Fainali ya AFCON kuamuliwa mahakamani – ni lini Morocco au Senegal watatawazwa kuwa mabingwa?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kila mtu anajua kuwa mechi ya soka inapaswa kudumu kwa dakika 90, lakini kwa namna yake, fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ya mwaka 2025 imekuwa ikiendelea kwa karibu miezi tisa sasa.

Sasa, hatimaye, timu moja kati ya hizo mbili - iwe Morocco au Senegal - itapata ushindi. Hata hivyo, wakati huo wa utukufu utatokea mahakamani,na sio uwanjani.

Siku ya Alhamisi, mamlaka ya juu kabisa ya kisheria katika michezo - Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) - itasikiliza rufaa ya Senegal dhidi ya uamuzi wa kuivua taji ambalo walidhani walikuwa wamelishinda mwezi Januari dhidi ya wenyeji jijini Rabat.

Lakini wale wanaosubiri kwa hamu kupata suluhu wameonywa kuwa haitapatikana siku hiyo hiyo.

Je, tulifikaje hapa? Na nini kitafuata?

Ni nini kilichotokea katika fainali ya Afcon?

Mbele ya mashabiki 66,000 wa nyumbani walioleta msisimko mkubwa ndani ya Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat, Morocco ilionekana kuwa tayari kuandika historia huku ikisaka taji lake la kwanza la Afcon tangu mwaka 1976.

Badala yake, fainali hiyo iligeuka kuwa vurugu kubwa katika dakika za nyongeza.

Wakati mechi ikiwa bado haina bao, Senegal ilidhani Ismaila Sarr amefunga bao la ushindi la kusisimua, lakini wakagundua kuwa mwamuzi Jean Jacques Ndala alikuwa tayari amepuliza filimbi kuashiria mpira wa adhabu (free-kick) kwa Morocco.

Utata uliongezeka katika dakika ya 98 wakati, baada ya mapitio ya VAR, Ndala alipoipa Morocco penalti.

Hali ya hasira ilipanda sana kando ya uwanja na kwenye majukwaa. Kocha wa Senegal, Pape Thiaw, aliwaongoza baadhi ya wachezaji na wafanyakazi wake kuondoka uwanjani kupitia njia ya kuingilia wachezaji, huku mashabiki wakizozana na maafisa wa usalama wakati utulivu ulipopotea kwa muda.

Mchezo ulianza tena hatimaye na, katika dakika ya 124, Morocco ilipoteza nafasi nzuri sana ya kumaliza kusubiri kwa miaka 50 kupata utukufu wa bara hilo wakati Brahim Diaz wa Real Madrid aliposhindwa kufunga penalti, akipiga mpira taratibu kwa mtindo wa 'Panenka' moja kwa moja mikononi mwa kipa Edouard Mendy.

Kisha, bao la Pape Gueye katika muda wa nyongeza liliihakikishia Senegal ushindi wa 1-0, na kuifanya itwae kombe hilo kwa mara ya pili.

Kwa nini matokeo ya fainali ya AFCON yalibatilishwa?

Haishangazi kwamba Shirikisho la Soka la Morocco (FMRF) liliwasilisha malalamiko haraka kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), likidai kuwa Senegal ilikiuka kanuni za mashindano.

Kifungu cha 82, kilicho chini ya sura yenye kichwa "Kujiondoa", kinasema: "Ikiwa, kwa sababu yoyote ile, timu... itaondoka uwanjani kabla ya muda rasmi wa kumalizika kwa mechi bila idhini ya mwamuzi," itachukuliwa kuwa "imepoteza mechi na itaondolewa kwenye mashindano hayo".

Mnamo mwezi Machi, bodi ya rufaa ya CAF ilikubaliana na hoja hiyo, ikiamua kuwa Senegal ilipoteza mechi hiyo na kuipa Morocco ushindi wa mabao 3-0.

Ingawa kuna mifano ya awali ya CAF kubadili matokeo wakati wa mashindano ya AFCON na hatua za kufuzu Kombe la Dunia, wengine akiwemo afisa mmoja wa zamani wa ngazi ya juu wa CAF walidai kuwa mwamuzi pekee ndiye mwenye mamlaka ya kusimamisha mechi iwapo timu itaondoka uwanjani.

FMRF ilisema ilikuwa ikitaka kanuni za mashindano zifuatwe ipasavyo, lakini shirikisho la soka la Senegal (FSF) lilielezea uamuzi huo kuwa "usio wa haki, usio na mfano wa awali na usiokubalika" na kukata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ni nini?

CAS ilianzishwa mwaka 1984 na ina makao yake makuu katika jiji la Lausanne nchini Uswisi; ilianzishwa kama chombo huru cha kisheria chenye lengo la kutatua migogoro wakati michezo duniani ilipoanza kuingiza mapato makubwa zaidi na, matokeo yake, kusababisha kesi nyingi zaidi za kisheria.

Kwa mashirikisho ya michezo yanayotambua mamlaka ya CAS, mahakama hiyo inachukuliwa kuwa chombo cha juu kabisa cha usuluhishi; hii ina maana kuwa uamuzi wake ni wa mwisho, isipokuwa katika hali nadra ambapo mahakama ya juu zaidi nchini Uswisi inaweza kuamua kuubatilisha uamuzi huo kwa kuzingatia sababu chache maalum za kisheria au kiufundi.

Zaidi ya kesi 900 huwasilishwa kila mwaka, zikihusisha zaidi ya aina 50 tofauti za michezo na kushughulikia masuala kama vile mikataba ya ajira na uhamisho wa wachezaji, matumizi ya dawa za kuongeza nguvu (doping), rushwa, haki za matangazo ya televisheni na, katika kesi hii, uandaaji wa matukio ya michezo.

