Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kinyesi chako kinavyoweza kukuokoa na kifo
- Author, Sofia Quaglia
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Mwaka 2013, Adam Fay alikuwa akijiuliza ni aina gani ya chakula inayoweza kumsaidia mtu kutoa kinyesi chenye ubora unaofaa zaidi kwa matumizi ya kitabibu?.
Wakati huo, Fay alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne wa udaktari, akijifunza namna ya kutibu maambukizi yanayosababishwa na bakteria aina ya Clostridioides difficile. Bakteria huyo husababisha maambukizi makali kwenye mfumo wa chakula na anaweza kuwa sugu kwa antibiotiki nyingi.
Mmoja wa wagonjwa wake, ambaye alikuwa mzee, alikuwa akisumbuliwa na maambukizi hayo mara kwa mara. Hali yake ilikuwa mbaya kiasi kwamba alihitaji kufanyiwa upandikizaji wa kinyesi.
Ni utaratibu unaohusisha kuingiza kinyesi cha mtu mwingine moja kwa moja kwenye utumbo mpana wa mgonjwa. Lengo ni kuingiza vijidudu vyenye manufaa ambavyo vinaweza kushindana na bakteria wanaosababisha maambukizi, na hivyo kusaidia kurejesha uwiano wa vijidudu kwenye utumbo.
Lakini kinyesi hicho kingepatikana wapi?
Wakati huo, benki za kukusanya kinyesi kwa ajili ya matumizi ya kitabibu zilikuwa chache sana. Familia na marafiki wa mgonjwa huyo hawakuweza au hawakuwa tayari kujitolea.
Hatimaye, Fay mwenyewe aliamua kutoa kinyesi chake.
Usiku kabla ya siku hiyo, alikula burrito, chakula cha Mexico kinachofanana na chapati iliyokunjwa na kujazwa vyakula mbalimbali.
Asubuhi iliyofuata, alijisaidia kwenye chombo maalumu cha kitabibu chenye rangi ya waridi, ndani ya chumba chake katika hosteli ya wanafunzi.
Baadaye, alichuja kinyesi hicho kwa kutumia kitambaa cha pamba kilicholowekwa kwenye maji yenye chumvi, kisha akakusanya kimiminika kilichopatikana kwenye chupa.
"Nakumbuka nilikiweka kwenye mfuko wa karatasi kwa sababu nilikuwa nimebeba chupa ya maji machafu," anasema.
Saa chache baadaye, wakati wa uchunguzi wa utumbo mpana kwa kutumia kamera, kinyesi hicho kiliingizwa kwenye utumbo wa mgonjwa.
Fay, ambaye sasa ni daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula katika NYU Langone Health, New York, baadaye alifahamishwa kuwa utaratibu huo ulifanikiwa.
Mgonjwa huyo hakupata tena maambukizi ya Clostridioides difficile.
Katika miaka ya hivi karibuni, wanasayansi wamekuwa wakichunguza kwa kina zaidi namna microbiome ya utumbo, yaani jamii ya vijidudu vinavyoishi kwenye utumbo, inavyohusiana na afya ya binadamu.
Utafiti huo umeongeza pia hamasa kuhusu upandikizaji wa vijidudu kutoka kwenye kinyesi, unaojulikana kwa Kiingereza kama fecal microbiota transplant.
Kwa sasa, upandikizaji wa kinyesi umeidhinishwa kutumika kutibu maambukizi yanayojirudia ya Clostridioides difficile.
Lakini wanasayansi wanachunguza iwapo utaratibu huo unaweza kusaidia katika kutibu magonjwa mengine, yakiwemo ugonjwa wa utumbo wenye muwasho, kisukari, usonji na osteoporosis, hali inayosababisha mifupa kuwa dhaifu.
Utafiti pia unaangalia uwezekano wa kutumia upandikizaji huo wa kinyesi katika kutibu baadhi ya matatizo ya afya ya akili na kupungua kwa uwezo wa kumbukumbu na kufikiri.
Kinyesi kinaweza kuingizwa moja kwa moja kwenye utumbo au kutayarishwa na kutolewa kwa njia ya vidonge.
Hata hivyo, kupata watu wanaoweza kutoa kinyesi kinachofaa kwa matumizi hayo si rahisi.
Watu wanaojitolea hufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya, na ni wachache sana wanaokidhi vigezo vinavyohitajika.
Watu wanaotoa kinyesi chenye sifa za kipekee kwa matumizi ya kitabibu huitwa kwa lugha isiyo rasmi super poopers.
Katika kuandaa makala hii, mwandishi alizifikia benki sita za kinyesi na maabara akitaka kuhoji baadhi ya watu wanaojitolea, lakini zote zilikataa.
Zilisema kupata watu wanaoaminika na wanaokidhi vigezo ni changamoto kubwa kiasi kwamba kuingilia faragha yao kunaweza kuwafanya waache kujitolea.
Ni akina nani wanaotoa kinyesi kinachotajwa kuwa na ubora wa kipekee? Na wanasayansi hutambuaje kinyesi kinachofaa zaidi kwa matumizi ya kitabibu?
Watu wanaojitolea kutoa kinyesi
Si kila mtu anayeamua kujitolea kutoa kinyesi anachaguliwa. Vigezo hutofautiana kati ya taasisi, kutegemea ugonjwa unaolengwa kutibiwa, lakini uchunguzi wa afya hufanywa kwa umakini mkubwa.
"Tunatafuta mtu mwenye afya bora kadiri iwezekanavyo," anasema Carl Crawford, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula katika Weill Cornell Medicine, New York. "Tunamchunguza kwa namna ileile tunavyomchunguza mtu anayejitolea kutoa kiungo cha mwili."
Kwa hiyo, mtu anayetaka kutoa kinyesi hufanyiwa uchunguzi wa kina, kama ilivyo kwa mtu anayejitolea kutoa figo au damu.
Mchakato huanza kwa kujaza dodoso mbalimbali kuhusu afya yake na kufanyiwa mahojiano. Baadaye, vipimo vya damu na kinyesi hufanywa ili kubaini iwapo ana magonjwa ya kuambukiza.
Vipimo hivyo vinaweza kuchunguza zaidi ya aina 30 za vijidudu, vimelea na bakteria wanaostahimili dawa.
Baadhi ya kliniki pia huhitaji watu wanaojitolea kupimwa Covid 19 na mafua.
Hii ni kwa sababu magonjwa mengi ya kuambukiza yanaweza kusambazwa kupitia kinyesi. Katika baadhi ya matukio, upandikizaji wa kinyesi umesababisha bila kukusudia kuenea kwa bakteria aina ya E. coli.
Virusi vinavyosababisha baadhi ya maambukizi ya mfumo wa upumuaji, ikiwemo Covid 19, vinaweza pia kusambaa kupitia chembechembe ndogo za kinyesi ambazo hutawanyika hewani wakati choo kinapovutwa.
Uchunguzi hauishii kwenye maambukizi pekee. Watu wanaojitolea huchunguzwa pia historia yao ya afya, ikiwemo iwapo wamewahi kuwa na baadhi ya magonjwa ya mfumo wa kinga au matatizo fulani ya afya ya akili.
Baadhi ya maabara huchunguza kwa karibu pia dawa na virutubisho vinavyotumiwa na watu wanaojitolea, ikiwemo multivitamin na vidonge vya madini ya chuma.
"Tunawauliza kwa kina kuhusu matumizi hayo na kuchunguza iwapo wanaweza kuacha kuyatumia," anasema Susan Poutanen, mtaalamu wa microbiolojia ya kitabibu katika Chuo Kikuu cha Toronto.
Katika taasisi hiyo, watu wanaojitolea huombwa pia kueleza vyakula walivyokula katika wiki iliyopita, hasa vile vinavyoweza kusababisha mzio.
"Wakati mwingine tunahitaji kinyesi ambacho hakina hata chembe za karanga," anasema.
Kwa kawaida, watu wanaojitolea kutoa kinyesi huwa na umri wa kati ya miaka 18 na 48. Hata hivyo, upandikizaji wa kinyesi unaweza kufanywa kwa watu wa umri wowote.
"Tumewatibu vijana wenye umri wa miaka 17 na hata watu wenye umri wa miaka 96," anasema Suzy Hotta, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza na upandikizaji wa kinyesi katika Chuo Kikuu cha Toronto.
Programu nyingi za upandikizaji wa kinyesi hazifuatilii kwa utaratibu maalumu mlo wa watu wanaojitolea.
Hata hivyo, mlo wao unapaswa kuwa na uwiano mzuri wa virutubisho na nyuzinyuzi nyingi.
Matunda, mboga na nafaka zisizokobolewa hutoa virutubisho muhimu vinavyosaidia vijidudu vyenye manufaa kwenye utumbo kukua na kustawi.
"Mtu anaweza kudhani kwamba wanaotoa kinyesi wanapaswa kuwa walaji wa mboga pekee, lakini watu wanaokula vyakula vya mimea na vya wanyama huwa na aina nyingi zaidi za vijidudu kwenye utumbo," anasema Crawford.
Hotta na Poutanen wanasema pia kuwa watu wanaojitolea wanapaswa kuwa na uzito unaofaa, ikiwezekana wasiwe na uzito kupita kiasi.
Katika kisa kimoja, mwanamke mwenye umri wa miaka 32, ambaye awali alikuwa na mwili mwembamba, alipata unene baada ya kufanyiwa upandikizaji wa kinyesi kutoka kwa mtoaji mwenye afya lakini aliyekuwa na uzito mkubwa.
Mbali na uzito, mambo mengine yanayozingatiwa ni matumizi ya pombe, mazoezi na namna mtu anavyolala.
Watu wanaojitolea wanaweza pia kuwekewa masharti makali kuhusu safari, ili kuepuka kukutana bila kukusudia na bakteria wa utumbo wanaostahimili dawa.
Crawford sasa hahusiki tena moja kwa moja na ukusanyaji wa kinyesi kwa ajili ya upandikizaji.
Hata hivyo, kutokana na uzoefu wake, anasema ni takribani asilimia tatu tu ya watu wanaofanyiwa uchunguzi wa awali wanaokidhi vigezo.
Kati ya hao, karibu nusu huwa na uwiano unaofaa wa bakteria unaowasaidia kupata haja kubwa kwa utaratibu wa kawaida.
Katika Toronto, Hotta anasema ni asilimia 1.6 pekee ya watu wanaojitolea wanaopitisha uchunguzi wa awali.
Kati yao, takribani asilimia 0.6 huchaguliwa kuwa watoaji wa kinyesi wa kudumu.
Wanasayansi wanaoendesha benki za kinyesi au kufanya utafiti kuhusu eneo hilo wanasema changamoto za kiutendaji na za mifumo zinazohusiana na utoaji wa kinyesi hazipaswi kupuuzwa.
Kisa cha Adam Fay si cha kawaida. Alijitolea kutoa kinyesi mara moja tu, kwa ajili ya mgonjwa aliyekuwa akimfahamu.
Lakini kwa wale wanaofaulu vipimo vinavyohitajika, huenda hatua inayofuata ikawa kushiriki katika programu ya kawaida ya kutoa kinyesi.
Katika programu hizo, watu wanaojitolea huhitajika kwenda maabara karibu kila siku na kujisaidia kwenye choo maalumu kilichotengwa kwa ajili yao.
Baadhi ya benki za kinyesi pia hulipa watu wanaojitolea.
Kwa mfano, nchini Marekani, malipo yanaweza kuwa kati ya dola 25, sawa na takribani pauni 19, na dola 100, sawa na takribani pauni 76.
Benki nyingi za kinyesi hupendelea kukusanya kinyesi kutoka kwa watu wachache wanaojitolea mara kwa mara, badala ya kutafuta watoaji wapya kila wakati.
"Ninaona inavutia sana kujenga uhusiano na watu wanaojitolea," anasema Suzy Hotta wa Chuo Kikuu cha Toronto.
Anasema uhusiano wa kuaminiana ni muhimu katika mchakato huo, huku kuheshimu uhuru wa watu wanaojitolea na maamuzi yao kukiwa jambo la msingi.
Kwa mfano, watu hao huombwa kutoa taarifa hata kuhusu mabadiliko madogo katika mtindo wao wa maisha.
Kinyesi chenye ubora wa kipekee
Vipimo vya awali vya afya haviwezi kutoa picha kamili ya ubora wa kinyesi cha mtu anayejitolea.
Kwa maambukizi yanayojirudia ya Clostridioides difficile, watu wote wanaokidhi vigezo vya uchunguzi wana nafasi inayokaribiana ya kufanikiwa kutibu ugonjwa huo kupitia upandikizaji wa kinyesi.
Lakini kwa baadhi ya magonjwa, tafiti zimeonyesha kuwa kinyesi kutoka kwa watoaji fulani kinaweza kuwa na ufanisi mkubwa zaidi, na kuongeza uwezekano wa ugonjwa kupungua au dalili kutoweka.
Kwa mfano, utafiti wa mwaka 2015 kuhusu upandikizaji wa kinyesi katika kutibu ulcerative colitis, ugonjwa sugu unaosababisha uvimbe na vidonda kwenye utumbo mpana, ulionyesha kuwa ni wagonjwa tisa kati ya 38 waliopata nafuu ya ugonjwa.
Wagonjwa saba kati ya hao walikuwa wamepandikizwa kinyesi kutoka kwa mtoaji mmoja.
Utafiti mwingine wa mwaka 2017 ulitumia mchanganyiko wa kinyesi kutoka kwa watoaji hadi saba tofauti.
Wagonjwa waliopokea mchanganyiko uliokuwa na kinyesi kutoka kwa mtoaji fulani walikuwa na uwezekano karibu mara mbili zaidi wa kupata nafuu, ikilinganishwa na wale waliopokea mchanganyiko ambao haukuwa na kinyesi kutoka kwa mtoaji huyo.
Lakini ni nini hasa kilichofanya kinyesi cha mtoaji huyo kuwa na ubora wa kipekee?
Kwa kawaida, uchunguzi wa kina wa microbiome nzima ya utumbo haufanywi wakati wa mchakato wa kuchagua watu wanaojitolea.
Hata hivyo, tafiti zimeonyesha kuwa kinyesi cha watu wanaoitwa super poopers kina idadi kubwa zaidi ya bakteria wa utumbo na aina nyingi zaidi za vijidudu.
Kinyesi chao pia huwa na bakteria wanaotajwa kuwa na manufaa kwa afya, wakiwemo Faecalibacterium prausnitzii.
Bakteria huyo huzalisha asidi ya mafuta inayojulikana kama butyrate, ambayo husaidia kupunguza uvimbe mwilini na kulinda ukuta wa ndani wa utumbo.
Hata hivyo, kinyesi kutoka kwa mtoaji mmoja hakiwezi kuwa na ufanisi sawa katika kutibu kila ugonjwa.
Fay anasema kinyesi cha mtoaji kinachofaa zaidi kutibu maambukizi ya Clostridioides difficile huenda kisiwe na ufanisi katika kutibu ugonjwa wa utumbo wenye muwasho au msongo wa mawazo kwa mtu mwingine.
"Bado tunajaribu kuelewa ni kitu gani cha kipekee kilichomo kwenye kinyesi hicho kinachokifanya kuwa na ufanisi mkubwa kiasi hicho," anasema.
Kutoka kinyesi hadi vidonge vya dawa
Hata kinyesi bora zaidi kutoka kwa watu wanaotajwa kuwa super poopers hakifanyi upandikizaji wa kinyesi kuwa matibabu yenye matokeo yanayoweza kutabirika kikamilifu.
"Jambo linalonipa wasiwasi mkubwa zaidi ni kutokuwa na uhakika kuhusu matokeo ya upandikizaji wa kinyesi," anasema Sarah Benterkia wa Chuo Kikuu cha Queen Mary, London. "Utaratibu huu unahusisha kuingiza jamii nzima ya vijidudu kwenye mwili wa mtu mwingine, kwa hiyo kuna mambo mengi yanayopaswa kuzingatiwa."
Mabadiliko katika microbiota ya utumbo yanaweza kutofautiana kutokana na mtoaji wa kinyesi, namna kinyesi kinavyotayarishwa na mgonjwa anayepokea upandikizaji.
Crawford anasema, hata hivyo, upandikizaji wa kinyesi unaweza kuwa hatua muhimu kuelekea maendeleo ya matibabu yenye viwango na taratibu zinazofanana zaidi katika siku zijazo.
Kwa mfano, kampuni ya dawa ya Ferring Pharmaceuticals hutengeneza bidhaa ya kuingiza kwenye utumbo kupitia njia ya haja kubwa, inayojulikana kama Rebiota.
Bidhaa hiyo hutayarishwa kutokana na kinyesi cha watu wanaojitolea ambao utumbo wao una idadi kubwa ya bakteria wenye manufaa.
Vilevile, kampuni ya Seres Therapeutics hutengeneza vidonge vinavyojulikana kama VOWST, ambavyo vina spora za bakteria maalumu zilizokusanywa kutoka kwenye kinyesi cha binadamu.
Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani, FDA, imeidhinisha bidhaa zote mbili kutumika kutibu maambukizi yanayojirudia ya C. difficile.
Crawford anasema matumizi ya vidonge katika kutibu maambukizi hayo yanaweza kuongezeka siku zijazo, kwa kuwa vidonge hivyo vina vijidudu vilivyochaguliwa kutoka kwenye kinyesi cha watu wenye afya na kuzalishwa kwa wingi katika maabara.
"Ninaamini matibabu yanayotegemea microbiome yana uwezo wa kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa tiba wa siku zijazo," anasema.
Hata hivyo, licha ya uwezekano mkubwa wa kutumia microbiome katika matibabu, Crawford ana wasiwasi pia kuhusu mustakabali wake.
Anasema mitindo ya maisha ya kisasa inaathiri kwa kiasi kikubwa microbiome ya asili katika miili yetu. Kwa mfano, ulaji wa vyakula vilivyosindikwa kupita kiasi hupunguza aina mbalimbali za vijidudu vinavyoishi kwenye utumbo.
"Nina wasiwasi kwamba huenda tunapoteza sifa za vijidudu vingi vinavyoishi kwenye mfumo wetu wa chakula, ambavyo vinaweza kutusaidia kukabiliana na wimbi lijalo la magonjwa," anasema Crawford.
Analinganisha uwezo wa vijidudu vya utumbo kusaidia katika matibabu na wingi wa kemikali zenye manufaa zinazopatikana katika mimea ya misitu ya kitropiki.
"Microbiome katika mfumo wetu wa chakula ina utajiri mkubwa wa aina mbalimbali za vijidudu na inaweza kutusaidia. Lakini mara nyingi tunapuuza umuhimu wake," anasema.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid