Mvutano kati ya Trump na Iran Unamnufaisha nani?

s
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 9

Hatuhitaji makubaliano na Iran," Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social Alhamisi, Novemba 12. "Siku za makubaliano zimepitwa na wakati.

Fedha zao, mamia ya mabilioni ya dola, ziko mikononi mwetu, na njia zao za baharini (Straits) ziko mikononi mwetu."

Kauli hizi zilitolewa siku mbili baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kueleza kuhusu kile alichokiita "mpango wa tatu" wa Donald Trump kwa Iran: kuendeleza udhibiti wa majini na shinikizo la kiuchumi, bila kurudi kwenye vita kamili na pia bila kusaini makubaliano ambayo Washington inaona hayafai.

Iwapo Marekani haioni umuhimu wa kufikia makubaliano na Iran nayo Iran inaendelea kupinga masharti ya Washington, hali hii inaweza kudumu kwa muda gani? Je, hali ya "bila vita, hakuna makubaliano" inaweza kuwa ya kudumu?

Howard Schatz, mchumi mwandamizi wa Shirika la RAND, aliiambia BBC Persian kuwa mkwamo huo unaweza kuendelea kwa muda mrefu katika mazingira fulani.

Kwa upande mwingine, Bilal Saab, mtaalamu wa masuala ya usalama wa Mashariki ya Kati kutoka taasisi ya Chatham House ya Uingereza, anaamini kuwa gharama za kiuchumi na kisiasa za kuendelea kwa hali hiyo hatimaye zitalazimisha pande zote mbili kufikia hatua muhimu ya maamuzi.

Mpango wa tatu wa Trump dhidi ya Iran ni upi?

s
Maelezo ya picha, Marco Rubio alisema katika mkutano wa G7 kuwa Marekani inaweza kufanikisha malengo yake dhidi ya Iran kupitia shinikizo la kiuchumi badala ya nguvu za kijeshi, akisisitiza kuwa hali ya sasa si mkwamo bali ni mkakati unaoendelea.

Axios iliripoti Novemba 10, ikinukuu washiriki wa mkutano wa faragha wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G7 uliofanyika Paris, kwamba Waziri wa mambo ya nje wa Marekani alisema Donald Trump ameamua kuendeleza sera ya sasa badala ya kurejea vitani au kukubali makubaliano yanayoonekana kuwa "yasiyofaa" kwa Marekani.

Anadai Washington haijaweka muda maalumu wa kusitisha sera hiyo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bw. Rubio aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran linaongezeka kila siku. Aliongeza:

"Iwapo tutafikia lengo lile lile kwa kutumia mbinu za kiuchumi na shinikizo la kiuchumi, hatuhitaji mashambulizi ya kijeshi. Huu si mkwamo."

Sera ya sasa ya Marekani, mbali na vikwazo vya kifedha na kibiashara, pia inajumuisha udhibiti wa kijeshi dhidi ya bandari za Iran.

Jeshi la wanamaji la Marekani limekuwa likizuia meli ili kutekeleza udhibiti huo, na wakati mwingine limetumia nguvu za kijeshi kushambulia maeneo ya kusini mwa Iran.

Hivi karibuni, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilitangaza kuundwa kwa kikosi kazi kinachoitwa "Iron Gate" (Lango la Chuma).

Kundi hilo, lenye takriban wanachama 20 wa kijeshi na kiraia, limeundwa kuratibu juhudi za taasisi mbalimbali za Marekani katika kuzuia usafirishaji wa silaha, teknolojia zinazoweza kutumika kwa matumizi ya kiraia na kijeshi, pamoja na bidhaa zilizowekewa vikwazo kupitia mipaka ya nchi kavu ya Iran na Bahari ya Caspian.

Je, Iran inataka kumaliza mkwamo huo?

Katika mahojiano na Al Jazeera, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, alisema Jamhuri ya Kiislamu imedhamiria kutoka katika hali ya "hakuna vita, hakuna amani", na kwamba kuimarisha uwezo wa kujilinda na kuzuia mashambulizi, ikiwemo nguvu za kijeshi, ni mojawapo ya njia za kufikia lengo hilo. Pia alisema Iran imewasilisha masharti yake kwa Washington kupitia Qatar na kwamba sasa "mpira uko upande wa Marekani."

