Rais wa Marekani Donald Trump amesema hatasita kuishambulia tena Iran akilazimika kufanya hivyo, ili kuizuia mpango wake wa nyuklia.
Katika mahojiano na kituo cha WBBC77, Bw. Trump alisema kuwa kama si hatua alizochukua, Israel na Mashariki ya Kati zingekuwa zimeshaangamizwa kufikia sasa.
Katika mahojiano hayo, alikiri kuwa aliamuru shambulio dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran wakati nchi hiyo ilipokuwa imesalia na wiki mbili tu kabla ya kutengeneza silaha ya nyuklia.
Bw. Trump alisema kuwa licha ya kile kinachoripotiwa kwenye vyombo vya habari, Marekani ndiyo inayodhibiti Mlango-bahari wa Hormuz.
Alisisitiza tena kuwa uwezo wa Iran wa makombora na ndege zisizo na rubani (droni) umedhoofishwa sana na uchumi wake uko ukingoni mwa kuporomoka.
Bw. Trump alilitaja makubaliano ya JCPOA kuwa "janga" na kuongeza kuwa kujiondoa katika makubaliano hayo ni jambo la lazima ili kuizuia Iran kupata silaha ya nyuklia.
Aliiita Iran kuwa "mdhalimu wa Mashariki ya Kati" na kusema: "Kama tulivyoona, Iran iliwahi kushambulia hata nchi kama Qatar, Bahrain, Kuwait, na UAE ambazo zilikuwa na uungaji mkono mdogo kwa Iran."
Rais wa Marekani alisisitiza kuwa kama Marekani isingechukua hatua za kijeshi, Iran ingeziharibu nchi hizo zote na ingekuwa ikijiandaa kushambulia Marekani.
FBI yamkamata mwanamke aliyepanga kulipua jengo la bunge Marekani
Chanzo cha picha, DOJ/FB
Shirika la Upelelezi la Marekani FBI limemkamata mwanamke mmoja wa New York ambaye inadaiwa alipanga kulipua jengo la Bunge ili kuwaua wabunge.
Waendesha mashtaka wanasema Jessica Bowie, 35, alikuwa mfuasi wa kundi la Islamic State.
Bi. Bowie pia anashtakiwa kwa kutoa msaada wa vifaa au rasilimali kwa shirika la kigaidi la kigeni.
Waendesha mashtaka wanasema Bi. Bowie "alifuatilia matukio katika jengo la Bunge mara kadhaa" na alikuwa amebeba bomu bandia na silaha isiyofanya kazi vizuri aliyopewa na maajenti wa FBI waliofichwa.
Kulingana na mashataka ya jinai, Bi. Bowie aliwaambia maafisa: "Nataka kuharibu sehemu kubwa ya jengo iwezekanavyo na kuwaua maseneta."
Haijabainika ikiwa ana mpango wa kujitetea dhidi ya mashtaka hayo.
Bi. Bowie, mkazi wa eneo la Albany kaskazini mwa New York, alidaiwa kufichua mipango yake na watoa habari wa FBI na alikuwa na maajenti walioifanya wanachama wa ISIS kwa wiki kadhaa.
Chanzo cha picha, DOJ/FBI
Maelezo ya picha, Jessica Bowie akinunua vifaa vya kutengenezea bomu katika duka la vifaa vya ujenzi la eneo hilo.
Waendesha mashtaka wanasema alichagua jengo la Bunge jijini New York katika eneo la Albany kwa sababu alidhani ingekuwa lengo rahisi zaidi kuliko White House.
Aliwaambia maafisa, "Nataka hili liathiri mfumo wa Marekani." Waendesha mashitaka wanasema alitembelea jengo hilo takribani mara tano katika misheni ya upelelezi kabla ya shambulio.
Makumi ya watu wafariki dunia baada ya boti kuzama kaskazini-magharibi mwa Nigeria
Chanzo cha picha, Reuters
Takriban watu 46 wamefariki dunia nchini Nigeria baada ya boti kuzama katika jimbo la Sokoto, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Maafisa wanasema boti hiyo iliaminika kubeba zaidi ya watu 70, wengi wao wakiwa watoto, na operesheni ya uokoaji inaendelea.
Msemaji wa polisi, Ahmad Rufai, ameimbia BBC siku ya Alhamisi kuwa miili 46 imepatikana karibu na Gorau katika eneo la Gorony.
Watu 16 wameokolewa, huku 15 wakiwa bado hawajapatikana.
Eneo hilo ni gumu kufikika, na vyombo vya usalama pamoja na huduma za dharura vinaelekea eneo la tukio, Rufai aliongeza.
Mashuhuda mmoja aliambia shirika la habari la Reuters kuwa anaamini watoto waliokuwemo ndani ya boti hiyo walikuwa wakisafiri na wamiliki wa mashamba pamoja na vibarua waliokuwa wakielekea kufanya kazi ya kuvuna mpunga.
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan, anayeshikiliwa gerezani, apelekwa hospitalini kwa matibabu
Chanzo cha picha, Reuters
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan, amewasili katika hospitali moja jijini Islamabad baada ya Mahakama ya Juu kuamuru kuwa aruhusiwe kutoka gerezani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.
Kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi huko Rawalpindi, ambako Bwana Khan amekuwa akishikiliwa kwa miaka mitatu.
Hii ndiyo nafuu kubwa zaidi ambayo Khan ameipata kutoka mahakamani tangu afungwe gerezani mwaka wa 2023 kwa tuhuma za ufisadi, ambazo anadai kuwa zilitokana na sababu za kisiasa.
Mbali na kuhamishiwa hospitalini, agizo hili la mahakama pia liliagiza kuwa Khan aruhusiwe kuonana na familia yake, jambo ambalo hajaliweza kulifanya kwa miezi kadhaa.
Usiku wa Jumanne, dada yake alimtembelea gerezani.
Chama cha kisiasa cha Khan, Tehreek-e-Insaf (PTI), kwa kawaida huwa cha kwanza kudai kuwa maamuzi ya mahakama yanayomkabili yamechochewa na siasa.
Hata hivyo, chama hicho hakijajihusisha hadharani na dhana kwamba uamuzi wa Mahakama ya Juu unaashiria kuwepo kwa hila za kisiasa nyuma ya pazia.
Khan alipatikana na hatia katika mashtaka ya ufisadi, ambayo anasema yalichochewa kisiasa.
Nchi za Magharibi zalaani mpango wa Israel wa kujenga makazi ya Walowezi Ukingo wa Magharibi
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mipango ya Israel ya kufungua zabuni za ujenzi wa takriban nyumba 1,200 za walowezi katika eneo lenye umuhimu wa kimkakati katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu imelaaniwa vikali na mataifa kadhaa ya Magharibi.
Katika taarifa ya pamoja, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, na Canada zilitaja uamuzi huo kuwa ''usiokubalika" na kuionya Israel kubatilisha mipango hiyo mara moja.
Makazi yote ya Walowezi ni haramu chini ya sheria za kimataifa na kutokana na shinikizo la kimataifa,
Israel ilisitisha kwa miongo kadhaa mipango ya kujenga makazi ya Walowezi katika eneo lijulikanalo E1 upande wa mashariki mwa Jerusalem.
Washirika wake wengi na Wapalestina walidai kuwa ujenzi huo ungedidimiza kwa kiasi kikubwa matumaini ya kufikiwa suluhisho la mataifa mawili, na kimsingi kuugawanya Ukingo wa Magharibi vipande viwili na kuitenga Jerusalem Mashariki.
Taarifa hiyo kutoka kwa washirika wa Israel wa Ulaya na Canada iliyochapishwa jana Alhamisi imesema "Wakati huu wa kukosekana kwa utulivu mkubwa katika Ukingo wa Magharibi kukiwa na viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa vya vurugu zinazofanywa na walowezi dhidi ya raia, na vizuizi vikubwa kwa uchumi wa Palestina, uamuzi huo wa kutaka kujenga makazi ya walowezi unatia wasiwasi mkubwa zaidi.
Katika taarifa tofauti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia alisema mpango huo unaleta "tishio la uwepo" kwa taifa linaloungana la Palestina. Msemaji wake Stephane Dujarric, amesema Katibu mkuu anatiwa wasiwasi mkubwa na hatua ya Israel.
"Katibu Mkuu amesikitishwa sana na ripoti za kuwepo makazi mapya haramu ya walowezi wa Israeli katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na zabuni mpya, zikiwemo za eneo la E1. Anatiwa wasiwasi mno na mipango hiyo ya kujengwa makazi eneo la E1, ambayo yatakata kabisa uhusiano kati ya kaskazini na kusini mwa Ukingo wa Magharibi.
Hali hiyo itakuwa na madhara makubwa kwa uhuru wa kujitawala katika maeneo ya Palestina na kutishia uwezekano wa kuwepo suluhisho la mataifa mawili''.
Mapema hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband pia alilaani vikali mpango huo wa Israel,mtizamo ambao ulimkera Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel.
Wizara ya nyumba ya Israel siku ya Jumatano wiki hii, ilitoa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 1,234 kati ya nyumba 3,401 zilizoidhinishwa na serikali ya Israel mnamo Agosti iliyopita. Inachukua takriban kilomita za mraba 12 kati ya Jerusalem Mashariki na makazi ya Maale Adumim.
Wakati wa kuzinduliwa kwake, Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich,mwanasiasa mwenye misimamo mikali na mlowezi,alisema wazo la kuwepo taifa la Palestina linafutwa.
Mwisho wa kupokea zabuni ni tarehe 19 Oktoba, siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Israel unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba,hatua inayoonekana kufanya iwe vigumu zaidi kwa serikali yoyote ya baadaye kubatilisha zabuni zilizotolewa.
Israel imejenga takriban makazi 160 yanayohifadhi Wayahudi laki saba tangu ilipokalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ardhi ambayo Wapalestina wanaitaka, pamoja na Gaza, kwa ajili ya taifa la baadaye linalotarajiwa.
Inakadiriwa kuwa Wapalestina milioni 3.3 wamelazimika kuishi sambamba na Wayahudi hao. Licha ya upinzani mkali wa kimataifa, serikali ya Israel imeruhusu makazi hayo kukua.