Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump anasema "tisho" liliifanya Marekani kuondoa ndege zake za kivita kutoka kambi ya ndege ya Uingereza

Rais wa Marekani Donald Trump anasema Marekani ilihamisha ndege zake za kivita kutoka kambi ya Jeshi la Anga la Uingereza huko Fairford kwa sababu ya "vitisho fulani" vinavyolenga kambi hiyo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafiki mwisho wa matangazo haya ya moja kwa moja kwa leo. Tukutane tena hapo kesho.

  2. Video: Tazama polisi mjini Paris walivyorusha mabomu ya kutoa machozi wakati wa maandamano ya kupinga 'uwekezaji mdogo' katika shule za sekondari

    Maelfu ya watu wanafanya maandamano kote Ufaransa, wakipinga kile wanachosema ni uwekezaji mdogo katika shule za upili

    Chama kimoja cha wafanyakazi kinasema shule 2,000 za upili zimefungwa - wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa ilikadiria mapema kwamba kulikuwa na waandamanaji 86,000 kote nchini, bila kujumuisha Paris

    Polisi wamefyatua gesi ya kutoa machozi katika mji mkuu na Marseille . Awali mwandishi wa BBC aliyepo mjini Paris alisema anaweza "kuhisi kwenye koo na macho yangu" muwasho.

  3. Wanawake saba wakamatwa kwa tuhuma za kutumia noti kutengeneza 'maua ya pesa' Ghana

    Mamlaka nchini Ghana imewakamata watu saba wanaoshutumiwa kutumia noti za benki kutengeneza kile kinachoitwa "maua ya pesa" na kupamba keki.

    Benki kuu ya taifa ya Ghana inasema kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kinahusisha matumizi mabaya ya sarafu ya Ghana, cedi.

    Polisi waliwakakamata baada ya taarifa kusambaa na kusababisha kukamatwa kwa washukiwa, wote wakiwa wanawake, wanaotuhumiwa kuuza "maua haya kwa pesa" katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Accra.

    Huu ulikuwa ni msako mkubwa wa kwanza dhidi ya matumizi mabaya ya fedha unaofanywa na vyombo vya sheria. Mnamo Julai (7) mwaka huu, Benki ya taifa ya Ghana ilitoa taarifa ikionya kwamba huu unaweza kuwa uhalifu.

    Wakati huo, benki hiyo iliwaonya watu kuepuka "shughuli zinazosababisha kushuka kwa thamani au uharibifu wa sarafu ya taifa, ikiwa ni pamoja na tabia yoyote inayodhoofisha thamani yake halali au matumizi yake halali."

    Maua yaliyotengenezwa kwa noti za benki au keki zilizopambwa kwa pesa mara nyingi huagizwa kama zawadi kwa ajili ya harusi, siku za kuzaliwa, mahafali, na matukio mengine.

    Polisi wameanzisha uchunguzi, na maafisa wanasema washukiwa watafikishwa mahakamani. Wanaweza kukabiliwa na faini au kifungo, ambacho kitaamuliwa na mahakama.

    Dinah Bonzi, afisa katika Idara ya Masuala ya Fedha ya Benki ya Kitaifa ya Ghana, alisema kwamba mtu yeyote anayewezesha au kuendeleza shughuli kama hizo anaweza pia kukamatwa na kushtakiwa.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Meli yazama na wafanyakazi wake hawajulikani walipo baada ya shambulio katika Bahari Nyeusi

    Meli ya mizigo ya raia imezama na wafanyakazi wake hawajulikani walipo baada ya kushambuliwa na ndege zisizo na rubani katika Bahari Nyeusi, maafisa wa Bulgaria wanasema.

    Waziri Mkuu Rumen Radev amesema kuwa meli ya pili iliyokuwa imebeba nafaka pia iligongwa ndani ya eneo la kiuchumi la Bulgaria. Wafanyakazi wake 18 waliokolewa.

    Radev hakusema ni nani aliye nyuma ya mashambulizi hayo, ambayo yanakuja huku Urusi ikizidisha mashambulizi katika Bahari Nyeusi, hasa upande wa mashariki, kama sehemu ya vita vyake dhidi ya Ukraine.

    Moscow haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo la hivi punde, siku moja baada ya kushutumiwa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa kugonga meli ya raia iliyokuwa imebeba mahindi. Rais wa Tume ya Ulaya (EU) Ursula von der Leyen amesema mashambulizi hayo "hayakubaliki".

    Ndege zisizo na rubani za angani na baharini zilihusika katika mashambulizi hayo yapata maili 70 (kilomita 112) kutoka mji wa pwani wa Byala mashariki mwa Bulgaria, Radev alisema.

    Meli iliyozama ilikuwa na bendera ya Togo, alisema. Ikiitwa Alfa Watan, ilikuwa meli ya jumla ya mizigo inayomilikiwa na Uturuki na inasemekana ilikuwa ikielekea Sulina, Romania.

    Haijulikani wazi ni nini kilikuwa kimebebwa na meli ya Alfa Watan au ni watu wangapi walikuwa ndani yake.

    Meli ya Bulgaria ilikuwa karibu, lakini walipofika walichokiona ni boti iliyopinduka pamoja na jaketi za kuokoa maisha. Operesheni ya msako umeanzishwa.

    Unaweza pia kusoma:

  5. Habari za hivi punde, Raia wa Uingereza akamatwa kuhusiana na tukio kwenye kambi ya kijeshi ya RAF Fairford

    Polisi wa kukabiliana na ugaidi wamesema raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 22 amekamatwa kwa tuhuma za kuandaa vitendo vya kigaidi kuhusiana na tukio lililotokea karibu na RAF Fairford.

    Alikamatwa huko Westminster, London, Jumanne kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hilo karibu na kambi ya wanajeshi wa anga Gloucestershire mwezi uliopita.

    Ni mtu wa saba kukamatwa kuhusiana na tukio hilo mbapo wanaume wengine sita wameachiliwa kwa dhamana.

    Tukio kubwa lilitangazwa na wakazi wa nyumba kadhaa wakahamishwa baada ya polisi kuarifiwa kuhusu "magari matatu yanayotiliwa shaka" karibu na kambi ya wanajeshi wa kikosi cha anga.

    Mratibu mkuu wa kitaifa wa polisi wa kupambana na ugaidi, Vicki Evans, amesema "bado ni uchunguzi wa moja kwa moja" na polisi wanaendelea "kufuatilia njia nyingi za uchunguzi".

    Wanaume wengine watano walikamatwa Jumapili tarehe 27 Septemba karibu na kambi hiyo kuhusiana na tukio hilo na baadaye waliachiliwa kwa dhamana ya polisi.

    Mwanamume wa sita, mwenye umri wa miaka 25 na raia wa Iran na Uingereza, alikamatwa tarehe 1 Oktoba huko Westminster na baadaye akaachiliwa kwa dhamana.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Mkuu wa zamani wa ujasusi wa Ujerumani akamatwa kwa tuhuma za ujasusi na uhaini

    Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Shirikisho la Ujerumani inasema aliyekuwa mkuu wa ujasusi wa Ujerumani August Hanning amekamatwa kwa tuhuma za ujasusi, uhaini na kupata taarifa za siri kwa ajili ya taifa la kigeni.

    Hanning aliongoza huduma ya uasusi ya shirikisho (BND) kuanzia 1998 hadi 2005 na tangu wakati huo amekuwa akifanya kazi kama mshauri binafsi.

    Waendesha mashtaka wanadai kwamba alitumia ujasusi wa siri "kuandika uchambuzi" kwa huduma moja ya ujasusi ya kigeni na aliendelea kuwasiliana na huduma nyingine ya ujasusi ya kigeni. Wachunguzi hawajafichua ni mataifa gani ya kigeni yaliyohusika.

    Polisi pia walimkamata mfanyakazi wa zamani wa BND Manfred D, wakimtuhumu kwa kumpa Hanning takriban hati 2,000 za siri kwa ajili ya pesa.

    Manfred D, ambaye alikuwa mkuu wa ofisi ya Hanning na alibaki katika BND hadi mwaka huu, anashtakiwa kwa kusaidia na kuunga mkono jaribio la uhaini na ujasusi wa uhaini.

    Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba Hanning alikamatwa nyumbani kwake huko Nordwalde karibu na Münster huku Manfred D akikamatwa huko Bavaria. Hanning anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatano na Manfred D atafikishwa mahakamani Jumanne.

    Unaweza pia kusoma:

  7. Abiy Ahmed: Kitu pekee ambacho maadui zetu wana wasiwasi nacho ni kupunguza nguvu ya Ethiopia katika Bahari Nyekundu

    Baada ya Baraza la Wawakilishi kumchagua tena Abiy Ahmed kuongoza serikali ya Ethiopia kwa miaka mitano ijayo, alielekeza hotuba yake kwenye mipango mikuu ambayo serikali yake ingetekeleza.

    Amesema kwamba juhudi kubwa alizoongoza katika miaka ya hivi karibuni ili kuhakikisha Ethiopia ina eneo huru la baharini zitaendelea kama ilivyokuwa hapo awali.

    Waziri Mkuu Abiy alsisitiza kwamba makundi aliyoyaelezea kama "maadui zetu" na ambayo hakuyataja yanajaribu kikamilifu kuzuia Ethiopia kuwa na ushawishi wowote katika eneo la Bahari Nyekundu.

    Abiy alisema, "Kitu pekee ambacho maadui zetu wana wasiwasi nacho ni kupunguza nguvu ya Ethiopia katika Bahari Nyekundu... na wamefanya uharibifu wa nchi yetu kuwa ndoto wanayotamani."

    Aliongeza kuwa suluhisho la mahitaji ya baharini ya Ethiopia linajumuisha kanuni ya "toa na upokee" kulingana na uelewa wa pande zote na maslahi ya pande zote.

    "Matatizo sugu ya Ethiopia yanaweza kutatuliwa tu wakati Ethiopia itajenga ustaarabu imara," Waziri Mkuu alisema, akisisitiza kwamba "ustaarabu wa Ethiopia hauwezekani bila bahari."

    Aliahidi kwamba serikali yake itafuatilia bila kuyumba dai la bahari ambalo imelitetea kwa nguvu katika miaka ya hivi karibuni, akithibitisha kwamba katika muhula ujao madarakani, watafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba "Ethiopia ina lango la kuingia na kutoka".

    Bwana Abiy, alikuwa akizungumza leo mbele ya Baraza la Wawakilishi akizungumzia "mawimbi ya mabadiliko" yanayoendelea katika Pembe ya Afrika, Bahari Nyekundu, Ghuba ya Uajemi, na Mashariki ya Kati kwa ujumla, na mara kwa mara alisisitiza kwamba Ethiopia ndiyo "nguzo kuu" ya utulivu katika eneo hilo.

    Huku vita Kaskazini mwa Ethiopia vikipamba moto tena, Abiy, ambaye aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa miaka mitano ijayo, alisisitiza katika hotuba yake kwamba nchi hiyo ina uwezo wa kushinda changamoto zinazoikabili.

    Unaweza pia kusoma:

  8. Nigeria yaomboleza vifo vya watu 32 kufuatia ajali ya ndege ya kijeshi huku msako wa miili ukiendelea

    Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ametangaza kipindi cha maombolezo cha siku tatu kufuatia ajali ya ndege ya kijeshi katika Jimbo la Ondo na kuagiza uchunguzi ufanyike kuhusu chanzo cha ajali hiyo.

    Tinubu pia ameamuru bendera zipeperushwe nusu mlingoti kwa heshima ya wanajeshi waliofariki katika ajali ya ndege.

    Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa rais, Bayo Onanuga, Jumatatu, Tinubu "alitoa rambirambi zake kwa familia za abiria 25 na wafanyakazi saba walioathiriwa na tukio hilo, Mkuu wa wahudumu wa jeshi la anga, Marshal wa Air Sunday Kelvin Aneke, na maafisa na wafanyakazi wote wa Jeshi la Anga la Nigeria."

    Ajali ya ndege hiyo iliwaua watu wote 32 waliokuwa ndani, wakiwemo abiria 25 na wafanyakazi 7.

    "Huu ni wakati wa huzuni sana kwa Jeshi letu na taifa kwa ujumla. Wafanyakazi wetu wa Jeshi la Anga wanahatarisha maisha yao kila siku ili kuhakikisha uwepo wa usalama wa Nigeria. Mchango wao hazitasahaulika kamwe," Tinubu alisema.

    Serikali ya Jimbo la Ondo sasa imezindua operesheni ya uopoaji kufuatia ajali ya ndege ya Jeshi la Anga la Nigeria iliyotokea katika eneo la Igbokoda la Eneo la Serikali ya Mtaa ya Ilaje la Jimbo la Ondo.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Trump anasema "tishio" liliifanya Marekani kuondoa ndege zake za kivita kutoka kambi ya ndege ya Fairford ya Uingereza.

    Rais wa Marekani Donald Trump anasema Marekani ilihamisha ndege zake za kivita kutoka kambi ya Jeshi la Anga la Uingereza huko Fairford kwa sababu ya "vitisho fulani" vinavyolenga kambi hiyo.

    Wizara ya ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilithibitisha Jumapili kwamba ilikuwa imeondoa ndege zake za kivita, zinazoaminika kuwa takriban ndege 12 aina ya B-1, kutoka kwenye kambi hiyo na kuzirudisha kwenye kambi za awali nchini Marekani.

    Akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akielekea Nebraska Jumatatu , Trump alisema Marekani ilikuwa na ufahamu wa "tishio," ambalo lilisababisha kupelekwa kwa ndege hizo za kivita.

    Mapema Jumatatu, msemaji wa Waziri wkuu wa Uingereza alisisitiza kwamba RAF Fairford iko salama, akimaanisha maoni ya Trump wiki iliyopita ambapo alisifu "polisi, ulinzi na huduma za usalama" za Uingereza kuhusiana na kambi hiyo.

    Operesheni hiyo iliharakishwa sana kiasi kwamba baadhi ya ndege zilizokuwa zimerusha mabomu ziliondoka kabla ya kuwezekana kupanga ndege za kuongeza mafuta angani ili kuzisaidia, kulingana na maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina, walipozungumza na The New York Times.

    Unaweza pia kusoma:

  10. Marekani yafuatilia kwa karibu kifo mhudumu wa maabara nchini Urusi

    Rais Donald Trump amesema Marekani inafuatilia kwa karibu kifo cha mhudumu wa maabara nchini Urusi aliyefariki katika kituo cha utafiti wa ugonjwa wa tauni huko Siberia.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema ya Marekani inafuatilia kwa makini hali hiyo kutokana na hofu kwamba ugonjwa huo unaweza kuenea, lakini akasisitiza kuwa hakuna sababu ya wananchi kuwa na hofu kwa sasa.

    Maafisa wa Urusi wamesema mwanamke huyo alikufa kutokana na nimonia ambayo chanzo chake bado hakijajulikana. Gavana wa Irkutsk, Igor Kobzev, alisema vipimo vya awali havikuonyesha dalili zozote za maambukizi ya tauni.

    Ripoti ambazo bado hazijathibitishwa zimedai kuwa huenda mwanamke huyo aliambukizwa baada ya kuvunja chupa ndogo za maabara zilizokuwa na vimelea vya ugonjwa huo, au wakati wa safari ya kazi katika eneo ambalo tauni hupatikana miongoni mwa panya wa porini.

    Trump alisema hajazungumza na serikali ya Urusi kuhusu suala hilo, lakini akaeleza kuwa Marekani iko tayari kusaidia ikiwa kutahitajika.

    "Sipendi kuona wakikabiliwa na tatizo hilo," alisema. "Tutasaidia. Mtu yeyote anayepata tatizo la aina hiyo, tutakuwa tayari kusaidia."

    Kwa upande mwingine, gavana Kobzev alisema hakuna mfanyakazi mwingine wa kituo hicho aliyeripotiwa kuugua tangu kifo hicho kitokee. Alinukuu shirika la afya la Urusi, Rospotrebnadzor, likisema hakuna dalili za kuenea kwa ugonjwa huo.

    Shirika hilo pia lilisema wataalamu wa usalama wa afya walikagua Taasisi ya Kupambana na Tauni ya Siberia na Mashariki ya Mbali mjini Irkutsk na hawakubaini tatizo lolote la dharura.

  11. OpenAI yakiri kutoshughulikia vya kutosha matukio ya udukuzi yaliyolenga taasisi za serikali ya Australia

    Kampuni ya OpenAI imekiri kuwa hatua ilizochukua "hazikutosha" baada ya mmoja wa mawakala wake wa akili mnemba (AI) kwenda nje ya mipaka iliyowekwa na kuvamia tovuti za serikali ya Australia mwezi Juni.

    Afisa Mkuu wa Mkakati wa kampuni hiyo, Jason Kwon, alifika mbele ya kikao cha bunge kuhusu AI mjini Sydney Jumanne, ambapo alisema tukio hilo "halikupaswa kutokea" na kwamba kampuni hiyo "ilipaswa kushughulikia majibu yake kwa njia bora zaidi."

    OpenAI ilikosolewa kwa kuchelewa kuijulisha serikali ya Australia kuhusu uvamizi huo. Inadaiwa kuwa ilichukua wiki kadhaa kabla ya taarifa kutumwa, tena kupitia barua pepe kwa kisanduku cha jumla cha mawasiliano badala ya kuwafikia moja kwa moja viongozi wa serikali.

    "Tunaomba radhi na tunajua kuwa tuna kazi kubwa ya kufanya ili kurejesha imani ya watu wa Australia," alisema Kwon.

    Tukio hilo lilitokea baada ya wakala wa OpenAI kwenda nje ya maelekezo yake na kuingia katika mfumo binafsi wa takwimu uliokuwa na taarifa zisizo nyeti kutoka mpango wa huduma za afya wa taifa wa Australia, Medicare.

    Wataalamu wa usalama wa mtandao walieleza kuwa huenda hili likawa tukio la kwanza la aina yake ambapo AI imehusishwa moja kwa moja na uvamizi wa mfumo wa kidigitali.

    Alipoulizwa kwa nini OpenAI haikuwasiliana moja kwa moja na mawaziri wa serikali mara tu ilipogundua uvamizi huo, Kwon alikubali kuwa hilo lilikuwa kosa.

    "Tuulipaswa kufanya kile mnachopendekeza," alisema, akijibu swali la kamati kuhusu kwa nini kampuni haikupiga simu moja kwa moja kwa viongozi wa serikali.

    Wakati huo huo, kampuni pinzani ya AI, Anthropic, nayo ilihudhuria kikao hicho na kusema kuwa uchunguzi wake wa hivi karibuni haukubaini ukiukaji wowote unaohusisha mifumo yake nchini Australia.

    Unaweza kusoma;

  12. New York Times: Hofu ya shambulio la droni za Iran yasababisha ndege za Marekani kuondolewa Uingereza

    Gazeti la New York Times limeripoti kuwa Marekani iliondoa kwa haraka ndege zake zote 12 za mabomu aina ya B-1 kutoka kambi ya jeshi la anga ya RAF Fairford kusini mwa Uingereza baada ya kupokea taarifa mpya za kijasusi kuhusu uwezekano wa shambulio la droni lililodaiwa kuandaliwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC).

    Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na Uingereza waliolizungumza gazeti hilo kwa masharti ya kutotajwa majina, mpango huo ulikuwa wa hatua kadhaa na ulilenga kushambulia ndege za Marekani na kuwaua mamia ya wanajeshi waliokuwa katika kituo hicho.

    Maafisa hao walisema ndege zote za Marekani zenye uwezo wa kubeba mabomu ziliondolewa mwishoni mwa wiki kama hatua ya tahadhari kufuatia taarifa hizo za kiusalama.

    Baadhi yao walieleza kuwa mpango huo huenda ulihamasishwa na operesheni ya Ukraine dhidi ya Urusi mwaka jana, ambapo droni zilirushwa kutoka ndani ya eneo la Urusi na kuharibu au kuathiri ndege kadhaa za kijeshi, zikiwemo baadhi ya ndege za kimkakati zenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.

    Makamu wa Rais wa Marekani, J.D. Vance, alisema Jumatatu kuwa Pentagon ilihamisha ndege hizo kwa haraka "kama hatua ya ziada ya tahadhari" ili kulinda wanajeshi wa Marekani. Alidai Iran ilikuwa inapanga shambulio dhidi ya Marekani, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu tishio hilo.

    Takriban saa moja baadaye, Rais Donald Trump alisema sababu ya kuondolewa kwa ndege hizo ilikuwa ni kupokelewa kwa "tishio mahususi", akisisitiza kuwa tishio hilo lilikuwa tofauti na tukio la usalama lililoripotiwa karibu na RAF Fairford wiki iliyopita.

    Soma Pia:

  13. Askari afariki, watano wajeruhiwa wakati wa mazoezi ya kijeshi

    Askari mmoja wa Australia amefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa baada ya gari la kijeshi kupinduka wakati wa mazoezi katika Northern Territory (NT).

    Polisi walisema ajali hiyo ilitokea Jumatatu mchana katika eneo la mafunzo la Mount Bundey, ambalo liko takriban kilomita 130 kusini mashariki mwa mji wa Darwin.

    Mwanajeshi mmoja alitangazwa kufariki papo hapo katika eneo la tukio, huku wanajeshi watano waliojeruhiwa wakisafirishwa kwa ndege kwenda hospitali mjini Darwin kwa matibabu.

    Eneo la Mount Bundey hutumiwa na jeshi la Australia kwa mazoezi ya matumizi ya silaha za moto. Pia lina historia ya tukio jingine la kusikitisha ambapo mwaka 2017 mwanajeshi Jason Challis alifariki baada ya kupigwa risasi kichwani wakati wa mazoezi ya kijeshi. Baadaye, Idara ya Ulinzi ilikiri kosa la kutofuata kikamilifu taratibu za usalama mahali pa kazi.

    Ajali hiyo ni kifo cha pili cha mwanajeshi wa Australia mwaka huu katika mazingira ya mazoezi ya kijeshi. Mwezi Mei, mwanajeshi wa kikosi cha miamvuli alifariki baada ya kugongana angani na mwanajeshi mwingine wakati wa mafunzo.

    Idara ya Ulinzi ya Australia ilithibitisha tukio hilo Jumanne lakini haikutoa maelezo zaidi, huku ikiomba faragha ya wanajeshi walioathirika na familia zao iheshimiwe.

    Waziri Mkuu wa Northern Territory, Lia Finocchiaro, alisema wanajeshi wawili waliojeruhiwa walifikishwa katika Hospitali ya Royal Darwin kwa helikopta, huku wengine watatu wakipelekwa kwa ndege baadaye jioni ya Jumatatu.

    Akitoa pole, alisema:

    "Mawazo na maombi yetu yako pamoja na familia ambayo imeathiriwa vibaya na msiba huu. Jamii yetu nzima ipo pamoja na wanajeshi wetu wote ambao bila shaka wanahisi maumivu makubwa kutokana na kupoteza mwenzao."

    Tukio hili limeibua tena maswali kuhusu usalama katika mazoezi ya kijeshi ya Australia, hasa baada ya vifo viwili vya wanajeshi kutokea mwaka huu wakati wa mafunzo.

  14. Watu 12 wakamatwa kwa kuendesha mtandao wa biashara haramu ya paka

    Polisi wa Ho Chi Minh City nchini Vietnam wamesema wanaume 12 wamekamatwa baada ya kudaiwa kukiri kuhusika katika wizi na uuzaji wa takribani paka 2,700.

    Wakati wa uchunguzi, polisi walikamata vifaa mbalimbali vinavyoaminika kutumika katika shughuli hizo, vikiwemo:

    • Mitego ya kunasia paka
    • Mashine za kuondoa manyoya
    • Mizani ya kupimia uzito

    Washukiwa hao wanatuhumiwa kuwapeleka paka hao kuchinjwa kwa ajili ya kuuzwa kama chakula.

    Kwa mujibu wa polisi, wanaume hao walikuwa wakizunguka maeneo ya makazi usiku kwa vikundi vidogo wakiwa kwenye pikipiki ili kuiba paka kutoka kwa wamiliki.

    Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kuwa walitumia vipande vya samaki kama chambo, wakitega mitego nje ya nyumba walizojua kuwa na paka. Kati ya paka waliookolewa, 13 tayari wamerudishwa kwa wamiliki wao.

    Shirika la ustawi wa wanyama la Humane World for Animals linakadiria kuwa kila mwaka nchini Vietnam takribani mbwa milioni tano na paka milioni moja hukamatwa, huibwa, husafirishwa na kuchinjwa kwa ajili ya nyama.

    Ulaji wa nyama ya mbwa na paka ni halali nchini Vietnam, na migahawa mingi hutangaza wazi vyakula hivyo kwenye menyu zao. Hata hivyo, wafanyabiashara wanatakiwa kuwa na vibali vinavyoonesha chanzo halali cha wanyama hao.

    Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, kila kikundi kati ya washukiwa hao kilikuwa kinaiba wastani wa paka kati ya wanne na 10 kila usiku.

    Mnamo tarehe 8 Julai, polisi walikamata:

    • Paka 50 waliokuwa hai
    • Mizani miwili
    • Mitego 55 ya paka
    • Mifuko 14
    • Simu za mkononi 13
    • Pikipiki saba
    • Mashine mbili za kuondoa manyoya
    • Dong milioni 6.7 za Vietnam (sawa na dola 257 za Marekani)

    Kesi hiyo imezua mijadala kuhusu ustawi wa wanyama na biashara ya nyama ya paka na mbwa nchini Vietnam, ambapo makundi ya kutetea haki za wanyama yamekuwa yakitaka udhibiti mkali zaidi wa biashara hiyo.

    Unaweza kusoma;

  15. Saudi Arabia yaombwa msamaha baada ya chapisho la kashfa Facebook

    "Ninaaomba msamaha kwa makosa aliyoyafanya mwanangu. Tafadhali msameheni na mumrudishe nyumbani kwetu."

    Akizungumza huku akitokwa na machozi, Rasamanickam Yogalakshmi alitoa ombi la dhati la kuokoa maisha ya mwanawe mkubwa, Anojan Sivarasa.

    Mfanyakazi huyo wa uhamiaji mwenye umri wa miaka 24 anakabiliwa na hukumu ya kifo nchini Saudi Arabia baada ya mahakama ya rufaa kumpata na hatia ya kukufuru Uislamu na Mtume Muhammad kutokana na maoni aliyochapisha kwenye Facebook.

    Kesi hiyo imezusha mshtuko mkubwa nchini Sri Lanka, na kuibua wasiwasi mkubwa pamoja na kampeni za maombi kutoka kwa makundi ya kiraia nchini humo. Vyama mbalimbali vya kisiasa na taasisi za serikali vimekuwa vikishirikiana katika juhudi za kidiplomasia kuomba msamaha kwa niaba yake.

    Hata hivyo, familia yake haijapata taarifa yoyote kuhusu hali yake tangu tarehe 28 Septemba. Serikali ya Sri Lanka imeielekeza familia hiyo kujiepusha na kutoa matamko zaidi wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea.

    Mamlaka za Saudi Arabia bado hazijatangaza rasmi ratiba ya utekelezaji wa hukumu hiyo, na haijulikani itatekelezwa lini. Saudi Arabia imewahi kutekeleza hukumu za kifo bila kutoa taarifa mapema kwa familia au balozi za nchi husika, huku ndugu wakipewa taarifa baada ya hukumu kutekelezwa.

    Anojan alishtakiwa kufuatia mabishano yaliyotokea kwenye mitandao ya kijamii baada ya tukio lililotokea wakati wa hija ya Wahindu nchini Sri Lanka.

    Mwishoni mwa mwezi Juni, video iliyoonesha kijana mmoja Mwislamu akimpiga teke mbwa aliyekuwa karibu na mahujaji wa Kihindu ilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na kuzua mjadala mkubwa wa kidini.

    Katika mabishano hayo mtandaoni, mtumiaji mmoja alichapisha maneno ya dharau dhidi ya mungu mmoja wa Kihindu. Kutokana na hilo, Anojan alijibu kwa kuandika ujumbe kwa lugha ya Kitamil uliokuwa na matusi dhidi ya Mtume Muhammad.

    Ingawa Anojan alifuta haraka maoni yake na baadaye kuchapisha video akiomba radhi, picha ya maoni hayo ilikuwa tayari imehifadhiwa na kuwasilishwa kwa mwajiri wake pamoja na maafisa wa Saudi Arabia, jambo lililosababisha kukamatwa kwake mwezi Julai.

    Unaweza kusoma;

  16. Jeshi la Yemen lasema limefanikiwa 'kudhibiti' njia ya Bahari ya Shamu

    Vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Yemen, kwa msaada wa Saudi Arabia, vimedai kuwa vimefanikiwa kuudhibiti Mlango Bahari wa Bab al-Mandab, ulioko kusini mwa Bahari ya Shamu, katika hatua za mwanzo za mashambulizi makubwa dhidi ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

    Jeshi la Yemen pia lilisema katika taarifa kuwa vikosi vya National Shield, Giants Brigades na Tihama Resistance vilifanikiwa kuingia na kuuteka mji wa bandari wa Mokha Jumatatu mchana kwa msaada wa mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia.

    Hata hivyo, taarifa nyingine zinakinzana na madai hayo. Vyanzo vya serikali na jeshi la Yemen vilivyozungumza na mashirika ya habari ya Reuters na AFP vilisema kuwa vikosi hivyo bado havijaingia katikati ya mji wa Mokha, bali vimefika tu maeneo ya pembezoni mwa mji huo.

    Kwa upande wa waasi wa Houthi, hakukuwa na tamko la haraka kuhusu hali ya Mokha.

    Vyanzo vinne vya serikali vililiambia Reuters kuwa vikosi vya serikali vilifika katika viunga vya Mokha mwishoni mwa Jumatatu, huku wapiganaji wa Houthi wakianza kuondoka katika baadhi ya maeneo.

    Vyanzo vya kijeshi vilivyozungumza na AFP havikuthibitisha kutwaliwa kwa mji huo, lakini vilisema kuwa:

    "Vikosi vyetu vimedhibiti uwanja wa ndege wa kijeshi wa Dhubab na kukata barabara inayounganisha wilaya ya Dhubab na eneo la Bab al-Mandab."

    Mapema, jeshi la Yemen lilitangaza kuwa vikosi vyake vilikuwa vimetwaa Uwanja wa Ndege wa Dhubab, ulioko takribani kilomita 45 kusini mwa Mokha, na kwamba vilikuwa vimezingira wapiganaji wa Houthi waliokuwa ndani ya mji wa karibu.

    Hata hivyo, vyombo vya habari vinavyoendeshwa na Houthi vilikanusha taarifa kwamba vikosi vya serikali vimepata mafanikio yoyote katika eneo la Dhubab.

    Unaweza kusoma:

  17. Tetesi za Soka Jumanne: Juventus na Atletico Madrid macho kwa Madueke

    Atletico Madrid na Juventus wanamfuatilia mshambuliaji wa Arsenal na timu ya taifa ya England, Noni Madueke.

    Chelsea, Arsenal, Liverpool, Manchester United na Manchester City zote zinaonesha nia ya kumsajili beki wa Barcelona na Ufaransa, Jules Kounde (miaka 27), huku klabu hiyo ya Hispania ikiwa tayari kusikiliza ofa kubwa.

    Mshambuliaji wa England, Harry Kane, yuko katika hatua za mwisho za kukubaliana mkataba mpya wa miaka mitatu na Bayern Munich.

    AC Milan inaweza kujaribu tena kumsajili mshambuliaji wa Manchester United, Joshua Zirkzee (miaka 25), mwezi Januari kwa mkopo wenye chaguo la kununuliwa moja kwa moja baadaye.

    Arsenal, Liverpool na Borussia Dortmund zinamuwania mshambuliaji wa Fulham, Josh King (miaka 19), ambaye thamani yake inakadiriwa kufikia pauni milioni 51.

    Real Madrid imepanga kusimama kidete katika uamuzi wake wa kutomuuza mshambuliaji wa Brazil, Endrick (miaka 20), licha ya kuvutiwa naye na Arsenal pamoja na Tottenham Hotspur.

    Nia ya Tottenham Hotspur ya kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez (miaka 26), inaonekana kuwa ngumu kufanikiwa kwa kuwa Muarjentina huyo bado anatamani kuhamia Barcelona.

    Wawakilishi wa klabu kadhaa za Premier League na Major League Soccer (MLS) wamekuwa wakimfuatilia mshambuliaji wa timu ya vijana ya Colombia chini ya miaka 20, Edmilson Herazo (miaka 18), anayekipiga katika klabu ya Barranquilla.

    Liverpool na Manchester United zinamfuatilia beki wa kushoto wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Alejandro Balde (miaka 22), ambaye pia anahitajika na Juventus.

    Paris Saint-Germain (PSG) imeonyesha tena nia ya kumsajili beki wa Manchester United na Ufaransa, Leny Yoro (miaka 20).

    Inter Milan na Juventus zote zinamfuatilia beki wa kati wa Liverpool, Giovanni Leoni (miaka 19), ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Italia anayechipukia.

    Unaweza kusoma;

  18. Trump aihusisha Iran na ajali ya FlyDubai na tishio la Fairford

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaamini Iran ilihusika na ajali ya ndege ya FlyDubai na huenda pia ikawa nyuma ya tishio la usalama lililosababisha kuondolewa kwa ndege za Marekani zenye uwezo wa kubeba mabomu kutoka kituo cha RAF Fairford nchini Uingereza.

    Kauli hiyo inaonekana kutofautiana na msimamo wa Makamu wa Rais J.D. Vance, ambaye amesema bado hakuna ushahidi wa uhakika unaoihusisha Iran na ajali ya FlyDubai. Naye Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alieleza kuwa kuhamishwa kwa ndege hizo huenda kulikuwa sehemu ya utaratibu wa kawaida wa kubadilishana wanajeshi na vifaa vya kijeshi.

    Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ikulu ya White House Jumatatu, Trump alisema kuondolewa kwa ndege hizo hakukutokea kwa bahati mbaya, bali kulichochewa na kile alichokiita "tishio mahususi".

    "Tulipokea taarifa za vitisho, hivyo hatukuona sababu ya kuendelea kuziweka ndege hizo hapo. Tukazihamisha kama hatua ya tahadhari," alisema.

    Trump aliongeza kuwa Marekani inawafahamu watu waliohusika na tishio hilo, ingawa hakuwataja majina. Alipoulizwa ikiwa tishio hilo lilihusiana na Iran, alijibu: "Linaweza kuhusishwa na Iran."

    Matamshi yake yanaonekana kuunga mkono ripoti za baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani zilizodai kuwa tishio jipya la usalama ndilo lililosababisha kuondolewa kwa ndege hizo kutoka RAF Fairford, baada ya tukio la Septemba 27 ambapo polisi walichunguza magari matatu yaliyotiliwa shaka karibu na kituo hicho.

    Kauli za Trump zinaibua tofauti za wazi ndani ya utawala wake kuhusu namna ya kueleza matukio hayo, huku Vance na Rubio wakichukua msimamo wa tahadhari zaidi na kuepuka kuihusisha Iran moja kwa moja bila ushahidi wa kutosha.

    Maelezo zaidi:

  19. Pezeshkian: Hakuna haja ya kujadiliana na adui anayetumia vikwazo na vitisho kila siku

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema taifa lake halioni sababu ya kuendelea na mazungumzo na upande ambao, kwa mujibu wake, unaendelea kutumia vitisho, vikwazo na shinikizo dhidi ya nchi yake huku ukishindwa kuzingatia makubaliano ya kimataifa.

    Akizungumza wakati wa mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia, Ararat Mirzoyan, Pezeshkian alisema Iran haiwezi kukubali mtazamo wa aina hiyo katika mahusiano ya kidiplomasia.

    "Kujadiliana na adui ambaye kila siku anatumia vitisho, vikwazo na shinikizo, na ambaye hatimizi ahadi zake, hakuna maana. Taifa letu haliwezi kukubali mtazamo wa aina hiyo," alisema.

    Pezeshkian alisema kuwa katika hotuba yake kwenye Umoja wa Mataifa, Iran ilionyesha utayari wa kufanya mazungumzo na kuruhusu uthibitishaji wa shughuli zake za nyuklia ili kujenga imani kwa jumuiya ya kimataifa.

    Hata hivyo, alidai kuwa Tehran imepoteza imani katika mchakato huo kutokana na kile alichokiita matumizi mabaya ya ukaguzi wa kimataifa.

    "Tulitangaza kuwa tuko tayari kwa mazungumzo na uthibitishaji kuhusu shughuli zetu za nyuklia. Lakini kila mara wakaguzi walipokuja Iran, vituo vyetu vya nyuklia na wanasayansi wetu walitambuliwa, kisha vituo hivyo vikashambuliwa na wanasayansi wetu kuuawa," alisema.

    Kauli ya Pezeshkian inakuja wakati mvutano kati ya Iran na mataifa ya Magharibi ukiendelea kuongezeka, huku suala la mpango wa nyuklia wa Iran likisalia kuwa moja ya maeneo makuu ya mzozo wa kidiplomasia.

    Soma zaidi:

  20. Natumai hujambo.