Wakati huo huo, Mohsen Rezaei, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, alionya katika mahojiano na mtandao wa Al-Mayadeen kwamba iwapo Marekani itafanya mashambulizi mengine, Iran haitajibu kwa kulenga kambi za Marekani katika Mashariki ya Kati pekee, bali pia itashambulia vituo vya Marekani barani Ulaya au maeneo mengine duniani vitakavyotumika kushambulia Iran.

Udhaifu wa hali ya sasa ulionekana zaidi Ijumaa, Novemba 13, wakati Jeshi la Iran (IRGC) lilipotangaza kuwa lililenga rada ya Marekani nchini Bahrain kujibu shambulio lililotokea Sirik, mkoani Hormozgan.

CENTCOM ilithibitisha shambulio hilo la ndege zisizo na rubani (drones), lakini ikasema ndege zote mbili zilitunguliwa na hakuna uharibifu uliotokea.

"Hakuna anayejua kiwango cha mwisho ambacho Iran inaweza kuvumilia," alisema mtaalamu wa usalama wa Mashariki ya Kati, Bilal Saab, katika mahojiano na BBC Persian. "Tunachojua ni kwamba Iran haitakubali kushinikizwa au kujisalimisha kimya kimya."

Katika uchambuzi aliouchapisha kwenye tovuti ya taasisi ya Chatham House Novemba 9, Saab alieleza kuwa shinikizo la kiuchumi linaweza kuwafanya viongozi wa Iran kuongeza kiwango cha mzozo, badala ya kuilazimisha Tehran kukubali masharti makubwa kutoka kwa Marekani.

Saab alikumbusha matukio ya mwaka 2019 wakati sera ya shinikizo la juu ya utawala wa kwanza wa Donald Trump ilipokuwa imefikia kilele chake.

Katika kipindi hicho, meli kadhaa za mafuta zilishambuliwa katika eneo la Ghuba, Iran iliidungua ndege ya upelelezi ya Marekani, na miundombinu ya mafuta ya Saudi Arabia pia ilishambuliwa.

Mchumi Howard Schatz pia anataja uwezekano wa Iran kuchukua hatua za kijeshi. Anasema ikiwa utawala wa Iran utahisi uwepo wake uko hatarini, unaweza kutumia nguvu za kijeshi kujaribu kuiondoa Marekani katika eneo hilo au kuzishinikiza nchi za kanda kudai kusitishwa kwa mzingiro dhidi ya Iran.

s
Maelezo ya picha, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, alisisitiza kuwa Iran imekusudia kuvunja mkwamo wa sasa unaojulikana kama hali ya "bila vita, hakuna amani."

Je, pande zote mbili zinaweza kubaki katika hali hii?

Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa hali ya sasa ya mvutano kati ya Marekani na Iran inaweza kuendelea kwa muda mrefu.

Mchumi Howard Schatz anasema hilo linawezekana ikiwa gharama za usumbufu wa biashara ya nishati zitapunguzwa, Iran itaendelea kustahimili shinikizo, na athari za mgogoro zitabaki kuvumilika kwa jamii ya Marekani.

Schatz anaeleza kuwa nchi zinazouza mafuta na gesi zikipata njia mbadala za kusafirisha bidhaa zao badala ya kutegemea Mlango wa Hormuz, gharama za kiuchumi zitapungua. Anasema maendeleo ya njia hizo mbadala tayari yanaendelea.

Kwa upande wa Iran, Schatz anaamini serikali inaonekana tayari kubeba gharama kubwa za kiuchumi na itaendelea kutafuta njia za kukwepa vikwazo.

Ripoti ya Washington Post pia ilinukuu tathmini ya CIA kwamba Iran imehifadhi chakula na mafuta ya kutosha kwa miezi kadhaa, jambo linaloweza kuisaidia kustahimili udhibiti wa kiuchumi.

Watafiti wengine wa RAND pamoja na aliyekuwa balozi wa Marekani James Jeffrey wanasema hakuna upande unaoweza kupata faida ya haraka kupitia vita au kulegeza shinikizo.

Kwa maoni yao, kuendelea na mkwamo wa sasa ndiyo chaguo lenye gharama ndogo zaidi kwa pande zote kwa sasa.

Hata hivyo, mtaalamu wa usalama Bilal Saab anaonya kuwa hali hiyo si thabiti kwa muda mrefu. Anaamini gharama za kisiasa na kiuchumi zitaongezeka hadi kufikia hatua ambayo Marekani na Iran zitalazimika kufanya maamuzi makubwa yatakayomaliza mkwamo huo.

Shinikizo la mafuta dhidi ya Iran na mabadiliko katika soko la nishati

s

Iran imeathirika zaidi na udhibiti wa Marekani kuliko wazalishaji wengine wa mafuta katika eneo hilo. Takwimu zinaonyesha kuwa Iran haijauza shehena mpya ya mafuta ghafi tangu Agosti, tofauti na kabla ya vita ambapo ilikuwa ikisafirisha wastani wa mapipa milioni 1.7 kwa siku.

Wakati mauzo ya mafuta ya Iran yakiwa yamepungua kwa kiasi kikubwa na Marekani ikidai kuizuia Iran kuuza mafuta yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 25, nchi nyingine za OPEC+ zimeweza kurejesha karibu uzalishaji wao wa kawaida.

Saudi Arabia imechangia kwa kuongeza uzalishaji na kutumia njia mbadala za usafirishaji.

Hata hivyo, gharama za usafirishaji na bima bado ni kubwa kuliko kabla ya vita, huku mashambulizi dhidi ya meli katika Mlango wa Hormuz yakiendelea. Wachambuzi wanaonya kuwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati au njia mbadala za usafirishaji yanaweza kuvuruga utulivu uliopo katika soko la mafuta.

Kuna gharama gani kwa Marekani kuendelea kuzingira bahari?

Kuendeleza udhibiti wa majini kunahitaji uwepo wa kudumu wa vikosi vya Marekani baharini na kujiandaa kwa uwezekano wa mapambano ya kijeshi, jambo linaloongeza gharama za operesheni.

Nchi za Ghuba nazo zinaendelea kubeba mzigo wa ongezeko la gharama za bima, usumbufu wa biashara na hatari ya kushambuliwa kwa miundombinu yao.

Ndani ya Marekani, vita dhidi ya Iran vimekuwa suala la kisiasa linalozua mjadala mkubwa.

Kura ya maoni ya Reuters/Ipsos inaonyesha kuwa asilimia 71 ya Wamarekani wanataka Bunge lipitishe sheria za kumaliza vita hivyo.

Baada ya Democrats kushinda uchaguzi wa katikati ya muhula na kutarajiwa kudhibiti Bunge, wanaweza kuongeza shinikizo kwa serikali kupitia bajeti na usimamizi, ingawa mamlaka ya rais yanaweka mipaka kwa uwezo wao wa kusitisha operesheni hiyo moja kwa moja.

Mchumi Howard Schatz anaamini kuwa namna umma wa Marekani utakavyobeba gharama za mgogoro huo ni moja ya mambo muhimu yatakayoamua ikiwa hali ya sasa ya mkwamo kati ya Marekani na Iran itaendelea au la.

Iraq na uezoefu wa miaka 12 ya vikwazo vya kiuchumi na makabiliano

Wachambuzi wanaona hali ya sasa ya Iran ikifanana zaidi na ile ya Iraq baada ya Vita vya Ghuba mwaka 1991 kuliko mifano ya Cuba au Urusi.

Baada ya vita hivyo, Iraq iliwekewa vikwazo vya kiuchumi, mizingiro ya baharini na mashambulizi ya mara kwa mara ya kijeshi yaliyodumu kwa zaidi ya muongo mmoja bila kuuangusha utawala wa Saddam Hussein.

Katika kipindi hicho, mataifa ya Magharibi yalidhibiti kwa karibu biashara ya Iraq. Meli za Marekani na washirika wake zilifanya ukaguzi wa maelfu ya meli ili kutekeleza vikwazo, huku maeneo ya marufuku ya ndege yakitekelezwa katika sehemu za Iraq na mashambulizi ya kijeshi yakifanywa mara kwa mara dhidi ya malengo ya kijeshi.

Hata hivyo, mwaka 1995 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mpango wa "Mafuta kwa Chakula" (Oil-for-Food) ulioruhusu Iraq kuuza mafuta chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa na kutumia mapato hayo kununua mahitaji muhimu.

Ripoti pia zilionyesha kuwa Iraq ilifanikiwa kukwepa baadhi ya vikwazo kupitia Jordan, Uturuki, Syria na njia za baharini katika Ghuba ya Uajemi.

Mkwamo huo ulimalizika mwaka 2003 baada ya Marekani kuivamia Iraq na kuuangusha utawala wa Saddam Hussein. Tofauti na Iran ya sasa, vikwazo dhidi ya Iraq vilikuwa vimeidhinishwa rasmi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Je, Israel inaweza kubadili mwelekeo wa mgogoro?

Nchini Israel, mjadala kuhusu uwezekano wa mashambulizi mapya dhidi ya Iran umeongezeka baada ya uchaguzi wa Oktoba.

Jeshi la Israel linaripotiwa kuongeza utayari wake wa kijeshi, huku baadhi ya maafisa wa usalama wakionya kuwa kuendelea kwa hali ya sasa kunaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana kutokana na mashambulizi yaliyopita dhidi ya Iran.

Hata hivyo, viongozi wengine wa kisiasa wameonya dhidi ya hatua za kijeshi zisizo za lazima. Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Israel, Gadi Eisenkot, amesema matumizi ya nguvu bila tishio la moja kwa moja yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa demokrasia na imani ya wananchi.

Tofauti ya mitazamo kati ya Israel na Marekani inaweza kuwa muhimu katika mgogoro huu.

Wakati Washington inapendelea shinikizo la kiuchumi na mzingiro, baadhi ya viongozi wa Israel wanaona hatua za kijeshi kama njia bora zaidi ya kuzuia Iran kuimarisha uwezo wake wa kijeshi.

Iwapo Israel itaamua kufanya shambulio jipya dhidi ya Iran, majibu ya Tehran yanaweza kuilazimisha Marekani kutathmini upya sera yake ya sasa na huenda ikajikuta ikirejea kwenye chaguo ambalo utawala wa Trump unajaribu kuliepuka, yaani vita vya moja kwa moja na Iran.

Je, mkwamo unaweza kumalizwa bila makubaliano?

Mchambuzi Howard Schatz anasema ni vigumu kubainisha jambo moja litakalomaliza mkwamo wa sasa.

Hata hivyo, anaona uwezekano kwamba Marekani inaweza kuamua kulegeza au kusitisha mzingiro dhidi ya Iran, ingawa kuondoa vikwazo vya kiuchumi kwa kiwango kikubwa kunaonekana kuwa jambo lisilo na nafasi kubwa kwa sasa.

Kwa upande wake, Bilal Saab anapendekeza kile anachokiita diplomasia ya hatua kwa hatua, ambapo Marekani itapunguza baadhi ya vikwazo na mzingiro wake kwa kubadilishana na Iran kufungua usafiri katika Mlango wa Hormuz na kusitisha mashambulizi dhidi ya meli.

Qatar inaendelea kufanya juhudi za upatanishi kati ya pande hizo mbili. Hata hivyo, viongozi wa Iran wanasema bado wanasubiri Marekani kujibu masharti yao, wakati Donald Trump amesisitiza kuwa Marekani haihitaji makubaliano mapya na Iran.

Kwa sasa, hatima ya sera ya "mpango wa tatu" wa Marekani haitegemei Washington pekee. Shambulio jipya kutoka Israel au hatua ya kijeshi kutoka Iran dhidi ya udhibiti huo inaweza kubadilisha mwelekeo wa mgogoro na kuiweka Marekani tena kwenye njia ya kuchagua kati ya kuendelea na shinikizo la kiuchumi au kurejea vitani.