Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Saudi Arabia yadungua kombora lililorushwa na Wahouthi kuelekea Riyadh

Mvutano kati ya Saudi Arabia na Wahouthi umeendelea kushuhudiwa licha ya juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo wa Yemen.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Tunakomea hapo kwaheri.

  2. Ombi la Argentina kuzuia mafuta ya Falkland lakataliwa

    Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari (ITLOS) inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imekataa jaribio la serikali ya Argentina la kuzuia mradi mkubwa wa uchunguzi wa mafuta karibu na Visiwa vya Falkland, eneo linalotawaliwa na Uingereza.

    Katika uamuzi uliotolewa Jumamosi kwa kura 18 dhidi ya 3, rais wa mahakama hiyo alieleza kuwa chombo hicho hakina mamlaka ya kisheria kuamua mizozo inayohusu umiliki wa ardhi.

    Argentina ilikuwa imetaka kusitishwa kwa mradi huo unaojulikana kama 'Sea Lion', ikidai kuwa hatua yoyote ya kiuchumi haipaswi kuchukuliwa wakati kukiwa na mzozo wa umiliki wa visiwa hivyo.

    Akijibu uamuzi huo, Rais wa Argentina, Javier Milei, alisisitiza kuwa hatua hiyo haihitimishi madai ya nchi yake, akisema, "Uamuzi huu si neno la mwisho," na kurejelea msimamo wa Buenos Aires kuwa visiwa hivyo ni mali ya Argentina.

    Kwa upande wake, serikali ya Uingereza ilikaribisha uamuzi huo kupitia taarifa ya pamoja ya Waziri wa Mambo ya Nje, Ed Miliband, na Mwanasheria Mkuu, Ellie Reeves.

    Viongozi hao waliitaka Argentina kuheshimu haki ya wakazi wa Visiwa vya Falkland kujiamulia mustakabali wao na kukomesha kile walichokiita "shinikizo pana la kiuchumi" dhidi ya eneo hilo.

    Mzozo huu wa hivi karibuni wa kidiplomasia unachochea upya mvutano wa kihistoria kati ya London na Buenos Aires, mataifa ambayo yaliingia katika vita vya siku 74 mwaka 1982 kugombea udhibiti wa visiwa hivyo.

  3. Nigeria, Tanzania zaungana kuongoza juhudi za kuboresha afya ya wanawake Afrika

    Mataifa ya Nigeria na Tanzania yanandaa kwa pamoja mkutano wa kwanza wa Afrika kuhusu afya ya wanawake, kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji na hatua madhubuti za kuboresha huduma za afya kwa wanawake na wasichana barani humo.

    Mkutano huo, wenye kaulimbiu ‘Nguvu kazi ya afya kwa uboreshaji wa afya ya wanawake’ , unatarajiwa kufanyika Jumanne ijayo katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 300, wakiwemo wakuu wa nchi na serikali, mawaziri wa afya, viongozi wa Umoja wa Afrika, wawekezaji na wataalamu wa afya.

    Majadiliano yataangazia afya ya uzazi, magonjwa yanayohusiana na mfumo wa uzazi wa wanawake, magonjwa yasiyoambukiza na changamoto za kiafya zinazowakabili wanawake wanapofikia ukomo wa hedhi.

    Waandaaji wanasema mkutano huo unalenga kupata ahadi kutoka kwa serikali na taasisi mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wanawake katika hatua zote za maisha yao.

    Waziriwa Afya na Ustawi wa Jamii wa Nigeria, Profesa Muhammad Ali Pate, amesema mkutano huo utatoa fursa kwa nchi za Afrika kubaini mapungufu katika mifumo yao ya afya, kuhamasisha rasilimali na kubadilishana uzoefu.

    "Mkutano wa Afya ya Wanawake Afrika ni jukwaa muhimu linalowakutanisha viongozi, watetezi wa haki, wataalamu, wasomi na wafadhili ili kubaini mapungufu, kuchochea hatua na kuwezesha nchi kujifunza kutokana na uzoefu wa nyingine," amesema.

    Ameongeza kuwa viongozi wa Afrika wana wajibu wa kuamua vipaumbele vyao katika sekta ya afya na kuhakikisha vinazingatiwa.

    Ushirikiano huo unaunganisha mataifa mawili yenye marais wanaotajwa kuwa vinara haswa kwenye afya ndani ya jumuiya ya Umoja wa Afrika.

    Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ni Balozi wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia Rasilimali Watu katika sekta ya afya na utoaji wa huduma za afya kwa jamii, huku Rais wa Tanzania, Samia Suluhu, akiwa Balozi wa Umoja huo anayeshughulikia Afya ya Mama na Mtoto.

    Kwa mujibu wa waandaji, Tanzania inatumia nafasi ya Rais Samia kuendeleza utekelezaji wa mpango kabambe wa Umoja wa Afrika wa mwaka 2026–2030, unaolenga kuimarisha afya ya uzazi, mama, watoto wachanga, watoto na vijana

    Rais Samia alizindua mpango huo mapema wiki hii katika Mkutano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

    Mpango huo uliweka malengo makuu matatu yanayopaswa kufikiwa ifikapo mwaka 2030: kumaliza uzazi wa nyumbani, kuzuia vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuepukika, na kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo.

    Hata hivyo, kuelekea mkutano ujao, Mshauri Maalumu wa Rais wa Tanzania kuhusu Afya ya Mama na Mtoto, Ummy Mwalimu, amesema ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ni muhimu katika kuhakikisha ahadi za Afrika zinageuzwa kuwa matokeo yanayoonekana.

    Amesema kufikiwa kwa malengo hayo kutategemea uwepo wa wahudumu wa afya wa mstari wa mbele wenye mafunzo na vifaa vya kutosha, mifumo madhubuti ya kuwaelekeza wagonjwa kwenye vituo vinavyoweza kutoa huduma zaidi, pamoja na kuimarisha huduma za afya katika jamii.

    Rais Samia alitaja mafanikio ya Tanzania katika kupunguza vifo vya uzazi, akisema uwiano wa vifo vya wajawazito ulikuwa 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16, kabla ya kushuka hadi 104 mwaka 2022.

    Mbali na masuala ya ujauzito na uzazi, mkutano huo unalenga kupanua mjadala kuhusu afya ya wanawake ili kujumuisha changamoto zinazowakabili katika hatua mbalimbali za maisha yao.

    Mshauri Mwandamizi Maalumu wa Rais wa Nigeria kuhusu Afya ya Wanawake, Dk Adanna Steinacker, amesema afya ya wanawake imekuwa ikipewa uzito mdogo kwa muda mrefu, huku mara nyingi ikihusishwa zaidi na kipindi cha ujauzito na uzazi.

    Mkutano huo pia utaangazia maeneo matatu makuu: ubunifu, ufadhili na utoaji wa huduma. Waandaaji wanatarajia kupata ahadi za awali kutoka kwa serikali na taasisi mbalimbali, ikiwemo kuchukua hatua dhidi ya magonjwa ya mfumo wa uzazi wa wanawake ambayo hayajapewa kipaumbele cha kutosha.

    Shirika la Pathfinder International linashiriki kama mshirika mkuu wa kitaalamu, likisaidia kuandaa programu ya mkutano, kujenga ushirikiano wa kimkakati na kuunganisha ahadi za kisiasa na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji.

    Waandaaji wanasema wanataka mkutano huo uwe mwanzo wa ushirikiano endelevu kati ya nchi za Afrika na kuweka mfumo wa kuwajibishana katika kuboresha afya ya wanawake hata baada ya mkutano kumalizika.

  4. Wanafunzi 10 wafariki katika mlipuko Afghanistan

    Takribani wanafunzi 10 wameuawa na wengine 110 kujeruhiwa kufuatia mlipuko karibu na shule moja nchini Afghanistan, msemaji ameiambia BBC.

    Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya serikali ya Taliban, tukio hilo lilitokea Jumamosi asubuhi katika eneo la Anderseir mjini Asadabad, makao makuu ya mkoa wa Kunar.

    Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Abdul Mateen Qani alisema kuwa kulingana na uchunguzi wa awali, mlipuko huo ulisababishwa na "uzembe na kutokuwa makini" katika ghala la vilipuzi linalomilikiwa na kampuni za uchimbaji madini zilizopo karibu.

    Aliongeza kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea.

    Mkurugenzi wa utamaduni na habari wa mkoa huo, Sami ul Haq Bayan, alisema mlipuko huo ulitokea katika nyumba moja karibu na Shule ya Kati ya Shagai mjini Asadabad, wakati vilipuzi vilipokuwa vikiandaliwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini na kulipua miamba, shirika la habari la AFP linaripoti.

    Shirika la habari la Associated Press pia limemnukuu afisa huyo akisema kuwa hadi watu 15 waliojeruhiwa bado wamelazwa hospitalini, huku wengine wakiruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata matibabu.

    Picha kutoka ndani ya darasa lililoharibika zinaonyesha vipande vya vioo vilivyovunjika na vifusi vilivyotapakaa karibu na viatu pamoja na mikoba ya shule iliyoachwa hapo.

  5. Mwanamieleka wa Australia Bronson Reed afariki dunia

    Mwanamieleka wa kulipwa Bronson Reed amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 38, shirika la World Wrestling Entertainment (WWE) limetangaza.

    Kampuni hiyo imesema mwanamieleka huyo, ambaye jina lake halisi ni Jermaine Haley, alifariki Ijumaa kutokana na matatizo ya kiafya, lakini haikutoa maelezo zaidi.

    Katika kutoa heshima za mwisho, WWE iliongeza: "Jermaine alikuwa mtu mwenye haiba kubwa na ya kipekee ndani ya WWE, lakini muhimu zaidi, alikuwa mtu wa ajabu, mtu aliyeijali sana familia yake, na mfanyakazi mwenza aliyependwa na wengi."

    Pia walitoa rambirambi kwa familia ya mwanamieleka huyo raia wa Australia, wakiwemo mke wake Paige, ambaye ni mjamzito.

    Haley alienziwa katika hafla ya WWE iliyofanyika Akins Ford Arena huko Athens, Georgia, siku ya Ijumaa.

    Tukio hilo lilianza kwa ishara ya kupigwa kengele mara 10 kwa ajili ya Haley, na katika pambano lake, mwanamieleka kutoka Canada, Kevin Owens, alivaa utepe mkononi ulioandikwa "Bronson" alipoingia ulingoni.

    Owens alisema Haley alipenda sana kufanya maonyesho hayo.

    Soma pia:

  6. Washambuliaji wenye silaha wateka meli ya mizigo nje ya pwani ya Yemen - ripoti

    Shirika la Uendeshaji Biashara ya Baharini la Uingereza (UKMTO) limeripoti kwamba washambuliaji wenye silaha wameteka nyara meli ya mizigo nje ya pwani ya kusini mwa Yemen.

    Shirika hilo lilitangaza: "Watu wasio na idhini wanadhibiti meli hiyo.

    Mamlaka husika zimearifiwa kuhusu shambulio hilo."

    Mamlaka ya Uendeshaji Biashara ya Baharini ya Uingereza ilisema washambuliaji hao walipanda meli ya mizigo takribani kilomita 120 (maili 70) kusini magharibi mwa eneo la Balhaf nchini Yemen.

    Meli katika eneo hilo zinashauriwa kuendelea kwa tahadhari. Tangu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari, ambayo yalisababisha kuanza kwa vita katika Mashariki ya Kati.

    Meli zinazopita karibu na Rasi ya Arabia pia zimekuwa zikikabiliwa na mapigano ya risasi na mashambulizi ya mara kwa mara ya kulipiza kisasi.

    Soma zaidi:

  7. Jeshi la Marekani 'lazuia ndege zisizo na rubani' karibu na kambi ya anga ya Uingereza

    Financial Times imeripoti kwamba jeshi la Marekani limezuia ndege sita zisizo na rubani zilizokaribia kambi ya anga ya Uingereza katika kundi mwezi huu.

    Ripoti hiyo inasema Iran inashukiwa kuhusika katika tukio hilo. Financial Times iliripoti eneo la tukio hilo kama Kambi ya Anga ya Laxmanith ya Jeshi la Anga la Royal Air Force, ambayo iko kaskazini mashariki mwa London kijiografia.

