Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi Marekani na Lebanon walivyomkinga jenerali wa Syria anayesakwa- uchunguzi wa BBC
- Author, Sara Obeidat
- Author, Josh Baker
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Uchunguzi wa BBC News umebaini kuwa jenerali wa zamani wa Syria anayesakwa kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu analindwa na kufadhiliwa na mamlaka za Marekani na Lebanon.
Bassam al-Hassan, ambaye aliwahi kusimamia mpango wa silaha za kemikali wa Syria na kuwa mshauri mkuu wa rais wa zamani Bashar al-Assad, anaishi nchini Lebanon tangu kuanguka kwa utawala wa Assad mwaka 2024.
Uchunguzi wa pamoja wa BBC na shirika la utangazaji la Marekani NPR umebaini kuwa Hassan ameruhusiwa kubaki nchini humo chini ya mpango unaohusisha FBI pamoja na mamlaka nyingine za Marekani na Lebanon. Vyanzo vimeeleza kuwa mpango huo unatokana na utayari wake wa kutoa taarifa kuhusu kutekwa nyara kwa mwandishi wa habari wa Marekani, Austin Tice, nchini Syria mwaka 2012, pamoja na intelijensia nyingine.
Mwezi uliopita, BBC ilifichua kuwa kutekwa nyara kwa Tice kulikuwa operesheni iliyopangwa, huku Hassan akitajwa kuwa sehemu ya mnyororo wa amri uliosimamia tukio hilo.
Maafisa kutoka idara mbili tofauti za serikali mpya ya Syria wameiambia BBC kuwa wanataka Hassan arejeshwe nchini humo ili akabiliwe na mashtaka. Hata hivyo, uchunguzi huo umebaini kuwa mamlaka za Marekani zinataka aendelee kubaki Lebanon, huku serikali ya Damascus ikiwa na uwezo mdogo wa kubadilisha hali hiyo.
BBC iliomba maoni kutoka kwa FBI, CIA na Kurugenzi Kuu ya Usalama wa Taifa ya Lebanon kuhusu matokeo ya uchunguzi huo. FBI pekee ndiyo iliyojibu, ikikataa kutoa maoni na badala yake kurejelea taarifa yake ya awali iliyosema kwamba lengo lake kuu linasalia kubaini ukweli kuhusu Austin Tice na kuhakikisha anapatikana na kuwajibishwa.
Akijibu matokeo ya uchunguzi huo, msemaji wa familia ya Tice, Phil Elwood, alisema: "Ikiwa madai haya ni ya kweli, basi ni jambo la kusikitisha kwamba fedha za walipa kodi zinatumika kumpatia maisha ya starehe mtu anayehusishwa na matumizi ya silaha za kemikali dhidi ya raia wa Syria na ambaye anadaiwa kuhusika katika kisa cha Austin Tice."
Aliongeza: "Huku ni kusaidia mtu anayesakwa kwa uhalifu wa kivita kuepuka mkono wa sheria. Raia wa Syria wanastahili haki, na anapaswa kurejeshwa ili akabiliwe na mashtaka."
Kama sehemu ya uchunguzi wa muda mrefu ulioangaziwa katika podcast mpya ya BBC, Where is Austin Tice? Series 3 of I'm Not A Monster Presents, BBC imepitia rekodi ya kina ya mkutano uliowahusisha Bassam al-Hassan, wawakilishi wa FBI na CIA, pamoja na maafisa wa usalama wa Lebanon, ambapo suala la Austin Tice lilijadiliwa.
Katika mkutano huo, Hassan aliahidiwa "haki ya kuishi", "ulinzi" na msaada wa kukidhi mahitaji yake ya msingi kwa kubadilishana na taarifa, hasa kuhusu kutoweka kwa Tice.
Vyanzo vinavyoufahamu mpango huo vimeiambia BBC kuwa Hassan hupokea fedha kupitia watu wanaofanya kazi kwa niaba ya mamlaka za Marekani, jambo linalofanya iwe vigumu kufuatilia malipo hayo. Hassan pia amewekewa vikwazo na Marekani.
Hata hivyo, watu wanaoshiriki katika uchunguzi wa Tice wanasema hawajaona hatua kubwa iliyopigwa tangu Hassan aanze kushirikiana chini ya makubaliano hayo, ambayo yanaaminika kufikiwa katika majira ya kuchipua ya mwaka 2025.
Baadhi ya vyanzo vimeeleza wasiwasi kuwa mpango huo unaweza kuendelea kwa muda usiojulikana, ukigharimu fedha nyingi bila kuleta matokeo makubwa.
Hassan si afisa pekee wa zamani wa utawala wa Syria anayenufaika kutokana na uhusiano wake na uchunguzi wa Tice. Afisa mmoja wa zamani aliiambia BBC kwamba alipokea malipo kutoka FBI kwa ushirikiano wake, huku akidai kuwa hakutoa taarifa zote mara moja ili kuendelea kupokea fedha hizo.
Mtu mwingine wa zamani wa utawala wa Assad, ambaye pia alihusishwa na suala la Tice, alisema anaishi Lebanon chini ya kile alichokiita "ufadhili" wa mamlaka za Marekani na kwamba hali hiyo inamzuia kuzungumzia kesi hiyo.
BBC pia ilizungumza na afisa mkuu wa zamani wa ujasusi wa Lebanon, ambaye alithibitisha kuwepo kwa ushirikiano kati ya mamlaka za Lebanon na Marekani katika baadhi ya uchunguzi, ingawa alisema hana taarifa kuhusu malipo yanayohusiana moja kwa moja na kesi ya Austin Tice.
Kufuatia kuanguka kwa utawala wa Assad mwanzoni mwa Desemba 2024, inaaminika kwamba Hassan alikimbilia Iran.
Hata hivyo, mfanyabiashara mmoja wa Syria mwenye uhusiano wa karibu na utawala wa zamani wa Assad na mamlaka za Lebanon aliiambia BBC kwamba baadaye kulifanyika mazungumzo yaliyohusisha Marekani, Lebanon na Iran ili kumhamishia Hassan nchini Lebanon.
Mfanyabiashara huyo, ambaye aliomba kutotambulishwa, alisema Hassan alionekana kuwa mtu wa thamani kubwa kwa pande husika. Mbali na madai kwamba huenda ana taarifa kuhusu kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Marekani Austin Tice, pia anadaiwa kuwa na ufahamu wa kina kuhusu mpango wa Syria wa silaha za kemikali na ushirikiano wa kijeshi kati ya Syria na Iran.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, taarifa hizo ni miongoni mwa sababu zilizofanya idara za ujasusi za Marekani kuvutiwa na Hassan na kutaka kupata maelezo zaidi kutoka kwake.
Hassan aliwaambia wachunguzi wa Marekani mwaka jana kwamba mwandishi wa habari wa Marekani Austin Tice aliuawa kwa amri ya rais wa zamani wa Syria, Bashar al-Assad. Hata hivyo, watu kadhaa wenye ufahamu wa uchunguzi huo wameeleza shaka kuhusu baadhi ya madai yake.
Hassan pia alitoa taarifa kuhusu eneo alilodai huenda lilikuwa na mabaki ya mwili wa Tice. Lakini eneo hilo lilipofanyiwa upekuzi, hakuna kilichopatikana, kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vilivyohusika katika operesheni hiyo. Matokeo hayo yameibua maswali kuhusu usahihi wa baadhi ya taarifa alizotoa.
Pamoja na hayo, bado kuna utata kuhusu upekuzi huo. Vyanzo viwili vilivyozungumza na BBC vimesema mamlaka za Marekani zilisitisha uchimbaji kabla ya operesheni kukamilika, huenda kutokana na sababu za kiusalama.
BBC ilipowasiliana na Hassan kwa simu mwaka jana kuomba mahojiano, alielekeza ombi hilo kwa FBI na CIA kupitia ubalozi wa Marekani mjini Beirut.
Uchunguzi wa BBC pia umebaini kwamba baadhi ya maafisa wa zamani wa Syria wanaohusishwa na kesi ya Tice wanaaminika kuishi nje ya nchi.
Miongoni mwao ni Mohammad Makhlouf, ambaye aliwahi kufanya kazi chini ya Hassan na amehusishwa na kuzuiliwa kwa Tice. Kwa sasa, inaaminika anaishi nchini Lebanon.
Mwingine ni Sakr Rustom, mpwa wa Hassan anayehusishwa na kutekwa nyara kwa Tice. Inaaminika kuwa husafiri kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Lebanon. BBC ilipomuuliza kuhusu kesi hiyo, alisema kuwa "anapendelea kuangazia mambo ya wakati ujao".
Pia yupo Ghassan Nassour, jenerali wa zamani wa Kikosi cha Walinzi wa Jamhuri ya Syria. Wanachama wa zamani wa Vikosi vya Ulinzi wa Taifa wanamtaja kuwa msimamizi wa gereza ambako Tice alizuiliwa. Kwa mujibu wa taarifa ambazo BBC imezipata, Nassour kwa sasa anaishi UAE pamoja na familia yake.