"Ingekuwa rahisi zaidi kuoa au kuolewa, lakini kwa sasa nitahifadhi mayai yangu ya uzazi" Mbunge wa Marekani

Chanzo cha picha, Alexandria Ocasio-Cortez
Wiki iliyopita, Mbunge wa New York mwenye umri wa miaka 36, Alexandria Ocasio-Cortez, alitangaza kwenye mitandao ya kijamii uamuzi wake wa kuhifadhi mayai yake ya uzazi. Alisema hakutaka kulifanya jambo hilo kuwa siri kwa wapiga kura wake na wafuasi wake, kwani aliona ni muhimu "kuhalalisha na kuweka wazi" mazungumzo kuhusu utaratibu huo.
Kufuatia tangazo hilo, Ocasio-Cortez alikosolewa pamoja na kulaaniwa na wanasiasa na wapiga kura wenye msimamo wa kihafidhina. Maoni makali hasa yalitoka kwa wafuasi wa Rais Donald Trump.
Alexandria Ocasio-Cortez alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha akichomwa sindano ya homoni, ambayo ni sehemu ya mchakato wa maandalizi ya kuhifadhi mayai ya uzazi. Katika video hiyo, anazungumzia gharama za kuhifadhi mayai nchini Marekani, dawa zinazotumika, na utaratibu wenyewe.
Kulingana na mwanasiasa huyo, "alifikiria sana kuhusu uamuzi huu" na "aliweka akiba ya fedha" kwa ajili ya utaratibu huo. Alikiri kuwa, kwa kuamua kuhifadhi mayai yake, alitaka kuhisi kuwa na udhibiti wa maisha yake mwenyewe.
Video hiyo ilirekodiwa na kuchapishwa saa chache tu kabla ya mwanasiasa huyo kuonekana katika kipindi cha "This Week" cha ABC News. Wakati wa mahojiano hayo, Ocasio-Cortez alisema kuwa bado kuna uwezekano wa yeye kugombea urais mwaka wa 2028.
Katika mahojiano mengine ya baadaye na ABC, alieleza kuwa alitaka "kuhalalisha na kufanya kuwa ya kawaida" mazungumzo kuhusu kuhifadhi mayai ya uzazi. Alisema jambo hili ni muhimu, hasa katika hali ya sasa ya kisiasa.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, chapisho la kwanza la mwanasiasa huyo kuhusu kuhifadhi mayai ya uzazi lina maoni zaidi ya 1,250, mengi yakiwa ya kuunga mkono na kutia moyo.
"Nilipokuwa na umri wa miaka 27, ilinibidi kufanyiwa utaratibu wa kuchukuliwa mayai ya uzazi kutokana na kugunduliwa kuwa na saratani. Wanawake wengi wenye umri mdogo wanakabiliwa na changamoto hii, na pia wanataka kupata watoto baadaye, kwani tiba za Chemotherapy hupunguza uwezekano wa mtu kuzaa kwa asilimia 50. Kwa muda mrefu vijana hawa hulazimika kulipia gharama hizi wenyewe kwani hailipwi na bima ya afya" aliandika mfuasi mmoja.
Licha ya hatari , ukosoaji mkubwa hasa kutoka kwa wanasiasa, utaratibu wa kuhifadhi mayai ya uzazi unazidi kuwa wa kawaida. Jennifer Eaton, rais wa Society for Assisted Reproductive Technology, aliliambia gazeti la New York Times kuwa, idadi ya wanawake wanaotaka kuhifadhi mayai yao ya uzazi imeongezeka zaidi ya mara sita kati ya mwaka wa 2014 na 2024, kutoka 6,090 hadi 38,930.
Imetafsiriwa na Laillah Mohammed












