Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Pete Edochie: Jina lililotikisa uigizaji na kutawala mitandao ya kijamii
- Author, Mansur Abubakar
- Akiripoti kutoka, Abuja
- Author, Wycliffe Muia
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa vizazi vya Wanigeria, Pete Edochie alikuwa zaidi ya mwigizaji maarufu.
Alikuwa Okonkwo, shujaa mwenye msimamo mkali, fahari na maisha yaliyogubikwa na changamoto nyingi. Kupitia uigizaji wake katika tamthilia ya Things Fall Apart, alijijengea umaarufu mkubwa, akawa jina linalofahamika karibu katika kila kaya na kujipatia nafasi ya pekee katika mioyo ya mamilioni ya watazamaji.
Hata baada ya kifo chake, Wanigeria wengi waliendelea kumtambua kwa jina la Okonkwo, jambo linaloonyesha athari ya kudumu ya uhusika huo katika maisha yake ya kisanii na katika kumbukumbu za watazamaji.
Edochie alifariki dunia tarehe 25 Novemba akiwa na umri wa miaka 79 katika jiji la Enugu, kusini mashariki mwa Nigeria, baada ya kuugua saratani ya tezi dume kwa muda mrefu.
Mwaka 1987, alicheza nafasi ya Okonkwo katika tamthilia ya televisheni iliyotokana na riwaya maarufu ya Things Fall Apart iliyoandikwa na Chinua Achebe. Uigizaji huo ulimfungulia milango ya mafanikio, ukimfanya kuwa mmoja wa waigizaji wanaoheshimika zaidi nchini Nigeria na kumjengea sifa zilizovuka mipaka ya nchi yake.
Tamthilia hiyo iliangazia athari za kuenea kwa Ukristo na utawala wa kikoloni wa Uingereza katika jamii za Kiafrika, mabadiliko yaliyotikisa misingi ya maisha, mila na desturi za jadi.
Joy Nnamdi, shabiki wa riwaya ya Things Fall Apart na tamthilia yake ya televisheni, anaamini kuwa Pete Edochie alikuwa chaguo bora kabisa kwa nafasi ya Okonkwo.
Kwa mujibu wake, ni vigumu kufikiria mwigizaji mwingine ambaye angeweza kuupa uhai na uzito uhusika huo kwa kiwango kilekile.
"Uigizaji wake kama Okonkwo uliipa sura na uhalisia riwaya hiyo maarufu," alisema Nnamdi katika mahojiano na BBC mjini Lagos, jiji kubwa zaidi nchini Nigeria.
Nafasi hiyo pia ilijenga taswira ya Edochie kama mwanamume mwenye msimamo mkali na asiyelegea, sifa iliyobaki kuwa sehemu ya utambulisho wake katika kipindi kikubwa cha maisha yake ya kisanii.
"Ilikuwa nadra sana kumuona akicheka kwenye filamu. Alikuwa mfano halisi wa mwanamume mwenye ukakamavu," aliongeza Nnamdi.
Akiwa na sauti nzito yenye mamlaka, uwepo wa kuvutia na uwezo wa kutumia methali za Kiafrika kwa ustadi mkubwa, Edochie aliweza kutawala skrini bila hata kupaza sauti.
Iwe aliigiza kama mzee wa kijiji, mfanyabiashara tajiri au kiongozi wa kimila mwenye ushawishi mkubwa, alibaki kuwa mfano wa kudumu wa mamlaka na uongozi wa kiume katika filamu za Kiafrika.
Baadaye, Edochie alijidhihirisha kama mmoja wa nyota wakubwa na wanaotambulika zaidi katika Nollywood, tasnia ya filamu ya Nigeria ambayo sasa ni miongoni mwa kubwa zaidi duniani.
Kupitia vituo vya Africa Magic vya kampuni ya MultiChoice, filamu zake zilifika katika mamilioni ya nyumba kote barani Afrika, kuanzia Kenya hadi Afrika Kusini, wakati Nollywood ilipozidi kuimarika kama nguvu kubwa ya kitamaduni na burudani.
Ingawa filamu zake nyingi zilijikita katika utamaduni wa jamii ya Waigbo, mada alizoshughulikia, zikiwamo uaminifu wa kifamilia, migogoro ya urithi, imani za kiroho na matumizi mabaya ya madaraka, ziliwagusa watazamaji ndani na nje ya Nigeria.
Kabla ya kujipatia umaarufu mkubwa katika sanaa ya uigizaji, Edochie alikuwa tayari amejijengea taaluma yenye mafanikio katika sekta ya utangazaji.
Alizaliwa tarehe 7 Machi 1947 mjini Zaria, kaskazini mwa Nigeria. Alisomea elimu ya msingi na sekondari katika jimbo la Kaduna kabla ya kwenda nchini Uingereza kusomea uandishi wa habari na televisheni.
Mwaka 1967 alijiunga na Shirika la Utangazaji la Nigeria Mashariki (Eastern Nigerian Broadcasting Corporation), mwaka huohuo ambao vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza nchini humo.
Wakati wa vita hivyo, alifanya kazi katika kituo cha Voice of Biafra, kilichokuwa sauti ya harakati za kujitenga za Biafra. Katika mahojiano ya baadaye, alitaja kipindi hicho kuwa miongoni mwa nyakati ngumu zaidi maishani mwake.
"Wakati wa vita, sisi Wabiafra tulipitia mateso makubwa. Ilikuwa vigumu sana kuendelea kuishi. Njaa ilitufanya kula chochote tulichoweza kupata," aliwahi kukumbuka.
Baada ya vita, alipanda ngazi za uongozi katika sekta ya utangazaji kabla ya kuhamia rasmi katika uigizaji. Katika taaluma iliyodumu kwa zaidi ya miongo minne, alishiriki katika filamu kadhaa maarufu, zikiwamo Igodo, Rituals na Billionaire's Club.
Kazi ya Edochie ilishuhudia pia mabadiliko kutoka enzi ya filamu za nyumbani hadi majukwaa ya kimataifa ya utiririshaji wa kidijitali.
Mwaka 2018, aliigiza katika Lionheart, filamu ya kwanza ya Kinigeria kutengenezwa mahsusi kwa ajili ya Netflix, hatua iliyosaidia kuifikisha Nollywood kwa hadhira pana zaidi duniani.
Pia alifanya kazi nchini Ghana, akionekana pamoja na baadhi ya nyota wakubwa wa filamu wa nchi hiyo katika vichekesho vya John and John mwaka 2017.
Mchango wake katika sanaa ulitambuliwa mwaka 2003 alipotunukiwa nishani ya kitaifa ya Member of the Order of the Niger (MON). Alipokea pia tuzo nyingine kadhaa, zikiwemo Industry Merit Award za Africa Magic Viewers' Choice Awards.
Katika miaka ya mwisho ya maisha yake, Edochie alipata umaarufu mpya kupitia mitandao ya kijamii. Sura yake ya kipekee, kauli za busara na matukio ya kukumbukwa kutoka filamu zake viligeuka kuwa meme maarufu, na kumtambulisha kwa kizazi kipya cha Waafrika.
Kwa wengi ambao hawakuwahi kutazama Things Fall Apart au filamu zake za awali, sura yake kali ikawa ishara ya kuonyesha kutokuamini, kutokubaliana au kukerwa katika mawasiliano ya mtandaoni.
Hata hivyo, kwa waliokua wakimtazama, Edochie alibaki kuwa mwigizaji mwenye haiba na ushawishi mkubwa. Sani Muazu anakumbuka jinsi wazazi mjini Kano walivyokuwa wakilitumia jina lake kuwaonya watoto waliokuwa na utundu.
"Walikuwa wakituonya kwa kusema, 'Okonkwo atakuja usipoacha tabia hiyo,' na mara moja tulirekebisha mienendo yetu," alisema.
"Kusema kweli, tulimuogopa. Ingawa tulimfahamu kupitia skrini pekee, baadhi ya nafasi alizoigiza zilifanya aonekane wa kutisha zaidi. Mara nyingi aliigiza wahusika waliokuwa na uhusiano na nguvu za giza au uchawi, na hata nafasi za wabaya zilimfaa sana."
Taarifa za kifo chake zilizua wimbi la maombolezo kutoka kwa mashabiki, waigizaji na wadau wa tasnia ya filamu, wengi wakimtaja kama gwiji aliyechangia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuunda sura ya Nollywood.
Mwigizaji maarufu Genevieve Nnaji alitoa salamu zake za rambirambi kupitia mtandao wa X.
"Nitafarijiwa na imani kwamba ulikuwa miongoni mwa walioteuliwa na sasa umerejea kwa Muumba wako. Roho ya simba wa kweli na ipumzike kwa amani. Tutakukumbuka daima."
Patience Ozokwor (Mama G):
"Alikuwa kama mzee mwenye hekima anayeketi na kusimulia hadithi za zamani na namna maisha yalivyokuwa wakati wake."
"Nilikuwa na uhuru wa kumpigia simu wakati wowote. Daima alikuwa tayari kunishauri kuhusu jambo la kufanya na la kuepuka."
Babangida Bangis:
"Siku chache zilizopita, katika warsha ya watengenezaji filamu kutoka sehemu tofauti za Nigeria, jina lake lilitajwa kama mfano wa ubora, taaluma na uimara katika uigizaji."
"Bila shaka kifo chake ni pigo kwa tasnia nzima ya uigizaji, sio kwa Nigeria au Afrika pekee. Wengi wetu tulikua tukimtazama na kumthamini."
Leo Edochie:
"Miongoni mwa urithi wote aliotuachia, naamini wengi watakubaliana kuwa kusema ukweli na kuishi kwa uadilifu ndizo tunu alizozithamini zaidi."
"Aliishi maisha ya mfano ambayo vijana wanaweza kujifunza na kuyaiga."
"Nina wajibu wa kuendeleza urithi huo na kuhakikisha maadili aliyoyasimamia yanaendelea kuishi ndani ya familia yetu."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi