mengine nia inathibitishwa kwa uchapishaji.

    Jaji: Ndiyo.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, niliulizwa na wakili...

    Katuga: Kwamba hii kesi imeshachunguzwa vilevile na Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa. Ikauliza mahakama yetu iko huru? Nikajibu iko huru. Pamoja na kwamba mahakama yetu iko huru, hizo taasisi nyingine zina umuhimu wake.

    Katuga: Yaleyale, waheshimiwa majaji, sababu alijibu na wala sikuuliza habari ya umuhimu. Sasa kwa namna hii tutamaliza kesi? Ndiyo maana tukasema hii itakuwa na changamoto zake. Ufafanuzi huu anaoufanya ni kuleta ushahidi mpya na sisi tuko macho, unless aiombe mahakama alete ushahidi mpya.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, huu si ushahidi mpya. Ameniuliza mwenyewe kama mahakama yetu inapangiwa na kama iko huru. Nafafanua wala si ushahidi mpya, waheshimiwa majaji.

    Jaji: Hili suala litatuchukua muda mrefu sana kama hatutafuata taratibu, na hata kwenye re-examination si kila swali. Hebu lisome tena hilo swali vyema.

    Lissu: Ninachotaka kusema ni kwamba mahakama zetu, licha ya kwamba hazipangiwi, hazinyimwi kutazama maamuzi ya taasisi nyingine za kimataifa.

    Katuga: Waheshimiwa majaji, yeye alishajibu iko huru. Hayo ya instruments nyingine mimi sikuuliza. Sasa kuyaleta sasa hivi halikuwa sehemu ya swali langu, mimi sikuuliza kabisa.

    Lissu: Mzigo wa kuthibitisha mashtaka ni wa upande wa waleta mashtaka.

    Jaji: Tuendelee.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, niliulizwa vilevile kwamba kwenye ushahidi wangu nilisema kwamba niliwahi kuwa Rais wa Tanganyika Law Society. Nikasema ni kweli, na nikaulizwa uliposhtakiwa ulikuwa bado Rais wa TLS, na nikaulizwa ulikuwa na kinga. Naomba nifafanue.

    Jaji: Unafafanua nini hapo? Naomba tuendelee.

    Lissu: Niliulizwa njia ya kupinga sheria zinazokinzana na Katiba. Nimesema kuna njia za kimahakama na zisizo za kimahakama, na nikaulizwa hiyo iko kwenye kifungu gani cha Katiba. Nikasema iko kwenye kifungu cha 20, kifungu kidogo cha kwanza.

    Sasa, waheshimiwa majaji, naomba kueleza haya majibu yangu. Hizo njia za kutaka mabadiliko ya sheria, ufafanuzi wangu ni kwamba hizo njia za nje ya mahakama zinatambulika kikatiba na zimethibitishwa hivyo na mahakama.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, nikaulizwa kama namfahamu Ishengoma Ndyanabo. Nikaulizwa alifanya nini, nikasema ninamfahamu na alikwenda mahakamani kupinga uchaguzi. Nikaulizwa kama ninamfahamu Mchungaji Mtikila ambaye aliomba mahakama itambue mgombea binafsi, na alishinda kesi Mahakama ya Afrika na mpaka sasa haijatekelezwa.

    Jaji: Sasa hapo unafafanua nini?

    Lissu: Ni sawa, waheshimiwa majaji.

    Jaji: Tuendelee.

    Lissu: Niliulizwa sana kuhusu kifungu cha 39(2)(d) kuhusu maneno yale "or" na mimi nikasema maneno haya yanafana. Wakili wa serikali alikuwa anasema maneno haya hayafanani. Ninaomba nifafanue hili, waheshimiwa majaji. "An act" or "did" ni same thing, maana yake ni matendo, na nilivyosema yanafanana nilikuwa na maana hiyo.

    Katuga: Sikwenda kwenye tafsiri na hakuna sehemu nilimuuliza tafsiri. Na hii tafsiri ameipata wapi? Wakati kwenye cross-examination hakukuwa na hilo swali, na tukasomeshana kisheria.

    Lissu: Waheshimiwa majaji, naomba mahakama itusomee rekodi ya hiki wakili wa serikali anachokisema.

    Jaji: Anasoma kile mahakama ilichokiandika, anasoma kwa Kiingereza.

    Lissu: Naendelea, waheshimiwa majaji. Niliulizwa kama ninafahamu mihimili mitatu na nikamwambia niitaje, na nikaulizwa kazi zake nikazitaja. Niliulizwa juu ya kazi za Bunge, nikasema kutunga sheria. Nikaulizwa kwa habari ya serikali, nikasema kusimamia sheria.

    Niliposema kazi ya Bunge ni kutunga sheria, sikuwa na maana kwamba hiyo ndiyo kazi pekee ya Bunge. Nikasema kazi nyingine ni kuisimamia serikali.

    Waheshimiwa majaji, kulikuwa na ushahidi wa mashahidi wa serikali ambao hawakuja kutoa ushahidi juu ya namna nilivyokamatwa, na nikasema uhalali wa kukamatwa kwangu ni suala tofauti. Kwa sababu, waheshimiwa majaji, sheria zimeweka utaratibu wa namna ya kukamata. Kama sheria ilifuatwa au la ni suala linalobishaniwa na lilihitaji kujibiwa na upande wa mashtaka.

    Soma Zaidi Hapa:

  8. Lissu: Waheshimiwa majaji naomba kuhojiwa tena

    Wakili wa Serikali (Katuga): Tunaombi waheshimiwa Majaji, upande wa Jamhuri tunafahamu kuhojiwa tena ni njia moja wapo ya shahidi kutoa ushahidi na ipo kisheria na ila tunaomba kwa mujibu wa sheria shahidi ajikite kwenye yale maswali ya kuhojiwa tena na tunajua mshitakiwa ni wakili na anajiwakilisha mwenyewe ni jinsi gani atajihoji ili kufikia lengo la kutoa ufafanuzi wa majibu yake wakati wa kuhojiwa na upande wa pili, suala ambalo tunaomba Mahakama hii tuulize, shahidi ni mtu ambaye anajiwakilisha mwenyewe sasa kuhojiwa tena itafanyikaje?

    Wakili Katuga: Ajiulize maswali mwenyewe na ajijibu mwenyewe kuna hatari ya kuleta ushahidi mpya kabisa maana lengo la kuhojiwa tena ni kufafanua sasa kujiuliza mwenyewe atakuwa hakimu wa mwenendo wako mwenyewe, sasa zile kanuni zetu zinakinzana na hiki, kama angekuwa na wakili sawa ila wewe mwenyewe ujiulize na ufafanue ili kuepuka mkanganyiko Mahakama inaweza ikamuuliza kwa vile vipande ambavyo inaona vinahitaji ufafanuzi

    Jaji: Maombi yako ni nini?

    Katuga: Tunaomba Mahakama imuelekeze shahidi atoe maelezo kama itahitajika kufanya hivyo kwenye majibu yake yenye maana zaidi ya moja na sio kufungua sababu ya kutoa uwanda wa kutoka nje ya yale ambayo yanayohitaji ufafanuzi. Ni hayo tu waheshimiwa majaji

    Lissu: Waheshimiwa majaji kabla sijajibu naomba wakili mkuu wa serikali mkuu aimbie mahakama kama ameleta pingamizi ili muitolee uamuzi na kama ni ushauri tu naomba yawekeni pembeni ili nifanye kazi ya kuhojiwa tena, kwa hiyo naomba majibu hili ni pingamizi au ni nini?

    Katuga: Waheshimiwa majaji tumeiomba Mahakama irejeee kifungu na itoe mwongozo hakuna sehemu tumesema tunapinga, tumeomba mwongozo.

    Lissu: Kwa kuwa ni mwongozo naomba nijibu hayo maombi ya mwongozo, kuhojiwa tena ni haki ya shahidi aliyekuwa aliyehojiwa na upande wa pili, ndio maana kifungu alichokitaja cha 156 moja shahidi atakuwa wakwanza kutoa ushahidi na kama upande wa pili utamhoji na shahidi huyo akitaka kuhojiwa tena ni haki yake na kama ni haki alipaswa kunyamaza kimya.

    Lissu: Wakili wa serikali mkuu anasema atajiongozaje sababu hana wakili, the fact kwamba shahidi ndiye mshitakiwa na anajiwakilisha mwenyewe (ukweli kwamba shahidi ndiye mshitakiwa na anajiwakilisha mwenyewe) kitakachofanyika ni kurejea maswali yaliyoulizwa na majibu yake na kufafanua kwa hiyo hakuna chochote cha kutolea mwongozo sheria iko wapi, hii inaweza kuwa ni fursa ya kuingiza mambo mapya?

    Lissu; Utaratibu uko wazi kama kutakuwa na mambo mapya watafanya pingamizi kwa hiyo hawapaswi kuwa na hofu ya bure sasa waheshimiwa majaji hamna mwongozo wa kutoa.

    Lissu: Baada ya kusema hayo naomba niendelee.

    Jaji: Sasa hayo uliyosema si ndo muongozo wenyewe

    Lissu: Waheshimiwa majaji kama mtatoa mwongozo kwenye jambo dogo hivi tutafika tumechoka sana ila kama anahitaji kuambiwa awe macho waheshimiwa majaji.

  9. Upande wa Mashtaka wamaliza kumdodosa Lissu

    Jaji Ndunguru: Shahidi unakumbushwa kiapo chako kinaendelea

    Lissu: Sawa sawa

    Wakili Nzengeli (Upande wa serikali): Shahidi unakumbuka jana tulipoishia naomba nikuulize swali moja la mwisho tuachane na wewe

    Lissu: Asante mmening'ang'ania sana

    Wakili wa Serikali- Nzengeli: Ni kweli au si kweli nia ya kutenda kosa inathibitishwa na matendo husika

    Lissu: Sio kweli

    Wakili Nzengeli: Waheshimiwa tulikuwa na hilo tu kwa shahidi huyu tunaomba kusema tumemaliza kwa shahidi huyu

    Upande wa Jamhuri umemaliza kumuuliza maswali Shahidi wa Kwanza wa utetezi, ambaye pia ni mshitakiwa katika kesi hiyo.

    Baada ya kukamilika kwa dodoso hilo, Tundu Lissu anatarajiwa kupewa nafasi ya kufanya majumuisho ya utetezi wake.

    Baada ya majumuisho hayo, mahakama itaendelea na hatua inayofuata ya kusikiliza ushahidi wa shahidi mwingine.

  10. Katika Picha: Matukio ya kabla ya kuanza kwa kesi ya Tundu Lisuu

  11. Kilichojiri jana Mahakamani

    Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, iliendelea jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, huku upande wa serikali ukiendelea kumuhoji Lissu kuhusu ushahidi alioutoa katika utetezi wake.

    Mawakili wa serikali walimhoji Lissu kuhusu kampeni yake ya “No Reforms, No Election”, wakitaka kujua kama mkutano alioufanya ulihitaji taarifa kwa polisi na kama ulikuwa unahusiana na uchaguzi.

    Lissu alisisitiza kuwa huo ulikuwa mkutano wa ndani na kwamba mikutano ya aina hiyo haihitaji kibali.

    Sehemu nyingine ya maswali ilijikita katika kauli za Lissu kuhusu mahakama.

    Wakili wa serikali Job Mtemba alimuuliza kama kauli kwamba majaji ni CCM na kwamba “mahakamani hapaendeki” ilikuwa na lengo la kupandikiza chuki dhidi ya mfumo wa utoaji haki.

    Lissu alikataa kauli hiyo na akasema alikuwa akizungumzia masuala ya uchaguzi.

    Lissu pia alikiri mbele ya mahakama kwamba uanaharakati na uanasiasa vina mipaka ya kisheria, na kwamba hakuna kinga inayomruhusu mwanaharakati au mwanasiasa kuvunja sheria.

    Hata hivyo, alisisitiza kuwa wananchi wana haki ya kupinga uchaguzi ambao wanaona si huru wala wa haki.

    Maswali mengine yalihusu video inayodaiwa kuwa na maneno yaliyosababisha kufunguliwa kwa kesi hiyo.

    Lissu aliendelea kusisitiza kuwa video hiyo ilipaswa kuwasilishwa mahakamani, akisema mashahidi waliodai kuiona na kuisikia hawawezi kuthibitisha kikamilifu yaliyomo bila kuwepo kwa video yenyewe.

    Katika sehemu nyingine, Lissu alihoji uaminifu wa baadhi ya mashahidi wa polisi na akaeleza kuwa hakuridhishwa na namna alivyokamatwa.

    Alisema baadhi ya malalamiko yake kuhusu kukamatwa na madai ya kushambuliwa hayakushughulikiwa na polisi, huku upande wa serikali ukimhoji kwa nini hakuchukua hatua nyingine za kisheria.

    Maswali ya upande wa serikali yaliendelea hadi mahakama ilipoahirisha mwenendo wa kesi hiyo.

    Leo kesi inatarajiwa kuendelea, Lissu akiendelea kujibu maswali ya dodoso kutoka kwa upande wa Jamhuri.

  12. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya kesi ya uhaini ya Tundu Lissu, tarehe 28/08/2026.

  13. Nzengeli ahoji uhalali wa kampeni ya ‘No Reforms, No Election’

    Nzengeli: Ni kweli kwamba wakati unafanya huo mkutano wa kuzuia uchaguzi hukuwa na kibali?

    Lissu: Mikutano ya ndani haihitaji kibali, inahitaji taarifa tu.

    Nzengeli: Hapo hukupi PGO?

    Lissu: Ndiyo.

    Nzengeli: Soma kifungu cha 40(3).

    Lissu: 40(3), aya gani?

    Nzengeli: Wakati natafuta, soma Sheria ya Vyama vya Siasa.

    Lissu: Nisaidie kusoma ili tusipoteze muda.

    Nzengeli: Soma kifungu cha 40(2), aya ya sita.

    Lissu: (Anasoma.)

    Nzengeli: Wewe umekielewaje?

    Lissu: Nilichoelewa ni kwamba wakati wa mikutano ya kampeni, wanasiasa watatoa taarifa kwa polisi.

    Nzengeli: Ni kweli au si kweli mkutano huo ulikuwa unazungumzia mambo ya uchaguzi?

    Lissu: Haukuwa mkutano wa kampeni, na uchaguzi ulikuwa bado miezi sita mbele.

    Nzengeli: Waheshimiwa majaji, ninaomba nimpe Sheria ya Vyama vya Siasa, kifungu cha 23.

    Lissu: Nisomee.

    Nzengeli: (Anasoma.)

    Lissu: Ahsante, uliza swali.

    Nzengeli: Je, kwa kifungu hiki ulipaswa kupeleka taarifa polisi?

    Lissu: Hapana, si kweli, kwa sababu ulikuwa mkutano wa wazi na ulikuwa mkutano wa ndani.

    Nzengeli: Shahidi, elewa swali.

    Lissu: Mikutano ya ndani, dada yangu, haihitaji notification.

    Lissu: Next.

    Nzengeli: Ni kweli au si kweli huo mkutano unaouita wa ndani ulikuwa na waandishi wa habari?

    Lissu: Ni kweli.

    Nzengeli: Ambao ulikuwa mubashara na kila mtu aliuona?

    Lissu: Ndiyo, ni mkutano wa ndani.

    Nzengeli: Una kifungu chochote kinachokupa ruhusa ya kufanya mkutano wa ndani?

    Lissu: Kifungu hicho hicho, kwa sababu hakuna mkutano unaohitaji ruhusa bali taarifa tu. Next.

    Nzengeli: Wewe usinipangie.

    Nzengeli: Je, maneno yaliyoko kwenye hati yako ya mashtaka unakiri uliyaongea?

    Lissu: Nimesema sijatangaza maneno ya uhaini mbele ya waandishi wa habari.

    Nzengeli: Uliyaongea au hukuyazungumza? Naomba uwaangalie majaji.

    Lissu: Nimeshitakiwa kwa kuchapisha maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini kwa zaidi ya saa tatu.

    Nzengeli: Uliyaongea au hukuyazungumza?

    Lissu: Nimeongea kwa zaidi ya saa tatu.

    Nzengeli: Je, ni kweli video ni kifaa tu kinachotumika kuchapisha?

    Lissu: Hiyo inahitaji wataalamu.

    Nzengeli: Kati yako na mahakama, nani anaweza kusema nani ni mhalifu?

    Lissu: Mahakama ndiyo inaweza kusema mtu huyu ni mhalifu.

    Nzengeli: Na ni kweli kwamba hujaleta namba za kesi za hao mashahidi wote ambao unasema ni wahalifu?

    Lissu: Mapolisi si walifuta?

    Nzengeli: Tuhuma ni shtaka au si shtaka?

    Lissu: Tuhuma si shtaka.

    Nzengeli: Shahidi, nimekusikia ukilalamika kuhusu mambo ya kukamatwa. Uliyapeleka hayo malalamiko mahakamani?

    Lissu: Niliyapeleka na hakimu wa mahakama niliyemkabidhi alikataa. Ulitaka nifanyaje wakati niko gerezani?

    Nzengeli: Unakubali kwamba sheria zote zilizotungwa na Bunge zinasimamiwa na Serikali?

    Lissu: Sheria ya uchaguzi inasimamiwa na Tume ya Uchaguzi, si Serikali.

    Nzengeli: Kwa hiyo sheria ya uchaguzi ni sheria kama sheria nyingine?

    Lissu: Ni sheria.

    Nzengeli: Ni kweli kwamba kuna tofauti kati ya kupinga uchaguzi na kuzuia uchaguzi?

    Lissu: Waheshimiwa majaji, sisi tulitaka kupinga uchaguzi mpaka mabadiliko yafanyike. Shughuli zote za uchaguzi, majimbo yasitangazwe, wagombea wasitangazwe, kwa ujumla kila kitu kisimame.

    Lissu: Utaratibu wetu wa saa kumi na moja umekuwa suspended.

    Jaji: Ngoja tuulize, tulikuwa tunajua anamalizia.

    Nzengeli: Kwa maelezo ya mshtakiwa, ni kweli amechoka na kibinadamu. Tunaomba tuahirishe.

    Lissu: Kesho nayo ni siku.

    Jaji: Tunaahirisha shauri mpaka kesho saa tatu asubuhi.

  14. Job ambana Lissu: “Je, ulipandikiza chuki dhidi ya mahakama?”

    Job: Kwa mujibu wa ushahidi ulioutoa mbele ya mahakama hii, ulisema majaji ni wa CCM na kwamba mahakamani hapaendeki. Je, ni sahihi kwamba kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya mfumo wa utoaji haki ni kosa kwa mujibu wa sheria zetu?

    Lissu: Kupandikiza chuki ni kufanya nini? Kupandikiza chuki ni kitu gani?

    Job: Hebu soma kifungu cha 52(1).

    Lissu: (Anasoma.)

    Job: Je, utakubaliana na mimi kwamba kwa maneno yako uliyoyatoa, ukisema majaji ni wa CCM na kwamba huko mahakamani hapaendeki, ulikuwa unapandikiza chuki?

    Lissu: Waheshimiwa majaji, sikubaliani na wakili.

    Job: Je, ni sahihi kwamba Mahakama Kuu ilishawahi kutoa amri ya ulinzi wa mashahidi?

    Lissu: Ndiyo.

    Job: Na swali lingine, je, ni sahihi kwamba shauri lililoamuru utolewaji wa ulinzi wa mashahidi ni tofauti na shauri hili?

    Lissu: Ni sahihi.

    Job: Na ni sahihi kwamba amri hiyo haijawahi kuondolewa na mahakama?

    Lissu: Ni sahihi.

    Job: Kama hukuridhishwa na amri hiyo, si ulikuwa na nafasi ya kuipinga, lakini hukuchukua hatua yoyote?

    Lissu: Hapana, sikuchukua hatua kwa sababu niko gerezani. Nitapigana vita ngapi?

    Job: Hao mashahidi unawakumbuka?

    Lissu: Niwakumbukeje wakati siwajui? Ninazikumbuka hizi herufi tu.

    Job: Ukiwa kama mwanasheria...

    Lissu: Mimi ni shahidi. Uliza swali kwa shahidi.

    Job: Utakubaliana na mimi kwamba uamuzi wa ulinzi wa mashahidi hauwezi kupingwa kupitia shauri hili?

    Lissu: Sikubaliani na wewe.

    Job: Ulieleza mahakama hii kwamba tarehe 12 Agosti 2024 ulipata pigo. Kuna kitu chochote uliwasilisha hapa mahakamani kama kielelezo?

    Lissu: Nilieleza kwa mdomo.

    Job: Ulieleza mahakama tarehe 23 Septemba 2024 kwamba ulivamiwa nyumbani kwako na Jeshi la Polisi. Je, ni sahihi kwamba hakuna ushahidi mwingine ulioutoa mahali pengine?

    Lissu: Nimeieleza mahakama hii hayo, na hakuna sehemu nyingine nilikotoa ushahidi huo.

    Job: Ulieleza mahakama hii kwamba PW1 George Bagemi alitoa maelezo kuhusu wewe kufunguliwa jalada.

    Lissu: Ndivyo yeye mwenyewe alivyosema.

    Job: Je, ni sahihi kwamba PW1 alitoa maelezo kuhusu kufunguliwa majalada mawili ya uchunguzi yenye namba zifuatazo... Utakubaliana na mimi kwamba wewe, ukiwa shahidi, hujui tofauti ya majalada hayo mawili?

    Lissu: Sijui sababu. Haiko kabisa kwenye notisi zangu. Nitajuaje wakati sikuiandika?

    Job: Katika kutokujua huko sasa, uliieleza mahakama hapa kwamba PW1, baada ya kuonyeshwa video na PW2, alipoamuru kufunguliwa kwa jalada la uchunguzi, hakukosea?

    Lissu: Sababu alipaswa amweleze DPP acoordinate uchunguzi wa masuala haya, na hakumwambia.

    Job: Kifungu gani?

    Lissu: Sina hapa, ila utaratibu uko hivyo. DPP ndiye msimamizi wa upelelezi wa masuala haya, na hayo majalada mengine unayoniambia siyafahamu kabisa.

    Job: Wakati wa kujitetea uliambia mahakama kufunguliwa kwa jalada hilo ilikuwa kinyume cha sheria, kwani kufunguliwa kwa jalada hilo kulikufanya uwe na hatia.

    Lissu: Walikuwa na majibu tayari, ndiyo maana walikuwa wanasema kosa la kwanza.

    Job: Hebu waambie majaji, ni chombo kipi chenye mamlaka ya kuamua nani ana hatia na nani hana hatia?

    Lissu: Ni mahakama.

    Job: Kwa hiyo utakubaliana na mimi kwamba jalada hili ambalo PW1 alielekeza lifunguliwe kwa ajili ya uchunguzi, ilikuwa si makosa kwa maneno aliyoyasema?

    Lissu: Ndiyo, sababu tayari walishaniamua nina makosa.

    Job: Ni wakati gani mshtakiwa anakutwa na hatia?

    Lissu: Ni baada ya mahakama kufanya maamuzi.

    Job: Je, mahakama hii tayari imeshaamua?

    Lissu: Hapana.

    Job: Waheshimiwa majaji, ninaomba kuishia hapo.

  15. Lissu: Watu wafuate sheria, lakini si kila mgogoro hukimbiliwa mahakamani

    Job: Wakati unatoa utetezi wako, ulieleza mahakama hii kwamba huwezi kuwa Rais wa TLS kama wewe ni mtu wa hovyo hovyo. Na wakati unashitakiwa tarehe 25, ulikuwa Rais wa TLS?

    Lissu: Hapana.

    Job: Kwa hiyo, baada ya kutoka kuwa Rais wa TLS unaweza kuwa mtu wa hovyo?

    Lissu: Mimi si mtu wa hovyo, hata kidogo.

    Job: Baada ya kukutwa una kesi ya kujibu, umekaribia kuwa mtu wa hovyo?

    Lissu: Mimi si mtu wa hovyo, hata kidogo.

    Job: Umewahi kuandika maelezo polisi kuhusu kushambuliwa kwako?

    Lissu: Hapana. Wamekataa, licha ya kushambuliwa. Wamekataa tangu nilipokuwa Nairobi, na ulinzi nikaondolewa.

    Job: Wewe si ulijinasibu kuwa mwanasheria?

    Lissu: Una shaka na hilo?

    Job: Mimi nauliza maswali kwa mujibu wa sheria. Waheshimiwa majaji, naomba mshitakiwa atusomee kifungu cha 1 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

    Lissu: (Anasoma.).

    Job: Kwa mujibu wa hicho kifungu, wewe unakielewaje?

    Lissu: Kina maana kwamba taarifa ya makosa ya jinai inaweza kutolewa kwa afisa wa polisi, kwa maneno au kwa maandishi, kuhusu kosa au taarifa za kosa.

    Job: Utakubaliana na mimi kwamba jinai haifi?

    Lissu: Niliporudi, nilikwenda kwa RPC Dodoma nikamwambia nimekuja nichukueni maelezo. Walikataa. Nikawaambia wanipatie gari yangu.

    Job: Umeleta chochote kama ushahidi kuhusu wewe kushambuliwa?

    Lissu: Nimeieleza mahakama.

    Job: Umesema wewe ulikuwa mwanaharakati kwa muda. Je, utakubaliana na mimi kwamba unapopata taarifa za vitisho au uvunjifu wa sheria, unatakiwa kutoa taarifa kwa polisi?

    Lissu: Huwezi kutoa taarifa polisi kama vitisho vyenyewe vinatoka polisi. Ramadhani Kingai na hawa polisi wanaotoa ushahidi, hawa lao ni moja.

    Job: Utakubaliana na mimi kwamba, kwa mujibu wa Katiba, mahakama inaongozwa kwa kufuata misingi ya haki?

    Lissu: Ndivyo Katiba inavyosema.

    Job: Na utakubaliana na mimi kwamba wananchi wa Tanzania, na watu wanaoishi hapa, inapotokea mgogoro sehemu yao ya kukimbilia ni mahakamani?

    Lissu: Inategemeana na mgogoro. Kama ni wa kisheria, wanakimbilia mahakamani; kama ni wa kidini, wataenda makanisani au misikitini; kama ni wa kisiasa, wanamaliza kisiasa.

    Job: Utakubaliana na mimi kwamba si sahihi kusema mahakama haifanyi haki kwa mujibu wa Katiba?

    Lissu: Sikubaliani na wewe. Tume ya Warioba ilisema majaji hawatendi haki.

    Job: Hiyo taarifa ya Warioba umeileta hapa?

    Lissu: Ripoti ilieleza wazi kwamba baadhi ya majaji hawatendi haki na kwamba kuna rushwa mahakamani.

    Job: Wewe, kwa namna unavyoamini, watu wasifuate mfumo wa kimahakama?

    Lissu: Hapana. Watu wafuate sheria.

  16. Lissu: Uanaharakati na uanasiasa havitoi kinga ya kuvunja sheria

    Job: Hebu waambie majaji, hakuna mahali sheria zetu zinaruhusu watu kujichukulia sheria mkononi, kuchoma mali za watu au kuharibu uchaguzi.

    Lissu: Hakuna sheria inayoruhusu watu au mtu kujichukulia sheria mkononi, ila uchaguzi usio huru wala wa haki ni haki ya wananchi kuuzuia.

    Job: Hivi ukiwa mwanaharakati una kinga ya kutofuata sheria?

    Lissu: Hakuna kinga ya namna hiyo.

    Job: Vivyo hivyo ukiwa mwanasiasa?

    Lissu: Hakuna kinga ya mtu kutofuata sheria.

    Job: Wakati unajitetea, ulieleza mahakama hii kwamba kesi hii ni ya kisiasa. Wewe umeshitakiwa kama Tundu Lissu au kama mwanasiasa?

    Lissu: Nimeshitakiwa kama Tundu Lissu. Nisingekuwa mwanasiasa, nisingekuwa hapa. Nisingekuwa Mwenyekiti wa Chadema, nisingekuwa hapa.

    Job: Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, kuna sehemu umeshitakiwa kama mwanasiasa?

    Lissu: Hati haisemi hivyo, ila mashahidi wote wanasema mwenyekiti wa Chadema, mwenyekiti wa Chadema, mwanasiasa. Maelezo yote yanasema hivyo.

    Job: Utakubaliana na mimi kwamba katika ushahidi wako huu ulioutoa mbele ya mahakama hapa, hujaieleza mahakama ulishitakiwa kwa kesi gani na namba gani?

    Lissu: Hapana, sikubaliani na hilo. Nimesema kesi namba, ila ndiyo sijaitaja..

    Job: Ni kweli au si kweli ulitaja namba? Hukuitaja?

    Lissu: Ni kweli, namba sikuitaja. Ukitaka nikukumbushe, nitakukumbusha.

    Job: Utanikumbusha baadaye.

  17. Lissu akiri uanaharakati una mipaka ya kisheria mahakamani

    Job: Je, ni kweli au si kweli kwamba wewe ni mwanaharakati, na ulianza lini harakati zako?

    Lissu: Nimekuwa mwanaharakati siku nyingi, tangu nilipokuwa shule ya sekondari, baadaye jeshini na kwingineko.

    Job: Hebu waeleze majaji, uanaharakati ni nini?

    Lissu: Ni mtu anayefanya mambo au jambo fulani kupigania kitu fulani.

    Job: Ulijitambulisha pia kuwa wewe ni mwanasheria. Huu uanaharakati uliokuwa ukifanya unatambulika kwa mujibu wa sheria za nchi yetu?

    Lissu: Ndiyo, unatambulika.

    Job: Hebu wasaidie majaji. Ni kifungu gani na sheria gani mahsusi inayoutambua?

    Lissu: Katiba yetu imetoa uwanda mpana kwa wananchi kupigania mambo ambayo tunaona yanastahili kupiganiwa.

    Job: Tunaomba shahidi atuonyeshe na atusomee ibara hiyo.

    Lissu: Nimesema...

    Job: Nimesema tusomee kifungu hicho kinachoruhusu kufanya harakati.

    Lissu: Katiba haiko hivyo, ila inatupa uhuru wa kufanya harakati.

    Job: Harakati unazozifanya zina mipaka ya kisheria?

    Lissu: Ndiyo, zina mipaka ya kisheria.

    Job: Je, unakubali kwamba unapotafuta haki za upande mmoja, hutakiwi kubughudhi haki za upande mwingine?

    Lissu: Sahihi, hilo ninafahamu.

    Job: Sasa hebu waambie waheshimiwa. Kama nimekusikia vizuri, wakati unaongozwa ulikubali kwamba yale maneno yaliyomo kwenye hati ni sahihi?

    Lissu: Ni sahihi.

    Job: Sasa utakubaliana na mimi kwamba waliyosikia yale maneno waliyatafsiri kadiri yalivyo?

    Lissu: Sina hakika.

    Soma Zaidi:

  18. Katuga ahoji msimamo wa Lissu kuhusu ushahidi wa polisi

    Katuga: Waheshimiwa majaji, tunaendelea na ushahidi wa PW16, ushahidi wa Amini Mahamba. Sasa shahidi, hebu iambie mahakama kama ni ushahidi wako kwamba wapelelezi hawajakupa nafasi au hawajakupa maana ya maneno yaliyoandikwa kwenye hati ya mashtaka.

    Lissu: Huo ndio ushahidi wangu.

    Katuga: Kama unakumbuka, wakati shahidi PW1 alisema ulipofikishwa kwake, anasema alikupa nafasi ya kukuhoji ili umwelezee kuhusu maneno yako.

    Lissu: Wala hakuniuliza maana ya hayo maneno. Si kweli. Aliniambia anataka kuchukua maelezo yangu tu.

    Katuga: Na wewe ulijibu nini?

    Lissu: Nilimjibu kwamba kwa kuwa mmeshanikamata na mmeshanishtaki, tutakutana mahakamani.

    Katuga: Waambie hawa majaji, hawa wapelelezi walikupa nafasi ya kukuhoji au la.

    Lissu: Hawakunipa nafasi kwa sababu tayari nilikuwa nimeshashtakiwa.

    Katuga: Kwa hiyo ni uelewa wako wa kisheria kwamba mtuhumiwa hakamatwi?

    Lissu: Mimi nilikamatwa, nikawaambia tutakutana mahakamani.

    Katuga: Ulizuiwa na nini kutoa maana ya maelezo yako?

    Lissu: Walitaka maelezo yangu ya nini wakati walikuwa wameshanikamata?

    Katuga: Je, pale ulipokuwa, ulishindwa na nini kumpa tafsiri ya maneno hayo na Bwana Bagemi alikupa nafasi ya kutoa maelezo?

    Lissu: Ningesema nini wakati nilikuwa nimeshashtakiwa? Nimeshtakiwa kwa kosa la kifo na watu walionitesa kwa miaka 24. Ulitaka nijieleze tu?

    Katuga: Ulisema maelezo D1 hadi D16 ni vielelezo vya utetezi wako, na nakumbuka katika utetezi wako ulirejea Kielelezo D15. Waambie majaji, ni kielelezo ambacho ulikiamini na kukirejea katika utetezi wako?

    Lissu: Maneno yapi? Sikumbuki.

    Katuga: Baada ya kuunda timu, mimi na timu nzima tulitazama na kusikiliza video hiyo ambayo bado ilikuwa mtandaoni, na kama nilivyotafsiriwa nikabaini kosa la kwanza ni uhaini na kuchapisha mtandaoni. Ukaambia mahakama kuwa PW16 tayari alikuwa amekuhukumu kwa uhaini.

    Lissu: Niliyarejea nikiunganisha na ushahidi wa PW1 na PW17.

    Katuga: Kwa hiyo, kwa mujibu wa maneno ya shahidi huyu, aliona uhaini kwenye kielelezo chake au hakuona uhaini?

    Lissu: Sikusema ninawaamini. Mimi siwaamini polisi hawa.

    Katuga: Umechukua maelezo ya mashahidi wawili tofauti kwa sababu uliwaamini na ukawaambia majaji kwamba maelezo yao yanatofautiana?

    Lissu: Mimi niwaamini polisi? Hapana. Mimi niliyatoa kwa sababu yana tofauti; mmoja ameona uhaini, mwingine hajaona.

    Katuga: Unajua nimekuuliza swali la kwanza. Je, hiki ni kielelezo chako cha utetezi kwa sababu unakiamini?

    Lissu: Niliomba kiwe kielelezo changu kwa sababu kinatofautiana na maelezo mengine kwa kuwa kinaonyesha mgongano wa maelezo (contradiction).

    Katuga: Kwa maelezo yako mwenyewe sasa, shahidi, uko timamu?

    Lissu: Wewe unanionaje?

    Katuga: Wewe iambie mahakama.

    Lissu: Move on.

    Katuga: Maelezo haya unayaamini au huyaamini?

    Lissu: Niyaamini kwa jambo gani?

    Katuga: Waambie majaji kama uliwaomba kwamba maelezo yaliyomo kwenye vielelezo hivi vyote yaweze kutumika.

    Lissu: Nimejibu hilo swali. Move on.

    Katuga: Waambie majaji vielelezo D1 mpaka D15 vitumike kuonyesha nini?

    Lissu: Vitumike kuonyesha omissions na contradictions.

    Katuga: Kwa kuwa umeiambia mahakama vielelezo hivi vitumike, je, kuna sehemu umesema vielelezo vitumike hapa na visitumike pale?

    Lissu: Waheshimiwa majaji, hilo nitalifanya wakati wa kuwasilisha hoja zangu za mwisho.

    Katuga: Swali ni, uliwaambia au hukuwaambia majaji?

    Lissu: Nitawaambia wakati wa kuwasilisha hoja zangu za mwisho.

    Katuga: Waheshimiwa majaji, naomba swali hilo lirudiwe na lijibiwe.

    Lissu: Sikuwaambia.

    Katuga: Je, ni haki ya mahakama kutumia vielelezo vyako?

    Lissu: Sasa hilo ni uamuzi wa mahakama kuona namna itakavyotumia vielelezo hivyo.

    Katuga: Waheshimiwa majaji, ikiwapendeza, naomba niishie hapa na nimkaribishe wakili mwenzangu wa serikali.

    Soma Zaidi:

  19. Lissu ang’ang’ania video iletwe mahakamani, Katuga apinga hoja

    Katuga: Kwenye ile video unachokiona ni nini, maneno au video?

    Lissu: Sijaiona, si hamjaileta?

    Katuga: Katika sheria ya ushahidi, mtu akikutolea ushahidi wa maneno, anatoa ushahidi wa kusikia?

    Lissu: Ndiyo, wa kusikia kama ni wa maneno tu, ila kama ni video ni wa kuona na kusikia.

    Katuga: Unatuhumiwa kufanya nini?

    Lissu: Kutoa maneno na kuyachapisha.

    Katuga: Umewaambia majaji kwamba upande wa Jamhuri haujathibitisha shtaka hilo kwa sababu video hawajaileta. Waambie mashahidi wa Jamhuri walisemaje.

    Lissu: Walisema wameona video na kusikia maneno.

    Katuga: Kwa hiyo waliona na kusikia?

    Lissu: Huwezi kutenganisha video na sauti, kwa hiyo lazima iwe kuona na kusikia.

    Katuga: Unajua kwamba kila shahidi ana haki ya kuaminiwa?

    Lissu: Ndiyo, ninajua, na anastahili kuaminiwa kama kuna misingi ya kumuamini.

    Katuga: Sasa iambie mahakama hii, katika mashahidi wa Jamhuri wale waliosema wameona video, ni kifungu kipi kinaelekeza kwamba lazima walete video hiyo mahakamani licha ya kwamba wameiona?

    Lissu: Lazima wailete mahakamani ili waaminike.

    Katuga: Iambie mahakama, ni kweli kwamba mtu anayepandisha video mtandaoni anaweza kuja kuifuta?

    Lissu: Ndiyo.

    Katuga: Unaelewa kwamba kitu fulani kinaweza kupotea ghafla. Kama mtu atakuwa amefanya kosa kwa kupandisha video yenye tatizo kisha akaifuta, iambie mahakama kwamba mtu huyo hawezi kuja mahakamani kutoa ushahidi? Kwa hiyo kilicholetwa hapa ni nini?

    Lissu: Maneno na video havitengani. Video yenyewe haijaletwa.

    Katuga: Tuiombe mahakama ikuchukulie wewe ni muongo?

    Lissu: Jaji alisema hakumbuki, tuendelee.

    Katuga: Unataka shahidi PW17, ambaye alisema alikusikia ukisema hayo maneno ya kukinukisha, ayalete hapa mahakamani?

    Lissu: Ndiyo, ayalete hapa.

    Katuga: Ni ushahidi wako kwamba mashahidi kutoka polisi waliandika maelezo yao wenyewe na kwa hiyo si wa kuaminika? Sasa mashahidi hawa wasiaminiwe kwa sababu wameandika maelezo wenyewe. Ni kifungu gani kinaipa mahakama mamlaka hayo?

    Lissu: Kifungu cha 11 kinaelekeza kwamba polisi ambao hawakufuata utaratibu hawaaminiki.

    Katuga: Wasomee majaji.

    Lissu: (Anasoma.)

    Katuga: Waambie majaji, kwa mujibu wa kifungu hicho, kimeeleza nini kuhusu polisi anayefanya upelelezi; anapaswa kuandika maelezo?

    Lissu: Kama afisa huyo ni shahidi, basi haandikiwi maelezo.

    Katuga: Afisa mdogo wa polisi anaweza kumwandikia afisa wa juu maelezo?

    Lissu: Ndiyo, anaweza.

    Katuga: Unajua kwamba maelezo ya shahidi yanaandikwa kwa mujibu wa sheria?

    Lissu: Sikumbuki.

    Katuga: Unajua kwamba tamko ni tamko la kiushahidi, na unajua kwamba shahidi lazima aonywe?

    Soma Zaidi Hapa:

  20. Lissu ajibu maswali kuhusu ushahidi wa video

    Katuga: Kama uliwaambia majaji hawa waendesha mashtaka hawajaleta video na kwamba, kwa kuwa mahakama haina video hiyo, wameshindwa kuthibitisha mashtaka yao, waambie majaji kama wakati unasema hayo ulikuwa unajua au umesoma mashtaka yanayokukabili.

    Lissu: Nilikuwa nimesoma mashtaka yanayonikabili na niliyaelewa kwa undani.

    Katuga: Kwa mujibu wa mashtaka, kuna sehemu unashtakiwa kwa kuchapisha video?

    Lissu: Nashtakiwa kwa kuchapisha maneno kwenye mtandao wa Jambo TV.

    Katuga: Je, nitakuwa sahihi nikisema video unasikia na kuona kama video hiyo ina maneno?

    Lissu: Video ni kuona na kusikia. Kwa mujibu wa sheria ya ushahidi, mtu akitoa ushahidi kuhusiana na maneno anakuwa ametoa ushahidi wa kusikia.

    Katuga: Kwa mujibu wa mashtaka, unatuhumiwa kuyachapisha na kutoa maneno kwenye mtandao wa YouTube wa Jambo TV. Uliiambia mahakama kuwa upande wa Jamhuri haujathibitisha mashtaka kwa sababu video hiyo hawajaileta?

    Lissu: Mashahidi wote wa Jamhuri walisema kuwa wameona na kusikia maneno.

    Katuga: Unafahamu kwamba kila shahidi ana haki ya kuaminiwa isipokuwa kama mahakama ina sababu za kutomuamini, na sababu hizo lazima zionyeshwe? Iambie mahakama hii, wale mashahidi waliosema wameona video, ni kifungu gani cha sheria kinachosema kuwa ili waaminiwe lazima walete video?

    Lissu: Si lazima sheria iseme hivyo, bali hiyo ni common sense.

    Katuga: Ni kweli kwamba mtu anayeipandisha video mtandaoni ana uwezo wa kuifuta?

    Lissu: Ana uwezo huo.

    Katuga: Je, mtu akiwa amefanya kosa kwa kuchapisha video mtandaoni halafu akaifuta, na mtu mwingine akaiona video hiyo kabla haijafutwa, ni ushahidi wako kwamba hawezi kuthibitisha alichoona?

    Lissu: Hawezi kuthibitisha.

    Katuga: Video na maneno, kilicholetwa hapa mahakamani ni nini?

    Lissu: Wameleta maneno tu, na hayo si maneno ya kwenye video, kwa sababu maneno ya video huwezi kuyatenganisha na video yenyewe.

    Katuga: Unakumbuka PW17 ndiye shahidi pekee aliyekuwa live eneo la tukio?

    Lissu: Ndiyo.

    Katuga: Unakumbuka shahidi PW17 alisema Lissu alisema atauzuia uchaguzi?

    Lissu: Sikumbuki.

    Katuga: Kwa kuwa shahidi alikuwa eneo hilo, alihitajika kuileta video hiyo?

    Lissu: Alipaswa kuileta video hiyo.

    Katuga: Anasema alikusikia ukisema unaenda kuzuia uchaguzi na kwamba utaenda kukinukisha. Je, unataka shahidi huyo alete video hapa mahakamani?

    Lissu: Ndiyo, lazima.

    Katuga: Ni ushahidi wako kwamba mashahidi kutoka Jeshi la Polisi hawaaminiki kwa sababu waliandika maelezo bila kufuata utaratibu?

    Lissu: Ni kweli hawaaminiki kwa sababu hawakufuata utaratibu.

    Katuga: Ni kweli kwamba mashahidi wote uliowataja walikuja hapa mahakamani kutoa ushahidi, na kwa kufanya hivyo mahakama imepata fursa ya kutathmini uaminifu (credibility) wao?

    Lissu: Hayo ni ya majaji.

    Katuga: Ni kifungu gani cha sheria kinachoipa mahakama mamlaka ya kutowaamini polisi waliokuja kutoa ushahidi?

    Lissu: Utaratibu wa kuandika maelezo upo chini ya Kifungu cha 11(4) cha CPA. Kifungu hicho hakijaeleza chochote kuhusu hilo.

    Katuga: Umesema maelezo haya yalitakiwa yaandikwe mbele ya afisa wa polisi na si mpelelezi.

    Lissu: Ndiyo.

    Unaweza kusoma;