Je, ungetaka kujua kama maisha yako yatakatizwa mapema?

    • Author, Emily Doughty
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Je, ungekubali kufanyiwa kipimo cha kujua kama maisha yako yatakatizwa mapema? Mimi nilikubali, na kilibadilisha maisha yangu

Ikiwa ungepewa nafasi ya kujua kama una jeni linaloweza kufupisha maisha yako, je, ungekubali?

Hilo ndilo swali gumu ambalo Laura Sides alikabiliana nalo baada ya kupewa fursa ya kufanyiwa kipimo cha kubaini kama amerithi aina nadra ya ugonjwa wa Alzheimer unaoanza mapema, ambao baba yake aligunduliwa nao akiwa katika umri wa miaka 40 na kitu.

Laura alizungumza na Dkt. Sian Williams, mtangazaji wa podikasti ya Life Changing ya BBC Radio 4, kuhusu uamuzi wake wa kufanya kipimo hicho na namna ambavyo maarifa hayo yameathiri maisha yake.

Uhusiano wa karibu na baba yake

Laura anasema alikuwa na ukaribu mkubwa na baba yake tangu utotoni kwa sababu walikuwa na tabia zinazofanana.

"Alikuwa daktari wa familia na baba mwenye upendo mkubwa," anasema.

Dalili za Alzheimer zilipoanza kuwa mbaya zaidi, Laura aliacha masomo yake ya chuo kikuu ili amhudumie.

"Tulikuwa na nyakati nzuri sana pamoja," anasema huku akikumbuka safari zao na mambo madogo madogo waliyofurahia.

"Nilikuwa nikimuogesha, nikimchezea muziki na kumhudumia. Alifurahia sana."

Habari iliyobadilisha maisha

Katika moja ya miadi hospitalini alipokuwa ameandamana na baba yake, daktari alimwambia Laura kuwa alikuwa na uwezekano wa asilimia 50 kwa 50 wa kurithi ugonjwa huo.

"Kitu pekee nilichoweza kufikiria ni kwamba hiyo ilikuwa kama kurusha sarafu hewani," anasema.

Kwa wakati huo, alikuwa amezama sana katika kumsaidia baba yake kiasi kwamba alisukuma mawazo hayo pembeni.

Baba yake alifariki mwaka 2009, mwaka mmoja tu baada ya mama yake kufariki.

Baada ya vifo hivyo viwili, Laura alihisi haja ya kuondoka na kuanza maisha mapya. Alisafiri peke yake duniani kote na hatimaye akaishi Melbourne, Australia.

Je, afanye kipimo au la?

Akiwa Australia, mawazo kuhusu kurithi ugonjwa wa baba yake yalianza kumrudia mara kwa mara.

Mwaka 2013 alimuona mtaalamu ambaye alimwambia kuwa kipimo kingeweza kubaini kwa uhakika wa karibu asilimia 100 kama angepata ugonjwa huo.

Iwapo angepatikana na jeni hilo, dalili zingetarajiwa kuanza kati ya umri wa miaka 46 hadi 48.

"Wakati huo nilihisi bado sijafika hatua ya kutaka kujua," anasema.

Lakini alipofika miaka ya 30, hamu ya kujua ukweli iliongezeka.

Kabla ya kufanyiwa kipimo, alihudhuria miezi sita ya ushauri wa kijenetiki.

"Huwezi kupata maeneo mengi maishani ambapo unaelezwa hatima yako mapema. Ni jambo zito sana kulikubali."

Matokeo mabaya

Baada ya kusubiri wiki sita, siku ya kupata majibu ilifika.

Laura alifika hospitalini peke yake.

"Nilisema, tuende moja kwa moja kwenye majibu."

Aliambiwa:

"Tunasikitika, habari si njema. Umerithi jeni hilo."

Laura anakumbuka kana kwamba kila kitu kiligeuka ukungu.

"Niliketi pale nikisikiliza tu."

Rafiki yake aliyekuwa akisubiri nje alianza kulia baada ya kumuona, lakini Laura hakutoa hisia zozote kwa wakati huo.

"Baadaye ndipo ukweli ulinipiga. Nilihisi hasira. Niliona si haki."

Kuishi na maarifa hayo

Baada ya muda, Laura alirejea Uingereza, hasa kwa sababu dada yake alikuwa anatarajia kupata mtoto.

Pia alijihusisha na majaribio ya kisayansi yaliyolenga kutafiti ugonjwa huo.

"Nilihisi angalau kuna jambo chanya linaweza kutoka katika hali hii mbaya."

Sasa akiwa na umri wa miaka 43, Laura amebakiza takriban miaka mitatu kabla ya kufikia umri ambao madaktari walitabiri dalili zinaweza kuanza kujitokeza.

"Ninaendelea kusubiri, lakini hali hiyo haininyimi usingizi."

Changamoto ya mahusiano

Moja ya mambo magumu kwake ni kuanzisha mahusiano mapya.

"Niwaambie au nisiwaambie? Na niwaambie lini?"

Anasema mara nyingi alipowaeleza watu ukweli huo, mahusiano yalivunjika.

Lakini pia amejifunza kitu muhimu.

"Nimeonyeshwa kwamba ninaweza kupendwa licha ya hali yangu."

Ndoto ya kuwa mama

Laura anasema siku zote aliamini angekuwa mama mzuri.

"Ni moja ya mambo machache ambayo sikuwahi kuyahoji kuhusu maisha yangu."

Lakini kutokana na hatari ya kurithisha jeni hilo kwa mtoto wake, aliamua kutopata watoto.

"Ni jambo gumu kulikubali."

Furaha katika mambo madogo

Leo, Laura anaishi kwa kuthamini mambo madogo.

"Hunisikii nikisema nataka kufika Grand Canyon au kutimiza malengo makubwa."

Badala yake, anathamini muda anaotumia na watu anaowapenda.

"Napenda mazingira ya asili. Napenda kuwa nje. Napenda maji."

Anasema:

"Inaweza kuonekana kama maneno ya kawaida, lakini kweli nimegundua kwamba mambo madogo ndiyo mambo makubwa katika maisha."

Na anapofikiria kuhusu miaka ijayo, ana matumaini rahisi lakini yenye maana.

"Natumaini nitakuwa na miaka michache mizuri duniani... nikinywa champagne na kula oysters, vitu viwili ninavyovipenda sana."