Mji unaomtengenezea Trump makombora

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mkazi mmoja anasema kuwa katika eneo la Kingsport, Tennessee, lililoko katika ukanda wa milima ya Appalachian, kuna makanisa mengi kiasi kwamba inaonekana kana kwamba kuna kanisa katika kila barabara.
Ukristo una nguvu kubwa katika eneo hili linalokaliwa na tabaka la wafanyakazi. Ubao wa matangazo juu ya Ukumbi wa kihistoria wa Lamplight Theater katikati ya mji huo unasomeka hivi: "Yesu anatangulizwa katika mambo yote."
Hata hivyo, wakati makanisa zaidi ya 300 katika eneo hilo yakihudumia mahitaji ya kiroho ya mji huo wenye wakazi 58,000, kuna taasisi nyingine ambayo pia inachochea uchumi wa mji huo.
Kiwanda cha Holston Army Ordnance kinazalisha vilipuzi vinavyotumika katika makombora ya Patriot, vichwa vya makombora, na silaha nyingine nzito, huku kukiwa na vita vya gharama kubwa na vya muda mrefu kati ya Marekani na Iran.
Vita hivyo na athari zake katika nyanja mbalimbali kuanzia bei ya mafuta hadi chakula vimesababisha kushuka kwa kiasi kikubwa kwa umaarufu wa Rais wa Marekani Donald Trump.
Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kiwango cha kukubalika kwake kimeshuka hadi asilimia 32, kiwango cha chini kabisa tangu aingie madarakani mwezi Januari 2025.
Hii ni kushuka kwa asilimia 14 ikilinganishwa na mwanzo wa kipindi cha urais wa Trump, na wahojiwa wengi wa chama cha Republican wametaja kutoridhishwa na sera zake kama sababu ya kutounga mkono utendaji wake.

Chanzo cha picha, Eloise Alanna
Sababu mbili kuu za kupungua kwa umaarufu wa rais ni gharama ya maisha na vita dhidi ya Iran, masuala haya mawili yanachukuliwa na wengi kuwa yameunganishwa. Vita hivyo vimesababisha bei ya petroli nchini Marekani kupanda na kuzidi dola 4 kwa pipa, ongezeko kubwa linalosababisha gharama nzito kwa biashara yoyote inayotegemea usafirishaji.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, huko Kingsport, uungaji mkono kwa Donald Trump umechukua mkondo kidini. Jiji hilo limemchagua Trump kwa wingi wa kura katika chaguzi zote tatu za urais. Jimbo la Tennessee, ambalo limekuwa likiunga mkono Chama cha Republican kwa zaidi ya miaka 25, nalo limefuata mkondo huo.
Kuhusu suala la vita na Iran, wakazi wengi ama wanaunga mkono hatua za kijeshi waziwazi au wanajaribu kuhalalisha ulazima wake, licha ya ahadi ya mara kwa mara ya Trump wakati wa kampeni ya "kumaliza vita."
"Ikiwa inaweza kumzuia mtu kupata bomu la nyuklia, ninaunga mkono kikamilifu," anasema Pam Robinson, mwenye umri wa miaka 65, ambaye amefanya kazi katika kiwanda cha kemikali cha eneo hilo kwa miaka 20.
"Sababu kuu ya sisi kuwepo huko, tukijaribu kudhibiti hali, ni kuzuia vitisho hivi kufika majumbani mwetu na nchini mwetu," anasema David Carter, mstaafu wa kijeshi mwenye ndevu ambaye huigiza kama Santa Claus wakati wa Krismasi.
Wengine huzungumza kwa uwazi zaidi.
"Kiukweli, nadhani tunapaswa kulisawazisha eneo hilo na kumaliza kabisa suala hilo," alisema James Kemper, mstaafu wa kijeshi mwenye umri wa miaka 63 ambaye alitoka dukani akiwa amevaa fulana yenye picha ya Trump.
Wanajeshi waliostaafu ni takriban asilimia 10 ya wakazi wa eneo hili, na familia nyingine nyingi pia zina wanachama wanaotumikia katika jeshi.
Pam Robinson, Mkristo mcha Mungu na mpiga kura huru ambaye anasema imani yake huathiri maamuzi yake ya kisiasa, anaamini kuwa umbali kati ya uwanja wa vita na Marekani unaweza kuwa sababu inayowafanya wakazi wa eneo hilo kutokuwa na malalamiko mengi dhidi ya Trump.
"Acha nikuambie hivi," anasema, "kama vita hivyo vingekuwa vya mapigano ya ana kwa ana na watu wengi zaidi wangeuawa, watu wangepinga vikali sana."

