Marekani inapoteza ushawishi Mashariki ya Kati?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Katika makala iliyochapishwa katika jarida la Foreign Affairs yenye kichwa cha habari "Mwisho wa Marekani Mashariki ya Kati," ya mwandishi Mark Lynch, anaamini kwamba nguvu zinazoongozwa na Marekani katika Mashariki ya Kati, tangu Vita vya Ghuba vya 1991, zimeisha kwa njia ile ile kama nguvu za Ulaya zilivyokwisha, akihusisha hili na mzozo kati ya Marekani na Israeli kwa upande mmoja na Iran kwa upande mwingine.

Anasema "kushindwa kwa Marekani kuwalinda washirika wake wa Ghuba kumetia dosari ufanisi wa kambi zake za kijeshi katika eneo hilo," na "kukataa kwa Israel kufikia makubaliano na Wapalestina kumemaliza nguvu za Marekani katika juhudi za kurekebisha uhusiano kati ya Waarabu na Waisraeli."

Lynch anaamini "wapangaji wa vita kati ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran walitia chumvi kile ambacho vikosi vya kijeshi vingeweza kufikia, walipuuza uwezo wa adui wao katika kuzuia vikosi hivyo, na kwa ukatili wamepuuza maisha ya watu wa kawaida," akibainisha kuwa vita hivyo vinaonyesha "kasoro katika mkakati wa Washington wa Mashariki ya Kati."

Mwandishi anatoa mtazamo wake kuhusu mwisho wa nguvu za Marekani katika Mashariki ya Kati kwa kukumbuka Mgogoro wa Suez wa 1956, ambao ulimaliza ushawishi wa Uingereza na Ufaransa katika eneo hilo.

Anasema kuna kufanana kati ya janga la leo la Marekani na mpango ulioshindwa wa Uingereza, Ufaransa na Israeli katika kuukamata Mfereji wa Suez.

Lynch anatabiri mgogoro wa muda mrefu katika miaka ijayo, akiamini kwamba "Israeli na Iran kwa sasa zina lengo moja la kuiweka Mashariki ya Kati katika hali ya machafuko na vurugu."

Kulingana na mwandishi, mchakato wa amani kati ya Waarabu na Israeli unaoongozwa na Marekani umesababisha mgawanyiko katika eneo hilo katika kambi mbili: ya kwanza, inayojumuisha washirika wa Marekani, na ya pili, inayojumuisha Iran na makundi yake katika eneo hilo.

Kuna fursa

Kwa upande mwingine, mwandishi anaona fursa kwa Washington kujenga nguvu mpya na bora zaidi ikiwa itaacha sera yake ya "kuwaunga mkono madikteta, kuwapa kinga washirika wake, na kudhibiti makundi hasimu kupitia nguvu za kijeshi," na anatabiri kwamba hatua hii "hatimaye itasababisha utulivu wa kudumu ambao Washington inadai kuutafuta kwa muda mrefu."

Anasema hata kama mfumo wa sasa wa Marekani umepata mafanikio ya kimkakati, iwe kwa kuleta kiwango fulani cha utulivu au kwa kulinda maslahi ya Marekani, lakini umeundwa kufadhili tawala za kidikteta, ambazo zinakandamiza demokrasia na kukuza ufisadi, kubinafsisha mali za umma, kufuatilia watu, na kukandamiza wapinzani."

Anasema kuanzisha sera mpya na imara kuelekea Mashariki ya Kati kunahitaji "kuondokana na uingiliaji kati wa kijeshi kama hatua ya kwanza na kujenga upya kambi za kijeshi za Marekani, kwa kuzingatia ulinzi dhidi ya makombora na kupeana taarifa za kijasusi, huku ikiiweka Iran katika usalama wa kikanda kama mshirika hai."

Anongeza kuwa kujenga utaratibu mpya pia kunahitaji "mapitio ya uhusiano wa Marekani na Israeli, shinikizo kwa Israeli kuheshimu haki za binadamu, kusimamisha upanuzi wake wa taratibu katika Ukingo wa Magharibi, na kukomesha kwa uingiliaji kati wake unaovuruga utulivu nchini Lebanon na Syria."

Kwa kumalizia, mwandishi anaitaka Marekani kuhimiza mageuzi ya kisiasa katika nchi za eneo hilo, badala ya kutegemea "tawala za kimabavu," hata kama hatua kama hiyo inaweza kusababisha matatizo zaidi kwa Marekani kwa muda mfupi.