Nani anafadhili magenge ya wahuni kuchochea ghasia za kisiasa Kenya?

    • Author, Na Laillah Mohammed
    • Akiripoti kutoka, BBC Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Tume ya uwiano na maridhiano ya kitaifa (NCIC) nchini Kenya, imemuomba mbunge wa Homa Bay Town, Peter Kaluma kufika mbele yake Jumatano Agosti 19, 2026 kuhusu kauli alizozitoa kwa lugha ya Dholuo, moja ya kabila katika eneo hilo mnamo Agosti 15, mwaka huu.

Kauli hizo zimeibua mjadala kuhusu nafasi ya wanasiasa katika kuchochea mvutano wa kisiasa, baada ya ghasia kuzuka mjini Homa Bay saa chache baadaye.

Katika mkutano wa kisiasa uliofanyika tarehe 16 Agosti mwaka huu, Mbunge Peter Kaluma alitoa agizo kwa wafuasi wake dhidi ya watu wanaozungumzia suala la Rais aliye madarakani ahudumu muhula mmoja pekee, pamoja na wale aliowatuhumu kufanya kazi na upande mwingine wa kisiasa akimaanisha upande wa upinzani.

"Kuanzia leo tunatoa agizo kwamba yeyote anayezungumzia 'Muhula Mmoja' (One Term), shughulikeni naye. Yeyote aliyefanya kazi na upande ule mwingine, hata kama alikuwa dereva na anahisi hawezi kushirikiana nasi, lazima aondoke mara moja. Tutafanya ukaguzi katika hoteli na nyumba zote walizokuwa wameziwekea nafasi, mwenye hoteli yeyote Homa Bay lazima atupe taarifa za wageni wake wote, kwani tutawashughulikia watu hao na huenda tukachukua hatua dhidi ya hoteli hiyo pia. Nimelipia mafuta mtakayotumia kuzunguka Homa Bay na Rodi. Hii ni ngome ya ODM na tunasisitiza kuwa Ruto anastahili mihula miwili. Mtu yeyote akizungumzia 'Muhula Mmoja,' shughulikeni naye," alisema Kaluma.

Saa chache baada ya kauli hizo, baadhi ya hoteli mjini Homa Bay zilivamiwa na makundi ya vijana waliodai taarifa kuhusu wageni waliokuwa wamefikia katika hoteli hizo.

Mali iliharibiwa na madirisha ya baadhi ya hoteli yakavunjwa, wakati kundi la kisiasa la Linda Mwananchi lilitarajiwa kufanya mkutano wa hadhara mjini Homa Bay.

NCIC imesema inachunguza mazingira ya kauli hizo na imechukua hatua ya kumwita Kaluma mbele ya tume.

Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika katika kituo kimoja cha televisheni nchini Kenya, Kamishena wa tume ya NCIC Danvas Makori amesema jukumu la tume hiyo ni kutoa taarifa muhimu kwa vyombo vya usalama kuhusu watu wanaoshukiwa kuchochea ghasia.

Makori amesema kauli na hatua za Kaluma zinapaswa kuchunguzwa kama suala la jinai.

"Jukumu letu kama tume ni kutoa taarifa muhimu kwa vyombo vya usalama kama DCI na kuwapa nguvu ya kuwachunguza wanaochochea ghasia. Lakini ni muhimu sote tuelewe kama Wakenya kwamba kuna tofauti kubwa hapa. Alichokisema na kukitenda Mbunge wa Homa Bay Town, Kaluma, sio hata matamshi ya uchochezi, hilo ni kosa la jinai na linapaswa kuchunguzwa na kitengo cha polisi cha DCI mara moja."

Uchunguzi wa uhalifu siasani

Kwa upande wake, msemaji wa Huduma ya Polisi nchini Kenya, Michael Muchiri, amesema watu wawili wamethibitishwa kufariki dunia katika ghasia zilizotokea Homa Bay kati ya Jumamosi na Jumapili iliyopita.

Polisi pia wanawashikilia takriban watu 37 waliokamatwa katika kaunti za Kisumu na Homa Bay.

Kwa mujibu wa Muchiri, washukiwa hao walikamatwa wakiwa na silaha na vifaa mbalimbali, vikiwemo vyuma, vifaa butu, mapanga, kamba, visu, marungu, mipini ya majembe na tochi.

"Watu hao walikamatwa wakiwa na silaha mbalimbali kama vyuma, vifaa butu, mapanga, kamba, visu, rungu, mipini ya majembe na matochi. Washukiwa hao wamefikishwa mahakamani huku uchunguzi zaidi ukiendelea," amesema Muchiri.

Kwa nini mikutano ya kisiasa hugeuka uwanja wa vita?

Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya usalama Hassan Khannenje, matumizi ya vijana katika vurugu za kisiasa ni jambo ambalo limewahi kushuhudiwa nchini Kenya, huku baadhi yao wakitumiwa na wanasiasa kutekeleza vitendo vya vurugu dhidi ya wapinzani wao.

Anasema tatizo linazidi kuwa kubwa pale ambapo wale wanaopanga au kufadhili makundi hayo hawachukuliwi hatua, hali inayoweza kuwapa nafasi ya kuendelea kutumia vijana katika migogoro ya kisiasa.

"Makundi ya kihalifu yaliyotumiwa na wanasiasa yalibadilika baadaye na kuwa tatizo kubwa kwa wale waliokuwa wakiyafadhili na hata kwa taifa zima. Mfano mkubwa ni Janjaweed, ambalo ni kundi linalokabiliana vikali na majeshi ya Sudan katika harakati za kutwaa udhibiti wa nchi hiyo," aliiambia BBC Swahili.

Khannenje anaonya kuwa Kenya imewahi kuona madhara ya kushindwa kudhibiti mapema makundi yanayotumiwa katika vurugu za kisiasa. Anarejelea ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, akisema kutokuchukuliwa hatua mapema na vyombo vya usalama kulichangia kuongezeka kwa vurugu na madhara yaliyofuata. Ripoti za kimataifa pia zimeonyesha kuwa ghasia hizo zilihusisha makundi yaliyotumiwa kisiasa pamoja na mapungufu katika taasisi za usalama na haki.

Nani anapaswa kukabiliana na matamshi ya uchochezi Kenya?

Wanasiasa kutumia maneno makali majukwaani imekuwa ni jambo linalotajwa na wachambuzi kuwa limezidi.

Mbunge wa Mukurweini, John Kaguchia, anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi mahakamani baada ya kukamatwa na maafisa wa DCI mapema mwezi Agosti.

Kaguchia anadaiwa kutoa kauli kali akiwaambia wakazi wa Kieni, Kaunti ya Nyeri, kuhusu watu wanaomuunga mkono Rais William Ruto, ambaye alimtaja kwa jina la utani la 'Kasongo'.

"Kama huko Kieni tutapata hata kura moja kwa ajili ya Kasongo au wafuasi wake, nawaombeni sana, tutawafuatilia na kuwatoa huko mlikojificha chini ya vitanda vyenu. Hii ni kwa sababu ni lazima tuwe na rekodi ya wale wanaomuunga mkono mtu huyo. Hatuwezi kukubali kumuunga mkono baada ya yale aliyomfanyia Rigathi na mambo yote aliyotutendea, ikiwemo kuua watoto wetu. Ukimuunga mkono Kasongo, basi tukisema kweli, ukifiwa hatutaomboleza nawe, na kama una sherehe ya mahari hatutapokea mbuzi hao; utawapeleka ***."

Kaguchia amekana shtaka la uchochezi na kesi yake inaendelea mahakamani.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Barack Muluka, anasema serikali inapaswa kuchukua hatua dhidi ya matamshi ya aina hiyo bila kuonekana kuchagua kesi za kushughulikia.

"Serikali inapaswa kuonekana ikikabiliana na uhalifu wa aina hii bila ya kuchagua ni kesi ipi ya kufikisha mahakamani na ipi ya kuwataka washukiwa kufika tu katika ofisi za tume ya NCIC", anasema Muluka.

Kisheria, NCIC ina jukumu la kushughulikia masuala yanayohusu uwiano wa kitaifa na matamshi ya uchochezi, lakini haina mamlaka ya kuwafungulia washukiwa mashtaka ya jinai.

Mamlaka ya kuwakamata washukiwa na kuwafungulia mashtaka iko kwa vyombo vya usalama na waendesha mashtaka.

Baadhi ya Wakenya wameelezea wasiwasi kuhusu mwenendo wa matamshi ya kisiasa nchini, wakisema serikali inaonekana kutoa maonyo mara kwa mara bila kuchukua hatua kali dhidi ya wanaovuka mipaka kupitia semi zao.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, amekuwa akizungumzia mara kwa mara suala la uchochezi wa kisiasa na kuwaonya wanasiasa dhidi ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi.

Je, polisi wameshindwa kudhibiti hali hii?

Tangu mwanzoni mwa mwaka 2026, zaidi ya visa kumi vya ghasia vinavyodaiwa kuhusisha makundi ya wahuni vimeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya.

Kabla ya ghasia za hivi karibuni katika Kaunti ya Homa Bay, ambapo baadhi ya wanachama wa msafara wa kundi la kisiasa la Linda Mwananchi walisema walipata hasara baada ya magari yao kuharibiwa na mali kuporwa, kisa kingine kiliripotiwa siku chache mapema katika Kaunti ya Nakuru.

Msafara wa aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ulikuwa ukiondoka eneo bunge la Molo kuelekea Rongai wakati makundi ya vijana yalipoushambulia kwa mawe.

Gachagua hakujeruhiwa katika shambulizi hilo, lakini magari kadhaa yaliharibiwa vibaya, huku watu kadhaa wakipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kupata majeraha.

Akizungumza alipofika Rongai, Gachagua alilaani shambulizi hilo na kudai kuwa anawafahamu watu wanaofadhili makundi hayo ya vijana.

Aliwataka Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, Katibu wa Wizara hiyo, Raymond Omollo, na Inspekta Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, kujiuzulu akidai wameshindwa kudhibiti makundi hayo.

Hata hivyo, Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amekanusha madai ya uzembe katika utekelezaji wa majukumu yake, akisema nchi iko salama.

Kanja amesema madai ya kuwepo kwa "taharuki nchini kutokana na ukosefu wa usalama" yanaweza kuwa juhudi za watu wanaotaka "kuwasha moto pasipo na moshi".

Vijana hawa ni kina nani?

Madai kwamba baadhi ya vijana wanalipwa ili kushiriki katika vurugu bado yanahitaji uchunguzi na ushahidi, huku polisi wakiendelea na uchunguzi kuhusu waliohusika na ghasia za Homa Bay.

Kwa yaliyotokea hivi punde, polisi wamesema wanamtafuta Oliver Jaoko, anayefahamika kama Olivetti, ambaye wanamtaja kama mmoja wa washukiwa wanaodaiwa kuhusika katika ghasia za Homabay.

Hadi sasa, polisi hawajaeleza hadharani ni nani anayefadhili makundi hayo au ikiwa kuna wanasiasa waliohusika moja kwa moja katika kuyaandaa.

Inadaiwa kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakiahidiwa au kulipwa kiasi kidogo cha fedha, ikiwemo takriban shilingi 500 za Kenya, ili kushiriki katika vitendo vya vurugu, hali inayozua wasiwasi kuhusu unyonyaji wa changamoto za kiuchumi za vijana kwa maslahi ya kisiasa.

Katika hatua ya kuzuia vurugu zaidi, polisi wamewataka wanasiasa kupanga mikutano yao kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa kumi na mbili jioni.

Lakini kabla ya mapambazuko ya Jumapili, Agosti 16, barabara kuu zinazoingia katika Kaunti ya Homa Bay zilifungwa na makundi ya vijana waliowasha moto na kuweka mawe barabarani.

Hatua hiyo ililenga kuzuia msafara wa Linda Mwananchi, unaoongozwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, kufika mjini Homa Bay.

Ghasia za Homa Bay: Je, ni mwanzo wa changamoto kubwa zaidi ya usalama?

Ghasia zilizotokea Homa Bay wakati wa ziara ya kundi la kisiasa la Linda Mwananchi zimeibua maswali kuhusu uwezo wa vyombo vya usalama kuzuia vurugu za kisiasa kabla hazijatokea.

Polisi wanasema watu 37 wamekamatwa kuhusiana na ghasia hizo, huku uchunguzi ukiendelea dhidi ya washukiwa wengine. Polisi pia wamesema maafisa wao waliathirika katika matukio hayo, huku mmoja akifariki na wengine kujeruhiwa.

Kundi la Linda Mwananchi kwa upande wake limedai kuwa zaidi ya magari 100 katika msafara wake yaliharibiwa na kwamba baadhi ya waandishi wa habari walishambuliwa. Madai hayo bado hayajathibitishwa kwa kujitegemea.

Mchambuzi wa masuala ya usalama, George Musamali, anaonya kuwa iwapo vyombo vya usalama havitachukua hatua madhubuti, ghasia kama hizi zinaweza kuwa ishara ya changamoto kubwa zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

"Inapaswa vitengo vya ujasusi vishirikiane kwa ukaribu na vile vya uchunguzi kuchukua hatua za dharura. Taarifa zinapopatikana kwamba kuna jambo limepangwa, basi linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na wahusika kukamatwa. Kuna wanasiasa wengi wanaotumia vijana na kuwalipa fedha kidogo kwa ajili ya kuleta vurugu, na tunawafahamu. Ni kwa nini hawachukuliwi hatua?" alisema Musamali.

Swali kubwa sasa ni iwapo hatua zinazochukuliwa na vyombo vya usalama zitatosha kuzuia matukio kama haya kujirudia, hasa wakati Kenya ikielekea katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwa wataalamu wa usalama, jibu linaweza kutegemea uwezo wa vyombo vya dola kutambua mapema mipango ya vurugu, kuwachukulia hatua wahusika bila upendeleo na kuhakikisha kuwa haki ya kushiriki katika siasa inalindwa kwa wote.

Imehaririwa na Mariam Mjahid