Chanzo cha picha, Eloise Alanna
Nafasi ya Kingsport kama mojawapo ya vituo vikuu vya utengenezaji wa zana za kivita nchini Marekani, pamoja na ukweli kwamba kiwanda cha Holston ndicho chanzo pekee cha ndani cha vilipuzi na kemikali muhimu za kurushia makombora, vimewapa wakazi wa mji huo mtazamo tofauti kuhusu vita dhidi ya Iran.
Kiwanda hicho kinaajiri takriban watu elfu moja na ni mojawapo ya viwanda vikubwa vinavyojitokeza wazi katikati ya mandhari ya kijani kibichi ya Milima ya Appalachian.
"Iwe tuko vitani au la, kiwanda kinaendelea kufanya kazi. Hiyo ndiyo hali halisi," alisema Daniel Overstreet, mwenye umri wa miaka 53, akiwa amesimama karibu na pikipiki yake aina ya Harley-Davidson katikati ya mji wa Kingsport.
Anaamini kuwa Donald Trump na utawala wake "wamefanya kazi nzuri," lakini "kuna watu wengi wanaotaka kupinga msimamo wake."
"Alisema angeidhibiti bei ya mafuta, na alifanya hivyo kwa muda. Alisema angepunguza bei ya chakula, lakini hana mamlaka nayo. Kimsingi, rais ni kama kibaraka mikononi mwa Bunge la Wawakilishi na Seneti," anasema Daniel Overstreet.
"Mikono yake imefungwa kwa kiasi fulani," anaongeza.
Sio kwamba watu hapa hawakulalamikii bei ya juu ya mafuta na chakula, mfumuko wa bei, na matatizo mengine ya kiuchumi, ni kwamba hawamwajibishi Trump kwa matatizo hayo.
"Amefanya vizuri katika baadhi ya maeneo, lakini nadhani anahitaji kushauriana na washauri wake kuhusu masuala fulani. Nadhani amepewa ushauri usio sahihi katika baadhi ya mambo," anasema Pam Robinson.
Hata hivyo, Trump mwenyewe ndiye aliyeamuru shambulio dhidi ya Iran mwezi Februari 2026 baada ya mazungumzo kufeli. Katika video ya dakika nane iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, alisema, "Lengo ni kuwalinda watu wa Marekani kwa kuondoa vitisho vya karibu kutoka kwa utawala wa Iran," na kudai kuwa Iran "haitawahi kumiliki silaha ya nyuklia."

Chanzo cha picha, Eloise Alanna
William Bogle, mhubiri wa Kikristo mwenye umri wa miaka 75, amempigia kura Donald Trump katika kila uchaguzi na anaamini kuwa rais huyo "anafanya kazi nzuri," ingawa anasema mkewe hulazimika kuwa mwangalifu sana na kubana matumizi ili kumudu gharama za mahitaji ya nyumbani.
"Trump anahitaji tu kufanya vizuri zaidi katika baadhi ya maeneo kuliko anavyofanya sasa," anasema.
William Bogle anaongeza, "Najua anataka nchi ipige hatua mbele."
Uungaji mkono huu thabiti unaakisi hali halisi ya ndani zaidi ambayo wakati mwingine hufichwa na vichwa vya habari vya matokeo ya tafiti za maoni.
Ingawa Trump amepoteza sehemu ya uungaji mkono miongoni mwa Wanarepublican wa msimamo wa kawaida na wapiga kura huru, kundi lake kuu la wafuasi, wale wanaojitambulisha kwa kaulimbiu ya "Make America Great Again" (Kuifanya Marekani Kuwa Kubwa Tena), linaendelea kumuunga mkono kwa uthabiti zaidi.
Wakati watu wengi nchini Marekani wakifuatilia athari za kupungua kwa umaarufu wa Trump kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba, katika maeneo ya Kusini mwa Marekani yenye msimamo wa kihafidhina na wa kidini, eneo linalojulikana kama "Bible Belt" wapiga kura wengi hawana chaguo jingine isipokuwa kuwaunga mkono Wanarepublican.
Wapiga kura walipojitokeza hivi karibuni kwa ajili ya uchaguzi wa majimbo, mgombea mmoja tu wa chama cha Democratic ndiye aliyekuwepo kwenye karatasi ya kupigia kura. Kati ya maeneo 11 ya uchaguzi wa wajumbe wa halmashauri ya kaunti, saba yalikuwa na wagombea wa Republican, na baadhi yao hawakuwa na wapinzani.
Wakazi wengi wanasema hawawezi na hawatampigia kura mgombea wa chama pinzani kwa sababu za kimaadili. Wanaona suala la utoaji mimba kuwa jambo muhimu zaidi katika uamuzi wao; vilevile, kupinga ujamaa na sera zinazounga mkono mabadiliko ya kijamii kuhusiana na haki za kijamii, ubaguzi, na masuala ya jinsia ni mambo muhimu kwao.
David Carter, mwenye umri wa miaka 66 babu, Mkristo mcha Mungu, na mstaafu wa jeshi, anasema kuwa masuala haya yana uzito mkubwa kuliko ukosoaji wowote wa kibinafsi anaoweza kuwa nao dhidi ya Trump.
Anakubali kuwa Trump anahitaji kuonyesha unyenyekevu zaidi, lakini anasisitiza kuwa atazingatia tu mgombea anayeunga mkono "maadili" yanayokubalika na watu wa eneo hilo.
Anasema hii inamaanisha, kwa mfano, kupinga utoaji mimba.

Chanzo cha picha, Eloise Alanna
Watu wenye mitazamo huru zaidi pia wanaishi Kingsport, lakini ni wachache na kwa kawaida huwa na mwelekeo mdogo wa kuelezea maoni yao hadharani.
Adam Teague, msanii wa kuchora tatoo mwenye umri wa miaka 44, ni shoga na mwanachama wa chama cha Democrats; anafanya kazi katikati ya mji wa Kingsport na ana tatoo nyingi mwilini mwake.
"Kabla Trump hajaingia madarakani, nilikuwa nikivaa mavazi yenye rangi za upinde wa mvua na vitu kama hivyo," anasema Adam Teague, ambaye alilelewa katika familia ya Kibaptisti. "Lakini sasa ninakuwa mwangalifu zaidi, ili nijihisi salama zaidi."
Trump alishinda uchaguzi wa mwaka 2024 kwa kiasi fulani kutokana na uwezo wake wa kuvutia muungano wa wapiga kura wa aina mbalimbali, kutoka rika na asili tofauti. Hata hivyo, wakati wafuasi wa vuguvugu la 'Make America Great Again' (Ifanye Marekani Kuwa Kubwa Tena) wakiendelea kumuunga mkono, tafiti zinaonyesha kuwa vijana wengi waliomsaidia kushinda dhidi ya Kamala Harris sasa wamekata tamaa au hawana imani naye tena.
Mary Heron, mwenye umri wa miaka 21, ambaye anatoka katika duka dogo la keki ndogo (cupcakes) akiwa na marafiki wawili, anasema ameona mabadiliko katika mitazamo ya vijana wenzake.
"Ninaona mabadiliko fulani katika kiwango cha uungaji mkono kwake, jambo ambalo si la kawaida sana hapa," anasema Heron, ambaye ni mwanafunzi na hufanya kazi kwa muda.
"Lakini nimekutana na watu wachache wanaosema, 'Ndiyo, nilimpigia kura, lakini simuungi mkono tena,'" anaongeza.

Chanzo cha picha, Eloise Alanna
Donald Trump aliingia katika siasa wakati wanawake hao wawili walipokuwa shule ya kati. "Watu wengi tuliokua nao walikubaliana kwa kiasi kikubwa na mitazamo ya kisiasa ya wazazi wao," anasema Emily Villapando, rafiki wa Mary Heron mwenye umri wa miaka 21.
"Lakini sasa kwa kuwa tumekua, tuna majukumu zaidi. Uchumi umekuwa na athari kubwa zaidi katika maisha yetu," anaongeza kijana huyo, ambaye anasoma sayansi ya tiba-hai (biomedical sciences) na anataka kuwa daktari.
Wanafunzi hao watatu,ambao kundi lao linakamilishwa na rafiki yao Cayden Biles, wanataja haki za wanawake na jinsi maafisa wa uhamiaji wanavyowatendea watu vibaya kama baadhi ya masuala yanayowatia wasiwasi zaidi, lakini wana mashaka kama kutakuwa na mabadiliko makubwa ya mitazamo au mwenendo wa upigaji kura katika eneo hilo.
Kayden Biles anasema ana matumaini kuwa kizazi cha vijana kinaweza kuleta mabadiliko, lakini "ukizingatia mahali tunapoishi... itakuwa vigumu sana."
William Bogle, anapoelezea hali iliyopo katika eneo la Kingsport, bila kukusudia anagusia masuala hayo hayo yanayoleta wasiwasi.
"Tunaishi mahali pazuri sana, na kama wewe si mtu mwenye msimamo wa kihafidhina, usije hapa," anasema mhubiri huyo wa Kikristo.
"Kwa sababu hutoweza kuendana na mazingira ya hapa," anaendelea. "Lakini kama una msimamo wa kihafidhina, karibu hapa. Tutakukaribisha."
William Bogle anasema atamwombea Donald Trump, kama anavyofanya Pam Robinson, licha ya Pam kuwa na misimamo ya wastani zaidi.
Pam Robinson anasema, "Unachoweza kufanya ni kuwaombea viongozi wako tu, na hatimaye Mungu atakupa kile unachotaka."















