Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, simu yangu inanisikiliza?
Ni vigumu kufikiria maisha ya kila siku bila simu za mkononi. Utafiti mmoja umeonyesha kuwa vijana, hususan, hutumia wastani wa saa nne na dakika 37 kwa siku kwenye simu zao janja.
Hata hivyo, kadiri utegemezi wetu wa vifaa hivi unavyozidi kuongezeka, ndivyo maswali kuhusu faragha yanavyoendelea kuibuka. Miongoni mwa hoja zinazozua mjadala mkubwa ni madai kwamba simu za mkononi husikiliza mazungumzo ya watumiaji.
Baadhi ya watu wanasema wamewahi kuzungumzia bidhaa au huduma fulani, na muda mfupi baadaye kuanza kuona matangazo yanayohusiana nayo kwenye simu zao. Jambo hilo limewafanya baadhi ya watu kuamini kuwa simu zao huenda zinawasikiliza bila wao.
Lakini je, madai hayo yana ukweli wowote? Au ni matokeo ya teknolojia za kisasa zinazokusanya na kuchambua taarifa zetu za mtandaoni kwa usahihi mkubwa kiasi cha kuonekana kana kwamba simu zetu zinajua tunachozungumzia?
Kwa nini watu wanafikiri simu zinawasikiliza?
Machapisho mengi kwenye mitandao ya kijamii yanadai kuwa simu za mkononi zinaweza kukusikia au hata kusoma mawazo yako. Kwa mfano, umewahi kuzungumza na mtu kuhusu jambo fulani, halafu ghafla ukaanza kuona matangazo kuhusu jambo hilo kwenye mitandao yako ya kijamii?
Watumiaji wa mitandao ya kijamii wameeleza wasiwasi wao na kusambaza nadharia mbalimbali za njama kuhusu jinsi kampuni zinavyoweza kuwafuatilia kupitia programu wanazotumia, jambo ambalo baadhi ya watu wanaamini.
Ukianza kuona matangazo kuhusu mada ambayo wewe na marafiki zako mmekuwa mkizungumzia, huenda ikawa ni bahati tu, lakini hali hiyo inaweza kukufanya ujiulize kwa nini jambo hilo linatokea.
Kulingana na kiwango ambacho unashirikiana na maudhui yanayohusiana na mada fulani, unaweza kuanza kuonyeshwa maudhui zaidi ya aina hiyo. Hii ni kwa sababu kanuni za mitandao ya kijamii hufuatilia tabia zetu mtandaoni na kuamua maudhui ya kutuonyesha kulingana na machapisho tunayoyatazama, kuyapenda au kuyashiriki.
Ni madai gani yanayozungumzwa mtandaoni kuhusu simu?
Baadhi ya watayarishaji wa maudhui wanadai kuwa programu zinakusanya taarifa za watumiaji na kwamba jambo hilo linaweza kuzuiwa kwa kubadilisha mipangilio ya simu, lakini hilo bado halijathibitishwa.
Baadhi ya watu pia wameibua nadharia za njama kwamba kampuni au hata serikali zinawapeleleza, ingawa haijulikani wazi kwa nini jambo hilo linafanyika.
Je, simu yangu kweli inanisikiliza?
Ndiyo na hapana, lakini si kwa namna unavyoweza kufikiria.
Simu nyingi husikiliza sauti kwa hali ya kusubiri ili kuwezesha wasaidizi wa sauti kama Siri, Alexa na Google Assistant. Vifaa hivi husubiri kusikia maneno kama "Hey Siri" ili viweze kutafuta mtandaoni kuhusu jambo unalouliza.
Simu pia husikiliza sauti ya mtumiaji ili wasaidizi wa sauti waweze kutoa mapendekezo yanayokufaa, kama vile mapendekezo ya programu.
Hata hivyo, hakuna ushahidi kwamba mazungumzo yetu ya kila siku yanarekodiwa. Instagram imewahi kukanusha madai kwamba mtandao huo wa kijamii unasikiliza mazungumzo ya watumiaji wanapokuwa kwenye programu hiyo.
Instagram ilisema kuna sababu mbalimbali zinazoweza kufanya jambo ambalo umelizungumzia lianze kujitokeza kwenye ukurasa wako. Huenda ikawa ni bahati tu, au huenda uliwahi kuingiliana na maudhui yanayohusiana na mada hiyo, au hata kuitafuta mada hiyo hapo awali.
Instagram ilisema inashirikiana na baadhi ya watangazaji ambao huipa taarifa kuhusu watu wanaotembelea tovuti zao. Taarifa hizo huwezesha programu kuwaonyesha watumiaji maudhui yanayohusiana na mambo wanayopenda na shughuli zao.
Nifanye nini ikiwa ninafikiri simu yangu inanisikiliza?
BBC iliwasiliana na Wizara ya Sayansi, Ubunifu na Teknolojia ya Uingereza ili kufahamu iwapo kuna taarifa rasmi kuhusu simu za mkononi "kusikiliza" mazungumzo ya watumiaji.
Msemaji wa wizara hiyo alisema: "Programu na mitandao ya kijamii hupata tu fursa ya kufikia sehemu za simu yako ambazo umewapa ruhusa kuzitumia, kama vile kamera kwa ajili ya kupiga picha au eneo ulipo kwa ajili ya ramani. Kwanza ni lazima zikuombe ruhusa na kueleza kwa nini zinahitaji fursa hiyo. Unaweza kukataa au kubadilisha ruhusa hizo kwenye mipangilio ya simu yako."
Pia inapendekezwa ufanye yafuatayo ikiwa una wasiwasi kuhusu taarifa zako binafsi:
- Tumia nywila imara na usimpe mtu mwingine.
- Tumia uthibitishaji wa hatua mbili au passkeys kulinda akaunti muhimu kama vile barua pepe.
- Kagua ruhusa za programu kabla ya kuzipakua.
- Shiriki taarifa zako binafsi kwenye tovuti unazoziamini pekee.
- Fikiria kwa makini kabla ya kuchapisha taarifa binafsi mtandaoni.
- Tumia mipangilio ya faragha kwenye mitandao ya kijamii.
Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa na Ambia Hirsi