Kwa nini wanasiasa Waislamu wanazua mijadala mikali nchini Marekani?

D
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Katika miaka ya hivi karibuni, wanasiasa kadhaa Waislamu wameanza kupata nafasi na ushawishi katika uongozi wa juu nchini Marekani. Hata hivyo, mafanikio yao yameibua mijadala mikali kati ya wanaowaunga mkono na wanaowapinga.

Miongoni mwa wanasiasa hao ni Mbunge Ilhan Omar, Meya wa New York Zohran Mamdani na Abdul El-Sayed, ambaye hivi karibuni alishinda kiti cha Seneti akiwakilisha jimbo la Michigan.

Kuibuka kwao kunaonyesha kuwa Waislamu nchini Marekani wanazidi kupata nafasi katika siasa na kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa nchi hiyo, licha ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Lakini kwa nini mafanikio yao yanazua utata mkubwa?

Kutoka kushukiwa baada ya mashambulizi ya 9/11 hadi kukubalika

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, Waislamu nchini Marekani walikabiliwa na ubaguzi, tuhuma na mashaka katika maeneo mbalimbali.

Wakati huo, changamoto kubwa kwa jamii hiyo ilikuwa kuhakikisha kuwa imani yao ya Kiislamu haiwazuii kufurahia haki zao kama raia kamili wa Marekani.

Lakini sasa, kuibuka kwa viongozi Waislamu katika siasa kunaonyesha kuwa jamii hiyo inazidi kupata nafasi katika uongozi wa nchi.

Viongozi hao pia wamekuwa wakizungumzia masuala yanayowagusa wananchi wa kawaida, kama vile uchumi, afya na elimu.

Je, siasa za Marekani zinabadilika?

Wataalamu wa masuala ya siasa za kimataifa wanaona kuongezeka kwa ushawishi wa wanasiasa Waislamu kama ishara kuwa siasa za Marekani zinazidi kuakisi utofauti wa watu wanaoishi nchini humo.

Hata hivyo, mafanikio yao hayajakosa ukosoaji. Wapinzani wao wanadai kuwa baadhi ya sera na misimamo yao haiendani na mwelekeo wanaoutaka kwa Marekani.

Pamoja na hayo, wanasiasa kama Ilhan Omar, Zohran Mamdani na Abdul El-Sayed wameonyesha kuwa Waislamu wanazidi kupata nafasi katika ngazi za juu za maamuzi. Hali hiyo inachangia kubadilisha sura ya siasa za Marekani.

Ilhan Omar

d
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mbunge Ilhan Omar amekuwa akivutana mara kwa mara na Rais Donald Trump, hasa kuhusu masuala ya uhamiaji, Uislamu, ubaguzi wa rangi, ugaidi na sera za Marekani katika mataifa mengine.

Omar anawakilisha jimbo la Minnesota katika Baraza la Wawakilishi la Marekani. Alizaliwa Somalia na baadaye kuhamia Marekani. Pia ni mmoja wa wakosoaji wakuu wa Trump.

Mwaka 2019, Trump alitoa matamshi ya kumdhalilisha Omar pamoja na wabunge wengine watatu wa chama cha Democratic. Wote walikuwa wanawake weusi au wenye asili ya uhamiaji.

Kupitia mtandao wa Twitter, Trump alisema kuwa kama hawaridhishwi na Marekani, warudi ''katika nchi walikotoka'' na kusaidia kutatua matatizo ya huko badala ya kuikosoa Marekani.

Kauli hizo zilisababisha ukosoaji mkubwa, huku baadhi ya watu wakimtuhumu Trump kwa ubaguzi wa rangi na kuchochea chuki.

Omar alimjibu kwa kumshutumu kwa kuendeleza ubaguzi unaotukuza wazungu na kujaribu kuwagawa Wamarekani.

Mzozo huo uliongezeka katika mkutano wa kampeni wa Trump uliofanyika Greenville, jimbo la North Carolina. Wakati Trump akimkosoa Omar, baadhi ya wafuasi wake walianza kupaza sauti wakisema, "Mrudisheni alikotoka!"

Omar pia amewahi kukosolewa kutokana na kauli yake kuhusu mashambulizi ya Septemba 11, 2001, maarufu kama 9/11. Katika hotuba moja, alitumia maneno "Baadhi ya watu walifanya jambo fulani" kuelezea mashambulizi hayo.

Alikuwa akizungumzia namna Waislamu nchini Marekani walivyokabiliwa na ukosoaji, mashaka na ubaguzi zaidi baada ya mashambulizi hayo.

Katika hatua nyingine, wabunge wa chama cha Republican katika Baraza la Wawakilishi walipiga kura ya kumuondoa Omar katika Kamati ya Masuala ya Kigeni, mojawapo ya kamati zenye ushawishi mkubwa katika baraza hilo.

Republican walisema hatua hiyo ilitokana na matamshi yake ya awali kuhusu Israel, ambayo waliyatafsiri kuwa ya chuki dhidi ya Wayahudi.

Omar aliomba radhi kwa baadhi ya kauli zake, lakini akasema kuondolewa kwake kwa kamati kulikuwa na sababu za kisiasa, badala ya matamshi yake.

Pia alidai kuwa alikuwa akilengwa kwa sababu ya kuwa mwanamke Mwislamu, akisema dini na asili yake vilimfanya akabiliwe na ukosoaji tofauti na wabunge wengine.

Zohran Mamdani

d

Zohran Mamdani, ambaye amekuwa Meya wa New York tangu Januari 2026, pia amekuwa akizua mijadala mikali kuhusu misimamo yake ya kisiasa.

Masuala yanayozua utata zaidi ni msimamo wake kuhusu mzozo wa Israel na Palestina, tuhuma za chuki dhidi ya Wayahudi, mageuzi katika idara ya polisi na sera zake za uchumi.

Mamdani amekuwa akitetea haki za Wapalestina na kuikosoa serikali ya Israel kuhusu hatua zake katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Msimamo huo umemfanya akosolewe na makundi yanayoiunga mkono Israel pamoja na baadhi ya wanasiasa, wanaodai kuwa anaegemea upande wa Palestina.

Baadhi yao wanasema matamshi yake kuhusu Israel na uungaji mkono wake kwa juhudi za kuiwekea nchi hiyo shinikizo vinaibua wasiwasi kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi.

Lakini Mamdani amekanusha tuhuma hizo. Anasema kuikosoa serikali ya Israel hakumaanishi kuwachukia Wayahudi.

Katika masuala ya ndani, Mamdani amependekeza kupunguza baadhi ya fedha zinazotengwa kwa Idara ya Polisi ya New York na kuelekeza fedha hizo katika huduma za makazi, elimu na ustawi wa jamii.

Wanaompinga wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kudhoofisha usalama wa wananchi. Hata hivyo, wanaomuunga mkono wanasema kuwekeza katika huduma hizo kutasaidia kushughulikia sababu zinazochangia uhalifu.

Mamdani pia anahusishwa na itikadi ya ujamaa wa kidemokrasia. Anataka serikali iwe na nafasi kubwa zaidi katika kusimamia uchumi.

Msimamo huo umewafanya baadhi ya Republican na Wademokrat wenye misimamo ya wastani kumkosoa, wakisema sera zake zinaweza kupanua mno nafasi ya serikali katika uchumi.

Hata hivyo, si wapinzani wake pekee wanaomkosoa. Baadhi ya wanaounga mkono haki za Wapalestina pia wamekuwa wakimshutumu kwa kutokuwa mkali vya kutosha katika baadhi ya masuala.

Kutokana na misimamo hiyo, Mamdani amekuwa mmoja wa wanasiasa wanaozungumziwa sana New York, huku akichochea mijadala katika pande tofauti za kisiasa.

Mohammed Abdul El-Sayed

S

Abdul El-Sayed pia amekuwa miongoni mwa wanasiasa wanaovuta hisia za wengi nchini Marekani mwaka 2026.

Ni mwanachama wa chama cha Democratic, daktari na aliyewahi kuwa mkuu wa bodi ya afya ya jiji la Detroit.

Kadiri alivyozidi kupata uungwaji mkono kisiasa, ndivyo alivyokabiliwa na mijadala na tuhuma mbalimbali zilizomfanya kuwa gumzo nchini humo.

Mojawapo ya tuhuma zilizozua mjadala zilihusu madai ya uhusiano wake na kundi la Muslim Brotherhood nchini Misri.

Tuhuma hizo ziliibuka baada ya dada yake wa kambo kuchapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akidai kuwa mama yao alikuwa amehusika katika shughuli za kundi hilo.

El-Sayed alikanusha madai hayo, akisema hajawahi kuwa mwanachama wa kundi hilo na kwamba hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa alikuwa na uhusiano wa moja kwa moja nalo.

Pia alikosolewa kutokana na uhusiano wake na Hasan Piker, mchambuzi wa masuala ya siasa anayejulikana kwa kutoa maoni yanayozua utata.

Piker amewahi kutoa kauli zenye utata kuhusu mashambulizi ya Septemba 11, ambazo baadaye aliziombea radhi.

Baadhi ya Republican na hata Wademokrat walimkosoa El-Sayed kwa kukubali kuungwa mkono na Piker. Hata hivyo, El-Sayed alisema maoni ya Piker hayawakilishi kampeni yake.

Mwezi Machi 2026, shambulizi lililotokea katika sinagogi la Temple Israel, nje ya Detroit, lilizua mjadala mwingine.

Baada ya kulaani shambulizi hilo, El-Sayed alisema kuwa "waliojeruhiwa ndio wanaowajeruhi wengine". Alikuwa akirejelea taarifa kwamba baadhi ya wanafamilia wa mshukiwa wa shambulizi hilo waliuawa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.

Kauli hiyo ilizua ukosoaji kutoka kwa watu walioiona kuwa jaribio la kutoa udhuru kwa shambulizi hilo.

Baadaye, El-Sayed aliomba radhi akisema kuwa hakupaswa kutoa kauli hiyo wakati huo.

Wakati wa kura za mchujo za chama cha Democratic kumtafuta mgombea wa kiti cha Seneti kutoka Michigan, wapinzani wake pia walimshutumu kwa kutoa matamshi yaliyowadhalilisha wanawake.

Ukosoaji huo ulihusu baadhi ya kauli zake kuhusu Gavana Gretchen Whitmer na wanawake wengine mashuhuri.

El-Sayed alikataa tuhuma hizo, akisema ukosoaji wake ulilenga taasisi za kisiasa na mfumo wa utawala, wala si wanawake kama jinsia.

Msimamo wake kuhusu Israel na Palestina pia umeibua mjadala mkubwa.

El-Sayed ameutaja vita vya Israel dhidi ya Gaza kuwa mauaji ya halaiki na kutaka Marekani isimamishe msaada wake wa kijeshi kwa Israel.

Msimamo huo umemkosesha uungwaji mkono wa baadhi ya makundi yanayoiunga mkono Israel. Baadhi ya makundi hayo yenye ushawishi mkubwa yametumia fedha nyingi kupinga azma yake ya kuingia Seneti.

Rais Donald Trump pia alimshambulia mara kadhaa wakati wa kampeni yake ya kuwania kiti hicho. Trump alimwita "mwenye misimamo mikali ya kijihadi" na kuhoji iwapo anafaa kuwa seneta kutokana na imani yake ya Kiislamu.

El-Sayed alijibu kuwa kulikuwa na juhudi za kuifanya dini yake kuwa suala la kisiasa badala ya kujadili sera zake kuhusu uchumi na ustawi wa jamii.

Licha ya mijadala hiyo, El-Sayed ameendelea kuwa mmoja wa wanasiasa wanaovuta hisia za wengi nchini Marekani. Kwa sasa ameshinda kiti cha useneti Marekani kupitia chama cha Democrats.

Safari yake ya kisiasa imeibua maswali kuhusu chuki dhidi ya Waislamu, mzozo wa Israel na Palestina, sera za uhamiaji na nafasi ya Waislamu katika nyadhifa za juu serikalini.

Hivyo, safari yake inaendelea kufuatiliwa na waandishi wa habari na wachambuzi wa siasa.

Sababu wanasiasa waislamu wanakubalika Marekani

Kwa nini wanasiasa Waislamu wanazidi kupata nafasi na kukubalika nchini Marekani?

Profesa Tukur Abdulkadir wa Chuo Kikuu cha Kaduna State nchini Nigeria anasema kuna sababu kadhaa zilizochangia mabadiliko hayo.

Anasema tangu mashambulizi ya Septemba 11, baadhi ya vyombo vya habari vimetumiwa kuichafua dini ya Kiislamu na Waislamu.

Hata hivyo, anaamini kuwa hali hiyo imeanza kubadilika kutokana na namna watu wanavyopata taarifa siku hizi.

"Katika karne ya 21, watu hawategemei tena televisheni na magazeti pekee kupata habari. Hapo awali, baadhi ya vyombo hivyo vilitumiwa kueneza propaganda, kuchafua watu na kudhoofisha maadili ya jamii," amesema.

Anaongeza kuwa mitandao ya kijamii imewapa watu nafasi ya kupata taarifa moja kwa moja, badala ya kutegemea yale yanayochaguliwa na wahariri wa vyombo vya habari.

Sababu nyingine anayoitaja ni mabadiliko ya mitazamo ya jamii kadiri muda unavyopita.

Anasema Uislamu unazidi kupata umaarufu miongoni mwa Wamarekani na kwamba hali hiyo inahitaji kueleweka katika muktadha wa mabadiliko ya jamii.

Mtaalamu huyo wa siasa za kimataifa pia anasema vita vya Israel vimechangia baadhi ya watu kuanza kuikosoa Marekani, Rais Donald Trump na sera zake katika masuala ya kimataifa.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid