"Kwa nini niliamua kuwa jambazi?"

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kiongozi mmoja wa makundi yenye silaha kaskazini mwa Nigeria amesema kuwa ubaguzi wa muda mrefu dhidi ya wafugaji wa Kifulani pamoja na vitendo vya unyang'anyi na rushwa vimechangia kuibuka kwa mgogoro unaoendelea kulitikisa eneo hilo.

Mwanaume huyo, anayejitambulisha kwa jina la Babangida, amesema tatizo hilo halitamalizika hadi pale ufisadi uliokithiri na ukosefu wa haki utakaposhughulikiwa kikamilifu.

Kwa miaka kadhaa sasa, makundi yanayojulikana nchini Nigeria kama "majambazi" yamekuwa yakifanya mashambulizi katika maeneo ya kaskazini-magharibi na katikati mwa nchi hiyo. Makundi hayo yanahusishwa na uporaji wa vijiji, wizi wa mifugo, utekaji nyara kwa ajili ya fidia na ulazimishaji wa wakulima pamoja na wachimbaji madini kulipa kodi haramu.

Kwa mujibu wa Babangida, shinikizo na mateso yanayodaiwa kuelekezwa kwa wafugaji wa Kifulani ndiyo yaliyochangia baadhi yao kuamua kubeba silaha.

"Njia pekee ya kuleta amani ni haki," amesema.

Chanzo cha mgogoro

.

Mzizi wa mgogoro huo ni migongano ya muda mrefu kati ya wafugaji na wakulima kuhusu matumizi ya ardhi ya malisho na vyanzo vya maji.

Mabadiliko ya tabianchi pamoja na ongezeko la idadi ya watu yamezidisha ushindani wa rasilimali hizo na kuongeza mvutano kati ya makundi hayo mawili.

Kadri muda ulivyopita, baadhi ya makundi yenye silaha yaliingia katika biashara ya utekaji nyara kwa ajili ya fidia na uhalifu uliopangwa, huku baadhi yao yakihusishwa na mitandao yenye uhusiano na makundi ya wanamgambo wa itikadi kali.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya juhudi za serikali, ghasia zinaendelea.

Wiki iliyopita, watu wenye silaha walidaiwa kuwaua watu 12 wa familia moja katika jimbo la Zamfara baada ya kuchoma nyumba yao.

Mapema mwezi huu, maafisa wanane wa polisi waliuawa, huku mwezi Septemba zaidi ya watu 80 wakitekwa nyara katika majimbo ya Zamfara na Niger.

Usalama umeendelea kuwa moja ya masuala makubwa katika mjadala wa kisiasa nchini Nigeria.

"Kuna Kitu Kilichonisukuma Kubeba Bunduki"

Babangida mwenye umri wa miaka 38, aliyekuwa amevaa shati la bluu na kubeba bunduki aina ya Kalashnikov, alisema kuwa si kila mtu anayebeba silaha huzaliwa mhalifu.

"Jambazi si mtu anayechukua bunduki na kuanza kufanya uhalifu bila sababu. Lazima kuna jambo linalomsukuma kufanya hivyo," alisema.

Anasema aliingia kwenye makundi ya silaha miaka 10 iliyopita baada ya operesheni ya polisi na vikundi vya kujilinda kusababisha kukamatwa kwa ng'ombe 97 waliokuwa wa familia yake.

Kwa mujibu wake, mamlaka zilikuwa zikifanya hivyo kwa imani kwamba wafugaji wote wa Kifulani walikuwa majambazi.

Anadai alilazimika kulipa mamilioni ya naira ili kuwatoa mama yake na ndugu yake waliokuwa wamewekwa rumande.

Baada ya kufanikiwa kurejesha ng'ombe 10 pekee kati ya waliokamatwa, anasema alitumia fedha zilizobaki kununua silaha na kuhamishia familia yake katika kambi iliyoko msituni.

