'Nilipunguza kukimbia kwa sababu ya kuvuja mkojo' - Mshindi wa fainali ya Jumuiya ya Madola Naomi Korir

    • Author, Celestine Karoney
    • Nafasi, BBC Michezo Afrika, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Safari ya kimichezo ya Naomi Korir ilifikia kilele mwezi Agosti aliposhika nafasi ya tano katika fainali ya mbio za maili moja kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Glasgow.

Hata hivyo, mambo yangeweza kuwa tofauti kabisa kwa mwanariadha huyu wa Kenya anayeshiriki mbio za masafa ya kati.

Mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 28 alizaliwa akiwa na tatizo la fistula, hali ya kiafya ambapo matundu yasiyo ya kawaida hutokea kati ya viungo vya mwili na kusababisha kuvuja kwa mkojo au kinyesi bila kudhibitiwa.

Ingawa Korir alipenda riadha tangu utotoni, hali hiyo ilimfanya awali atafakari upya mipango yake ya kuwa mwanariadha.

"Nilishiriki michezo mingi: soka, netiboli, riadha, na hata raga," alisema.

"Lakini ilikuwa vigumu kwa sababu ya kufanya mazoezi, huku mkojo ukinivuja bila kukoma. Ilikuwa hali mbaya.

"Nilipunguza umbali wa mbio zangu ili kupunguza kuvuja kwa mkojo.

"Nilianza kushiriki mbio za mita 100 za vikwazo."

Licha ya changamoto hizo, mapenzi ya Korir kwa michezo wa riadha pia yalikuwa njia ya kujiliwaza na kuhisi kuwa sehemu ya jamii.

"Nilifanya hivyo kwa sababu nilipenda," alieleza.

"Kwa kuwa watu wengi waliniepuka, nilijishughulisha na mambo mengi ili tu kutohisi kutengwa."

Operesheni tatu na fursa ya pili

Shirika la msaada la madaktari wasio na mipaka (Doctors Without Borders) linakadiria kuwa wanawake 500,000 duniani kote wanaishi na tatizo la fistula.

Baadhi hupata fistula baada ya kujifungua, huku kwa wengine kama vile Korir tatizo hilo huwa ni la kuzaliwa nalo.

Upatikanaji wa huduma bora za uzazi au upasuaji rahisi umesaidia karibu kutokomeza tatizo hili katika baadhi ya nchi, lakini bado ni changamoto kubwa katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo ni vigumu kupata huduma bora za afya.

Korir alizaliwa na fistula ya njia ya mkojo na viungo vya uzazi mbapo tundu lililopo kati ya kibofu cha mkojo na uke linasababisha kuvuja kwa mkojo.

Upasuaji ulihitajika, lakini upasuaji wa kwanza na wa pili haukufanikiwa kutatua tatizo hilo.

Mnamo Agosti 2013, upasuaji wa tatu hatimaye ulileta nafuu kwa msichana huyo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 13.

Utaratibu huo ulifanyika katika mji wake wa nyumbani, Eldoret, katika Hospitali ya Gynocare, ambayo ina utaalamu wa kutibu fistula na kutoa huduma za uzazi na afya ya uzazi.

"Ni hali ngumu kuishi nayo kila siku," alisema Mkurugenzi wa Gynocare, Caroline Mabeya, alipozungumza na BBC Sport Africa kuhusu unyanyapaa na kutengwa wanakokumbana nako wanawake wenye tatizo hili.

"Wanatengwa na jamii. Hiyo ndiyo adhabu ya kisaikolojia wanayokabiliana nayo kutokana na fistula."

Hospitali hiyo imekuwa ikihudumia wagonjwa kutoka kote Afrika Mashariki tangu ilipoanza kazi mwaka 2011. Shughuli zake zinavuka mipaka ya upasuaji pekee, kwani ina mpango maalum wa baada ya upasuaji unaolenga kuwasaidia wanawake kurejesha kujiamini kwao.

"Tunatoa matibabu ya bure kwa wanawake hawa katika hospitali ya Gynocare kwa sababu wengi wao ni maskini sana," alieleza Mabeya.

"Wanapofika hapa, wanakuwa wamevunjika moyo na kujiona duni. Hivyo, juhudi kubwa huwekwa ili kuwapa nguvu ya kutosha kurejea na kuunganishwa tena na jamii."

'Bingwa wa michezo'

Kwa Korir, upasuaji huo uliofanikiwa ulikuwa mwanzo wa maisha mapya, ukimfungulia milango ya mafanikio uwanjani na kielimu.

Mbali na kurejea kwenye mbio, aliendelea na masomo yake kupitia Mpango wa GynoCare kwa Vijana Wenye Tatizo la Fistula.

"Nina familia yangu huko GynoCare, makazi ya waathiriwa wa fistula," alisema.

"Baada ya upasuaji, hapo ndipo nilipoendelea na masomo yangu hadi nikahitimu elimu ya sekondari."

Mwaka 2019, Korir alianza kushiriki mashindano ya kitaalamu ya riadha. Miaka miwili baadaye, aliandika historia akiwa mmoja wa Wakenya wawili waliotwaa medali ya fedha katika mbio za kupokezana vijiti za mchanganyiko za mita 2x400 kwenye Mashindano ya Dunia ya Mbio za Kupokezana Vijiti nchini Poland, pamoja na Ferguson Rotich.

Mwaka uliofuata, aliongeza mafanikio yake kwa kutwaa medali ya dhahabu akiwa sehemu ya timu ya Kenya ya mbio za kupokezana vijiti za mita 4x400 kwenye Mashindano ya Afrika yaliyofanyika Mauritius.

Kushiriki fainali ya mbio za maili moja katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka huo kulikuwa hatua nyingine muhimu katika safari yake, ikiwa ni mara yake ya kwanza kufika fainali kubwa ya kimataifa.

Korir anasema mafanikio yake ni ujumbe wa matumaini kwa wasichana na wanawake wanaopitia changamoto kama alizowahi kukabiliana nazo.

"Nataka kuwapa matumaini wanawake vijana ambao huenda wamekata tamaa. Wanapaswa kujua kwamba wanaweza kurejea katika maisha ya kawaida na kuyafurahia tena," alisema.

Kwa upande wake, Mabeya anasema mabadiliko ya Korir yamekuwa chanzo cha hamasa kwa wanawake wengi wanaopata matibabu katika GynoCare.

"Anawafanya waone kwamba inawezekana kushinda changamoto hizi na bado kufanikiwa maishani. Naomi ni mmoja wa wagonjwa wanaotupa nguvu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kwa sababu tunapambana pamoja na wanawake hawa. Kazi hii si rahisi."

Akiwa mtoto, Korir alipenda muziki, akiimba kanisani na kupiga kinanda, na wakati huo aliamini muziki ndio ungekuwa taaluma yake ya baadaye kuliko riadha.

"Lakini sasa niko katika taaluma tofauti na nina furaha sana," alisema huku akitabasamu.

Na huku macho yake yakielekezwa kwenye Mashindano ya Dunia mwaka ujao pamoja na Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles mwaka 2028, Korir anaamini bado ana mengi ya kuyafanikisha.

"Najua mimi ni bingwa maishani, kwa sababu kushinda tatizo la fistula pekee ni ushindi mkubwa. Sasa ninataka kuwa bingwa pia katika uwanja wa michezo."

"Sasa ninatarajia kuwa bingwa katika michezo."