Tundu Lissu kuanza kujitetea baada ya kukutwa na kesi ya kujibu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tundu Lissu
    • Author, Humphrey Mgonja
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam , Tanzania
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa uamuzi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, na kumkuta ana kesi ya kujibu.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Ndunguru, anayeongoza jopo la majaji linalosikiliza shauri hilo, amesema baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka unaowakilishwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), mahakama imejiridhisha kuwa kuna ushahidi wa kutosha unaomfanya Lissu awe na kesi ya kujibu.

Uamuzi huo unamaanisha kuwa kesi hiyo sasa inaingia katika hatua muhimu ambapo Tundu Lissu atapewa fursa ya kuwasilisha utetezi wake mbele ya mahakama.

Katika hatua hiyo, upande wa utetezi unaweza kuwasilisha ushahidi pamoja na kuwaita mashahidi wake ili kujibu hoja na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Lissu alikamatwa mkoani Ruvuma kabla ya kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam, ambako alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa rasmi mashtaka yanayohusiana na uhaini pamoja na makosa mengine yanayodaiwa kuhusiana na kauli na shughuli zake za kisiasa.

Upande wa mashtaka umekuwa ukidai kuwa baadhi ya kauli na matendo ya Lissu yalilenga kuzuia au kuvuruga mchakato wa uchaguzi mkuu na kuchochea uasi dhidi ya serikali.

Madai hayo ndiyo ambayo yamekuwa msingi wa mashtaka yanayomkabili mwanasiasa huyo.

Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya Tanzania kutokana na uzito wa mashtaka pamoja na nafasi ya Lissu katika siasa za Tanzania.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwenendo wa kesi hiyo pia umeibua mjadala mkubwa kuhusu haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na namna sheria za uhaini zinavyotumika katika mazingira ya kisiasa.

Jumuiya na taasisi mbalimbali za kimataifa zimeonyesha wasiwasi kuhusu mwenendo wa kesi hiyo na zimekuwa zikitoa wito wa kuhakikisha mchakato wa kisheria unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia haki za msingi za mshtakiwa.

Baadhi yao wamekuwa wakitaka mamlaka kuhakikisha kuwa Lissu anapata dhamana, matibabu na mazingira yote muhimu ya kisheria yanayostahili, huku wengine wakitoa wito wa kuachiwa kwake.

Hata hivyo, uamuzi wa mahakama kwamba Lissu ana kesi ya kujibu sio hukumu ya kuwa amepatikana na hatia. Ni hatua ya kisheria inayomaanisha kuwa mahakama imeona kuna msingi wa yeye kuitwa kutoa upande wake wa utetezi dhidi ya ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

Kwa sasa, macho yanaelekezwa katika hatua inayofuata ya kesi hiyo, ambapo Tundu Lissu atapata nafasi ya kujibu mashtaka, kupinga ushahidi uliowasilishwa dhidi yake na kuwasilisha ushahidi wa upande wa utetezi.