Wafugaji wa Kifulani wanalalamika nini?

Kwa karne nyingi, wafugaji wa Kifulani wamekuwa wakihamahama na mifugo yao kutoka kaskazini mwa Nigeria kuelekea maeneo ya kati na kusini kufuata malisho kulingana na misimu.

Hata hivyo, viongozi wa jamii za wafugaji wamekuwa wakilalamikia kile wanachodai kuwa ni kushindwa kwa serikali, polisi na jeshi kulinda njia za malisho dhidi ya uvamizi wa wakulima.

Pia kumekuwa na madai kwamba baadhi ya maafisa wa serikali hushirikiana na wakulima katika kunyakua ardhi za wafugaji.

Madai ya Ubaguzi

Ingawa wakulima na wafugaji wote wamepoteza maisha na mali kutokana na mgogoro huo, wafugaji wa Kifulani wanadai kuwa serikali imekuwa ikiwatenga na kuwachukulia kama wahalifu kabla hata ya uchunguzi kufanyika.

Babangida anasema kwamba pale ng'ombe wanapoharibu mazao ya mkulima, wazee wa eneo hilo huwaweka wafugaji faini kubwa kuliko thamani ya mazao yaliyoharibiwa.

Lakini iwapo mkulima ataua mifugo ya mfugaji, anadai hakuna fidia inayotolewa na mara nyingi lawama humwangukia mfugaji.

Anasema pia kwamba pale wazee wanapoliita polisi kuingilia kati, baadhi yao hushirikiana na mahakama kuongeza adhabu kwa wafugaji.

Je, Madai Hayo Ni ya Kweli?

Jeshi la Nigeria limekuwa likiyaelezea makundi ya silaha kama makundi ya kigaidi na limeendesha operesheni maalumu za kijeshi katika maeneo ya kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu madai ya Babangida, Kamishna wa Usalama wa Ndani wa Jimbo la Katsina, Nasiru Mu'azu, alikubali kwamba baadhi ya hoja hizo zina msingi.

"Anachokisema ni kweli, na hiyo ni moja ya sababu zilizochangia kuibuka kwa uhalifu huu," alisema.

Mu'azu amesema serikali imekuwa ikijaribu kuanzisha mazungumzo ya amani na kushughulikia sababu za msingi zinazochochea migogoro hiyo.

Ameeleza kuwa mapigano yanayoendelea kaskazini-magharibi mwa Nigeria yalianza kama mgogoro wa ndani wa jamii na ni tofauti na uasi wa makundi ya wanajihadi yanayopatikana kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wake, changamoto kubwa ni jinsi ya kusawazisha operesheni za usalama na juhudi za kidiplomasia ili kutafuta suluhisho la kudumu.

"Fedha na Kisasi"

Katika baadhi ya maeneo, makundi yenye silaha yamekuwa yakitoza kodi haramu kwa wakulima wanaoendelea kuishi vijijini.

Wakati huo huo, jeshi la Nigeria limekuwa likifanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo yanayodaiwa kutumiwa na makundi hayo.

Wachambuzi wanasema mauaji ya wafugaji yanayotekelezwa na baadhi ya vikundi vya kujilinda yameendelea kuchochea hisia za kisasi na kuathiri juhudi za kufikia makubaliano ya amani.

Kwa wengi, simulizi ya Babangida haiondoi uzito wa uhalifu unaofanywa na makundi ya silaha. Hata hivyo, inaangazia upande mwingine wa mgogoro huo, unaohusisha malalamiko kuhusu ubaguzi, rushwa, ukosefu wa haki na vita ya muda mrefu ya kugombea ardhi na rasilimali.

Na hadi sababu hizo za msingi zitakapopatiwa ufumbuzi, wengi wanaamini kuwa mzunguko wa vurugu unaoikumba kaskazini mwa Nigeria utaendelea.

Imefasiriwa na Asha Juma