Mipango ya Israel ya kufungua zabuni za ujenzi wa takriban nyumba 1,200 za walowezi katika eneo lenye umuhimu wa kimkakati katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu imelaaniwa vikali na mataifa kadhaa ya Magharibi.
Katika taarifa ya pamoja, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, na Canada zilitaja uamuzi huo kuwa ''usiokubalika" na kuionya Israel kubatilisha mipango hiyo mara moja.
Makazi yote ya Walowezi ni haramu chini ya sheria za kimataifa na kutokana na shinikizo la kimataifa,
Israel ilisitisha kwa miongo kadhaa mipango ya kujenga makazi ya Walowezi katika eneo lijulikanalo E1 upande wa mashariki mwa Jerusalem.
Washirika wake wengi na Wapalestina walidai kuwa ujenzi huo ungedidimiza kwa kiasi kikubwa matumaini ya kufikiwa suluhisho la mataifa mawili, na kimsingi kuugawanya Ukingo wa Magharibi vipande viwili na kuitenga Jerusalem Mashariki.
Taarifa hiyo kutoka kwa washirika wa Israel wa Ulaya na Canada iliyochapishwa jana Alhamisi imesema "Wakati huu wa kukosekana kwa utulivu mkubwa katika Ukingo wa Magharibi kukiwa na viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa vya vurugu zinazofanywa na walowezi dhidi ya raia, na vizuizi vikubwa kwa uchumi wa Palestina, uamuzi huo wa kutaka kujenga makazi ya walowezi unatia wasiwasi mkubwa zaidi.
Katika taarifa tofauti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia alisema mpango huo unaleta "tishio la uwepo" kwa taifa linaloungana la Palestina. Msemaji wake Stephane Dujarric, amesema Katibu mkuu anatiwa wasiwasi mkubwa na hatua ya Israel.
"Katibu Mkuu amesikitishwa sana na ripoti za kuwepo makazi mapya haramu ya walowezi wa Israeli katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na zabuni mpya, zikiwemo za eneo la E1. Anatiwa wasiwasi mno na mipango hiyo ya kujengwa makazi eneo la E1, ambayo yatakata kabisa uhusiano kati ya kaskazini na kusini mwa Ukingo wa Magharibi.
Hali hiyo itakuwa na madhara makubwa kwa uhuru wa kujitawala katika maeneo ya Palestina na kutishia uwezekano wa kuwepo suluhisho la mataifa mawili''.
Mapema hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband pia alilaani vikali mpango huo wa Israel,mtizamo ambao ulimkera Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel.
Wizara ya nyumba ya Israel siku ya Jumatano wiki hii, ilitoa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 1,234 kati ya nyumba 3,401 zilizoidhinishwa na serikali ya Israel mnamo Agosti iliyopita. Inachukua takriban kilomita za mraba 12 kati ya Jerusalem Mashariki na makazi ya Maale Adumim.
Wakati wa kuzinduliwa kwake, Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich,mwanasiasa mwenye misimamo mikali na mlowezi,alisema wazo la kuwepo taifa la Palestina linafutwa.
Mwisho wa kupokea zabuni ni tarehe 19 Oktoba, siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Israel unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba,hatua inayoonekana kufanya iwe vigumu zaidi kwa serikali yoyote ya baadaye kubatilisha zabuni zilizotolewa.
Israel imejenga takriban makazi 160 yanayohifadhi Wayahudi laki saba tangu ilipokalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ardhi ambayo Wapalestina wanaitaka, pamoja na Gaza, kwa ajili ya taifa la baadaye linalotarajiwa.
Inakadiriwa kuwa Wapalestina milioni 3.3 wamelazimika kuishi sambamba na Wayahudi hao. Licha ya upinzani mkali wa kimataifa, serikali ya Israel imeruhusu makazi hayo kukua.