Sheikh Hasina atangaza tarehe ya kurejea nchini Bangladesh kutoka uhamishoni India
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina, amesema yuko tayari kurejea nchini Bangladesh.
Waziri mkuu huyo wa zamani aliyeondolewa madarakani ametangaza tarehe ya kurejea kwake nyumbani, kuwa Disemba 16, na hata kueleza namna anavyopanga kufanya safari hiyo.
Serikali ya Dhaka, ambayo awali ilikuwa imepuuzilia mbali uwezekano wa kurejea kwake, sasa inaonekana kuchukulia kwa uzito zaidi tangazo lake la hivi karibuni la kurejea nchini humo.
Hasina, mwenye umri wa miaka 79, alikimbilia mjini Delhi nchini India mwezi Agosti 2024, baada ya maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi kukomesha utawala wake wa miaka 15.
Msemaji wake amesema anapanga kurejea Bangladesh siku ya kuadhimisha ushindi wa nchi hiyo dhidi ya Pakistan, katika vita vya ukombozi vya mwaka 1971.
Hasina alihukumiwa adhabu ya kifo baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kutokana na nafasi yake katika operesheni ya ukandamizaji wa waandamanaji. Kesi hiyo iliendeshwa bila yeye kuwepo mahakamani, hali iliyoibua maswali kuhusu haki ya kufuata taratibu za kisheria.
Chama chake cha Awami League kimepigwa marufuku nchini Bangladesh.
Serikali ya Bangladesh imesema Hasina atakamatwa mara moja iwapo atarejea nchini humo na imeahidi kutekeleza hukumu ya kifo dhidi yake.
Sasa Hasina anaitaka serikali ya Bangladesh kupanga ndege ya kumrejesha kutoka Delhi. Iwapo hilo halitawezekana, anaweza kutumia usafiri wa kawaida wa kibiashara au kuvuka mpaka kwa njia ya nchi kavu.
"Hata yuko tayari kuingia Bangladesh kwa miguu," Abu Obaidha Arin, mmoja wa wasaidizi wake wakuu, aliiambia BBC.
Hata hivyo, serikali ya Dhaka imejibu kwa msimamo mkali, ikisisitiza kuwa Hasina lazima arejeshwe nchini kupitia utaratibu wa kumrejesha mtuhumiwa au mhalifu kutoka nchi nyingine.
Soma pia: