Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Lissu: Nina chuki dhidi ya serikali sababu ya uonevu wake

Lissu anaamini kuwa ameonewa, amesema ana chuki dhidi ya serikali sababu ya uonevu wake.

Muhtasari

Moja kwa moja

Elizabeth Kazibure, Rashid Abdallah & Asha Juma

  1. Maswali ya dodoso kwa Lissu yakiendelea

    Katuga: Kama nimekusikia vyema umesema ulitoa hotuba kwa watia nia wa Chadema na pia ulitoa hotuba hii mbele ya waandishi wa habari waambie majaji kama katika ushahdi wako umewaambia waandishi wa habaari wasipeleke rekodi zile na yale mliyozungumza.

    Lissu: Hapana sikuwaambia.

    Katuga: kwa hiyo ulitaka habari yako iende kwa walaji?

    Lissu: Ndio nilitaka iwafikie wananchi.

    Katuga: Katika ushahidi wako ulisema kama ulitoa mipaka kwa watu wanaopaswa kusikia ile hotuba.

    Lissu: Hapana sikutoa mipaka

    Katuga: Wale watia nia ulikua nao pale ambao ndio ulikuwa umewakusudia?

    Lissu: Ndio walikuwepo

    Katuga: Waambie majaji kama unakumbuka mkutano ulikuwa mubashara.

    Lissu: Ndio ni kweli

    Katuga: Waambie majaji kama uliwapa waandishi wa habari hotuba yako kabla kuzungumza.

    Lissu: Hapana sikuwapa.

    Katuga: Hivyo walikuwa hawajui unakwenda kuzungumza nini?

    Lissu: Ni sahihi

    Katuga: Kwa kuwa walikuwa hawajui nitakuwa sahihi nikisema haya maneno PW17 na wenzake walikuwa hawajui kabla ya wewe kuyatamka.

    Lissu: Ndio walikuwa hawajui.

    Katuga: Unakumbuka mashahidi walisema ulikuwa umevaa kombat na tishrt nyeusi?

    Lissu: Ndio nakumbuka.

    Katuga:Kuna sehemu umekanusha vazi ulilokuwa umevaa.

    Lissu: Ningekanushaje vazi langu rasmi la chama?

    Katuga: Kwa kuwa unasema ilikuwa hivyo nitasema mashahidi wa jamuhuri walikutambua kwa usahihi baada ya kutazama ile video.

    Lissu: Ninasema mashahdi wa jamhuri wananitambua siku nyingi ni sahihi nilikua nimevaa hivyo.

    Katuga: Unajua Principle ya constructive possession na constrtuction

    Lissu: Hapana siijui.

    Katuga: Umeiambia mahakama unakumbuka PW 17 alisema alichapisha kupitia wewe?

    Lissu: Hapana alisema walichapisha wao kupitia Mimi. Waheshimiwa majaji naomba nikae hii mvua ya maswali inanielemea.

    Jaji: Kaa.

    Katuga: Unapotoa hotuba kila mtu si ana haki ya kuelewa na kutelekeza vile alivyoelewa?

    Lissu: Ndio ni kweli

    Katuga: Maneno ya kwamba tutazuia uchaguzi si kila mtu ana haki ya kuelewa alivyolewa?

    Lissu: Ndio Maneno kama Tutazuia uchaguzi si kila mtu ana haki ya kuzuia uchaguzi kwa kutumia njia yake mwenyewe

    Katuga: Unakumbuka PW3 alipotoa ushahidi na kusema walipanga kuzuia uchaguzi kwa kurusha mawe kuchoma moto baada ya kauli zako walipanga kurushia watu mawe wasiende kupiga kura iambie mahakama hii kwamba uchaguzi upo kwa mujibu wa sheria.

    Lissu: Ndio

    Katuga: Mojawapo ya kazi za serikali ni kusimamia sheria

    Lissu: Ndio

    Katuga: Je, kuzuia watu kwenda kupiga kura kwa kuwarushia mawe ni uvunjifu wa amani sio ubunjifu wa amani?

    Lissu: Ndio ni uvunjifu wa amani

    Katuga: Na Jeshi la polisi liko chini ya nani?

    Lissu: Jeshi la Polisi liko chini ya serikali

    Katuga Unapotishia kuvunja amani umemlenga nani?

    Lissu: Hapana unapovunja amani hujalenga polisi.

    Katuga: Utanijibu tu ujanja hauna.

    Lissu: Twende

    Katuga: Anapotishia kuvunja amani anakuwa amefanyaje?

    Lissu: Anakuwa analipa Jeshi la polisi kazi ya kumzuia asivunje amani.

    Katuga: Kama niko sahihi ulisema unataka kuhamasisha maandamano ya kidemokrasia, je, kwenye haya maneno kuna maneno utahamasisha uasi wa kidemokrasia?

    Lissu: Hapana

    Katuga : Je, video ililetwa mahakamani au haikuletwa wewe si mkweli?

    Lissu: Ililetwa ikakataliwa na mahakama.

    Katuga: Je, wewe ungependa kuiona na kuiomba mahakama hii tukufu iilete mahakamani?

    Lissu: Hapana hamuwezi mkaleta takataka nije niwasaidie mimi.

    Katuga: Demokrasia inatoa haki kwa wote waounga mkono na wasio unga mkono yule anapenda kupiga kura. Je, yale maneno kuzuia uchaguzi yanatokana na demokrasia gani?

    Lissu: Kama kuna jambo mnaona halipendezi mna haki ya kukipinga na kuliondoa kwa mujibu wa sheria.

    Katuga: Je, unajua kuzuia uchaguzi ni kosa?

    Lissu: Hapana sheria haijasema.

    Katuga: Je, bado unasisitiza katiba inasema ni haki ya kikatiba kumzuia mtu kupiga kupiga kura kwa kufanya fujo?

    Lissu: Katiba sio ibara moja.

    Katuga: Tafsiri ya adhabu inaposema shall be liable pale ambapo kifungu cha sheria kinatoa maneno shall be liable je, kuna descretion ya mahakama?

    Lissu: Hapana.

    Katuga: Uko aware na kesi ya Shengi Muhagama?

    Lissu: Niko Gerezani nitajuaje?

    Katuga: Si ulikua unatoa kesi hapa?

    Lissu: Wewe unaangalia mtandaoni hapo mimi naanngalia wapi?

    Katuga: Si una watafiti we mzee?

    Lissu: Waambie mmenishtaki kunyongwa kosa la bure.

    Katuga: Unaweza kuisaidia mahakama tofauti ya mkanganyo na hapa halipo.

    Lissu: Mkanganyiko ni kama jambo linalokuwa na maelezo mawili yanayotofautiana lakini omission ni jambo ambalo halipo lakini limechomekewa.

    Katuga: umewahi kufungua shauri kwa jina lako kupinga sheria ya uchaguzi?

    Lissu: Hapana, kwa chama changu Yes

    Katuga: Kama nilikusikia vyema umeleta mambo ya jaji chande sana ya 29/10

    Lissu: Ndio

    Katuga: Je ni kweli kwamba ripoti yake ilisema pia matukio haya yalipangwa kabla kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya mifumo ya uchaguzi, katiba ajira ……

    Lissu: Nisomeee unikumbushe.

    Katuga: Kwenye hotuba yako tuambie kama ulisema tukikinukisha watatufanya nini?

    Lissu: Hapana.

    Katuga: Sasa ulisema watanikamata watanifungulia kesi ya uhaini?

    Lissu: Hapana.

    Katuga: Unakumbuka kuwaambia majaji ni ma CCM?

    Lissu :Ndio.

    Katuga: Waheshimiwa majaji bado tuko nusu ila nikiangalia muda naona ni saa 11

    Jaji: Mshtakiwa unasemaje?

    Lissu: Waheshimiwa majaji kama ni saa 11 inatosha nimesimama ya kutosha kwa leo.

    Jaji: Kimsingi tunatamani kuanza saa tatu kamili ili tuwe tumetumia muda vyema. Tutakapowahi tutaanza.

    Tunahirisha mpaka kesho saa tatu asubuhi.

  2. Lissu: Nina chuki dhidi ya serikali sababu ya uonevu wake

    Katuga: Nimekusikia umesema vitu vingi sana kuhusiana na CV yako pamoja na matatizo yaliyokukuta wewe unayaita mapambano sasa hivyo vitu vyote iambie mahakama wewe ni mtu mwenye chuki dhidi ya serikali

    Lissu: Ndio nina chuki dhidi ya watu kuonewa

    Katuga: Unaamini umeonewa na una chuki na mahakama i note unachuki.

    Lissu: Ndio nina chuki dhidi ya serikali sababu ya uonevu wake.

    Katuga: Kama mwanasiasa nia ya chama cha siasa ni kushika Dola.

    Lissu: Ndio kushika dola ni moja wapo.

    Katuga: Iambie mahakama hii kama unafahamu mihimili mitatu ya dola.

    Lissu: Ndio ninaifahamu ni serikali, mahakama na bunge

    Katuga: Uko kwenye nafasi nzuri sana ya kunipa elimu, kwenye swali la kisheria hii mihimili mitatu kazi yake ni nini?

    Lissu: Bunge kazi yake ni kutunga sheria

    Katuga: Kazi ya mahakama ni nini?

    Lissu: Ni kutafsiri sheria na inatengua sheria na ikitengua maana yake bunge limetunga sheria ya hovyo.

    Katuga: Kazi ya serikali baada ya sheria kutungwa ni nini?

    Lissu: Kuzilinda sheria.

    Katuga: Mtu akitengeneza nia ya kutishia serikali tafsiri kama mwanasheria kuna takwa kisheria kwamba lazima hiyo serikali lazima iwe imetishika.

    Lissu: Hakuna hiyo provision lakini.

    Katuga: Hapana swali langu ushajibu.

    Lissu: Nataka kuisaidia mahakama, kwenye sheria bado inaeleza lazima kuwe na matokeo.

    Katuga: Leo tutakesha

    Lissu: Nimekaa mwaka na miezi mitano unaogopa kukesha?

    Katuga: Umesema baadhi ya mashidi ni mapolisi walioko kwenye jeshi linaloendeshwa na IGP wambura na DCI Kingai iambie mahakama ulikuepo au umesikia au ilikuwaje?

    Lissu: Ndio ni mapolisi wanaotumia jeshi linaloongozwa na wambura na Kingai ambao wamenipersecute kwa muda mrefu na nilisema hivyo sababu ya maandishi ya mashahidi hao.

    Katuga: Ni kweli umewataja watu hawa waje kukutetea mahakamani?

    Lissu: Ndio

    Katuga: Kwa hiyo ni mashahidi wema

    Lissu: Hapana sio wema nitakuja kuwauliza waeleze jinsi wanavyoelewa kesi hii

    Katuga: Lissu ulikamatwa au ulichukuliwa?

    Lissu: Nilikamatwa kama hujawahi kamatwa huwezi kuelewa

    Katuga: Unajuaje kama sijakamatwa

    Lissu: Nyie mnawekelea watu maneno mnakamatwa namna gani?

    Katuga: Kama nimekusikia vyema embu iambie mahakama dhumuni la kuwa na hoja za awali preliminary hearing.

    Lissu: Lengo lake ni kuchambua na kuweka kando vitu ambavyo vinabishaniwa.

    Katuga: Unajua yale mambo ambayo hayaihitaji kubishaniwa hayahitaji mashahidi na ulikubali hayana ubishani?

    Lissu: Ndio

    Katuga: Wakati unaeleza majaji mashahidi wawili walikuwa Mbinga wakati wa ukamataji ulitaka waje wafanye nini?

    Lissu: Ndio nilitaka waje waieleze mahakama kila kitu, nilikamatwa kweli lakini uhalali wa ukamataji hilo ni suala jingine.

  3. Lisu aendelea kujibu maswali ya dodoso

    Katuga: Kaka yetu wewe msomi sana historia ulisoma pia?

    Lissu: Ndio nimesoma historia

    Katuga: Kuna wakoloni waliingia mkataba ya kilaghai na baadhi ya viongozi ili waweze kutawala baadhi ya maeneo

    Lissu: Hapana ilikuwa mikataba ya kuwanufaisha viongozi wenyewe waaliingia mikataba na machifu, machifu ndio akina Samia wa sasa hivi.

    Katuga: Unataka tukae sana huko.

    Lissu: Twende kaka

    Katuga: Isaidie mahakama, kama unakumbuka awamu ya tano ilizuia makinikia kutoka na wewe ukatetea makinikia yatoke sababu wazungu watatudai mapesa mengi.

    Lissu: Hapana sikusema hivyo nilieleza hasara ya kufanya hivyo unataka nikueleze mashtaka ya Tanzania huko duniani?, huko usiende

    Katuga: Tuendeleee leo niko na wewe, unakumbuka wewe ulisema ulikuwa Rais wa TLS iambie mahakama wakati unashtakiwa ulikuwa Rais wa TLS?

    Lissu: Hapana

    Katuga: Kama nilikusikia vyema unasema wewe ni mwaminifu umeongoza vita vya kupigania haki za binadamu na rasilimali na ulipigana vipi hii vita?

    Lissu: Ndio nilieleza kazi nilizofanya kupigania rasilimali za nchi hii.

    Katuga: Kama nilikusikia vizuri ulisema wewe ni mtaalamu sana wa sheria za uchaguzi na wewe ni mtaalamu wa sheria.

    Lissu: Ndio

    Katuga: Tanzania kupinga sheria fulani inayokinzana na katiba utaratibu uko vipi?

    Lissu: Kuna njia nyingi unaweza kuleta petition, kuhamasisha wanachi kufanya maandamano kupinga sheria husika na moja wapo hii ya kuja mahakamani.

    Katuga: Kifungu cha nne

    Lissu: Ndio au kama unaanzia mahakama ya chini kifungu cha tisa

    Katuga: Iambie mahakama na hiyo ya kupinga sheria kwa maandamano iko kwa kifungu gani

    Lissu: Iko kwa kifungu cha 20:1 inayoruhusu watu kufanya mijumuiko kidemokrasia maandamano ya kidemokrasia yanaruhusiwa kikatiba na kisheria unatumia vyombo vya habari na yote haya ni njia za kubadilisha sheria.

    Katuga: Waheshimiwa majaji tunaomba atusomee

    Lissu anasoma, kila mtu ana haki ya kukutana na watu wangine kwa amani na kutoa maoni yake kwa uhuru na amani.

    Katuga: Hicho ulichoelewa

    Lissu: Ndio, ndio ushahidi wangu

    Katuga: Unamjua mtu anaitwa Francis Ndyanabo

    Lissu: Julius Francis Ishengoma Ndyanabo, wakili mwenzangu alifungua shauri kupinga sheria ya uchaguzi.

    Katuga: Alishinda, alishindwa?

    Lissu: Alishinda

    Katuga: Na Mtikila unamfahamu?

    Lissu: Kuhusu mgombea binafsi Mchungaji Christopher Mtikila alishinda hapa ndani na mahakama ya Afrika na serikali unayoitumikia imekataa kutekeleza uamuzi huo mpaka leo.

    Katuga: Umemtaja sana Rugemeleza Nshala iambie mahakama hii kama Nshala ni shahidi wako.

    Lissu: Hapana ni wakili mwenzangu yuko hapa na alikuwa mshitakiwa mwenzangu.

    Katuga: Kuna njia ngapi za kudhurisha nia

    Lissu: Publication, or oral

    Katuga: Iambie mahakama linapotumika neno or yanatumika kwa pamoja au vipi?

    Lissu: Hapana ila yanaweza kufana au yasifanane na kiswahili chake ni kitendo

  4. Upande wa jamhuri unamuuliza maswali mshtakiwa

    Baada ya mlo wa mchana, upande wa jamuhuri wako tayari kwa ajili ya maswali ya dodoso kwa mshtakiwa.

    Nassoro Katuga: Shahidi pole na ushahidi mrefu

    Lissu: Ahsante sana

    Katuga: Kama nimekusikia vyema ulisema utatuacha sisi ndugu zako tukuulize maswali.

    Lissu: Sahihi.

    Katuga: Waambie majaji hiki tunachokifanya ni kitu cha kisheria na hakina nasaba nyingine yeyote.

    Katuga: Uliiambia mahakama wewe ni wakili wa mahakama kuu na una ujuzi wa kisheria.

    Lissu: Ndio

    Katuga: Hebu waambie majaji Tanzania ilipata uhuru mwaka gani.

    Lissu: 9/12/1961

    Katuga: Kwa majibu hayo Tanzania ni nchi huru.

    Lissu: Ndio

    Katuga: Chombo cha mwisho cha kufanya maamuzi ya mwisho kwa mujibu wa kisheria ni ni kipi?

    Lissu: Mahakama

    Katuga: Mahakama haitakiwi kuingiliwa na mtu yeyote inapotoa maamuzi na pia mahakama hailazimishwi wala haipingwi na mtu au chombo chochote toka nje au ndani.

    Lissu: Sahihi haipangiwi walakulazimishwa.

    Katuga: Umetuambia wewe ni Mwenyekiti wa Chadema, Je katika utetezi wako umeimbia mahakama hii kuwa mwenyekiti wa Chadema ana kinga?

    Lissu; Hapana na sina kinga hiyo

    Katuga: Ndugu shahidi kama nilikupata vyema ulieleza sifa nyingi kukuhusu wala sizikatai iambie mahakama hizi tuzo ulizopewa ziko kwenye form gani kama maandishi au katika hali gani.

    Lissu: Ziko katika hali ya maandishi, na ile alama yenyewe

    Katuga: Ka object flani hivi.

    Lissu: Ndio

    Katuga: Embu iambie haya matuzo yote haya umeyaleta mahakamani

    Lissu: Hapana na sina sababu ya kuyaleta.

    Katuga: Twende pole pole tutakuwa na siku saba hapa.

    Lissu: Hakuna neno

    Katuga: Wewe umeleta nini hapa

    Lissu: Maneno

    Katuga: Sasa wewe uliposema mashahidi wa jamuhuri wameleta meneno ulimaanisha nini?

    Lissu: Siwajibiki kufanya hivyo mimi nimeleta maneno sababu sina kesi ya kuthibitisha

    Katuga: Sheria inasemaje?

    Lissu: Sheria inataka mtu alete ushahidi pamoja na vithibitisho

    Katuga: Unajua usilete ujuaji

    Lissu: Yes mimi mjuaji

    Katuga: Principles gani zinakutaka ulete maneno bila vithibitisho?

    Lissu: Mimi sina wajibu wa kuthibitisha lolote.

    Katuga: Unajua kifungu cha sheria kinasema yule anasema ana wajihi fulani anapaswa kuthibitisha.

    Lissu: Ndio ninathibitisha

    Katuga: Ulisema mahakama ni chombo huru wale uliosema wameelekeza uachiwe na unakubali mahakama ni chombo huru ndani ya nchi huru ya Tanzania?

    Lissu: Ndio, Kamati ya haki za binadamu ya Umpja wa Mataifa

    Katuga: Shahidi kuna mahali popote kwenye ushahdi wako kuna umekanusha maneno haya ya tunakwenda kukinukisha kweli kweli?

    Lissu: Nimesema hivi maneno hayo ukitaka kuyaelewa unabidi usikilize hotuba yote.

    Katuga: Mimi siwezi kukuuliza una akili timamu wewe ni kaka yangu

    Lissu: Niulize tu

    Katuga: Siwezi swali langu kuna mahali umekanusha maneno haya

    Lissu: Hapana

    Katuga: Kwa maana hiyo maneno haya huyakatai

    Lissu: Siyakatai wala hayana shida.

    Katuga: Nilitaka tu hicho

    Lissu: Nimesema mara kadhaa.

  5. Lissu: Mashahidi 17 wote maelezo yao hayalingani na yaliyoletwa mahakamani

    Waheshimiwa majaji mashahdi wote waliandika maelezo na maelezo ya mashahidi 16 ni vielelezo vya ushahidi wa utetezi wangu.

    Wote 17 wametoa ushahidi kwenye kizimba hiki ushahidi wa meneno na wote wametoa ushahidi hapa mbele ya mahakama ambao haulingani na maelezo yao yaliyoletwa mahakamani.

    Wote wameongeza mambo ambayo hayapo kwenye ushahidi wao wa maandishi.

    Wameongeza yaliyokuwa kwenye maelezo yao .Waheshimiwa majaji ni ushahdi wangu kwamba ushahidi wa meneno usiolingana na ushahidi wa maneno kwenye jambo hilohilo ni ushahidi usioaminika.

    Ni ushahidi wangu kwamba ushahidi wote wa mashahidi wa upande wa mashtaka hauaminiki.

    La mwisho waheshimiwa majaji kuhusiana na huo ushahdi usio aminika, ushahidi wa P1, P2, P3, P6, P9, P12, P19 mashahidi hawa wote ni mapolisi waliandika maelezo.

    Polisi waliandika wenyewe wakajikana wenyewe, wakajishuhudia wenyewe niliwauliza hapa sheria gani inayoruhusu haya wakasema polisi ndivyo tunavyofanya.

    Sasa waheshimiwa majaji uthibitisho wa hayo ni vilelezo D1, D5, D8, D11, D15 wamejiandikia wenyewe wamejikanya wenyewe wamejishudia wenyewe wamejikanya wenyewe sababu ni mapolisi.

    Ni shahidi mmoja tu ambaye aliandika maelezo yake mbele ya polisi mwingine kama sheria inavyotaka P15 maelezo yake DD14.

    Inspeka wa Polisi Amani Michael yeye ndio alizingatia utaratibu tu.

    Wale maaskari wa kule Ruvuma nao maelezo yao yaliandikwa kwa usahihi mbele ya askari wengine, lakini hawakuletwa kuja kutoa ushahidi.

    Waheshimiwa majaji nimemaliza mtanisamehe nimevuta muda kidogo ushahidi wangu ndio huo.

    Ukawa wakati wa mapumziko....

  6. Lissu: Nilimuuliza OCCID kwanini mmenikamata na kunidhalilisha namna hii?

    Waheshimiwa majaji kuhusu ukamataji, nilikamatwa mbinga kwenye mkutano wa haadhara, Mimi ndio nilikua nahutubia mkutano nilikuwa jukwaani na kabla sijashuka jukwaani mkutano wetu unaisha saa 12 nilifuatwa na afisa wa Polisi aliyejitambulisha ndiye OCD mbinga nimemsahahu jina.

    Waheshimiwa majaji, akaniambia nakutaka kituoni sasa hivi.

    Nikamuuliza unanitakia nini wewe Polisi, nimefanya kosa gani akaniambia twende wewe utajua hayo mbele ya safari nikamwambia afande huo sio utaratibu wa kisheria wa nchi hii, niambie kosa langu tutaenda usiponiambia hatuendi, niambie kosa langu usiponiambia siendi.

    Waheshimiwa majaji huyo bwana OCD alishuka jukwaani nikaendelea kuwaaga wananchi ghafla nikasikia kishindo cha mabomu ya machozi, walipiga mabomu ya machozi mengi sana na waliwapiga watu kwa marungu sana.

    Mimi nilikua jukwaani ila sijui nilishukaje nilijikuta nimeshakalishwa chini kwemye gari ya polisi chini sakafuni sikuwa peke yangu nikapelekwa mpaka kituo cha Polisi Mbinga, walinipeleka mpaka Chumba ofisi ya OCCID sio lockup sitatoa ushuhuda wa uongo walinipeleka kwenye ofisi ya OCCID, waliponiingiza niliingizwa na mtu aliyejitambulisha kuwa yeye ndiye OCCID Lugano Gwasa super intendent wa Polisi.

    Nikamuuliza nimekaa pale karibu saa nzima waheshimiwa majaji na nilimuuliza kwanini mmenikamata na kunidhalilisha namna hii na aliniambia sisi tumeletewa amri ya kukukamata na RPC wetu, hatujaambiwa kosa lako, hilo utaenda kulijua mbele ya safari.

    Waheshimiwa majaji baada ya kukaa pale Mbinga giza likiwa limeshaingia kama saa moja nikapakiwa kwenye gari nikapelekwa mpaka Songea mjini ofisini kwa RPC na nilimkuta na nikamuuliza hawa watu wako wa mbinga wamesema wewe ndio umesema nikamatwe niambie nimetenda kosa gani?

    RPC Chilya aliniambia yeye anatekeleza amri iliyotoka makao makuu ya Polisi Dodoma ambayo ilielekeza nikamatwe nipelekwe Dar es salaam ambako kuna kesi imefunguliwa dhidi yangu na hakunieleza ni kesi gani waheshimiwa majaji.

    Waheshimiwa majaji ni RPC Chilya ndiye aliyeniambia tunakusafirisha kwenda Dar es salaam usiku huuhuu.

    Na siku hiyo muda nakamatwa hiyo jioni mimi, wenzangu tulikua tumezunguka siku nzima kufanya mikutano na tulikuwa tumechoka na hatujala kabisa nikamuomba afande ampigie dada yangu aniliteee chakula na kumpigia kaka yangu amueleze nimekamatwa na RPC Chilya hakunieleza kosa langu nitakuja kuelezwa Dar es salaam kesho yake.

    Katika orodha ya mashahidi ni pamoja Lugano Gwasa OCCID na RCO Ruvuma hawakuletwa kuja kutoa ushahidi na kama wangeletwa wangethibitisha jinsi zoezi la ukamataji lilivyokiukwa.

    Waheshimiwa majaji sehemu yangu ya mwisho ya ushahdi haitakuwa ndefu ninaelekea kumaliza.

  7. Lissu: Hiyo serikali mnayodai nimeitishia ni ipi?

    Lissu: Shahidi PW16 Amini Mahamba ambaye alichukua uongozi wa timu ya upelelezi tarehe 8, siku nne baadaye alisema alipokutana na timu na kuangalia ile video pamoja nao siku hiyohiyo alibaini kuna uhaini hakukuwa na presumption of innocence ndio maana hawakwenda usalama wa taifa kwa wanasheria yani walikuwa na majibu yao tayari.

    Na kwa vile walikuwa na majibu waheshimiwa majaji waliulizwa mmewatafuta viongozi wa Chadema muwaulize walisema hapana,

    Mlinitafuta Mimi mniulize niwaeleze ilimaanisha nini walisema hapana na haikuwa na maana sababu tayari kwao nilikuwa na kosa na kwa sababu hiyohiyo ya Polisi kuwa na majibu hata walipoletewa ushahidi na PW17 kutoka dodoma maelezo ya P yanasema yeye ndiye alichapisha na kusambaza kwao.

    Maelezo ya shahidi P hayakuwa na maana sababu tayari wao walikuwa na majibu.

    Nilimuuliza P16 kama alisoma maelezo ya baadhi ya mashahidi yanayoonesha nani alipiga zile video maelezo yanayosema ni P17 na watu wake wa Jambo ndio walirekodi kuchapisha na kusammbaza lakini kwa sababu kwao tayari nilikuwa na makosa haikuwa na maana kufuata taratibu.

    Waheshimiwa majaji ukiukaji mwingine wakati wa upelelezi niliwauliza kwenye PGO aya ya 25 ni matendo yanayoendana na makosa mpaka sheria iseme hivyo?

    Nikawauliza waangalie sheria kuwa nilikuwa na nia ya kuzuia na kuvuruga uchaguzi wakasema haipo.

    Nikawaonesha ibara ya 151 /1 ya katiba juu ya maana ya serikali, wakaona serikali ni kitu gani, nikawauliza waambieni majaji kama kwenye maneno yangu kuna serikali ya jamuhuri?... hakuna, serikali ya mapinduzi ya zanzibar?... hakuna. kuna rais wa jamuhuri hakuna kuna serikali ya halmashauri hakuna.

    Nikawauliza kuna neno mkuu wa mkoa fulani?..hakuna.

    Nikawauliza kwenye hayo maneno kuna mahali mamlaka za mji au serikali za mitaa imetajwa?.. wakasema hakuna.

    Nikawauliza kuna jina au neno linalomhusisha Rais, Makamu wake au Waziri Mkuu? wakasema hakuna.

    Nikawauliza kuna neno au jina linalomhusisha kiongozi yeyote wa serikali iwe kuu au serikali za mitaa? Nikawauliza hiyo serikali mnayodai nimeitishia ni Ipi? ..waheshimiwa majaji hawakuwa na lolote la kusema.

  8. Lissu: Niliwauliza mashahidi mnayolalamikia yanakosa gani lakini hawakuwa na cha kusema

    Lissu: Shahidi P17 anasema alikuwepo mtu mmoja alikuwa na jina la kibantu na simkumbuki na huyo mtu hakuja kutoa ushahidi kwa hiyo upelelezi wa kesi ya uhaini haukumshirikisha mwendesha mashitaka na wanasheria wake.

    Lissu: Waheshimiwa majaji shahidi namba moja namba mbili na namba 16, Amin Mahamba waliulizwa kwamba kwenye PGO mnatambua kwamba mmeelekezwa kuna haki ya kikatiba ya watuhumiwa na haki yenyewe ni kutoa maoni kujieleza, haki ya kumlinda wakasomewa wakasema ndio wanafahamu na nikawauliza mnafahamu kwenye PGO mmeamriwa kutokutoka nje ya hiyo amri wakasema wanafahamu.

    Nikawauliza waleze jinsi walivyozingatia haki zangu kama wanavyoelekezwa na PGO kuwa walizingatia haki zangu waheshimiwa majaji hawakuwa na lakusema.

    Waheshimiwa majaji mashahidi haohao PW1 PW2 na PW16 niliwaonesha mimi matakwa ya vifungu vya 52, 2:B vinavyosema ukipinga serikali, ukitoa kauli za kuishambulia serikali, ukitoa maneno ambayo katika mazingira mengine yanaweza kuwa kosa la jinai lakini ukiyatoa kwa lengo kutaka kuonesha serikali imekosea kwenye utendaji wake na kwa lengo la kutaka kubadilisha mambo vifungu hivyo viwili vinasema hujatenda kosa.

    Niliwauliza hayo maneno mnayolalamikia yanakosa gani wakati yalitolewa yakitaka kuonesha ubovu wa katiba, madhaifu kwenye mifumo na si vinginevyo na hawakuwa na chochote cha kusema waheshimiwa majaji.

    Pia niliwaonesha kifungu cha 52:2 cha sheria ya vyombo vya habari kinachosema sio kosa la jinai kusema ubovu wa katiba na madhaifu mengine ya serikali kwa nia ya kutaka kubadilisha mambo na walisema ndio waheshimiwa majaji na nikawauliza mlizingatiaje haya kwenye maelezo yenu?, mlizingatiaje vifungu hivi?', hawakuwa na ya kusema waheshimiwa majaji.

    Kadhalika niliwaonesha hawa mashahidi watatu PGO namba moja aya ya 24 ambayo inasema nguzo kuu wakati wa upelelezi wa makosa ya jinai ni presumption of innocence mfanye upelelezi mkijua mtuhumiwa hana hatia na nilipowaonesha hiyo walisema ndio ni hivyo

    Na kwenye PGO hiyo hiyo nikawaonesha Polisi wakifuata misingi mingine nje ya PGO hiyo hamtafuata taratibu sahihi za kujua ukweli na haki haitatendeka na walisema ndio ni kweli.

    Sasa waheshimiwa majaji ushahidi wa mashahidi hawa unaonesha hivi waliona ile video tarehe 4/04/2025 huo ni ushahdi wa PW1 na PW2 kosa limefanyika tarehe tatu na siku iliyofuata PW1 akampelekea PW2 na akamuonesha vipande vipande na siku hiyo hiyo akaamuru nifunguliwe jalada la uhaini yaani hakukua na wanasheria yani hakukuwa na presumption of innocence.

  9. Kuhusu ushahidi dhidi yake

    Anazungumzia ushahidi wenyewe uliotolewa na mashahidi hawa na atatoa ushahidi wake kuonesha kuwa ushahidi uliotolewa upande wa mashtaka hauoneshi kuwepo kwa kosa la uhaini au kosa la jinai.

    Wakati wa PH upande wa mashtaka ulileta orodha ya mashahidi 30 ambao walisema hao ndio watakaoleta ushahidi wa kuthibitisha tuhuma za uhaini dhidi yake.

    Anasema kuwa upande wa mashtaka haukuleta Mashahidi wote hawa 30 na Badala yake walileta 17 Pekee.

    Katika Mashahidi 17 ambao walioletwa 8 ni Askari Polisi 9 waliobaki ni wa Kificho na hawa 9 mahakama haiwafahamu majina yao na wala haifahamu wanaishi wapi haifahamu wanafanya kazi gani na haifahamu chochote zaidi majina waliopewa haya ya akina P na inaweza kuwa wamekuwa hapa muda wote kesi inaendelea maana mahakama haiujui na upande wa utetezi haiwajui.

  10. Karibu katika siku nyingine ya taarifa zetu za moja kwa moja kutoka mahakamani, ambapo Tundu Lissu anatoa ushahidi wake dhidi ya upande wa mashtaka.

  11. Lissu: Kauli zangu zilinyofolewa nje ya muktadha

    Nilisema hivi: mabadiliko yanahitaji muda, na kama kweli kulikuwa na utayari wa kufanya mageuzi, basi uchaguzi ungeweza kuahirishwa ili kutoa nafasi ya kuyatekeleza. Hata hivyo, CCM ilikataa kabisa wazo hilo.

    Matokeo yake, watu waliuawa. Kwa mujibu wa Tume ya Jaji Chande, watu 518 walipoteza maisha, huku hatima ya wengine ikiwa haijulikani. Ninaamini kuwa kama uchaguzi ungeahirishwa, maafa hayo yangeweza kuepukika.

    Baadaye nikaelezwa kuwa nilisema "nitakinukisha" na kwamba nilihamasisha maandamano. Lakini maneno hayo yalinyofolewa ‘nje ya muktadha’.

    Katika mazungumzo yale, sikuzungumzia tutaifanyaje serikali hii. Hayo hayakuwa sehemu ya ajenda yangu.

    Leo ninaambiwa nilikuwa na nia ya kuitishia serikali. Ilitoka wapi? Mliambiwa na nani?

    Nia yangu ilikuwa kuwaelewesha watia nia wa chama changu kuhusu matatizo ya mfumo wetu wa uchaguzi ili waweze kuelewa na kuunga mkono msimamo wa CHADEMA wa "No Reforms, No Election".

    Haikuwa kuitishia serikali, kwa sababu hilo halikuwa lengo wala ajenda yangu.

    Sikuhamasisha watu kufanya fujo. Mimi ni mwanasheria, na hakuna sheria yenye masuala ya "kukinukisha."

    Kusudi letu lilikuwa kuwaelimisha na kuwahamasisha Watanzania nchi nzima.

    Tutakapokutana kesho kutwa, nataka niwapitishe kwenye ushahidi uliowasilishwa mbele yenu muone kama unajitosheleza kunyonga mtu.

    Kwa kuwa muda umeisha, naomba niishie hapa kwa leo. Tukutane tena Jumatano.

    Zaidi soma hapa:

  12. Lissu: Mfumo wa uchaguzi unaitetea CCM

    Lissu: Kwa hiyo mfumo wa kampeni wa uchaguzi umekaa katika namna inayoipendelea CCM. Kuna fujo sana. Mimi nimefanyiwa fujo, nimepigwa na mabomu ya polisi Tarime, Serengeti, nimesimamishiwa kampeni kwa siku kumi.

    Mfumo mzima wa kampeni unaumiza upinzani.

    Majaji, nilizungumza na watia nia kuhusu maadili ya uchaguzi. Utafikiri wanapenda maadili ya uchaguzi, lakini ni silaha nyingine ya kuchangia uonevu. Wanaosimamishiwa kampeni ni wapinzani halisi.

    Wale ambao si upinzani wa kweli hawana shida nao.

    Nilizungumza juu ya masuala ya media na election. Majaji, vyombo vya habari vya nchi, vya serikali na visivyo vya serikali, vyote vinakuwa CCM wakati wa uchaguzi.

    Mwaka 2020, ripoti ya utazamaji wa ndani wa uchaguzi ya Research for Independent Democracy Tanzania, iliyoandikwa na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliandika kitu muhimu sana, kwamba vyombo vya habari vyote wakati wa uchaguzi ni CCM.

    BBC walilipishwa faini ya zaidi ya milioni kumi kwa kufanya interview na mimi na TCRA. Jambo TV yenyewe imefungiwa mara nyingi sana na TCRA.

    Masuala yanayohusu siku ya uchaguzi, hilo somo nimelizungumza kwenye mihadhara mingi na matatizo yake. Mnabadilishiwa matokeo, ukishinda kishambashamba wanakubadilishia matokeo, ukipinga unakutana na FFU.

    Hayo ndiyo matatizo ya wagombea wa udiwani na urais niliyoyazungumza nao pale.

    Nilizungumza nao kuhusu what happens baada ya uchaguzi. Kimsingi, nilichowaambia ni kwamba mahakamani haiwezekani kwa sababu hizo taratibu za kutengua matokeo ya uchaguzi, kwa sababu the law is designed in such a way, ina-defend CCM.

    Licha ya kuwa matatizo ya uchaguzi ni makubwa na kila mtu anafahamu.

    Nikawaambia hii ndiyo reform tunayoipigania, hii ndiyo tunayoitaka, na hii ndiyo ya kuwahamasisha Watanzania waidai.

    Soma pia:

  13. Lissu: Mgombea wa upinzani hashindani na wapinzani pekee

    Lissu: Mama amepata asilimia 98 ya kura, lakini swali langu ni: kura hizo zilipatikana kutoka kwa wapiga kura gani, na kwa utaratibu gani?

    Haya ni baadhi ya masuala ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwa muda mrefu katika ripoti mbalimbali za waangalizi na wasimamizi wa uchaguzi.

    Pia tulizungumza na watia nia kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea na namna baadhi yao walivyoenguliwa katika chaguzi tofauti.

    Nilieleza jinsi sheria na mamlaka za uchaguzi zinavyotumika kuwaengua wagombea wa upinzani.

    Katika historia ya uchaguzi nchini, sijawahi kuona wagombea wa CCM wakienguliwa kwa kiwango kinachoonekana kwa wagombea wa upinzani. Hilo ndilo lilikuwa moja ya maeneo ya mjadala wetu kuhusu mfumo wa uchaguzi.

    Nilizungumza pia kuhusu mazingira ya kampeni za uchaguzi.

    Waheshimiwa Majaji, kwa uzoefu wetu wa kushiriki uchaguzi, mgombea wa upinzani hukutana na changamoto nyingi wakati wa kampeni.

    Mara nyingi hulazimika kushughulika na vikwazo vinavyotokana na mamlaka mbalimbali za serikali katika maeneo anayosafiri kufanya kampeni.

    Nilieleza kuwa, kwa mtazamo wangu, mgombea wa upinzani hukabiliana na mfumo mpana unaojumuisha wasimamizi wa uchaguzi, vyombo vya dola na maafisa mbalimbali wa serikali.

    Changamoto hizo, kwa mujibu wa maelezo yangu, zinaweza kuathiri usawa wa ushindani wa kisiasa wakati wa uchaguzi.

    Aidha, nilisema kuwa mgombea wa upinzani anaposhiriki uchaguzi hukutana na ushindani ambao hauhusishi wagombea wengine pekee, bali pia mifumo ya usimamizi wa uchaguzi iliyopo.

    Maelezo zaidi:

  14. Lissu: Shahidi wa mashtaka ndiye aliyechapisha video

    Lissu: George Bagyemu ndiye aliyeniambia makosa niliyokuwa nashtakiwa nayo.

    Kuhusu suala la uchapishaji, kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, shahidi pekee aliyekuwepo mkutanoni, aliyeyaona na kuyasikia maneno yangu moja kwa moja ni PW17.

    Mashahidi wengine wote hawakuwepo katika mkutano huo.

    PW17 ndiye aliyeieleza mahakama kuwa alirekodi mkutano huo, akaifanyia uhariri na baadaye akaichapisha katika mitandao ya kijamii kupitia video zilizorekodiwa kwa kamera.

    Kuhusu uchapishaji wenyewe, PW17 alisema wazi kuwa yeye ndiye aliyefanya hatua zote za uchapishaji. Kwa maneno mengine, he did everything, si mimi.

    Alipoulizwa nani aliyemualika, alisema aliwasiliana na Mkurugenzi wa Jambo TV, John Maro, ambaye naye alielekezwa na afisa wa CHADEMA, Brenda Rupia.

    Maelezo hayo yote yalikuwa mikononi mwa vyombo vya uchunguzi tangu tarehe 8 Aprili.

    Walikuwa wanajua nani aliandaa mkutano na nani alichapisha maudhui yake. Hata hivyo, wananituhumu kuandaa mkutano ambao uliandaliwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama, na pia wananituhumu kuchapisha maneno ambayo, kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wao wenyewe, yalichapishwa na mtu mwingine.

    Mwishowe wakafungua kesi dhidi yangu, na leo nimekaa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja.

    Sasa, nilizungumza nini katika mkutano huo?

    Majaji, katika saa hizo takribani tatu, nilizungumza na watia nia kuhusu mfumo wa uchaguzi nchini.

    Niliwaeleza changamoto zilizopo katika Katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na namna mfumo wa usimamizi wa uchaguzi ulivyojengwa.

    Pia nilizungumzia muundo wa Tume ya Uchaguzi na hoja mbalimbali zinazotolewa kuhusu uhuru wake.

    Kwa mfano, niliwatajia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Augustino Ramadhani, na mjadala uliowahi kuwepo kuhusu ushiriki wake katika siasa.

    Aidha, nilitoa mfano wa mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

    Niliwaeleza kuwa Dar es Salaam ndiyo mkoa wenye idadi kubwa ya wakazi nchini, lakini Zanzibar ina uwakilishi mkubwa wa majimbo ukilinganisha na idadi yake ya watu.

    Hoja yangu ilikuwa kwamba mfumo wa ugawaji wa majimbo haujazingatia idadi ya watu pekee, bali pia vigezo vingine vya kijiografia na kiutawala ambavyo vimekuwepo tangu zamani.

    Soma zaidi:

  15. Lissu: Nilivamiwa na kukamatwa nikiwa nahitimisha mkutano Songea

    Lissu: Tarehe 4 Aprili 2025, mimi na John Heche tulianza ziara ya kusini kwa kuanzia mkoani Lindi. Akiwa huko, Askofu wa Jimbo la Lindi alitupa nafasi ya kukutana naye na tukamueleza msimamo wetu kuhusu ajenda ya "No Reforms, No Election." Baada ya mazungumzo hayo alinipa rozari, ambayo bado ninaivaa hadi leo.

    Baadaye tulielekea mkoani Ruvuma. Tarehe 9 Aprili, majira ya saa kumi na mbili jioni, nilikuwa nikihitimisha mkutano wangu wa hadhara pale Songea, ghafla polisi walivamia mkutano huo.

    Mimi na viongozi wenzangu tulipigwa na kukamatwa, kisha nikapelekwa katika Kituo cha Polisi Songea.

    Baadaye nilipelekwa katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma (RPC), Michael Chiriwa. Wakati huo nilikuwa na njaa sana, hivyo nikaomba dada yangu aruhusiwe kuniletea chakula. Baada ya kuwasiliana naye, alifika na chakula na nikala nikiwa ofisini kwa RPC.

    RPC Chiriwa aliniambia kwamba ningesafirishwa kwenda Dar es Salaam usiku huo huo kwa maagizo yaliyotoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

    Usiku huo nilipakiwa kwenye gari la polisi na kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam. Mmoja wa maafisa aliyekuwa kwenye msafara huo alijitambulisha kwangu kama RCO Makunja.

    Tulisafiri usiku kucha hadi Dar es Salaam, ambapo nilifikishwa mahabusu katika Gereza la Shimoni.

    Soma zaidi:

  16. Lissu: Tulizungumza hadharani, Hatukuwa na mpango wa uhaini

    Lissu: Nilialikwa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda mwezi Machi 2025 kutoa mhadhara kuhusu urithi wa Mwalimu Julius Nyerere na nafasi yake katika Afrika Mashariki.

    Katika mhadhara huo nilizungumzia mchango wa Nyerere pamoja na changamoto za mfumo wa uchaguzi ambazo Tanzania inaendelea kukabiliana nazo.

    Baadaye nilialikwa Luanda, Angola. Niliporejea Tanzania baada ya takribani wiki moja, tulipanga kuanza ziara ya kitaifa kueleza msimamo wa "No Reforms, No Election".

    Ziara hiyo ilianza tarehe 22 Machi na kuhitimishwa tarehe 31 Machi 2025, ikihusisha mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini. Tulizungumza hadharani bila kuficha jambo lolote.

    Hatukuwa na mpango wa kufanya uhaini. Kila tulichokuwa tukifanya kilikuwa wazi kwa umma.

    Nilihitimisha ziara hiyo Iringa tarehe 31 Machi. Nikiwa huko, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Amani Golugwa, alinifikishia taarifa kwamba chama kilikuwa kimeandaa kikao cha watia nia kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

    Lengo lilikuwa kujadili namna ya kuwapa maelekezo watia nia hao kuhusu msimamo wa chama wa "No Reforms, No Election".

    Tukakubaliana kuwa tukirejea Dar es Salaam tarehe 3 Aprili, tungezungumza nao na kuwaeleza msimamo rasmi wa chama.

    Mimi na John Heche tulimaliza ziara tarehe 31 Machi na kurejea Dar es Salaam tarehe 1 Aprili.

    Tarehe 3 Aprili 2025 ndipo kikao hicho kilifanyika, ambacho baadaye kikawa sehemu ya msingi wa kesi hii.

    Katika kikao hicho, mimi ndiye nilikuwa mzungumzaji mkuu kwa sababu jukumu la Mwenyekiti wa chama ni kuelezea na kutetea misimamo ya chama.

    Kikao hicho kiliandaliwa na Sekretarieti ya chama chini ya Katibu Mkuu, si Mwenyekiti wa chama.

    Mimi niliarifiwa tu kuwa kutakuwa na kikao hicho kupitia Naibu Katibu Mkuu. Kwa hiyo, madai kwamba Mwenyekiti wa Taifa ndiye aliyeandaa mkutano huo yanaonesha kutoeleweka kwa mfumo wa uendeshaji wa chama.

    Majaji, ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi 17 unaonesha kuwa mkutano huo ulikuwa mrefu.

    Mimi mwenyewe sikumbuki nilizungumza kwa muda gani. Hata video inayodaiwa kurushwa na Jambo TV sijawahi kuitazama hadi leo.

    Hata mngeniuliza nilizungumza kwa muda gani, nisingeweza kusema kwa uhakika. Ninachoweza kusema ni kwamba nilizungumza kwa muda mrefu sana.

    Katika ushahidi wangu, nitaeleza kwa muhtasari yale niliyoyasema ili mahakama iamue yenyewe kama yalikuwa ya uhaini au la.

    Mimi ni mzungumzaji wa muda mrefu, jambo ambalo naamini wengi wameliona. Watu waliouliza maswali walijibiwa, na ndiyo maana mkutano huo ulidumu kwa muda mrefu.

    Inawezekana ulikuwa wa saa nne au tano, kwa sababu ulikuwa mrefu sana.

    Kama shahidi PW17 alivyosema, ni kweli Jambo TV walikuwepo. Tulikuwa tumefanya kazi nao kwa muda mrefu, na pia kulikuwa na vyombo vingine vya habari.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Lissu: CHADEMA ilihamasisha ‘No Reforms, No Election’ Nchi Nzima

    Baada ya hapo, tulianza kuandaa mkakati wa kutekeleza sera ya "No Reforms, No Election". Tulifanya kikao Bagamoyo na kukubaliana kutumia njia zinazotambuliwa kisheria, ikiwemo mikutano ya hadhara, kampeni za uhamasishaji, maandamano ya amani na hatua nyingine za kidemokrasia.

    Tulikubaliana kuwa tungehamasisha wananchi kutumia haki zao za kikatiba kwa njia za amani. Hatukupanga kutumia vurugu wala kuharibu mali za mtu yeyote.

    Aidha, tuliona ni muhimu kuzungumza na makundi mbalimbali ya Watanzania. Tulianza kwa taasisi za kidini na kukutana na viongozi wa Kiislamu kutoka Shura ya Maimamu na taasisi nyingine za Kiislamu.

    Pia tuliomba kukutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) pamoja na Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), ingawa hatukufanikiwa kufanya mikutano hiyo.

    Tulikutana pia na Jukwaa la Wahariri Tanzania pamoja na viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ili kuwaeleza msimamo wetu.

    Kwa kuwa Tanzania ina marafiki na washirika katika ukanda huu, tuliamua pia kuonana na baadhi ya viongozi wa kikanda. Mimi, John Heche na Godbless Lema tulisafiri kwenda Nairobi na kukutana na Raila Odinga.

    Vilevile tulikutana na baadhi ya wazee wa taifa, akiwemo Jaji mstaafu Joseph Warioba, na kuzungumza naye kuhusu hoja ya "No Reforms, No Election".

    Kwa ujumla, tulifanya kila tulichoweza kuhakikisha kuwa msimamo wetu unaeleweka kwa umma kwa njia ya wazi na ya amani.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Lissu: 'No Reforms, No Election' haikuwa kauli yangu pekee

    Lissu: Mwezi Desemba 2024 ndipo kauli ya "No Reforms, No Election" ilipoibuka rasmi ndani ya CHADEMA.

    Tulijiuliza tufanye nini katika mazingira hayo, na tukakubaliana kwenda kuzungumza na Watanzania kuhusu msimamo wetu ili marafiki na wapinzani wetu wote wauelewe.

    Tarehe 10 Desemba 2024, msimamo huo ulitangazwa rasmi chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CHADEMA wakati huo, Freeman Mbowe.

    "No Reforms, No Election" si kauli ya Lissu, bali ilikuwa msimamo wa Mwenyekiti wa CHADEMA wakati huo, Freeman Mbowe.

    Katika vikao vya chama tulijadili namna ya kutekeleza msimamo huo. Wakati huo tulikuwa tunakaribia uchaguzi mkuu wa chama uliopangwa kufanyika Januari 2025, hivyo tukakubaliana kuumaliza kwanza kabla ya kuendelea na hatua nyingine.

    Majaji, tarehe 20 Januari 2025 tulifanya kikao cha Baraza Kuu la CHADEMA, ambalo kimsingi ni chombo kikuu cha maamuzi ya chama.

    Kamati Kuu iliwasilisha mapendekezo ya kuifanya sera ya "No Reforms, No Election" kuwa msimamo rasmi wa chama. Baraza Kuu lilikubali mapendekezo hayo na kuyapeleka kwenye Mkutano Mkuu wa chama uliokuwa ufanyike siku iliyofuata, tarehe 21 Januari 2025.

    Tarehe 21 Januari 2025, Mkutano Mkuu ulijadili na kupitisha rasmi sera ya "No Reforms, No Election". Wakati huo Freeman Mbowe alikuwa Mwenyekiti wa chama, nami nilikuwa Makamu Mwenyekiti.

    Katika mkutano huo pia tulifanya uchaguzi wa viongozi wa chama kwa uwazi, huku waangalizi mbalimbali wakialikwa kufuatilia mchakato huo. Baadaye nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA.

    Kufuatia uchaguzi huo, nilimteua John Mnyika kuendelea kuwa Katibu Mkuu wa chama pamoja na viongozi wengine katika nafasi mbalimbali.

    Soma zaidi:

  19. Lissu asimulia mchakato wa maridhiano na CCM

    Lissu: Baada ya kushambuliwa kwa risasi wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, nilikwenda uhamishoni. Nilinusurika kuuawa na hatimaye nikakimbilia katika Ubalozi wa Ujerumani.

    Tarehe 17 Februari 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa katika ziara barani Ulaya kwa mkutano uliowakutanisha viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU), nilipokea ujumbe kupitia watu wangu kwamba alikuwa anataka kuonana nami.

    Wakati huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alikuwa gerezani kwa takribani miezi sita au saba akikabiliwa na kesi ya ugaidi.

    Nilipopata ujumbe huo, nilishauriana na viongozi wenzangu. Tuliona ilikuwa ni hatua nzuri, hivyo nikaenda kukutana naye. Aliniambia alikuwa na nia ya kuyamaliza matatizo yaliyokuwa yamejitokeza wakati wa utawala uliopita.

    Nikamwambia aanze kwa kumwachilia Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe, ndipo mazungumzo mengine yaweze kuendelea. Pia nikasema tunahitaji kuzungumzia Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi. Alijibu kuwa alikuwa tayari kufanya mazungumzo hayo.

    Aidha, nilimweleza kuwa mimi, Godbless Lema na wengine tulikuwa tumekimbia nchi kutokana na hofu ya usalama wetu, hivyo tulihitaji uhakikisho kwamba ilikuwa salama kurejea nyumbani. Baadaye, alitangaza bungeni kuwa Watanzania waliokuwa uhamishoni warejee nchini. Mbowe naye aliachiwa huru, jambo lililotupa faraja ya kurudi nyumbani.

    Tuliporejea, tulipendekeza kuwa watu wote waliokuwa wamefunguliwa kesi ambazo tuliamini zilikuwa na misingi ya kisiasa wafutiwe mashtaka, na baadhi ya kesi hizo zilifutwa.

    Baadaye yakaanza mazungumzo kati ya CHADEMA na CCM. Tulipeleka mapendekezo mbalimbali kuhusu Katiba Mpya, muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi na ratiba ya utekelezaji wa mageuzi hayo.

    Kwa upande wetu, tulitaka mchakato wa Katiba Mpya ukamilike kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Hata hivyo, tulianza kuona hakuna hatua za kutosha zilizokuwa zinachukuliwa. Mara nyingi tuliwasilisha mapendekezo kwa maandishi lakini majibu yalitolewa kwa njia ya mazungumzo badala ya maandishi rasmi.

    Takribani mwaka mmoja ulipita bila majibu rasmi ya maandishi kuhusu mapendekezo yetu.

    Mwaka 2025, tuliendelea kusisitiza kuwa majibu yatolewe kwa maandishi ili kuwe na uwazi kuhusu mambo yaliyokubaliwa na yaliyokataliwa.

    Tarehe 21 Mei 2025, tulipokea majibu ya maandishi yaliyokataa mapendekezo yetu yote.

    Baada ya hapo, tulikaa na kujiuliza maana ya maridhiano ikiwa hakuna makubaliano yanayotekelezwa zaidi ya vikao vya mazungumzo. Tukafikia hitimisho kwamba ni lazima kurejea kwa wananchi.

    Tarehe 31 Mei 2025, tuliamua kama chama kuanzisha kampeni ya kuhamasisha madai ya Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi. Tulizunguka nchi nzima kuzungumza na wananchi kuhusu masuala hayo.

    Kadiri joto la kisiasa lilivyoongezeka, ndivyo madai ya kukamatwa kwa wanachama na viongozi wa upinzani pamoja na kesi mbalimbali yalivyoendelea kujitokeza.

    Hali hiyo iliendelea hadi uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji wa Novemba 2024.

    Ndani ya chama kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo kutokana na kutokuwepo kwa mageuzi yaliyokuwa yanadaiwa. Hatimaye, CHADEMA iliamua kushiriki.

    Lissu alidai kuwa uchaguzi huo ulisimamiwa na mfumo wa utawala wa serikali kupitia TAMISEMI, huku watendaji mbalimbali wa uchaguzi wakiwa ni wateule wa mamlaka ya serikali.

    Pia alidai kuwa wagombea wengi wa upinzani walienguliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali ambayo, kwa mujibu wake, iliathiri ushindani wa kisiasa katika uchaguzi huo.

    Lissu alidai kuwa wagombea wengi wa upinzani walienguliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali ambayo, kwa mujibu wake, iliathiri ushindani wa kisiasa katika uchaguzi huo.

    Alisema waliopinga matokeo hayo walikumbana na nguvu za dola katika maeneo mbalimbali, akidai kuwa watu kadhaa waliuawa Tarime.

    Baada ya uchaguzi huo wa Novemba 28, wiki iliyofuata, tarehe 3 Desemba, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana kujadili hatua za kuchukua kufuatia yaliyotokea katika uchaguzi na mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo nchini.

    Pia unaweza kusoma:

  20. Lissu: Masuala ya uchaguzi si ya kuyachukulia kwa wepesi

    Lissu: Majaji, masuala ya uchaguzi, Katiba na uendeshaji wa nchi yasipowekwa sawa yanaweza kusababisha maafa.

    Leo, mtu anayezungumzia masuala hayo hawezi kuonekana kama chawa. Kabla ya Oktoba mwaka jana, mtu aliyesema hivyo mara nyingi alionekana kwa mtazamo huo.

    Sisi ni Jamhuri ya Muungano, lakini wengi wetu hatufundishwi historia yake kwa kina. Watu wengi hufahamu tu majina ya Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume bila kuelewa mazingira yaliyopelekea kuundwa kwa Muungano.

    Inaitwa Jamhuri ya Muungano kwa sababu Zanzibar ilipitia Mapinduzi ya mwaka 1964, yaliyotanguliwa na migogoro mikubwa ya kisiasa na uchaguzi. Ushahidi wangu ni Ripoti ya Tume ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1991.

    Tume hiyo ilieleza kuwa, baada ya wananchi wa Zanzibar kuchoshwa na hali ya kisiasa ya wakati huo, kulitokea mapinduzi yaliyoambatana na umwagaji wa damu. Kwa hiyo, historia ya Jamhuri hii inaonesha madhara yanayoweza kutokea pale malalamiko ya kisiasa na uchaguzi yanapopuuzwa.

    Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, tumekuwa tukishuhudia malalamiko kuhusu uchaguzi na madai ya kutotendewa haki katika ushindani wa kisiasa.

    Ripoti za Tume ya Nyalali, Tume ya Jaji Othman Chande pamoja na ripoti mbalimbali za waangalizi wa uchaguzi zimeendelea kubainisha changamoto hizo kwa miaka mingi.

    Madai ya Katiba Mpya, usawa wa vyama vya siasa na kuimarishwa kwa demokrasia yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika mijadala ya kisiasa nchini.

    Katika ushahidi wangu nitaonesha jinsi tulivyojaribu, mwaka 2025, kuhimiza mabadiliko kwa njia za amani ili kuepusha migogoro, lakini hatukusikilizwa.

    Waheshimiwa Majaji, masuala ya uchaguzi si ya kuyachukulia kwa wepesi. Mfumo wetu wa uchaguzi una changamoto ambazo zimekuwa zikijulikana kwa miaka mingi. Changamoto hizo zimeandikwa katika ripoti za ndani na za kimataifa, na mara nyingi zimeambatana na onyo kwamba zisipotatuliwa zinaweza kuendelea kuleta migogoro.

    Soma Zaidi: