Jinsi sumu za wanyama zinavyoleta mapinduzi ya tiba duniani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Hatari zinazotokana na sumu za wanyama zimeandikwa kwa kina, lakini sumu hizi hatari pia zinaweza kuokoa maisha.

Daktari Zoltan Takacs, mtaalamu wa sumu za viumbe hai, anasema: "Sumu za wanyama zina molekuli ambazo ni za kipekee duniani, kwa kuwa zimechaguliwa na mchakato wa mageuzi kwa lengo la kuua kiumbe ndani ya chini ya dakika moja."

Sumu za wanyama ni mchanganyiko changamani wa kemikali za kibayolojia zenye molekuli hai zenye nguvu kubwa na zinazolenga mifumo maalumu ya mwili. Molekuli hizo ni pamoja na peptidi, vimeng'enya na misombo midogo ya kikaboni.

Ingawa hapo awali sumu hizi zilihusishwa zaidi na madhara kwa viumbe, sasa zinatambuliwa kama chanzo chenye matumaini cha kutengeneza dawa za kutibu magonjwa mbalimbali. Utafiti kuhusu uwezo wake katika tiba unaangazia namna zinavyofanya kazi, ikiwemo kudhibiti njia za ioni, kulenga vipokezi vya seli na kuzuia utendaji wa vimeng'enya.

Katika makala iliyochapishwa mwaka 2015 katika gazeti la New Zealand Herald, David Warrell, mtaalamu wa tiba za magonjwa ya kitropiki katika Chuo Kikuu cha Oxford, alikadiria kuwa watu 200,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na kuumwa na nyoka.

Utengenezaji wa dawa mpya za kukabiliana na sumu za wanyama bado unakabiliwa na changamoto. Hata hivyo, watafiti wamegundua kuwa sumu hizo zinaweza pia kusaidia kutibu magonjwa mengine, na tayari kuna baadhi ya dawa zilizotengenezwa kutokana na sumu hizo ambazo zinatumika.

Hizi hapa ni aina nne za viumbe ambao sumu zao zinatumika kwa manufaa ya binadamu.

1. Nyoka

Sumu za nyoka zinajumuisha aina nyingi zenye sifa tofauti. Baadhi huua haraka, huku nyingine zikichukua muda kabla ya kuleta madhara.

Nyoka wengi huingiza sumu kupitia meno marefu na makali yanayofanya kazi kwa namna inayofanana na sindano. Jino linapochoma mwili wa mnyama anayeshambuliwa, sumu hupitia ndani ya jino na kuingia moja kwa moja katika mfumo wa damu wa mnyama huyo.

Hata hivyo, kuna nyoka wanaotema sumu, kama vile cobra anayetema sumu wa Msumbiji (Naja mossambica).

Kwa kuwa sumu za nyoka hutofautiana kwa kiasi kikubwa, matumizi yake katika tiba pia hutegemea aina ya nyoka husika. Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ni miongoni mwa maeneo ambayo tayari yanatumia dawa zilizotengenezwa kwa kutumia sumu za nyoka.

"Sumu za nyoka zimetumika kama kielelezo katika utengenezaji wa baadhi ya dawa muhimu zaidi zinazotumika kutibu shinikizo la juu la damu, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri na mshtuko wa moyo," anasema Takacs.

"Chanzo cha kundi la dawa zinazozuia kimeng'enya cha angiotensin-converting enzyme (ACE), ambalo hutumika kutibu shinikizo la juu la damu, ni nyoka aina ya Jararaca pit viper (Bothrops jararaca). Inaweza kusemwa kuwa nyoka huyu ameokoa maisha ya binadamu wengi zaidi kuliko mnyama mwingine yeyote katika historia ya binadamu."

"Inaweza kusemwa kuwa nyoka aina ya Jararaca pit viper ameokoa maisha ya binadamu wengi zaidi kuliko mnyama mwingine yeyote katika historia ya binadamu." ameeleza Dkt Zoltan Takacs, Mtaalamu wa sumu za viumbe hai

2. Komodo

Tezi za sumu za joka la Komodo hufanya kazi tofauti na zile za nyoka. Tofauti na nyoka anayetumia meno yake kuingiza sumu kama sindano, joka la Komodo hutoa sumu inayotiririka.

Sumu hiyo hutoka katika mifuko kadhaa iliyopo kati ya meno yake wakati anapofunga taya na kumng'ata mnyama anayemshambulia.

Sumu hiyo huchanganyika na damu ya mnyama na kuzuia damu kuganda. Hii ndiyo sababu mawindo ya joka la Komodo huendelea kuvuja damu hata baada ya kushambuliwa.

Ingawa sumu hiyo ni hatari kwa wanyama wanaowindwa, uwezo wake wa kuzuia damu kuganda unaweza kuwa na manufaa katika tiba.

Sumu hizo zinaweza kusaidia katika matibabu ya kiharusi, mshtuko wa moyo na kuziba kwa mishipa ya damu ya mapafu, hali ambazo zinaweza kusababishwa na kuganda kwa damu.

3. Nge

Zaidi ya watu milioni 1.2 huumwa na nge kila mwaka, huku takribani watu 3,250 wakifariki dunia kutokana na kuumwa nao, kulingana na utafiti wa mwaka 2008.

Licha ya jina lake linalotisha, nge aina ya Deathstalker (Leiurus quinquestriatus) anaweza kuwa na mchango muhimu katika matibabu ya saratani, kama ilivyoripotiwa na kituo cha habari cha CBS News.

Sumu yake yenye nguvu ina dutu iitwayo chlorotoxin, ambayo inafanyiwa utafiti kwa ajili ya kusaidia kutambua saratani na kutengeneza mifumo ya kupeleka dawa moja kwa moja kwenye uvimbe wa saratani.

4. Panya-jusi mwenye mkia mfupi wa kaskazini

Kwa kawaida, sumu haipatikani kwa wingi miongoni mwa mamalia. Ingawa sumu ya panya-jusi huyu mwenye mkia mfupi si kali kiasi cha kumuua binadamu, inaweza kusababisha maumivu na uvimbe.

Mnyama huyu mwenye sumu huenda hajavutia sana umma, lakini amevutia umakini wa wanasayansi. Sababu ni kwamba sumu yake inafanyiwa utafiti ili kubaini uwezekano wa kuitumia katika matibabu ya saratani.

Takacs anasema uwezekano huo unatokana na ukweli kwamba baadhi ya seli za uvimbe wa saratani zina molekuli ambazo kimuundo zinafanana kwa karibu na molekuli ambazo sumu hiyo hulenga kwa kawaida.

"Kwa kutumia mfanano huo, inawezekana kuibadilisha sumu na kuifanya kuwa dutu inayoweza kutumika kutibu saratani au kusaidia kuitambua," anasema.

Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa na Ambia Hirsi