Rufaa hiyo itasikilizwa na jopo la wasuluhishi watatu waliochaguliwa na CAS kutokana na utaalamu wao katika sheria za michezo.

Katika tukio hili, jopo hilo litaongozwa na Mfaransa mwenye umri wa miaka 76, Gerald Simon, ambaye ni mwanzilishi wa Maabara ya Sheria za Michezo katika Chuo Kikuu cha Burgundy na amekuwa mwanachama wa CAS kwa miaka 23.

Iwapo jopo hilo litashindwa kufikia makubaliano ya pamoja, mwenyekiti wake atatoa uamuzi wa mwisho.

Tutapata lini uamuzi?

Ingawa usikilizaji wa kesi hiyo—utakaofanyika faraghani kwa ombi la pande husika—unatarajiwa kumalizika Alhamisi alasiri, CAS tayari imetahadharisha kuwa huu ni mwanzo tu wa majadiliano ya jopo husika.

Katika taarifa yake, mahakama hiyo ilisema "haiwezi kusema ni lini uamuzi wa mwisho utatolewa, lakini hautatolewa siku hiyo ya usikilizaji."

Baada ya kusubiri kwa karibu miezi tisa kufikia hatua hii, habari mbaya ni kwamba kanuni za CAS zinaelekeza kuwa maamuzi ya rufaa yanapaswa kutolewa ndani ya kipindi cha juu cha miezi minne baada ya usikilizaji, ingawa miongozo pia inataka majopo kulenga kukamilisha mchakato huo ndani ya muda usiozidi miezi mitatu.

Habari njema ni kwamba mchakato huo unaweza kukamilika kwa haraka zaidi.

Mwaka 2020, klabu ya Manchester City ilikata rufaa CAS kupinga uamuzi wa UEFA wa kuifungia kushiriki mashindano ya klabu za Ulaya kutokana na kukiuka kanuni za usawa wa kifedha (Financial Fair Play).

Usikilizaji wa kesi hiyo ulifanyika tarehe 8 Juni, na uamuzi uliotoka tarehe 13 Julai ulipendelea upande wa Manchester City.

Je, ni nini kinaweza kuwa matokeo ya muda mrefu?

Ingawa bodi ya rufaa ya CAF inafanya kazi kwa uhuru, kubatilishwa kwa uamuzi wake kungelitia doa zaidi sifa ya shirikisho hilo linalosimamia soka barani Afrika, ambalo tayari limekabiliwa na ukosoaji mkali kutokana na uamuzi wake wa awali wa kuikabidhi Morocco taji hilo.

Rais wa CAF, Patrice Motsepe, alisema mwezi Machi kuwa watazingatia na kuheshimu uamuzi wowote utakaotolewa na CAS; hivyo, iwapo uamuzi utaipendelea Senegal, huenda ikabidi kanuni za mashindano ya AFCON zifanyiwe marekebisho.

Hata hivyo, kitendo cha timu ya Teranga Lions kutoka uwanjani kimeshasababisha mabadiliko katika kanuni za soka.

"Mwamuzi anaweza kutoa kadi nyekundu kwa mchezaji yeyote anayeondoka uwanjani kuonyesha kupinga uamuzi wa mwamuzi," ilisema IFAB, chombo kinachotunga sheria za mchezo huo, mwezi Aprili.

"Kanuni hii mpya itawahusu pia maafisa wa timu wanaowachochea wachezaji kuondoka uwanjani. Timu itakayosababisha mechi kusimamishwa na kutokamilika, kimsingi, itapoteza mechi hiyo." Thiaw tayari amefutwa kazi na Senegal baada ya timu hiyo kutolewa katika hatua ya timu 32 bora ya Kombe la Dunia, huku Walid Regragui, aliyekuwa kocha wa Morocco mwezi Januari, akitimuliwa mwezi Machi.

Bila shaka, wote wawili wataendelea kuona mafanikio katika kesi ya CAS kama ushindi wa kimaadili.

Vyovyote vile matokeo yatakavyokuwa, kuna uwezekano mkubwa wa uhasama kuendelea kuwepo kati ya mashirikisho hayo mawili.

Viongozi wa ngazi ya juu wa FMRF walikasirishwa sana na tabia ya Senegal, wakiamini kuwa picha zilizosambazwa duniani kote ziliharibu vibaya sifa ya michuano ya kwanza ya AFCON kuandaliwa na ufalme huo tangu mwaka 1988—michuano ambayo ilikuwa imetumia muda na fedha nyingi sana.

Wakati huo huo, FSF na serikali ya Senegal zimeunga mkono hisia zilizoenea kote barani Afrika kwamba Morocco ina ushawishi mkubwa kupita kiasi katika soka la Afrika.

Matukio mengine pia yaliwakera, kama vile kuelekezwa kwa mwanga wa leza kwenye macho ya wachezaji na kitendo cha wavulana wanaookota mipira kuhamisha taulo ya kipa Mendy; jambo ambalo hatimaye lilisababisha tukio la kushangaza ambapo kipa wa akiba Yehvann Diouf alishambuliwa na kuangushwa chini na wavulana watatu wa kuokota mipira alipojaribu kuingilia kati.

Huku michuano ijayo ya AFCON ikipangwa kufanyika mwezi Juni na Julai mwakani, wazo la kuwepo kwa mechi nyingine ya hadhi ya juu kati ya timu mbili bora barani Afrika linavutia sana.

Lakini ingawa vurugu za fainali ya mwaka huu zinaweza kuwa zimeanzisha uhasama mpya unaowapa mashabiki kitu cha kujadili na kufurahia, kuna makubaliano ya pamoja kwamba mechi kama hizo zinapaswa kuamuliwa uwanjani na si mahakamani.