Mji mkuu wa kwanza duniani kuachana na pesa taslimu

s
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Serikali ya Pakistan imetangaza mpango wa kuifanya Islamabad kuwa "mji mkuu wa kwanza duniani usiotumia fedha taslimu" na pia "mji wa kwanza nchini humo unaotumia mfumo wa malipo ya kidijitali."

Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya mambo ya ndani Ijumaa (Novemba 13), serikali imeweka tarehe 31 Desemba kuwa tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa mpango huo.

Hatua hii imelenga kuhakikisha kwamba kufikia tarehe hiyo, biashara zote na wafanyabiashara wote mjini Islamabad wanaunganishwa na mfumo wa malipo ya kidijitali.

Kwa mujibu wa Wizara ya mambo ya ndani, kikao muhimu kuhusu mradi huo ulioitwa kwa lugha ya kimombo "Cashless Islamabad" kiliongozwa na Waziri wa nchi anayeshughulikia Mambo ya ndani, Talal Chaudhry.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa mamlaka ya maendeleo ya Jiji la Islamabad (CDA), Sohail Ashraf, pamoja na wawakilishi wa sekta ya benki na maafisa wengine waandamizi.

Kikao hicho kilijadili mapendekezo na mikakati mbalimbali ya kubadilisha mfumo wa malipo wa Islamabad kuwa kidijitali kwa asilimia 100.

Talal Chaudhry alisema kuwa ushirikiano na mashauriano ya wadau wote ni muhimu ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

Alisema kuwa "Waziri wa Mambo ya Ndani wa Shirikisho, Mohsin Naqvi, amemuahidi Waziri Mkuu kwamba Islamabad itakuwa mji wa kwanza nchini Pakistan usiotumia fedha taslimu na mji mkuu wa kwanza duniani kuwa wa namna hiyo."

Kwa mujibu wake, kuanzia baada ya Novemba 30, fedha taslimu hazitakubaliwa tena katika idara yoyote ya Islamabad Capital Territory (ICT) na Mamlaka ya Maendeleo ya Jiji la Islamabad (CDA).

Talal Chaudhry alisema lengo ni kuhakikisha kuwa biashara zote za Islamabad zinaingia kwenye mfumo wa malipo ya kidijitali ifikapo Desemba 31.

Aliongeza kuwa matumizi makubwa ya malipo ya kidijitali yatasaidia kuongeza uwazi katika miamala ya kifedha, kuboresha ufuatiliaji wa ukusanyaji wa kodi, na kuimarisha mchakato wa ununuzi na manunuzi ya serikali.

Waziri wa Mambo ya Ndani alisema kuwa hadi sasa wafanyabiashara 26,000 wamejiandikisha kutumia mfumo wa malipo ya kidijitali mjini Islamabad.

Serikali imeeleza kuwa lengo la kuifanya Islamabad kuwa mji usiotumia fedha taslimu ni kurahisisha matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wananchi, na si kuwalazimisha watu kuacha kabisa kutumia fedha taslimu.

Islamabad itafanyaje kutotumia fedha taslimu?

s
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Akizungumza na BBC Urdu, Waziri anayeshughulikia mambo ya ndani, Talal Chaudhry, alisema serikali imekusudia ifikapo Desemba 31 kila biashara, iwe ni duka dogo au taasisi kubwa ya kibiashara, itakuwa na uwezo wa kupokea malipo ya kidijitali.

Alisema kuwa chini ya mradi huo, kila biashara mjini Islamabad itawezeshwa kupokea malipo ya kidijitali endapo mteja atapendelea kutumia njia hiyo.

Akitolea maelezo zaidi mradi huo, Talal Chaudhry alisema malipo ya kidijitali yatawezeshwa katika ngazi zote, kuanzia wafanyabiashara wadogo wa mitaani hadi kampuni kubwa za biashara.

Kadhalika wafanyabiashara watapatiwa akaunti za bure na neno siri ili kurahisisha kupokea malipo ya kielektroniki.

