Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mabwawa 5 makubwa ya umeme Afrika: Nyerere la ngapi?
Tanzania imezindua rasmi mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), kwenye Mto Rufiji, moja ya miradi mikubwa zaidi ya miundombinu nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa za serikali, kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha megawati za umeme 2,115 kupitia mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa MW235. Kampuni ya Arab Contractors, ambayo ni sehemu ya muungano uliojenga mradi huo, inaeleza kuwa bwawa lina urefu wa mita 1,025 na kimo cha mita 131, huku hifadhi yake ikiwa na uwezo wa takriban mita za ujazo bilioni 34 za maji.
Kwa Tanzania, huo ni mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa maji kuwahi kujengwa nchini, ukitimiza ndoto ya miaka karibu 60 ya kuwa na mradi wa aina hiyo.
Lakini ukubwa wake unaonekana vizuri zaidi unapowekwa katika muktadha wa bara zima la Afrika.
Je, megawati 2,115 zinaifanya Julius Nyerere kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya maji ya umeme Afrika? Na ni miradi ipi mingine mikubwa kwa uwezo wa kuzalisha umeme Afrika? Hii hapa ni miradi mitano mikubwa ya umeme Afrika.
1. Grand Ethiopian Renaissance – Ethiopia- MW5,150
Uwezo wa kuzalisha umeme: MW5,150
Kwenye kulinganisha na Nyerere kuna mradi wa umeme wa Grand Ethiopian Renaissance Dam, maarufu kama GERD, nchini Ethiopia.
Kwa mujibu wa Ethiopian Electric Power, GERD ina uwezo uliowekwa wa kuzalisha megawati 5,150 na sasa imefikia uwezo wake kamili wa uendeshaji.
Huo ni uwezo unaozidi mara mbili ule wa bwala la Julius Nyerere.
Ofisi rasmi ya GERD inaeleza kuwa hifadhi ya bwawa hilo ina uwezo wa mita za ujazo bilioni 74 za maji, na eneo la hifadhi lina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 1,874. Bwawa kuu lina urefu wa takriban kilomita 1.8 na kimo cha mita 145.
GERD imejengwa kwenye Mto Blue Nile katika eneo la Benishangul-Gumuz.
Kwa nchi ya Ethiopia, mradi huu ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme na kupanua upatikanaji wa umeme nchini, huku pia ukiwezesha mauzo ya umeme kwa nchi jirani. Ethiopian Electric Power inasema GERD imekuwa chanzo muhimu cha uzalishaji katika mfumo wa taifa wa umeme.
Lakini mradi huo pia umehusishwa na mzozo wa muda mrefu kati ya Ethiopia, Misri na Sudan kuhusu namna ya kutumia na kusimamia maji ya Mto Nile.
Kwa kipimo cha uwezo wa kuzalisha umeme, GERD iko mbali ukilinganisha na miradi mignine ya umeme Afrika, ukiwemo wa Nyerere.
2. Kariba – Zambia na Zimbabwe - MW2,130
Uwezo wa kuzalisha umeme: MW2,130
Kwenye Mto Zambezi, mpakani mwa Zambia na Zimbabwe, kuna Bwawa la Kariba.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya mto zambezi (Zambezi River Authority), kituo cha Kariba Kaskazini nchini Zambia kina uwezo wa kuzalisha MW1,080, huku Kariba Kusini nchini Zimbabwe kikiwa na uwezo wa MW1,050. Kwa pamoja, vituo hivyo vina uwezo wa MW2,130.
Hivyo tofauti kati ya Kariba na Julius Nyerere ni MW15 pekee. Lakini ukubwa wa hifadhi ya maji unatofautiana kwa kiasi kikubwa.
Zambezi River Authority inaeleza kuwa hifadhi ya Kariba, katika kiwango chake cha juu cha kuhifadhi maji, ina uwezo wa mita za ujazo bilioni 185. Hifadhi hiyo ina urefu wa takriban kilomita 280 na upana wa hadi kilomita 32 katika sehemu yake pana zaidi.
Kariba ilijengwa kama mradi wa pamoja wa Zambia na Zimbabwe, na vituo vyake viwili vya kuzalisha umeme vinatumia hifadhi hiyo hiyo.
Kwa hiyo, kwa uwezo wa kuzalisha umeme, Kariba iko juu kidogo ya Julius Nyerere; lakini kwa kiasi cha maji kinachoweza kuhifadhiwa, tofauti ni kubwa sana.
3. Julius Nyerere (JNHPP) – Tanzania - MW2,115
Uwezo wa kuzalisha umeme: MW2,115
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la umeme Tanzania, TANESCO, Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), lina mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa MW235, na hivyo kufikisha jumla ya MW2,115.
Taarifa ya Arab Contractors, kampuni iliyotekeleza mradi kwa pamoja na Elsewedy Electric, inaeleza kuwa bwawa kuu lina urefu wa mita 1,025, kimo cha mita 131 na hifadhi ya takriban mita za ujazo bilioni 34 za maji.
Mradi huo ulijengwa katika eneo la Stiegler's Gorge kwenye Mto Rufiji.
Kwa mujibu wa TANESCO, Julius Nyerere inalenga si kuzalisha umeme pekee, bali pia kuchangia katika udhibiti wa mafuriko na matumizi ya rasilimali za maji katika Bonde la Rufiji.
Kwa uwezo wa kuzalisha umeme, Julius Nyerere iko karibu sana na Kariba.
Lakini tofauti ya MW15 tu kati ya miradi hiyo miwili inaonyesha kwamba nafasi ya Julius Nyerere katika orodha ya miradi mikubwa ya umeme wa maji Afrika ni ya juu.
4. Bwawa Kuu la Aswan – Misri - MW2,100
Uwezo wa kuzalisha umeme: MW2,100
Kwenye Mto Nile nchini Misri kuna Bwawa Kuu la Aswan, moja ya miradi mashuhuri zaidi ya maji barani Afrika.
Serikali ya Misri inasema kituo cha umeme cha Bwawa Kuu la Aswan kilikuwa na uwezo wa MW2,100. Mwaka 2025, Wizara ya Umeme ya Misri ilitangaza mpango wa kukarabati na kuboresha mitambo ili kuongeza uwezo wa kituo hicho kutoka MW2,100 hadi MW2,400.
Kwa hiyo, kwa uwezo wake uliopo wa kuzalisha umeme, Julius Nyerere (JNHPP), liko juu kwa MW15.
Bwawa Kuu la Aswan lilianza kujengwa mwaka 1960, na mradi ulikamilika katika miaka ya 1960; Serikali ya Misri inaeleza kuwa uzalishaji wa umeme ulianza mwaka 1967 na uzinduzi rasmi wa bwawa ukafanyika mwaka 1971.
Kwa upande wa maji, Serikali ya Misri inaeleza kuwa hifadhi ya maji inayoundwa nyuma ya bwawa ina uwezo wa mita za ujazo bilioni 169 katika kiwango cha juu cha kuhifadhi.
Hifadhi hiyo ndiyo Ziwa Nasser, ambalo lina jukumu muhimu katika kuhifadhi maji ya Nile, kudhibiti mafuriko na kusaidia upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali nchini Misri.
Hivyo, kwa uwezo wa kuzalisha umeme, Julius Nyerere na Aswan ziko karibu sana; lakini kwa kiasi cha maji kinachohifadhiwa, tofauti ni kubwa.
5. Cahora Bassa – Msumbiji - MW2,075
Uwezo wa kuzalisha umeme: MW2,075
Kwenye Mto Zambezi nchini Msumbiji kuna Cahora Bassa, mojawapo ya vituo vikubwa vya umeme kwa maji kusini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa Hidroeléctrica de Cahora Bassa, kampuni inayomiliki na kuendesha mradi huo, kituo kina uwezo uliowekwa wa MW2,075.
Hiyo inauweka mradi wa Cahora Bassa MW40 kuwa chini ya mradi wa Julius Nyerere.
Cahora Bassa ilianza kujengwa mwaka 1969 na kampuni hiyo iliundwa mwaka 1975. Mradi huo umekuwa sehemu muhimu ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme wa Msumbiji na ukanda wa kusini mwa Afrika.
Kwa hiyo, kwa uwezo wa kuzalisha umeme, Cahora Bassa iko katika kiwango kinachokaribiana sana na Julius Nyerere.