    Gazeti hilo, likiwanukuu watu wanaofahamu jambo hilo, liliandika kwamba Marekani ilitumia teknolojia ya kupambana na ndege zisizo na rubani kukabiliana na ndege hizo zisizo na rubani, lakini vikosi vya Uingereza au Marekani havikuweza kuzipata ndege hizo zisizo na rubani.

    Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Uingereza aliiambia Reuters: "Polisi wa Wizara ya Ulinzi na polisi wa kikanda walifanya kazi kwa karibu na vikosi vya usalama vya Jeshi la Anga la Marekani kuchunguza ripoti za shughuli zisizo na rubani zisizoidhinishwa katika Kambi ya Anga ya Lakenheath mnamo Novemba 13.

    Hali hiyo ilitatuliwa haraka na Lakenheath ikarudi katika usalama wa kawaida na ulinzi wa nguvu." Ikulu ya White House na Idara ya Ulinzi ya Marekani hawajajibu.

    Wakati wa tukio hilo, vikosi vya Jeshi la Anga la Marekani vilivyokuwa kwenye kambi hiyo vilijibu "shughuli zisizo na rubani zisizo na rubani zinazoshukiwa."

    Msemaji wa Jeshi la Anga la Marekani alisema wakati huo kwamba hakuna wanajeshi, ndege au miundombinu ya kambi iliyojeruhiwa.

    Mnamo Septemba, tukio katika Kambi ya Anga ya Farford, kambi nyingine ya Uingereza inayotumiwa na Jeshi la Anga la Marekani, lilisababisha kuondolewa kwa ndege za kivita za Marekani aina ya B-1 kutoka kambi hiyo kutokana na tishio linalohusiana na Iran.

    Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekana kuhusika kokote katika tukio la Farford au vitendo vingine vya uadui nchini Uingereza.

    Soma pia:

  8. Mashtaka 241 yawasilishwa mahakamani Iran dhidi ya Marekani na Israel

    Afisa mwandamizi wa mahakama nchini Iran amesema kuwa mashtaka 241 yamewasilishwa katika mahakama za makosa ya jinai nchini humo dhidi ya Marekani na Israel, yakihusiana na migogoro ya kijeshi iliyoelezwa na Tehran kuwa vita vya siku 12 na siku 40.

    Nasser Siraj, Katibu wa Makao Makuu ya Haki za Kibinadamu na Naibu Waziri wa Masuala ya Kimataifa katika Idara ya Mahakama ya Iran, alisema lengo la hatua hiyo ni kufungua kesi zinazohusu madai ya uhalifu wa kivita na kutafuta fidia kwa wahanga.

    Kwa mujibu wa Siraj, mashtaka hayo yanashughulikiwa katika mahakama mbalimbali nchini Iran kama sehemu ya mchakato wa kisheria unaolenga kuwawajibisha wanaodaiwa kuhusika na mashambulizi hayo.

    Wakati huohuo, kesi inayohusiana na shambulio la kijeshi dhidi ya Shule ya Minab ilisikilizwa wiki iliyopita katika Mahakama ya Juu mjini Tehran.

    Marekani na Israel hazijatoa maoni ya haraka kuhusu hatua hiyo ya kisheria iliyotangazwa na maafisa wa Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Uturuki yaweka Halk TV chini ya usimamizi, mmiliki alalamika

    Mamlaka za Uturuki "zimedhibiti" moja ya vituo vya habari vinavyotazamwa zaidi nchini humo, mmiliki wake anayeishi London ameiambia BBC.

    Akizungumza na kipindi cha Newshour cha BBC, Cafer Mahiroğlu alisema watu tisa wanaohusishwa na Halk TV walikamatwa wiki hii wakikabiliwa na mashtaka yakiwemo utakatishaji fedha, rushwa na kusambaza taarifa za kupotosha.

    Mahiroğlu alisema baadhi ya jamaa wa familia yake ni miongoni mwa waliokamatwa wakati kituo hicho kinachounga mkono upinzani kilipowekwa chini ya usimamizi wa serikali mwezi uliopita. Aliongeza kuwa madai dhidi yake na Halk TV ni "ya uongo kabisa".

    Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Istanbul ilisema watangazaji wawili wa zamani wa habari wa kituo hicho walikuwa miongoni mwa kundi la hivi karibuni la watu waliowekwa kizuizini.

    Katika taarifa, waendesha mashtaka waliwashutumu watangazaji hao kwa kutengeneza "taarifa za uongo" kwa malipo ya fedha.

    Mamlaka pia zimetoa hati ya kukamatwa kwa mratibu wa habari wa kituo hicho, Kürşad Oğuz, ambaye "yuko nje ya nchi", taarifa hiyo ilisema bila kubainisha alipo.

    Mahiroğlu aliiambia BBC kuwa anaweza kufungwa jela iwapo atajaribu kurejea Uturuki.

    "Serikali inataka kudhibiti vyombo vyote vya habari... Nina wasiwasi zaidi kuhusu nchi yangu na demokrasia yangu kuliko kuhusu kituo changu," alisema.

    Makao makuu ya Halk TV yalivamiwa na mamlaka za Uturuki mwezi uliopita, jambo lililosimamisha matangazo ya moja kwa moja ya kituo hicho. Hili ni tukio la hivi karibuni katika mfululizo wa hatua dhidi ya vyombo vya habari vinavyoonekana kuikosoa serikali ya Rais Tayyip Erdoğan.

    Baadaye serikali ilimteua msimamizi mpya kuendesha kituo hicho.

    Serikali ya Erdoğan inadhibiti sehemu kubwa ya vyombo vya habari nchini humo, ambayo imeorodheshwa miongoni mwa nchi zenye viwango duni zaidi vya uhuru wa vyombo vya habari duniani, ingawa serikali inasisitiza kuwa haiwakamati wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa kutekeleza shughuli za uandishi wa habari.

    Hata hivyo, rais huyo ameongeza hatua dhidi ya sauti za upinzani tangu ushindi wake mwembamba katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2023.

  10. Taharuki baada ya mabawa ya ndege za American Airlines kugusana kabla ya kuruka

    Ndege mbili za American Airlines ziligusana ncha za mabawa katika Uwanja wa Ndege wa Kitaifa wa Ronald Reagan Washington wakati zikielekea kwenye njia ya kurukia ndege siku ya Ijumaa.

    Ncha za mabawa ya ndege hizo ziligusana mwendo wa saa saa kumi na moja na dakika kumi kwa saa za Mashariki mwa Marekani (22:10 GMT), kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA). Hakuna majeruhi walioripotiwa, na FAA imesema itachunguza tukio hilo.

    American Airlines ilisema ndege zote mbili zilirejeshwa kwenye lango la kuondokea na kuondolewa kwenye ratiba ili kukaguliwa.

    Tukio kama hilo limewahi hilo kutokea katika uwanja huohuo ambapo watu 67 walifariki katika mgongano kati ya ndege ya abiria na helikopta ya jeshi mwezi Januari 2025.

    “Ndege ya American Airlines nambari 638 iligusa bawa la ndege ya American Airlines nambari 2152 wakati zinaelekea kwenye njia ya kurukia ndege kwa ajili ya kuondoka,” FAA ilisema.

    Katika rekodi ya mawasiliano ya redio, waongozaji wa trafiki ya anga wanasikika wakisema ndege mbili aina ya Boeing 737 ziligusana kwenye eneo la kuendeshea ndege ardhini. Kisha waliomba huduma za dharura na zimamoto kuelekezwa kwenye ndege hizo kabla ya kuziagiza kurejea langoni.

    American Airlines ilisema “ncha za mabawa za ndege zote mbili aina ya Boeing 737-800 ziligusana”.

    Mmoja wa abiria wa safari nambari 2152 iliyokuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa O'Hare mjini Chicago aliiambia BBC kwamba alihisi “mtikisiko mkubwa” upande wa kulia wa ndege wakati ilipokuwa ikielekea kwenye njia ya kurukia ndege.

    Ndege ya pili nambari 638, ilikuwa ikielekea uwanja wa ndege wa Dallas-Fort Worth.

    Abiria huyo alisema ndege ilitikisika kwa nguvu baada ya kugusana na kwamba alisikia sauti za mshangao kutoka kwa abiria wengine. Alielezea tukio hilo kuwa la “kushtua”, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.

    Alipotazama nje kupitia dirishani, alisema aliona kipande kikiwa kimeanguka ardhini. Alisema kilionekana kuwa ncha ya bawa, huku bawa la ndege nyingine likiwa limeingiliana na la ndege aliyokuwa ameabiri.

    BBC imewasiliana na American Airlines kuhusu taarifa za ncha ya bawa iliyoharibika.

    Walipokuwa wakirejea langoni, abiria huyo alisema aliona gari la huduma za uwanja wa ndege likichukua kipande hicho kilichoanguka.

    Abiria huyo alisema ukweli kwamba hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hilo kutokea katika uwanja huo wa ndege ulikuwa “wa kutisha kwa hakika”.

    Mwaka uliopita, kulitokea mgongano angani kati ya ndege nyingine ya American Airlines na helikopta ya jeshi katika Uwanja wa Reagan National.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Wahudumu wawili wa MSF wauawa katika shambulio Israel Gaza

    Wafanyakazi wawili wa shirika la misaada ya matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF) wameuawa katika shambulio la Israel huko Gaza, kulingana na shirika hilo.

    MSF ilisema shambulio hilo lililenga moja kwa moja mojawapo ya kliniki za shirika hilo, ambayo eneo lake linqjulikana na jeshi la Israel.

    Katika taarifa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema watu hao wawili walikuwa wanamgambo wa Hamas "waliokuwa wakifanya kazi kama walinzi katika kliniki inayoendeshwa na MSF". IDF iliongeza kuwa shambulio hilo "halikulenga hospitali" na halikusababisha uharibifu wowote kwa miundombinu ya matibabu.

    Kwa mujibu wa jeshi hilo, watu hao wawili walikuwa wakifanya kazi kama walinzi katika kliniki hiyo, huku mmoja wao akitajwa kuwa kamanda wa kitengo cha mizinga cha Hamas.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, shirika hilo limesema alama zake zilikuwa zimewekwa wazi kwenye majengo husika na eneo la kliniki lilikuwa limewasilishwa kwa jeshi la Israel.

    Hata hivyo, jeshi la Israel limekanusha kulenga hospitali au kuharibu miundombinu ya matibabu wakati wa operesheni hiyo.

    Katika ujumbe uliochapishwa kwenye Telegram, jeshi hilo limesema tukio hilo linaonyesha kile lilichodai kuwa ni ushawishi wa Hamas ndani ya mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi katika Ukanda wa Gaza.

    Tukio hilo linakuja huku mapigano kati ya Israel na Hamas yakiendelea katika maeneo mbalimbali ya Gaza, huku mashirika ya misaada yakionya kuhusu hatari zinazokabili huduma za afya katika eneo hilo.

  12. Saudi Arabia yadungua kombora lililorushwa na Wahouthi kuelekea Riyadh

    Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umetangaza kuwa umefanikiwa kudungua kombora la masafa marefu lililorushwa na waasi wa Kihouthi kuelekea mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.

    Taarifa hiyo ilitolewa Jumamosi, saa chache baada ya vyombo vya habari vinavyohusishwa na Wahouthi kuripoti mashambulizi ya anga yaliyofanywa na vikosi vya Saudi Arabia nchini Yemen.

    Msemaji wa muungano huo, Turki al-Maliki, alisema mifumo ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kulizuia na kuliangamiza kombora hilo kabla halijafikia lengo lake katika eneo la Riyadh.

    Wakati huohuo, vyombo vya habari vya Wahouthi vilidai kuwa mashambulizi ya Saudi Arabia katika eneo la makazi la Bir Abu nchini Yemen yalisababisha uharibifu wa nyumba nane na maduka matatu, huku watu 13 wakijeruhiwa.

    Mvutano kati ya Saudi Arabia na Wahouthi umeendelea kushuhudiwa licha ya juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo wa Yemen uliodumu kwa miaka kadhaa.

    Soma zaidi:

  13. Natumai hujambo.