Waziri huyo alisisitiza kwamba serikali inashughulikia vifaa vinavyoitwa "voice boxes" katika maeneo mbalimbali ya biashara.

Vifaa hivyo vitatoa taarifa za sauti mara moja kuthibitisha kuwa malipo yamepokelewa.

Kwa mujibu wake, hatua hiyo itaongeza imani na kuondoa hofu kwa wanunuzi na wauzaji wakati wa kufanya miamala.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa upinzani kutoka kwa wamiliki wa malori na wafanyabiashara wadogo, Talal Chaudhry alisema kuwa mashauriano na tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara wadogo tayari wanafahamu jinsi ya kutuma na kupokea fedha kwa kutumia simu za mkononi.

Aliongeza kuwa serikali inataka kupanua matumizi hayo kupitia kampeni za uhamasishaji na kuweka mazingira rafiki yatakayorahisisha matumizi ya malipo ya kidijitali.

Pia alisema kwamba maeneo ya biashara katika mji wa Islamabad yataonyesha wazi kuwa huduma za malipo ya kidijitali zinapatikana.

Kwa mujibu wa Talal Chaudhry, mradi wa "Cashless Islamabad" ni sehemu ya maono mapana ya Waziri Mkuu wa Pakistan, yenye lengo la kuifanya Islamabad kuwa mji mkuu wa kwanza nchini humo usiotumia fedha taslimu.

Hata hivyo, sio kila sekta ina matumaini makubwa kuhusu mpango huo. Vyama vya wafanyabiashara vinasema kuwa kutokana na kiwango cha sasa cha ushirikishwaji wa huduma za kifedha na uelewa wa teknolojia za kidijitali nchini Pakistan, ni vyema mabadiliko hayo yakatekelezwa kwa hatua na kwa awamu badala ya kufanywa mara moja.

Je umma na wafanyabiashara wadogo wako tayari?

s

Ajmal Baloch, rais wa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Pakistan amesema bado idadi kubwa ya watu nchini humo hawana simu janja, akaunti za benki wala huduma za malipo ya kidijitali.

Akizungumza na BBC Urdu, alisema kuwa iwapo wafanyabiashara wadogo na wauzaji wa mitaani hawataweza kujiunga na mfumo wa kidijitali, hali hiyo inaweza kuwaathiri moja kwa moja watumiaji wa kipato cha chini.

Kwa sababu hiyo, huenda wakalazimika kusafiri hadi kwenye vituo vikubwa vya ununuzi ili kupata mahitaji yao ya kila siku.

Hata hivyo kwa mujibu wa Ajmal Baloch, changamoto hizi haziwahusu wafanyabiashara pekee bali pia watumiaji wa kawaida, hasa wale ambao bado hawajazoea huduma za benki za kidijitali na malipo ya mtandaoni.

Alisema wengi nchini Pakistan bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu miamala ya kidijitali, na matatizo kama kutuma fedha kwenye akaunti au namba isiyo sahihi hutokea mara kwa mara.

"Iwapo mabadiliko haya yatatekelezwa kwa wakati mmoja, wananchi wengi watakumbana na matatizo."

Ajmal Baloch aliongeza kuwa changamoto hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi kwa wafanyabiashara wadogo na wauzaji wa mitaani kuliko kwa wafanyabiashara wakubwa, kwani wengi wao hawana akaunti rasmi za benki.

Pia alionya kuwa kadiri matumizi ya malipo ya kidijitali yanavyoongezeka, ndivyo hatari za utapeli wa mtandaoni zinavyoongezeka.

Kwa mujibu wake, watu wasio na elimu ya kutosha au wasioufahamu vizuri teknolojia mara nyingi huwa wahanga wa udanganyifu, na wakati mwingine fedha hutolewa kwenye akaunti zao bila ridhaa yao.

Alisema serikali inapaswa kwanza kujenga imani kwa wadau wote, hasa wafanyabiashara wadogo, wamachinga na watumiaji wa kawaida, kabla ya kutekeleza mradi huo kikamilifu.

Aidha, serikali inapaswa kuongeza uhamasishaji na ushirikishwaji wa wananchi huku ikielekea taratibu kwenye mfumo usiotumia fedha taslimu.

"Hili linaweza kuwa mwelekeo mzuri, lakini katika nchi yenye changamoto za kiuchumi kama Pakistan, ni vyema mabadiliko ya aina hii yakaanzishwa hatua kwa hatua."

Mbali na masuala ya upatikanaji wa huduma za kifedha na wasiwasi wa wafanyabiashara, wataalamu pia wanaelekeza macho yao kwenye suala lingine muhimu, ambalo ni usalama wa mtandao (cybersecurity).

Changamoto za kiusalama na kiufundi zitakazokabili mfumo huu

Kwa mujibu wa mshauri wa usalama wa mtandao, Mirza Burhan Baig, hatari kubwa zaidi ya mfumo usiotumia fedha taslimu ni kile kinachoitwa "single point of failure". Hii ina maana kwamba iwapo mfumo wa benki, mtandao wa simu au jukwaa kuu la malipo utapata hitilafu au kusimamishwa kwa sababu yoyote, shughuli za kifedha za wananchi zinaweza kuathirika kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza na BBC Urdu, alisema kuwa mitandao ya simu nchini Pakistan wakati mwingine huzimwa kwa sababu za kiusalama au kiutawala. Hivyo, ikiwa malipo yote yatategemea njia za kidijitali pekee, wananchi wanaweza kukumbana na ugumu wa kununua, kuuza na kufanya miamala mingine ya kila siku.

Kwa mujibu wa Burhan Baig, katika uchumi unaotegemea malipo ya kidijitali, pia huongezeka hatari za uhalifu wa mtandaoni kama vile:

Wizi wa utambulisho (identity theft),

Misimbo bandia ya QR (fake QR codes),

Wizi wa akaunti za watumiaji (account takeovers).

Alisema kuwa ikiwa mhalifu atafanikiwa kupata taarifa za siri za mtumiaji, anaweza kuingia kwenye akaunti hiyo na kuitumia vibaya, huku mmiliki halisi akilazimika kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kurejeshewa udhibiti wa akaunti yake.

Mirza Burhan Baig alieleza kuwa miradi mikubwa ya kidijitali ya serikali na sekta binafsi mara nyingi hutegemea kampuni mbalimbali za programu, ushirikiano wa kiteknolojia na huduma za wahusika wengine. Endapo kutakuwa na udhaifu wa kiusalama katika sehemu yoyote ya mfumo huo, inaweza kuhatarisha mfumo mzima.

Aliongeza kuwa wananchi wanaweza kukumbwa na matatizo ya haraka ya kifedha iwapo simu zao zitapotea, kuibiwa au hata akaunti zao za benki zikafungwa kwa muda, hasa ikiwa hawana mbadala wa kutumia fedha taslimu.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa usalama wa mtandao, mafanikio ya mfumo usiotumia fedha taslimu hayategemei teknolojia pekee, bali pia kiwango cha uelewa wa wananchi.

Alisema kuwa bado watu wengi nchini Pakistan hawana uelewa wa kutosha kuhusu fedha za kidijitali, uhamishaji wa fedha kwa njia ya kielektroniki na malipo kwa simu.

Kutokana na hali hiyo, mabadiliko ya aina hii yanapaswa kutekelezwa kwa awamu sambamba na kampeni kubwa za elimu na uhamasishaji kwa umma.

Mirza Burhan Baig alibainisha kuwa katika nchi nyingi duniani, mifumo ya malipo yasiyotumia fedha taslimu imeanzishwa hatua kwa hatua.

Kwanza hujaribiwa katika maeneo au sekta chache kupitia miradi ya majaribio, kabla ya kupanuliwa kitaifa. Kwa maoni yake, mkakati kama huo wa taratibu unaweza kuwa na mafanikio zaidi nchini Pakistan.