Heche: 'Ni kama Simba na Yanga wanacheza, halafu Yanga ndiye anamchagua refa'

Chanzo cha picha, Facebook/Heche
Lissu: Kiswahili cha No Reforms, No Election ni nini?
Heche: Bila mabadiliko hakuna uchaguzi.
Lissu: Ni mabadiliko gani yaliyoazimiwa na Kamati Kuu?
Heche: Kamati Kuu iliazimia mabadiliko ya kikatiba na kisheria ili kuondoa mamlaka makubwa ya Rais ya kuunda Tume ya Uchaguzi, wakati yeye mwenyewe ni mgombea. Ni kama simba anacheza na Yanga halafu Yanga ndiye anachagua refa.
Lissu: Una maana gani unapozungumzia tume?
Heche: Tume Huru ya Uchaguzi ambayo haitakuwa na upendeleo wala kuingiliwa na mgombea ambaye ana maslahi.
Lissu: Usinitangulie, ukinitangulia... anaonesha majaji wa serikali. (Kicheko mahakamani.)
Lissu: Shahidi, nataka uwaeleze majaji uzoefu wako na matatizo ya chaguzi za nchi hii.
Heche: Waheshimiwa majaji, mimi nimegombea mara kadhaa. Nimekuwa diwani na nimekuwa mbunge katika chaguzi za nchi hii. Nimeshiriki maeneo mbalimbali katika kampeni za chama.
Chaguzi zote hizi, waheshimiwa majaji, ziliambatana na maumivu makubwa; kutekwa, kuenguliwa kwa wagombea wetu, kuibiwa kwa fomu za viapo vya mawakala, ratiba zetu kuingiliwa na polisi, kupigwa kwa watu katika mikutano ya kampeni, wagombea wetu kunyimwa fomu za matokeo, kura za uongo kuingizwa kwa maboksi na mabegi na askari polisi ambao walitakiwa kusimamia uchaguzi. Wagombea wetu walienguliwa kwa kuambiwa hawajui kusoma na kuandika.
Naomba nitafafanua jambo moja baada ya jingine.
Nitaanza na mauaji.
Katika uchaguzi wa Arumeru, Katibu wetu wa USA River, Bwana Msafiri Bwambo, aliuawa kwa kuchinjwa kwa chainsaw. Watu waliosadikiwa kuwa wanachama wa CCM walihusishwa na tukio hilo, na mpaka leo hakuna mtu aliyekamatwa au kufungwa kwa mauaji hayo.
Lissu: Tukio lingine, shahidi.
Heche: Hapa Dar es Salaam, Kinondoni, aliuawa Mwenyekiti wa CHADEMA wa Ananasi, Dani Yona. Vilevile hakuna uchunguzi uliokamilika wala mtu aliyekamatwa, waheshimiwa majaji.
Mwanachama wetu Akwilina Akwilini, ambaye wakati huo Kamanda wa Polisi, Bwana Mambosasa, alithibitisha aliuawa kwa risasi ya polisi. Hakuna askari aliyekamatwa wala kushitakiwa.
Badala yake, nilishtakiwa mimi, John Mnyika, ambaye wakati huo alikuwa Katibu Mkuu; Freeman Mbowe ambaye alikuwa Mwenyekiti; Vincent Mashinji aliyekuwa Katibu Mkuu; Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; na Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.
Lissu: Waeleze majaji mlishtakiwa kwa kosa gani na kesi iliishia wapi?
Heche: Kwanza nieleze jambo moja. Wote hao walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama. Walishtakiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo uchochezi na kushiriki kusanyiko lisilo na kibali.
Lissu: Kabla sijasahau, hiyo kadhia ilinikosaje mimi?
Heche: Waheshimiwa majaji, Mwenyekiti wetu wa sasa alikuwa ameshambuliwa vibaya kwa risasi na alikuwa akipatiwa matibabu nje ya nchi. Wakati huo alikuwa Makamu Mwenyekiti.
Lissu: Uamuzi wa hiyo kesi ulikuwaje?
Heche: Tulihukumiwa kifungo cha miezi sita au kulipa faini. Mimi nililipa faini ya shilingi milioni 40. Kwa ujumla ilikuwa karibu shilingi milioni 300.
Lissu: Ilikuwa katika mahakama gani?
Heche: Ilikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na ilisikilizwa na hakimu ambaye baadaye alipandishwa cheo na kuwa jaji.
Lissu: Baada ya kuhukumiwa, nini kilifuata?
Heche: Tulikata rufaa Mahakama Kuu, na baadaye hukumu ile ilitupiliwa mbali. Mahakama ikaamuru turejeshewe fedha zetu, lakini mpaka leo sijawahi kurejeshewa, licha ya amri hiyo.
Lissu: Ni jaji gani wa Mahakama Kuu aliyetoa amri hiyo?
Heche: Jaji Mgeta, waheshimiwa.
Lissu: Sasa shahidi, ulisema kulikuwa na mauaji ya Akwilina Akwilini. Hiyo habari iliishia wapi?
Heche: Kama zilivyo habari nyingine za mauaji.
Jaji: Tuambie iliishia wapi.
Heche: Iliishia hapo, na hakuna aliyeshitakiwa wala kufungwa kwa mauaji hayo.
Unaweza Kusoma;











