"Sikuwahi kuhisi kuwa nina pesa nyingi": Jinsi J Paul Getty alivyokuwa mtu tajiri zaidi duniani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Jumba la kifahari la bilionea wa mafuta wa Marekani la karne ya 16 nchini England lilikuwa makazi ya mkusanyiko wa kuvutia wa kazi za sanaa na simba aliyeitwa Nero. Mwaka 1963, BBC ilimtembelea humo ili kuzungumzia "mafanikio yake makubwa".

Mnamo Julai 1960, J Paul Getty aliandaa sherehe ya kuhamia nyumba mpya iliyogharimu pauni 10,000, sawa na takriban pauni 300,000 au dola 400,000 za sasa, katika Sutton Place, jumba la Tudor la karne ya 16 huko Surrey alilolinunua mwaka mmoja kabla.

Zaidi ya watu 2,000 kutoka tabaka la juu la kijamii, familia za kifalme na watu maarufu walihudhuria hafla hiyo. Tukio hilo liligonga vichwa vya habari baada ya mpiga picha wa habari aliyekuwa akijaribu kusogea karibu zaidi ili apige picha kutupwa kwenye bwawa la kuogelea.

Akiwa na hofu ya kusafiri kwa ndege au kuvuka bahari kwa meli kubwa za abiria, Getty aliishi katika jumba hilo hadi alipofariki mwaka 1976 akiwa na umri wa miaka 83. Aliweka simu za kulipia kwa sarafu kwa wageni wake ili kuwazuia kupiga simu za mbali ambazo zingeongeza gharama kubwa.

Mwaka 1963, Alan Whicker wa BBC alimhoji Getty, ambaye alijulikana kwa kutopenda kujitokeza hadharani, katika jumba hilo ambalo wakati mmoja lilikuwa makazi ya kiangazi ya Mfalme Henry VIII.

Picha za kumbukumbu zinaonyesha maisha ya ndani ya bilionea huyo katika jumba lililokuwa na ulinzi mkali. Anaonekana akipita karibu na michoro ya wasanii maarufu wa zamani na kula katika meza yenye urefu wa futi 16, akifuatana tu na mbwa wake wa ulinzi aina ya Alsatian.

Na ilikuwa kutoka katika nyumba hiyo kubwa ya mashambani nchini Uingereza, badala ya jengo refu la Manhattan au ikulu ya mtawala wa Mashariki ya Kati, ambapo Getty aliendesha himaya yake kubwa ya biashara ya mafuta katika miaka yake ya mwisho.

Getty aliingia katika Kitabu cha Guinness cha Rekodi za Dunia mwaka 1966 kama mtu tajiri zaidi duniani. Alipata milioni yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 24 wakati kisima cha mafuta katika ardhi aliyomiliki Oklahoma kilipoanza kutoa mafuta.

Wakati wa kifo chake, utajiri wake ulikadiriwa kuwa karibu dola bilioni nne, sawa na dola bilioni 23.5 au pauni bilioni 17.5 kwa thamani ya sasa. Alikuwa akipata zaidi kwa siku moja kuliko mtu wa kawaida angepata katika maisha yake yote.

Moja ya kauli zake maarufu kuhusu mafanikio ilikuwa: "Amka mapema, fanya kazi kwa bidii, na ugundue kisima cha mafuta."

Hata hivyo, alipokuwa akitafakari kuhusu utajiri wake mwaka 1963, Getty alisema hakuweza kueleza kwa uhakika ni nini hasa kilichomfanya kuwa bilionea.

"Tofauti kati ya mfanyabiashara aliyefanikiwa na yule ambaye hajafanikiwa sana huenda ikawa ni sifa chache tu. Labda mafanikio makubwa yanahitaji sifa 37. Mtu akiwa na 35 kati ya hizo, anaweza kufanikiwa kwa kiwango cha kawaida. Lakini hizo sifa mbili zinazofanya tofauti ni zipi hasa, sijui," alisema.

Alipoulizwa na Alan Whicker kwa nini yeye alifanikiwa wakati wengine walishindwa, Getty alijibu kuwa hakujiona tofauti sana na watu wengine.

"Sifahamu kama nina sifa yoyote ya pekee ambayo watu wengine hawana."

Akitaja bidii, akili na ubunifu kama baadhi ya sifa alizoshiriki na wengine, alisema bado alihisi kuna mambo ambayo angependa kuboresha kuhusu nafsi yake.

"Sikuzote nilitamani ningekuwa na haiba nzuri zaidi, ningeweza kuwavutia watu zaidi na kuwa mzungumzaji bora. Sikuzote nilihofia huenda sikuwa mtu wa kuvutia sana katika mazungumzo."

Licha ya kusita kutaja siri ya mafanikio yake, Getty alisema mchango wa baba yake ulikuwa muhimu sana katika safari yake ya biashara.

"Mafanikio hayo yalitokana kwa kiasi kikubwa na kwamba baba yangu alikuwa ameanzisha biashara kubwa iliyokuwa ikiendelea vizuri. Nilikuwa mtoto wake wa pekee, hivyo ilinibidi kuendeleza biashara hiyo."

Kuligeuza jumba la kifahari kuwa ngome

Bilionea huyo pia alizungumzia tabia yake ya kubana matumizi mwaka 1963. Alisema aliwahi kusubiri hadi karibu na mwisho wa maonesho ya mbwa ili kulipa ada ya kuingia iliyopunguzwa kwa shilingi mbili au tatu, na kula katika migahawa usiku sana ili kuepuka ada ya ziada ya muziki wa moja kwa moja.

Licha ya kuwa mmoja wa watu matajiri zaidi duniani, Getty alisema hakuwahi kujiona kuwa na pesa nyingi.

"Sikuwahi kuhisi kuwa nina pesa nyingi," alimwambia Whicker.

Kisha akaongeza: "Kama ningeuza kila kitu nilichomiliki, huenda ningekuwa na pesa."

Getty alikwepa kueleza wazi kile alichokuwa anakihofia alipoulizwa kuhusu hatua zake za kuimarisha ulinzi wa jumba lake.

"Siwezi kusema ninaogopa jambo maalum. Ni tahadhari ya kawaida tu, nadhani," alisema.

Alipoendelea kuulizwa kuhusu uwezekano wa vitisho, alijibu kuwa huenda kulikuwa na "watu wenye mawazo ya ajabu" ambao wangeweza kulipua eneo hilo.

Hata hivyo, kuhusu mbwa wake wa ulinzi, alisema:

"Nina mbwa hao hasa kwa sababu ninawapenda."

Je, pesa zinaweza kununua furaha?

Mbali na watu waliomzunguka, bilionea huyo aliyependelea kujitenga na wengine aliishi maisha ya upweke. Hata hivyo, alisema hakuwahi kujihisi mpweke kwa kiwango kikubwa.

"Nimekuwa nikishughulika mno kiasi cha kutopata nafasi ya kujisikia mpweke. Ni kama mnyama anayekimbia kwenye gurudumu bila kusonga mbele. Unakimbia ili ubaki pale pale ulipo."

Pamoja na utajiri wake mkubwa, Getty hakuamini kuwa majukumu makubwa ya kifedha huleta furaha.

"Kuwa na majukumu makubwa ya kifedha hakumaanishi kuwa mtu atakuwa na furaha," alisema.

Whicker alipomwambia kuwa mara nyingi alionekana mwenye huzuni kiasi kwamba watu walidhani utajiri wake haukumletea furaha, Getty alieleza kwamba hisia hizo huenda zilitokana na mzigo wa majukumu aliyorithi.

"Huenda hiyo ikatokana na uzito wa majukumu. Tangu baba yangu alipofariki na kuniachia biashara, sijawahi kuwa na hali ile ile ya furaha niliyokuwa nayo hapo awali."

Alipoulizwa kuhusu baadhi ya nyakati alizozifurahia zaidi maishani, jibu lake halikuhusisha mabilioni ya dola, bali mambo rahisi kabisa.

"Nadhani baadhi ya nyakati zangu bora zaidi maishani hazikuhitaji kutumia pesa hata kidogo," alisema.

Akikumbuka muda aliotumia ufukweni akiteleza juu ya mawimbi, aliongeza:

"Mawimbi hayalipiwi. Mwangaza wa jua nao hauna gharama."