Iran yafichua 'mji mpya wa makombora'

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Siku ya Jumanne, jeshi la Iran, Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran (IRGC) walitoa picha za kile walichokiita "mji mpya wa makombora", kituo kikubwa cha chini ya ardhi kinachotumiwa kuhifadhi makombora na mifumo ya kuyarusha.

Picha hizo zinamuonyesha Mkuu wa Majeshi ya Iran, Ali Abdollahi, pamoja na Kamanda wa Kikosi cha Anga cha IRGC, Majid Mousavi, wakikagua kituo hicho. Kama ilivyokuwa katika picha zilizowahi kutolewa za vituo vingine vya makombora, eneo hilo linaonekana kuwa na aina mbalimbali za makombora ya balestiki, cruise na vifaa vya kuyarusha.

Kuonyeshwa kwa picha hizo kumekuja wakati ambapo Marekani na Israel zimekuwa zikifanya mashambulizi kulenga miundombinu ya makombora ya Iran, ikiwemo vituo vya uzinduzi wa makombora, maeneo ya uzalishaji na vifaa vya maendeleo ya teknolojia hiyo wakati wa vita vya siku 40 vilivyotikisa eneo la Mashariki ya Kati.

Licha ya mashambulizi hayo, Iran inaonekana kuwa imeweza kudumisha sehemu kubwa ya uwezo wake wa makombora na kuendeleza juhudi za kurejesha baadhi ya miundombinu iliyoharibiwa. Hata hivyo, bado haijulikani kwa kiwango gani uwezo huo umeathirika ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya vita.

Hapo awali, uchambuzi wa picha za satelaiti uliofanywa na BBC Verify ulionyesha kuwa Iran ilikuwa imeanza kujenga upya baadhi ya vituo vyake vya makombora, ikiwemo kambi ya Garmdara iliyopo Karaj na kambi ya Imam Ali katika jimbo la Kermanshah.

Kwa kweli, mpango wa Iran wa kujenga "miji ya makombora" si jambo jipya. Serikali ya Tehran imekuwa ikifichua mara kwa mara uwepo wa vituo vya chini ya ardhi katika miaka ya karibuni. Hata hivyo, kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya miundombinu ya makombora, umuhimu wa vituo hivyo sasa umeongezeka zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Je, 'mji wa makombora' ulioonyeshwa ni mpya kweli?

Hili ndilo eneo ambalo linazua maswali mengi.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Iran kufichua kituo kama hicho katika kipindi cha karibu miaka miwili. Hata hivyo, hadi sasa IRGC haijatoa taarifa kuhusu eneo halisi la kituo hicho, lini kilijengwa, ukubwa wake, idadi ya makombora kilichonacho au uwezo wake wa kiutendaji.

Kwa sasa jambo pekee linaloweza kuthibitishwa kwa uhakika ni kwamba mamlaka za Iran zimeonyesha picha za kituo cha chini ya ardhi kilichojaa makombora na vifaa vya kijeshi. Hakuna njia ya kuthibitisha kwa uhuru ikiwa ni kituo kipya kabisa, uwezo wake halisi au kama kiko tayari kutumika kikamilifu vitani.

Katika video iliyochapishwa na IRGC, handaki moja linaonekana mara kadhaa kutoka pembe tofauti za kamera. Hali hii imewafanya baadhi ya wachambuzi kuhoji ikiwa sehemu za vituo vya zamani zimewasilishwa kama kituo kipya kwa lengo la kuonyesha nguvu kubwa zaidi za kijeshi.

Lakini hata kama kituo hicho si kipya, muda uliochaguliwa kukitangaza una umuhimu mkubwa.

Katika vita vya hivi karibuni, Marekani na Israel zilishambulia maeneo muhimu ya uzinduzi wa makombora, maghala ya kuhifadhi silaha, viwanda vya kutengeneza makombora pamoja na miundombinu ya mafuta na vifaa vingine vinavyohusiana na sekta hiyo.

Katika mazingira hayo, kuonyeshwa kwa kituo kipya cha chini ya ardhi kunaonekana kuwa na ujumbe kadhaa.

Kwanza, Iran inataka kuonyesha kwamba mashambulizi hayo hayakufanikiwa kuharibu miundombinu yake yote ya makombora na kwamba bado ina uwezo wa kuendelea kutengeneza, kuhifadhi na kutumia silaha hizo.

Pili, Tehran inaonekana kusisitiza mkakati wake wa kuhamisha makombora mengi chini ya ardhi ili kupunguza hatari ya kushambuliwa kutoka angani.

Jambo hili ni muhimu hasa kutokana na ukweli kwamba Marekani na Israel zilikuwa na ubora mkubwa wa anga wakati wa vita, lakini baadhi ya maghala ya chini ya ardhi ya Iran yalibaki salama.

Tatu, na pengine muhimu zaidi, picha hizo zina lengo la kuimarisha uwezo wa Iran wa kuzuia mashambulizi kutoka kwa maadui wake kwa kuonyesha kwamba bado ina uwezo wa kujibu mashambulizi yoyote ya kijeshi.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kwamba picha hizo peke yake haziwezi kuthibitisha kwamba kituo hicho kilijengwa baada ya mashambulizi ya hivi karibuni wala kwamba mfumo mzima uliopo ndani yake uko tayari kufanya kazi mara moja.

Makombora gani yanaonekana kwenye picha?

.

Hadi sasa Walinzi wa Mapinduzi hawajatoa taarifa rasmi kuhusu majina ya makombora yaliyopo, uwezo wake, aina ya mafuta yanayotumiwa au idadi kamili ya silaha zilizohifadhiwa humo.

Shirika la habari la Tasnim linalohusishwa na IRGC limeripoti kuwa kituo hicho kina aina mbalimbali za makombora ya balestiki na cruise pamoja na vifaa vya kuyarusha.

Hata hivyo, ukilinganisha na picha za awali za miji ya makombora, safari hii kunaonekana kuwa na idadi ndogo zaidi ya vizindua makombora ya balestiki.

Uchambuzi wa picha unaonyesha uwepo wa makombora ya balestiki ya aina ya Shahab pamoja na makombora ya cruise ambayo tayari yanajulikana ndani ya jeshi la Iran.

Pia kuna kombora moja ambalo sehemu yake ilifichwa kwa makusudi kwenye picha zilizotolewa.

Mtaalamu wa makombora na ndege zisizo na rubani, Fabian Hinz, anaamini kwamba kombora hilo linafanana kwa ukubwa na muundo na toleo la kisasa zaidi la kombora la Paveh.

Paveh ni kombora la cruise la masafa ya kati ambalo ni sehemu ya familia ya makombora ya Soumar. Iran inadai kwamba kombora hilo lina uwezo wa kushambulia malengo yaliyo umbali wa hadi kilomita 1,650.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa kombora hilo linaweza kusafiri kwa kutumia njia tofauti kuelekea kwenye lengo na kuendesha mashambulizi kwa uratibu wa makombora mengine.

Inaaminika kuwa Iran ilitumia kombora hilo katika mashambulizi yake ya kwanza dhidi ya Israel mwaka 2024.

Paveh ilizinduliwa rasmi mwaka 2023, na wakati huo Iran ilisema kwamba masafa yake yanatosha kufika Israel kutoka ndani ya ardhi yake.

Mbali na hilo, picha hizo pia zinaonyesha kombora jingine jeusi la cruise ambalo halijawahi kuonyeshwa rasmi hapo awali. Hata hivyo, hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu uwezo wake au jina lake rasmi.

Kwa nini Iran inasema makombora yake yatawashangaza maadui?

Akiwa katika ziara hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Anga cha IRGC, Majid Mousavi, alisema kwamba makombora ya kisasa ya Iran yana uwezo wa "kuwashangaza maadui katika uwanja wa vita."

Kauli hiyo inaonekana kuhusiana na madai kwamba Iran imeendelea kuboresha teknolojia ya makombora yake licha ya vikwazo vya kimataifa na mashambulizi yaliyolenga miundombinu yake.

Wakati wa ziara hiyo pia, Mkuu wa Majeshi ya Iran, Ali Abdollahi, alionya kwamba ikiwa Iran itashambuliwa tena, majibu yake yanaweza kufika mbali zaidi ya eneo la Mashariki ya Kati.

Kauli hiyo inaendana na matamshi ya hivi karibuni ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ambaye alisema kuwa majibu dhidi ya maadui yanapaswa kuwa ya haraka, yenye nguvu na yasiyozuiliwa na mipaka ya kijiografia.

Wachambuzi wengi wanaona tamko hilo kama ishara kwamba Iran inaweza kuwa inazingatia kuongeza uwezo wa makombora yenye masafa marefu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Baadaye, msemaji wa Walinzi wa Mapinduzi pia alieleza kwamba vikwazo vilivyowekwa katika matumizi ya makombora vinaweza kuondolewa huku uzalishaji wa makombora na ndege zisizo na rubani ukiendelea kuhamishwa kwenye vituo vya chini ya ardhi.

Kwa miaka mingi, masafa ya juu ya makombora ya Iran yamekadiriwa kuwa kati ya kilomita 2,000 na 2,500.

Jeshi la Iran limeeleza kwamba hapo awali kulikuwa na mwongozo ulioweka kikomo cha masafa ya makombora hadi kilomita 2,000 pekee, jambo ambalo lilizorotesha maendeleo ya makombora yenye uwezo wa kufika mbali zaidi.

Miundombinu ya makombora ya Iran imeathirika kwa kiwango gani?

.

Ili kuelewa umuhimu wa kuonyeshwa kwa "mji mpya wa makombora", ni muhimu kuangalia hali ya miundombinu ya Iran baada ya vita vya siku 40.

Gazeti la Washington Post liliripoti mapema mwaka huu kuwa vituo vinne muhimu vya uzalishaji wa makombora ya balestiki na angalau maeneo 29 ya uzinduzi wa makombora viliharibiwa katika wiki za kwanza za mashambulizi ya Marekani na Israel.

Miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni Khajir, Parchin, Hakimiyya na Shahroud, ambayo yana umuhimu mkubwa katika uzalishaji wa mafuta ya makombora na uunganishaji wa mifumo ya silaha.

Aidha, baadhi ya milango ya kuingia kwenye maghala ya chini ya ardhi yaliyotumika kuhifadhi makombora iliharibiwa au kufungwa kutokana na mashambulizi hayo.

Hata hivyo, wataalamu walioshiriki katika uchunguzi huo walisisitiza kwamba uharibifu huo haukumaanisha mwisho wa mpango wa makombora wa Iran.

Picha za satelaiti pia zimeonyesha shughuli kubwa za ukarabati na ujenzi karibu na vituo vikuu vya makombora vilivyoathiriwa wakati wa vita.

Katika kambi ya makombora ya Kermanshah, majengo mapya yamejengwa juu ya maeneo yaliyokuwa yameharibiwa. Vivyo hivyo, mabaki ya majengo yaliyoharibika yameondolewa katika eneo la kijeshi la Parchin mashariki mwa Tehran.

Jim Lamson, mchambuzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), amesema kuwa shughuli za uchimbaji zinazoshuhudiwa karibu na Shahroud zinaweza kuwa zinahusiana na uzalishaji wa makombora.

Ripoti nyingine ya Taasisi ya Foreign Policy Research Institute ilichunguza vituo vya Parchin, Khajir na Shahroud kwa kutumia picha za satelaiti za kibiashara.

Ripoti hiyo iligundua kuwa shughuli kadhaa zilikuwa zikiendelea katika maeneo ya chini ya ardhi ya vituo hivyo, ingawa kulikuwa na ushahidi mdogo wa kurejea kwa uzalishaji kamili katika sehemu za juu ya ardhi.

Katika Parchin, kituo cha kutengeneza makombora ya mafuta magumu kilionekana bado hakijarejea katika hali yake ya kawaida.

Khajir nayo ilionyesha dalili za uharibifu mkubwa katika sehemu zinazohusika na utengenezaji wa makombora ya mafuta magumu na yale ya mafuta ya kioevu.

Shahroud ilionekana kupiga hatua zaidi katika shughuli za ukarabati kuliko vituo vingine, lakini bado hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kurejea kwa uzalishaji wa kiwango cha awali.

Jambo moja lililovutia watafiti ni kuendelea kupanuliwa kwa handaki za chini ya ardhi katika Shahroud.

Wataalamu wanaamini kuwa handaki hizo zinaweza kuwa zimejengwa ili kulinda shughuli zinazohusiana na mpango wa makombora wa Iran, ingawa hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuhusu matumizi yake halisi.

Kwa ujumla, picha za satelaiti zinaweza kuonyesha kiwango cha uharibifu au shughuli za ujenzi zinazoendelea, lakini haziwezi kueleza kwa uhakika kinachoendelea ndani ya vituo vya chini ya ardhi.

Ndiyo maana kuonyeshwa kwa "mji mpya wa makombora" kunaonekana kuwa na lengo la kuonyesha kwamba, licha ya hasara zilizosababishwa na vita, Iran bado ina uwezo mkubwa wa kuhifadhi, kuzalisha na kuendeleza makombora yake, huku ikijaribu kuwashawishi maadui wake kwamba uwezo huo unaweza kuleta mshangao wowote katika mzozo wa baadaye.

Imefasiriwa na Asha Juma