Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Tume yaanza kuwasaka wapangaji wa ghasia za Uchaguzi Tanzania

Kwa mujibu wa Jaji Lila, Tume itachunguza madai ya watu kupata majeraha makubwa kutokana na matumizi ya silaha za moto kinyume na sheria, taratibu na miongozo iliyopo

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Tume yaanza kuwasaka wapangaji wa ghasia za Uchaguzi Tanzania

    Tume iliyoundwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuchunguza wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa sheria wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, imeanza rasmi kazi yake.

    Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, amesema Tume inalenga kubaini wahusika wa ghasia hizo, namna walivyohusika pamoja na waliohusika kusababisha vifo, majeraha na watu kupotea wakati na baada ya uchaguzi.

    Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ulifanyika tarehe 29 Oktoba 2025, lakini katika baadhi ya maeneo kuliripotiwa ghasia na matumizi ya nguvu yaliyosababisha vifo, majeraha na uharibifu wa mali.

    Tume hiyo mpya imeundwa kufuatia mapendekezo ya Tume ya awali iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande, ambayo ilichunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi.

    Kuchunguza matumizi ya silaha

    Kwa mujibu wa Jaji Lila, Tume itachunguza madai ya watu kupata majeraha makubwa kutokana na matumizi ya silaha za moto kinyume na sheria, taratibu na miongozo iliyopo.

    Pia itachunguza madai ya watu kupigwa risasi nje ya maeneo ya ghasia, pamoja na taarifa za watu waliopotea wakati na baada ya uchaguzi.

    Tume pia imepewa jukumu la kuchunguza iwapo nguvu iliyotumika kudhibiti ghasia ilikuwa imezidi kiwango kinachoruhusiwa kisheria.

    Miongoni mwa masuala mengine yatakayochunguzwa ni vifo visivyo vya kawaida vya watoto na watu wa makundi maalum vilivyotokana na hatua za kudhibiti ghasia.

    Wahusika wa ghasia

    Tume inatarajiwa kuchunguza ushiriki wa waliopanga, waliofadhili, walioratibu au kutekeleza ghasia hizo.

    Kwa mujibu wa hadidu rejea zake, Tume pia inaweza kuchunguza jambo jingine lolote itakaloona ni muhimu na linaloendana na majukumu yake.

    Uchunguzi utafanywa kwa kutumia ushahidi wa moja kwa moja, nyaraka pamoja na taarifa zitakazopatikana wakati wa kutembelea maeneo yaliyokumbwa na matukio hayo.

    Tume imesema itazingatia pia haki ya kusikilizwa kwa wale wote ambao wanaweza kuguswa na taarifa zitakazowasilishwa wakati wa uchunguzi.

    Tume ina siku 150

    Tume hiyo ina makamishna sita na inaongozwa na Jaji Mstaafu Shaban Ally Lila. Makamishna wengine ni Jaji Petrus Tileinge Damaseb wa Namibia, Jaji Barishaki Bonny Cheborion wa Uganda, pamoja na Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishiel Nelson Sumari.

    Katibu wa Tume ni Paul Kadushi.

    Tume imepewa siku 150 tangu kuzinduliwa kwake kukamilisha uchunguzi na kuwasilisha taarifa yake.

    Mwenyekiti wa Tume ametoa wito kwa wananchi, waandishi wa habari na mtu yeyote mwenye taarifa zinazohusiana na hadidu rejea za Tume kuwasilisha taarifa hizo ili kusaidia uchunguzi.

    Soma pia:

  2. Watu wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kuwapa sumu tembo Kenya

    Maafisa nchini Kenya wanasema kuwa watu wanne wamekamatwa kama sehemu ya uchunguzi kuhusu mfululizo wa vifo vya kutatanisha vya tembo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

    Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) limeiambia BBC kuwa Wakenya watatu na raia mmoja wa Tanzania wanashikiliwa kwa tuhuma za kuwatilia sumu tembo 18 katika Hifadhi ya Taifa ya Amboseli.

    Uchunguzi unatathmini iki tembo hao walikufa kutokana na sumu ya 'cyanide' baada ya kula kiasi kikubwa cha nyanya zilizonyunyiziwa dawa haramu za kuua wadudu.

    Vipimo vya awali vya maabara vimebaini kuwepo kwa chembechembe za 'cyanide' katika sampuli za mabaki ya chakula yaliyochukuliwa kutoka kwenye matumbo ya tembo hao.

    Tembo wote walioathirika - hasa majike na ndama wao - pia walionyesha dalili za kupooza, jambo ambalo mamlaka zinaamini kuwa ni ishara nyingine ya sumu ya 'cyanide'.

    Mashamba ya nyanya yanapatikana katika eneo la Kimana, ambalo ni sehemu ya njia ya wanyama inayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Amboseli na Hifadhi ya Taifa ya Tsavo kusini mwa Kenya.

    Hili ni eneo kubwa linalojulikana kama mfumo wa ikolojia wa Amboseli, linalopakana na Tanzania, ambapo zaidi ya tembo 2,000 huzunguka wakitafuta malisho na maji.

    Dawa za kuua wadudu ambazo ni marufuku nchini Kenya wakati mwingine huingizwa kimagendo kupitia mpaka huo ulio wazi na Tanzania na kutumika katika mashamba ya eneo la Amboseli, ambapo tembo huishi karibu na makazi ya watu na wakatiti mwingine huvamia mashamba wakitafuta malisho.

  3. Polisi wazingira Mahakama Zambia muda wa mwisho kuwasilisha pingamizi la uchaguzi ukikaribia

    Majengo ya mahakama katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka, na maeneo mengine yamefungwa huku muda wa mwisho wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa urais ukikaribia.

    Polisi wanashirika doria huku baadhi ya mahakama zikizingirwa kwa utepe ili kuzuia watu kuingia.

    Mgombea wa upinzani Brian Mundubile amesema atapinga matokeo ya uchaguzi huo, akitaja kasoro mbalimbali, baada ya kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 38 ya kura.

    Rais aliyeko madarakani, Hakainde Hichilema, alishinda muhula wa pili kwa kupata asilimia 60 ya kura.

    Mundubile anajificha kutokana na madai ya vitisho dhidi yake, katika kipindi hiki cha baada ya uchaguzi kilichogubikwa na utata, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa kiongozi wa upinzani na kukamatwa kwa watu wengine.

    Leo Jumatatu ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais.

    Pingizi hilo linaweza kuathiri sherehe za kuapishwa kwa Hichilema, ambazo zimepangwa kufanyika tarehe 1 Septemba.

    Siku ya Jumatatu, mawakili waliofika mahakamani waliambiwa waondoke.

    Wakili mmoja aliambia BBC kuwa watu watatu wenye silaha walimfuata kwenye gari lake, wakajitambulisha, na kumwagiza aondoke eneo hilo.

    Mahakama zilizofungwa ni pamoja na Mahakama Kuu jijini Lusaka, Mahakama ya Juu (ambayo pia ina Mahakama ya Katiba), na mahakama kadhaa za ngazi ya chini.

    Maelezo zaidi:

  4. Mzozo wa Iran: Juhudi za kidiplomasia zaongezeka

    Kamanda wa Jeshi la Pakistan Asim Munir, amewasili jijini Tehran.

    Katika taarifa, idara ya uhusiano wa umma ya jeshi la Pakistan imelezea ziara hiyo kuwa sehemu ya juhudi za Pakistan "kukuza amani na utulivu katika eneo mashariki ya kati na kutatua migogoro unaoendelea kwa njia ya amani."

    Taarifa hiyo ilisema: "Asim Munir atakutana na viongozi wakuu wa Iran wakati wa ziara yake nchini humo ili kuendeleza juhudi zinazoendelea za kufikia suluhisho lla amani kwa migogoro inayoendelea Mashariki ya Kati."

    Hii ni safari ya nne ya Asim Munir anazuru Tehran katika kipindi cha chini ya miezi sita.

    Shirika rasmi la habari la Iran, IRNA, limeandika: "Msururu wa safari nne za Asim Munir mjini Tehran unaonyesha wazi kuwa njia ya kidiplomasia kati ya Iran na Marekani, licha ya panda shuka za mara kwa mara, juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mzozo huu zinaendelea kupitia mkondo wa Pakistan."

    IRNA pia iliangazia msimamo wa kidiplomasia wa serikali ya Iran: ''Katika hatua ya kwanza, Iran inataka Marekani izingatie ahadi ilizotia saini katika Hati ya Makubaliano ya Islamabad ambayo haikutekeleza.''

    Soma pia:

  5. Uturuki yaagiza kukamatwa kwa Netanyahu kufuatia shambulio la Fotilla

    Uturuki imesema itaomba Interpol kutoa ilani nyekundu ya kimataifa ya kumtafuta na kumkamata Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika kesi inayohusiana na shambulio dhidi ya wanaharakati waliokuwa wakijaribu kupeleka misaada ya kibinadamu Gaza.

    Waziri wa Sheria wa Uturuki, Akin Gurlek, amesema hati za kukamatwa zimetolewa dhidi ya Netanyahu na mshukiwa mwingine kwa tuhuma zikiwemo mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mateso.

    Kesi hiyo inawahusisha watu 35 kufuatia hatua ya Israel kuingilia boti za Global Sea Flotilla katika maji ya kimataifa, ambazo zilikuwa zikielekea Gaza kupeleka misaada.

    Uturuki ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa operesheni za kijeshi za Israel Gaza na imekuwa ikitaka hatua za kimataifa zichukuliwe dhidi ya Israel. Israel inakanusha tuhuma za ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.

  6. Maafisa wa kijeshi wa Uganda na Burundi wazuru Israel kujadili kupeleka wanajeshi Gaza

    Maafisa wa kijeshi kutoka Uganda na Burundi walizuru Israel wiki iliyopita kujadili uwezekano wa kupeleka wanajeshi Gaza, kama sehemu ya kikosi cha kimataifa cha usalama kinachopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump.

    Kwa mujibu wa maafisa, mazungumzo hayo yalihusu mpango wa kikosi hicho kinacholenga kusaidia kudumisha usitishaji mapigano dhaifu uliopo Gaza.

    Afisa mmoja wa Bodi ya Amani, mpango unaohusishwa na Trump, amesema maafisa wa Uganda walijiunga na ujumbe wa kijeshi kutoka Burundi.

    Amesema Uganda inakamilisha mipango ya kushiriki baada ya Bunge la nchi hiyo kuidhinisha mwezi huu mchango wa wanajeshi katika kikosi hicho.

    Kwa upande wa Burundi, bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa, ingawa afisa huyo amesema nchi hiyo imeonyesha nia ya kuanza mchakato wa kushiriki.

    Afisa mmoja wa kijeshi wa Burundi pia amethibitisha kuwa maafisa wakuu watatu wa kijeshi waliongoza ujumbe huo nchini Israel, akisema Burundi inaonekana kuwa tayari kujiunga na mpango huo.

    Hata hivyo, bado haijafahamika Burundi zitatoa wanajeshi wangapi, wala itapata nini kwa kushiriki katika mpango huo.

    “Tumeshirikishana uzoefu na maarifa muhimu, na wawakilishi wa Burundi wameonyesha nia ya kushiriki katika mpango wetu,” alisema afisa huyo wa Israel.

    Iwapo Burundi itaendelea na mpango huo, nchi hiyo itakuwa miongoni mwa mataifa ya Afrika kujiunga na kikosi cha kimataifa cha Gaza, baada ya Morocco, Kosovo, Kazakhstan na Albania kutoa ahadi za kushiriki.

    Uganda imeahidi kutuma takribani wanajeshi 1,200, huku Morocco ikiahidi hadi 500. Kosovo, Kazakhstan na Albania kwa pamoja zimeahidi kutuma takribani wanajeshi 80.

    Soma Zaidi:

  7. Papa Leo atoa wito wa kimataifa kukabili Ebola DRC

    Papa Leo XIV ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kudhibiti mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,DRC.

    “Naishauri Jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zinazowahusisha pia jamii za wenyeji katika juhudi za kuzuia Ebola, ili kuokoa maisha ya watu wengi,” alisema Papa.

    Haya yanajiri baada ya Ebola kutajwa kuwa janga mbaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya DRC.

    Mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, umefikia maambukizi 5,515 yaliyothibitishwa na kusababisha vifo vya watu 2,642.

    Kwa mujibu wa takwimu za serikali, visa vipya 51 vimeripotiwa katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini.

    Mlipuko huo, uliotangazwa katikati ya Mei, ni wa 17 wa Ebola nchini humo na umetangazwa na Shirika la Afya Duniani, WHO, kuwa dharura ya afya ya umma yenye umuhimu wa kimataifa. Tahadhari hiyo pia inahusisha Uganda jirani.

    Kwa mujibu wa serikali, kiwango cha vifo miongoni mwa walioambukizwa kimeongezeka kutoka takribani asilimia 20 mwanzoni mwa Juni hadi karibu asilimia 48 sasa, ikimaanisha kuwa karibu mtu mmoja kati ya wawili walioambukizwa wamefariki dunia.

    Soma Zaidi:

  8. Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC akosoa madai ya kuilenga Afrika

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka kutoka kwa baadhi ya nchi, hususan barani Afrika.

    Katika mazingira hayo, Naibu Mwendesha Mashtaka wa ICC, Msenegali Mame Mandiaye Niang, amekuwa Dakar kama sehemu ya ziara yake katika nchi wanachama wa Mkataba wa Roma. Lengo lake ni kueleza jukumu la mahakama hiyo na kujibu shutuma zinazoikabili.

    Akizungumza na BBC News Africa, Niang amekanusha madai kwamba ICC inalenga Afrika, akisema mahakama hiyo imeanzisha uchunguzi kadhaa barani humo kwa ombi la nchi zinazohusika.

    Amesema ICC inazingatia kanuni ya ukamilishano, ambapo mahakama ya kimataifa huingilia pale mifumo ya kitaifa inaposhindwa au kutokuwa tayari kushughulikia uhalifu mkubwa.

    Niang pia amekataa tuhuma kwamba ICC inaingilia mamlaka ya nchi, akisisitiza kuwa waathiriwa wa ukatili barani Afrika bado wanahitaji haki.

    “Bado kuna watu wanaoteseka, kuna waathiriwa wengi. Na kama hatuwezi kuwarudishia kila kitu walichopoteza, basi angalau tunapaswa kuwapatia haki kwa kiasi fulani'', anasema Mame Mandiaye.

    Kuhusu baadhi ya nchi za Afrika, zikiwemo wanachama wa Muungano wa Nchi za Sahel, AES, kutangaza kujiondoa ICC, Niang amesema ni jambo la kusikitisha kuona kutokuelewana kuhusu jukumu la mahakama hiyo.

    Amesema licha ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya baadhi ya maafisa wa ICC, mahakama hiyo haitarudi nyuma katika kutekeleza majukumu yake.

    “Ni vikwazo tunavyovijutia, lakini havitatufanya turudi nyuma,” amesema Niang.

    Soma Zaidi:

  9. Watu 30 wamefariki dunia baada ya dampo la taka kuporomoka Guinea

    Takribani watu 30 wamefariki dunia baada ya mlima wa taka kuporomoka na kuangukia nyumba zilizokuwa karibu katika mji mkuu wa Guinea, Conakry, kufuatia mvua kubwa.

    Watu wengine 22 wamejeruhiwa, huku sita kati yao wakiwa katika hali mbaya.

    Tukio hilo lilitokea majira ya saa nane usiku katika eneo la Dar es Salaam jijini Conakry. Serikali ya Guinea imesema dampo hilo liliporomoka ghafla baada ya mvua kubwa, huku ikihofiwa kuwa watu kadhaa wamekwama chini ya vifusi.

    Serikali imetuma idadi kubwa ya vikosi vya usalama, ikiwemo jeshi, kushiriki katika shughuli za uokoaji.

    Akizungumza na vyombo vya habari vya ndani, mwanamke mmoja amesema watoto wake watano wamefariki katika tukio hilo.

    Mamlaka zinaendelea na shughuli za uokoaji, huku zikihofia kuwa watu zaidi huenda wamefunikwa na vifusi na hivyo idadi ya vifo ikaongezeka.

    Waziri Mkuu wa Guinea, Amadou Ouari Ba, ametembelea eneo la tukio na kutathmini hali ilivyo.

    Awali, kiongozi wa eneo hilo, Lansine Sila, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kulikuwa na hofu ya idadi kubwa ya waathiriwa. Amesema hadi wakati huo miili 18 ilikuwa imepatikana na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Waziri Mkuu wa Uingereza aanza ziara yake ya kwanza nje ya nchi

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, anatarajiwa kuzuru Kyiv Jumatatu ya tarehe 24 Agosti 2026, katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipokuwa Waziri Mkuu.

    Burnham anatarajiwa kuonyesha mshikamano wa Uingereza na Ukraine, huku akishiriki pia katika maadhimisho ya miaka 35 tangu Ukraine ilipopata uhuru.

    Pia ataongoza kwa mara ya kwanza mkutano wa Coalition of the Willing, muungano ulioanzishwa na Uingereza na Ufaransa chini ya Waziri Mkuu wa zamani, Keir Starmer.

    Burnham pia atapokea tuzo kwa niaba ya wananchi wa Uingereza, ikiwa ni kutambua mchango wa Uingereza katika kuiunga mkono Ukraine, kabla ya kushiriki katika sherehe za Siku ya Uhuru.

    Ziara hiyo inafanyika wakati mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yakiongezeka. Ijumaa, shambulio katika kituo cha ununuzi liliripotiwa kuua watu wasiopungua 16.

    Burnham amesema Ukraine ina uhakika na uungwaji mkono wa Uingereza.

    Wakati huo huo, Moscow imeionya Uingereza kuhusu "madhara" yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya ndege zisizo na rubani zinazotolewa na Uingereza kwa Ukraine, ambazo Kyiv imekuwa ikitumia kushambulia miundombinu ya Urusi.

  11. Tangazo la Marekani la mashambulizi ya kiuchumi ni kukiri kushindwa kijeshi - Iran

    Brigedia Jenerali Hossein Mohebibi, msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, amesema kauli za Marekani kuhusu mashambulizi ya kiuchumi ni sawa na kukiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa imepata pigo kubwa katika vita vya kijeshi.

    Akizungumza na waandishi wa habari katika mkoa wa Alborz kaskazini mwa Iran, Mohebibi amesema kama Marekani na washirika wake wangekuwa wamefanikiwa kijeshi, kusingekuwa na haja ya kuzungumzia hatua hizo za kiuchumi.

    Amesema majeshi yanayoichukia Iran yamelazimika kwa kiasi kikubwa kuondoa meli zao katika eneo hilo, huku juhudi za kufungua Mlango wa Hormuz na kudhoofisha uwezo wa Iran wa kujilinda zikishindwa.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, IRNA, msemaji huyo amezitaka vyombo vya habari nchini humo kuwaelimisha wananchi kuhusu uhalisia wa vita na pande zinazohusika, kwa kutoa taarifa sahihi.

    Amesema vyombo vya habari havipaswi kuruhusu upande ulioshindwa kwenye vita vya kijeshi kujijenga mbele ya umma kama mshindi.

    Soma pia:

  12. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 24 Agosti 2026.