Je, al-Shabaab inaweza kuteka Mogadishu baada ya kuondoka kwa vikosi vya kigeni?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Wakati vikosi vya kigeni vinavyoisaidia Somalia vinapoanza kujiondoa, taifa hilo linakabiliwa na mtihani mpya wa uthabiti wake. Wakati huohuo, ufadhili kwa vyombo vya usalama unaendelea kuwa na mashaka, huku mzozo mkali wa kisiasa ukitishia kuvuruga mipango ya kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa moja kwa moja nchini humo katika miongo kadhaa.

Mchanganyiko wa changamoto hizi umeibua maswali kuhusu uwezo wa serikali ya Somalia kujilinda dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab, huku ikijaribu kudhibiti migawanyiko inayozidi kuongezeka miongoni mwa makundi ya kisiasa.

Baadhi ya wachambuzi wana hofu kwamba hali hiyo inaweza kulipa nguvu zaidi kundi la al-Shabab, ambalo lina uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, na hata kuliwezesha kulidhibiti mji mkuu wa Mogadishu.

Kundi hilo tayari linadhibiti maeneo makubwa ya Somalia licha ya uwepo wa wanajeshi wapatao 12,000 wa Umoja wa Afrika (AU) wanaoiunga mkono serikali.

Kuondoka kwa vikosi vya kigeni, pamoja na shughuli za wanamgambo wa kikabila wanaoungwa mkono na makundi pinzani ya kisiasa, kumeongeza wasiwasi kuhusu uwezo wa serikali kuendelea kudhibiti hali ya usalama.

Wanajeshi wa Uganda, ambao ndio kundi kubwa zaidi ndani ya kikosi cha AU, walianza kujiondoa mwezi uliopita na wanatarajiwa kukamilisha mchakato huo ifikapo mwaka ujao.

Ethiopia, ambayo pia ni mchangiaji mkubwa wa vikosi vya AU ikiwa na zaidi ya wanajeshi 7,000, inadaiwa kupanga kuondoa karibu nusu ya wanajeshi wake.

Marekani, ambayo awali ilitangaza kupunguza ufadhili kwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Usaidizi nchini Somalia (UNSOS), baadaye ilisema itaendelea kufadhili kwa mwaka mmoja zaidi. Washington huchangia takriban robo ya bajeti ya kila mwaka ya UNSOS ya dola milioni 500 za Marekani, fedha zinazosaidia vikosi vya usalama vya Somalia, misheni za AU na nchi zinazotoa wanajeshi.

Kutokana na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu msaada wa kijeshi na changamoto zinazoongezeka kisiasa, wachambuzi wanahoji kama vikosi vya usalama vya Somalia viko tayari kusimama peke yake.

Hofu hizo ziliongezeka baada ya al-Shabab kudai kuwaua mamia ya wanajeshi maalumu wa Somalia katika shambulio la hivi karibuni. Serikali ilikiri kutokea kwa shambulio hilo lakini haikufichua idadi ya waliouawa.

Abdisalam Guleid, aliyewahi kuwa naibu mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Taifa la Somalia, amesema hali ya usalama nchini humo inazidi kuwa ya hatari.

Anaonya kuwa kuondoka kwa vikosi vya kigeni kunaweza kuiacha Mogadishu katika mazingira sawa na yale ya Afghanistan mwaka 2021, wakati Taliban walipotwaa madaraka baada ya kuondoka kwa majeshi ya Marekani na NATO.

"Sidhani kama Mogadishu itaweza kujilinda yenyewe. Hali kama ile ya Taliban ndiyo jambo linalowezekana zaidi ninapolitazama sasa," alisema.

Anasema hali ya namna hiyo ilishawahi kutokea Somalia hapo awali.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, makundi ya waasi wa kikabila yalivamia Mogadishu kutoka pande mbalimbali na kumwondoa madarakani Rais Mohamed Siad Barre.

Kuondolewa kwake kulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, maafa makubwa ya kibinadamu na kusambaratika kwa taasisi za serikali. Hali hiyo baadaye ilitoa nafasi kwa makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, yakiwemo al-Shabab, kuimarisha ushawishi wao.

Guleid anasema wanajeshi wa Uganda wamekuwa muhimu katika kuzuia hali kama hiyo tangu walipopelekwa Somalia mwaka 2007.

Walikuwa na mchango mkubwa katika kuliondoa kundi la al-Shabab kutoka Mogadishu na miji mingine mikubwa, pamoja na kulinda maeneo muhimu kama uwanja wa ndege, bandari, taasisi za serikali na balozi mbalimbali.

Baadaye wanajeshi kutoka Burundi, Djibouti, Kenya, Sierra Leone na Ethiopia walijiunga na misheni ya AU, huku mataifa kama Uturuki na Marekani yakiendelea kuwa na uwepo wa kijeshi na kutoa mafunzo pamoja na vifaa kwa vikosi vya Somalia.

Hata hivyo, Guleid anaamini kuwa miaka ya msaada wa kimataifa haijatosha kuifanya Somalia ijitegemee kijeshi.

Anasema serikali imezoea ulinzi wa nje kiasi kwamba haikujiandaa vya kutosha kuchukua jukumu hilo yenyewe.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari wa Somalia, Abdifatah Qasim Mohamud, amekanusha madai kwamba nchi hiyo haitamudu kuhimili kuondoka kwa vikosi vya kigeni.

Aliiambia BBC kuwa wanajeshi wa Somalia tayari wamechukua baadhi ya maeneo yaliyoachwa na wanajeshi wa Uganda na wako tayari kubeba jukumu kubwa zaidi la ulinzi wa taifa.

Anasema Somalia haiwezi kutegemea vikosi vya kigeni milele.

"Naamini hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu suala hili. Hakutakuwa na mabadiliko yoyote katika hali ya usalama nchini au katika maeneo ambayo wameyaacha," alisema.

Rais Hassan Sheikh Mohamud pia amekuwa akitafuta kuendelezwa kwa msaada wa kimataifa.

Katika ziara yake Uganda tarehe 23 Novemba, yeye na Rais Yoweri Museveni waliitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono Somalia.

Si kila mtu anaamini kuwa kuondoka kwa vikosi vya kigeni kutasababisha kuporomoka kwa usalama.

Mchambuzi wa masuala ya usalama kutoka Uganda, Freddie David Egesa, anasema miaka ya msaada wa kijeshi wa kimataifa imeisaidia Somalia kujenga taasisi zinazoweza kubeba jukumu kubwa zaidi la usalama.

Kwa maoni yake, kuondoka kwa vikosi hivyo kutatoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana.

Pia anaamini hatua hiyo itawalazimisha viongozi wa kisiasa nchini humo kuweka kando tofauti zao na kuchukua jukumu kubwa zaidi kwa mustakabali wa taifa.

Lakini wachambuzi wengine wanaonya kwamba muda wa kuondolewa kwa vikosi hivyo ni mbaya sana.

Omar Mahmood wa International Crisis Group anasema vikosi vya Somalia viko chini ya shinikizo kubwa kutokana na vita dhidi ya al-Shabab, huku vikijaribu kuchukua maeneo yaliyoachwa na majeshi ya kigeni.

Anasema hilo ni jukumu kubwa kwa jeshi ambalo bado linaendelea kujijenga.

Pia anataja mapigano katika eneo la Bay, ambapo wanajeshi watiifu kwa aliyekuwa Rais wa Jimbo la Kusini Magharibi, Abdiaziz Hassan Mohamed, wamekuwa wakipambana na serikali ya shirikisho.

Kuondoka kwa wanajeshi wa Uganda katika eneo la Lower Shabelle kunaweza kuongeza changamoto za kiusalama, anasema.

Mahmood pia anaeleza kuwa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu ni changamoto nyingine inayochangia kuzorota kwa hali ya usalama.

Zaidi ya masuala ya kijeshi, anasema serikali lazima itafute suluhu ya mgogoro wa kisiasa kuhusu muda na mfumo wa uchaguzi.

Somalia imekuwa ikijaribu kuachana na mfumo wa uchaguzi usio wa moja kwa moja ambapo wazee wa koo huchagua wabunge, nao wakamchagua rais, na badala yake kuanzisha mfumo wa kura za moja kwa moja.

Hata hivyo, mabadiliko hayo yamegawanya serikali na upinzani, huku kukiwa na kutokubaliana kuhusu namna uchaguzi utakavyofanyika.

Mvutano uliongezeka mwaka huu baada ya rais kusukuma mbele marekebisho ya katiba yaliyoongeza muda wa urais kutoka miaka minne hadi mitano, hatua ambayo kwa vitendo iliahirisha uchaguzi hadi mwaka 2027.

Mwezi huu, Mahakama Kuu ilipinga hatua hiyo na kuwataka viongozi wa kisiasa kukubaliana kuhusu ramani ya uchaguzi ndani ya siku 30 na kufanya uchaguzi ndani ya miezi mitatu.

Serikali ya Somalia imekataa uamuzi huo.

Siku moja kabla ya hukumu hiyo, rais alimwondoa madarakani Jaji Mkuu Baashe Yusuf Ahmed. Tangu wakati huo, suala hilo limefikishwa katika Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Tanzania.

Mahmood anasema migogoro ya kisiasa na kiusalama imeungana kwa kiasi kikubwa, na kwamba kukosekana kwa makubaliano kuhusu uchaguzi kunafanya serikali ishindwe kuelekeza nguvu zote katika mapambano dhidi ya al-Shabab.

Naye Guleid anaonya kuwa tishio kwa utulivu wa Somalia halitokani tu na al-Shabab bali pia kwa wanamgambo wa kikabila wanaozidi kuipinga serikali ya shirikisho.

"Leo tunao wanamgambo wa kikabila wanaopigana bega kwa bega na al-Shabab dhidi ya serikali ya shirikisho," alisema.

Anaongeza kuwa uongozi wa nchi unaonekana kushindwa kutambua ukubwa wa changamoto zinazokuja.

Nani atajaza pengo la washirika wa kigeni?

Changamoto za usalama nchini Somalia zinaongezwa na utegemezi mkubwa wa msaada wa kifedha kutoka nje.

Takwimu za Wizara ya Fedha zinaonyesha kuwa misaada kutoka kwa wafadhili inachangia takriban theluthi mbili ya bajeti iliyopangwa ya dola bilioni 1.36 kwa mwaka 2026.

Hata hivyo, wizara hiyo ilisema imepokea dola milioni 314 pekee katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka, sawa na asilimia 35 tu ya misaada iliyotarajiwa.

Mahmood anaamini kwamba licha ya kupungua kwa baadhi ya misaada ya kijeshi, washirika wengine wanaweza kusaidia kuziba pengo hilo kupitia makubaliano ya moja kwa moja na kuendelea kutoa msaada.

Lakini Guleid ana shaka kwamba nchi kama Uturuki, Qatar na Misri zinaweza haraka kuchukua nafasi ya mchango wa kijeshi na kifedha uliokuwa ukitolewa na Uganda na Marekani.

Anasema utegemezi wa Somalia kwa msaada wa nje unaifanya kuwa katika mazingira magumu pale washirika wa kimataifa wanapobadilisha vipaumbele vyao.

Utegemezi huo pia umechangia kuzorota kwa uhusiano kati ya Somalia na baadhi ya serikali za kigeni.

Somalia imeishutumu Falme za Kiarabu (UAE) kwa kufadhili makundi yenye silaha na kudhoofisha mamlaka yake, madai ambayo UAE imeyakanusha.

UAE pia ilimjibu vikali rais wa Somalia kwa kumtaja kama "rais anayemaliza muda wake," kutokana na mzozo kuhusu muda wake wa kuendelea madarakani.

Ingawa nchi hizo mbili zilikata rasmi uhusiano mapema mwaka huu, UAE imekuwa mshirika muhimu wa Somalia katika masuala ya usalama na uchumi.

Kwa upande wa Egesa, kuondoka kwa vikosi vya kigeni kunaweza kuwa fursa kwa Somalia kuonyesha maendeleo iliyopiga katika kujenga taasisi zake za usalama.

Anaamini kuondoka kwa hatua kwa hatua kutazipa nguvu vikosi vya Somalia kuchukua majukumu zaidi huku ikiwalazimu wanasiasa wenye misimamo tofauti kufanya kazi pamoja.

Lakini Guleid anaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa.

Anasema bila kushughulikia udhaifu wa kijeshi, migawanyiko ya kisiasa na ushawishi unaokua wa makundi yenye silaha, Somalia inaweza kupoteza mafanikio ya kiusalama yaliyopatikana katika miaka ya karibuni.

Kwa sasa, nchi hiyo inakabiliwa na jukumu gumu la kupambana na uasi uliokita mizizi, kusimamia migongano ya kisiasa na kujiandaa kwa uchaguzi wenye mvutano mkubwa, wakati baadhi ya washirika wake wa kijeshi wakijiandaa kuondoka.

Iwapo Somalia itaweza kustahimili shinikizo hizi zote bila kurejea katika kipindi cha machafuko na ukosefu wa utulivu, bado ni swali ambalo halijapatiwa jibu.

Imefasiriwa na Asha Juma