Tembo 'wanajitibu' kwa dawa za mitishamba - Utafiti wagundua

x
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Tembo wa Afrika wanaweza kutumia aina kadhaa za mimea ya dawa kujitibu wanapougua, huku tembo majike wakiripotiwa kuwapa watoto wao baadhi ya mimea hiyo.

Hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na watu wanaoishi na kufanya kazi karibu na tembo katika Mlima Elgon, nchini Kenya.

Tembo hao wamekuwa wakivutia wanasayansi kwa muda mrefu kutokana na tabia yao isiyo ya kawaida. Wamepewa jina la tembo wachimbaji chumvi kwa sababu huingia kwenye mapango na kukwangua miamba kwa kutumia mikonga yao ili kupata madini wanayohitaji mwilini.

Utafiti huo mpya umeonyesha kuwa tembo hao pia hutumia aina mbalimbali za mimea inayopatikana msituni kwa madhumuni ya kujitibu.

Mmoja wa waandishi wakuu wa utafiti huo, Dkt Elodie Freimann, mwanasayansi katika Chuo Kikuu cha Brown nchini Marekani, amesema matokeo hayo yanazua swali kuhusu iwapo ukataji wa misitu unaweza kuwanyima wanyama na binadamu mimea yenye dawa wanazohitaji ili kuwa na afya bora.

"Matokeo haya yanaonyesha jinsi dawa tunazotumia zilivyo na uhusiano wa karibu na viumbe wengine katika mazingira ya asili," aliiambia BBC News.

Mimea ya dawa kwa ajili ya watoto wa tembo

g

Wanasayansi walishirikiana na taasisi ya Mount Elgon Foundation, inayojihusisha na uhifadhi wa mazingira. Walizungumza na wakazi wa eneo hilo, wakiwemo walinzi wa wanyamapori na wazee wa jamii.

Katika mahojiano hayo, baadhi ya watu walisema kuwa tembo hula mimea fulani wanapojisikia vibaya, huku tembo majike wakiwapa watoto wao sehemu za mimea inayotumika kama dawa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kutokana na maelezo hayo, watafiti, wakiwemo wanasayansi kutoka Makumbusho ya Kitaifa ya Kenya jijini Nairobi, walibaini kuwa tembo hao hutumia aina 35 za mimea. Kati ya hizo, aina 25 zinajulikana na wenyeji kuwa na sifa za kutibu magonjwa.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Scientific Reports haukutaja majina ya watu waliohojiwa. Utambulisho wao ulifichwa ili waweze kutoa maelezo yao kwa uhuru.

Kuna simulizi kadhaa za kuvutia katika mahojiano hayo. Kwa mfano, mlinzi mmoja wa wanyamapori alisema alimwona tembo akitumia mmea unaoitwa Angurweet kuwapa watoto wake kama dawa.

Mmea huo hutumika kutibu matatizo mbalimbali, yakiwemo maumivu ya tumbo.

Kwa mujibu wa mlinzi huyo, aliwahi kuona tembo jike akiutayarisha mmea huo kwa mdomo wake. Aliondoa majani na kuyatafuna pamoja na mizizi ya miti mingine hadi vilainike.

Alisema baadaye tembo huyo alichanganya mchanganyiko huo na maziwa yake na kuwapa watoto wake.

"Aliwapa watoto wake, nao wenyewe waliutafuna na kutema sehemu ngumu," alisema.

x

Hata hivyo, Profesa Michael Huffman, mtaalamu wa tabia za nyani na wanyama wengine wa jamii hiyo katika Chuo Kikuu cha Nagasaki nchini Japan, amesema taarifa hizo zinavutia lakini ushahidi zaidi unahitajika kuthibitisha kuwa tembo huwapa watoto wao dawa maalumu.

Wanasayansi tayari wameanza kukusanya ushahidi huo. Wamewapatia wataalamu wa eneo hilo kamera ili kurekodi tabia za tembo wanaowafuatilia.

Pia wanachunguza mimea inayotumiwa na tembo hao ili kubaini iwapo inaweza kuwa chanzo cha dawa mpya.

Dkt Fabien Schulz, mwandishi mwingine mkuu wa utafiti huo kutoka Taasisi ya Bernhard Nocht ya Tiba za Kitropiki mjini Hamburg, Ujerumani, aliiambia BBC News kuwa maarifa ya wenyeji yaliwapa mwongozo wa kuanza utafiti.

"Maarifa ya wenyeji yalitupa ramani," alisema.

Aliongeza kuwa sasa wanataka kuwafuatilia tembo hao ili kubaini iwapo huchagua mimea maalumu kulingana na ugonjwa au hali yao ya kiafya, na kama mimea hiyo ina athari za kibiolojia zinazoweza kuthibitishwa.

Wanyama ni viwanda vya asili vya dawa

f

Si tembo pekee wanaotumia mimea na tiba nyingine za asili kujitibu. Wanyama wengi wana tabia hiyo.

Taarifa za kwanza za kisayansi kuhusu tembo kujitibu zinaanzia mwanzoni mwa karne ya tatu baada ya Kristo.

Mwandishi wa Kirumi, Claudius Aelian, aliandika katika kitabu chake De Natura Animalium, kinachohusu maisha ya wanyama, kuhusu tembo aliyejeruhiwa kwa mikuki na mishale. Tembo huyo alikula maua na mafuta ya mzeituni na hatimaye akapona kabisa.

Karne nyingi zimepita tangu wakati huo, na wanasayansi wanaendelea kuchunguza kile wanachoweza kujifunza kuhusu sifa za mimea inayopatikana katika mazingira ya asili ambamo wanyama wameishi na kubadilika kwa muda mrefu.

"Kuna viumbe katika sayari hii vyenye uwezo wa ajabu wa kutengeneza dawa," Dkt Freimann aliiambia BBC News. "Ni viwanda vya asili vya dawa vinavyotuzunguka."

d

Profesa Huffman, ambaye hakushiriki katika utafiti huo, alisema wanasayansi sasa wanajua kuwa mbu na nzi wa matunda wanaweza kujitibu, na hata nyuki wana uwezo huo.

Alisema tabia hiyo inapatikana pia kwa viumbe wengine wengi katika mnyororo wa mageuzi, hadi kwa nyani wakubwa wanaopatikana Afrika na Asia.

"Kwa kila aina mpya ya mnyama tunayemchunguza, tunapata taarifa zaidi kuhusu jinsi mababu zetu walivyotumia dawa," alisema.

Kwa upande wa Dkt Freimann, matokeo ya utafiti huo yanaweza pia kuwa funzo kuhusu namna ya kulinda afya ya binadamu katika siku zijazo.

Alisema dawa nyingi tunazonunua kwenye maduka ya dawa hutokana na kemikali zinazopatikana kwenye miti, mwani, fangasi na miamba ya matumbawe.

"Kwa hiyo, kulinda misitu hii na kuhifadhi vyanzo hivi vya asili vya dawa kuna manufaa kwetu sote. Tukivihifadhi kwa muda mrefu, tunaweza kugundua tiba mpya za asili zitakazoweza kuokoa maisha yetu siku zijazo."