Ulaya yaamua: Wahamiaji wanaofukuzwa kwa nchi hizi 5 kupelekwa Rwanda

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Olivia Ireland
- Author, Bethany Bell
- Akiripoti kutoka, Vienna
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Nchi tano wanachama wa Umoja wa Ulaya zinapanga kuanzisha kituo cha kuwahamishia wahamiaji nchini Rwanda kuanzia mwaka 2027.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za mataifa hayo kudhibiti uhamiaji na kuongeza idadi ya wahamiaji wanaoondolewa katika nchi zao.
Nchi zinazohusika ni Ujerumani, Denmark, Austria, Ugiriki na Uholanzi.
Kituo hicho kitakachojulikana kama return hub kitakuwa mahali pa kuwapokea wahamiaji wanaoishi kinyume cha sheria katika nchi hizo na ambao wamekamilisha taratibu zote za kisheria za kukata rufaa dhidi ya kuondolewa nchini.
Serikali ya Uholanzi imesema mpango huo utatoa njia mbadala kwa wahamiaji ambao hawawezi kurejeshwa katika nchi walikotoka.
Wahamiaji watapewa nafasi ya kuanza maisha Rwanda
Kwa mujibu wa nchi hizo tano, wahamiaji watakaopelekwa Rwanda watakuwa na chaguo la kujumuika katika jamii ya nchi hiyo au kurejea katika mataifa yao ya asili.
Wale watakaoamua kubaki Rwanda watapewa haki ya kuishi nchini humo na kupata huduma za elimu, afya, ajira pamoja na mfumo wa haki.
Katika taarifa yake, serikali ya Uholanzi ilisema hatua ya kwanza ya mpango huo itawahusu wanaume wasio na wenza pekee.
Iliongeza kuwa kwa upande wa Uholanzi, kipaumbele kitakuwa kwa wahamiaji wanaotoka katika mataifa yaliyo katika ukanda mmoja wa kijiografia na Rwanda.
Kabla ya kutangazwa kwa mpango huo, vyanzo vya kidiplomasia vililiambia shirika la habari la AFP kuwa kituo hicho kitaanza kama mradi wa majaribio, kikitarajiwa kupokea takribani watu 100.
Kila moja ya nchi hizo tano inaweza kutuma wahamiaji wapatao 20.
Rwanda yasema iko tayari kushirikiana na Ulaya
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Rwanda, Vincent Biruta, alisema nchi yake imejizatiti kushirikiana na washirika wake wa Ulaya kutafuta suluhisho salama, halali na lenye kuheshimu utu wa wahamiaji.
Alisema Rwanda pia itashirikiana na nchi hizo kukabiliana na tofauti za fursa za kiuchumi duniani, ambazo alizitaja kuwa miongoni mwa sababu kuu zinazochangia ''uhamiaji usiofuata taratibu za kisheria''.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, huenda likashiriki katika mpango huo.
Shirika hilo limesema lina uzoefu wa kusaidia wahamiaji walio katika mazingira magumu na tayari linafanya mazungumzo na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu uanzishaji wa vituo vya aina hiyo.
Tofauti na mpango wa zamani wa Uingereza
Mpango huo utawahusu wahamiaji ambao wamekamilisha njia zote za kisheria za kupinga kuondolewa katika nchi hizo tano na ambao hawana tena haki ya kuendelea kuishi humo.
Hii ni tofauti na mpango wa zamani wa Uingereza uliolenga kuwapeleka wahamiaji nchini Rwanda ili maombi yao ya hifadhi yashughulikiwe wakiwa huko.
Mpango huo wa Uingereza haukuwahi kutekelezwa kutokana na changamoto za kisheria na hatimaye ulifutwa mwaka 2024 baada ya serikali ya Chama cha Labour kuingia madarakani.
Hata hivyo, Uingereza haijaondoa uwezekano wa kujiunga na mpango mpya wa Umoja wa Ulaya. Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaufuatilia kwa karibu kabla ya kuamua hatua inayofuata.
Mpango huo mpya unawezekana kufuatia mageuzi ya hivi karibuni ya sheria za uhamiaji za Umoja wa Ulaya, yaliyoruhusu nchi wanachama kuanzisha vituo vya kuwahamishia wahamiaji katika mataifa yaliyo nje ya umoja huo
Mpango huo wakosolewa na Uhispania
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, mpango huo haujakubaliwa na kila mtu.
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez ameukosoa, akisema hauwezi kuwa na mustakabali wala utu.
"Siioni mustakabali wala utu katika mpango huo. Huo si suluhisho," alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Telecinco, kwa mujibu wa AFP.
Nchi hizo tano zinasema mpango huo unazingatia sheria za Umoja wa Ulaya na sheria za kimataifa.
Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuwa unaweza kuhatarisha haki za wahamiaji.
Mpango huo unafuatia mageuzi ya hivi karibuni ya sera za uhamiaji za Umoja wa Ulaya yaliyoruhusu mataifa wanachama kuanzisha vituo vya kuwahamishia wahamiaji nje ya mipaka ya umoja huo.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika Vienna siku ya Jumatatu, Kansela wa Austria Christian Stocker alisema nchi hizo tano zinalenga kupunguza mzigo katika mifumo ya Ulaya ya kushughulikia maombi ya hifadhi.
Alisema pia zinataka kudhibiti mitandao ya magendo ya binadamu inayowapanga wahamiaji kusafiri katika safari hatari kuvuka Bahari ya Mediterania.
Wasiwasi kuhusu Rwanda kuwa mwenyeji wa wahamiaji hao
Shirika la Human Rights Watch limeeleza wasiwasi kuhusu uamuzi wa kuifanya Rwanda kuwa mwenyeji wa kituo hicho.
Mtafiti mkuu wa shirika hilo anayeshughulikia masuala ya Afrika, Clementine de Montjoye, amesema Rwanda ina historia ya kukandamiza wapinzani, kuwakamata watu kiholela na kuwatesa walio kizuizini.
Alisema Rwanda ina historia inayojulikana ya kukandamiza wapinzani, kuwakamata watu bila kufuata taratibu za kisheria na kuwatesa watu walio kizuizini.
Pia aliituhumu Rwanda kwa kuunga mkono makundi yenye silaha katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
"Kuilipa Kigali ili iwe mwenyeji wa mpango wa kuwahamisha wahamiaji hakutasababisha tu mateso na madhara kwa watu watakaopelekwa huko, bali pia kutaiwezesha serikali inayohusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi kupata fedha na ushawishi wa kisiasa," alisema.
Kwa upande wake, Shirika Huru la Umoja wa Ulaya la Haki za Msingi limesema nchi yoyote isiyo mwanachama wa EU itakayokuwa mwenyeji wa kituo hicho lazima iheshimu haki za msingi za binadamu.
Limesisitiza kuwa watu hawapaswi kupelekwa katika nchi ambako wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuteswa au kunyimwa haki zao.
Shirika hilo pia limesema watoto wanaosafiri bila kusindikizwa na wazazi au walezi hawapaswi kupelekwa katika vituo hivyo.
Serikali ya Uholanzi imethibitisha kuwa watoto wa aina hiyo hawatajumuishwa katika mpango huo.
Uhamiaji barani Ulaya wapungua
Mpango huo unakuja wakati serikali kadhaa za Ulaya zikikabiliwa na shinikizo la kuonyesha kuwa zinaweza kudhibiti uhamiaji, hasa wakati uchaguzi unapokaribia katika baadhi ya nchi.
Masuala ya usalama, changamoto za kiuchumi na kutoridhishwa kwa wananchi na serikali zao yamechangia kuongezeka kwa mjadala kuhusu uhamiaji.
Hata hivyo, takwimu za Shirika la Ulaya la Usimamizi wa Mipaka na Walinzi wa Pwani zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaoingia katika Umoja wa Ulaya kwa njia zisizo rasmi imepungua.
Katika miezi 10 ya kwanza ya mwaka 2026, karibu watu 110,000 walivuka mipaka ya Umoja wa Ulaya kwa njia zisizo rasmi.
Hiyo ni pungufu kwa asilimia 29 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025.
Katika mwezi Oktoba pekee, takribani watu 18,100 waligunduliwa wakivuka mipaka hiyo.
Idadi hiyo ilikuwa chini kwa asilimia sita ikilinganishwa na Oktoba 2025, lakini ilikuwa juu kwa asilimia 22 ikilinganishwa na Septemba mwaka huu.
Ongezeko hilo lilichangiwa zaidi na kuongezeka kwa wahamiaji waliotumia njia ya Afrika Magharibi kuelekea Visiwa vya Canary vya Uhispania.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid































