Kwa nini watu wanapogombana huwatukana mama na dada za wenzao?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Maryam Sultana
- Akiripoti kutoka, BBC Bangla
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Fikiria watu wawili wamekosana. Labda ni majirani, marafiki au hata watu wasiofahamiana. Mwanzoni wanabishana kuhusu jambo fulani, lakini kadiri hasira zinavyoongezeka, wanaanza kurushiana maneno makali.
Ghafla, ugomvi wao unahama kutoka kwenye jambo lililowakosanisha na kuanza kuhusisha mama, dada, wake au hata watoto wa kila mmoja.
Cha kushangaza ni kwamba wanawake hao hawahusiki kabisa na ugomvi unaoendelea, lakini ndio wanaogeuzwa kuwa sehemu ya mashambulizi hayo ya maneno.
Na huenda umewahi kushuhudia hali kama hii mtaani, kwenye foleni, kwenye daladala au hata kwenye mitandao ya kijamii.
Mtu anapokosa maneno ya kumjibu mwenzake, anaanza kumtukana mama yake, kumdhalilisha dada yake au kutumia maneno machafu yanayohusisha wanawake wa familia yake.
Lengo huwa ni kumuumiza, kumwaibisha au kumkasirisha zaidi mtu anayegombana naye.
Ingawa tabia hii imezoeleka zaidi miongoni mwa wanaume, baadhi ya wanawake pia huitumia wanapokuwa katika mabishano.
Nchini Bangladesh, mjadala kuhusu tabia hiyo umeibuka tena baada ya mwigizaji wa filamu za Kibengali, Pony Moon, kuingia katika mabishano makali ya maneno na mwandishi wa habari.
Tarehe 5 Novemba mwaka huu, Bi Moon alielekea mahakamani kuhusiana na kesi inayomkabili baada ya kumtukana mwandishi huyo hadharani, kumtukana mama yake na kumtishia kumuua.
Tukio hilo limeibua tena swali kuhusu kwa nini katika ugomvi au mzozo kati ya watu wawili, wanawake wasiohusika, hasa wa familia zao, ndio wanaolengwa kwa matusi na kudhalilishwa.
Kwa nini tabia hii imekuwa kama desturi katika baadhi ya jamii, na ina mizizi gani katika mitazamo ya kijamii na kimila?
Katika makala haya tumeichambua kiundani na kwa upana zaidi.
Matusi yanayofanana katika lugha na jamii mbalimbali

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kutumia maneno ya kudhalilisha wanawake wa familia ya mtu mwingine kwa lengo la kumuumiza au kumdhalilisha si jambo linalopatikana katika jamii moja pekee. Ni tabia inayojitokeza katika tamaduni na lugha mbalimbali duniani haswa uswahilini yaani maeneo ya pwani.
Utafiti uliochapishwa mwaka 2024 katika jarida la Behavioral Research Methods kuhusu matumizi ya lugha ya matusi ulibaini kuwa katika jamii na lugha mbalimbali, matusi mengi huhusisha jinsia ya mtu na viungo vya uzazi ambavyo kwa kawaida havitajwi hadharani.
Utafiti huo ulihusisha lugha 13 katika nchi 17.
Watafiti waliwaomba washiriki kukusanya maneno yasiyofaa yanayotumiwa katika jamii zao kama matusi au katika mizaha ya kawaida.
Matokeo yalionyesha kuwa matusi yanayotumiwa sana katika lugha mbalimbali yanahusiana na viungo vya uzazi vya wanawake na vitendo vya kufanya nao ngono.
Katika baadhi ya lugha, kuna maneno mengi ya kudhalilisha yanayomhusisha mama wa mtu, mtoto aliyezaa, utambulisho wake na hata nasaba yake.
Matusi yanayohusisha viungo vya uzazi vya wanaume pia yapo, lakini utafiti huo unaonyesha kuwa hayatumiki kwa kiwango sawa na yale yanayowalenga wanawake.
Kwa nini watu wanaoheshimiwa ndio wanaodhalilishwa?
Katika dini na tamaduni mbalimbali duniani, mama anachukuliwa kuwa mtu anayestahili heshima kubwa na mwenye nafasi ya pekee katika jamii.
Kwa mujibu wa watafiti, katika baadhi ya jamii, neno mama halitumiki tu kumrejelea mwanamke aliyemzaa mtu, bali pia hutumiwa kama ishara ya heshima kwa wanawake wengine.
Katika baadhi ya tamaduni, nchi pia huitwa mama, huku baadhi ya dini zikitumia jina hilo kuwarejelea miungu fulani.
Dini ya Kiislamu inasisitiza umuhimu wa kuwatendea wazazi kwa wema, huku ikitambua nafasi na juhudi za mama katika kumlea mtoto.
Katika Ukristo, Maria, mama wa Yesu Kristo, anaheshimiwa kwa namna ya pekee na kutazamwa kama ishara ya umama na usafi wa moyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata hivyo, pamoja na heshima hiyo, kwa nini mtu humtukana mama wa mwenzake na hata kutumia maneno yanayodhalilisha viungo vyake vya uzazi?
Akijibu swali hilo, Zubaida Nasreen, profesa wa Anthropolojia katika Chuo Kikuu cha Dhaka nchini Bangladesh, anasema sababu kubwa inatokana na nafasi ya heshima aliyopewa mama katika jamii.
Anasema watu hutumia matusi yanayomlenga mama kwa sababu wanajua kuwa kumdhalilisha mtu anayeheshimiwa na mwenzake kunaweza kumuumiza zaidi.
"Katika jamii, dini na tamaduni mbalimbali, mama hupewa nafasi ya heshima. Lakini mtu anapochafua heshima yake kwa kuhusisha jina lake na masuala ya kingono au kumtilia shaka kuhusu uadilifu wake, anakuwa pia anawadhalilisha watoto wake," amesema katika mahojiano na BBC Bangla.
Bi Nasreen anaongeza kuwa kumtukana mama wa mtu mwingine ni njia ya kumletea maumivu makubwa ya kihisia na kumwaibisha.
Anasema mashambulizi hayo ya maneno yanaweza kusababisha msongo mkubwa wa kihisia kwa anayelengwa.
Profesa Nasreen anasisitiza kuwa hakuna jamii wala dini inayoruhusu mtu kumvunjia heshima mama au wanawake wa familia ya mtu mwingine.
Naye Tanya Haque, profesa wa masomo ya jinsia katika Chuo Kikuu cha Dhaka, anasema mtu anapotumia maneno yanayomdhalilisha mama au dada wa mwenzake, mara nyingi lengo huwa ni kumuumiza kisaikolojia na kihisia.
Kwa upande mwingine, baadhi ya jamii zimezoea kutumia maneno yanayowadhalilisha wanawake hata katika mizaha na utani wa kawaida.
Huenda umewahi kusikia mtu akimtukana mwenzake kisha akajitetea kwa kusema alikuwa anatania tu.
Wengine wamezoea kutumia matusi yanayowalenga mama na dada kiasi kwamba hawafikirii hata maana ya maneno wanayotamka.
Profesa Nasreen anaamini kuwa iwe ni kwa mazoea au kwa makusudi, matumizi ya lugha hiyo kimsingi yanadhalilisha wanawake na yanaakisi dhana fulani ya uanaume inayohusishwa na utawala wa wanaume.
Profesa Tanya Haque naye anasema pale lugha ya matusi inapodumu kwa muda mrefu katika jamii, watu huanza kuichukulia kama jambo la kawaida na kupuuza madhara yake.
Kwa mujibu wake, katika jamii ambako utamaduni wa kuheshimiana haujajengeka imara, matusi na lugha ya kudhalilisha huweza kuwa sehemu ya mawasiliano ya kila siku.
Kwa nini hata wanawake wenyewe huwatukana wanawake wenzao?

Chanzo cha picha, Getty Images
Jambo jingine linalozua mjadala ni kwamba matusi yanayowalenga mama na dada hayatumiwi na wanaume pekee.
Baadhi ya wanawake pia huyatumia. Kwa nini mwanamke amdhalilishe mama wa mtu mwingine kwa kutumia maneno yanayohusisha jinsia au viungo vyake vya uzazi?
Wachambuzi wanasema mfumo dume hauendelezwi na wanaume pekee. Wanawake pia hukulia katika jamii hizo hizo na huweza kujifunza na kuendeleza lugha ya matusi wanayoisikia katika mazingira yao.
Profesa Zubaida Nasreen anasema mwanamke anapomtukana mama wa mtu mwingine, kimsingi anatumia lugha ambayo ameizoea katika jamii inayomzunguka.
Anaongeza kuwa, "Mwanamke pia anaweza kutumia lugha hiyo akifikiri kwamba ikiwa mwanamume anaweza kumtukana kwa namna hiyo, kwa nini yeye asifanye hivyo?"


































