Edwin Sifuna: Je, mwanasiasa huyu wa Kenya anaweza kugeuza umaarufu wake na kuitumia kuwania urais?

.
Maelezo ya picha, Edwin Sifuna ni Seneta wa Nairobi kwa sasa
    • Author, Wycliffe Muia
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Bado hajatangaza rasmi nia yake ya kuwania urais, lakini baadhi ya vijana nchini Kenya tayari wameamua kuwa Seneta Edwin Sifuna ndiye mgombea wanayemtaka kuliongoza taifa katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Akitambulika kwa kauli zake kali, uwezo wa kujibu hoja kwa haraka na idadi inayoongezeka ya watu wanaohudhuria mikutano yake ya kisiasa, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 44 anajitokeza kama nguvu mpya isiyotarajiwa inayoweza kumpa changamoto Rais William Ruto, mwenye umri wa miaka 59, pamoja na kuwa kikwazo kwa baadhi ya viongozi wa upinzani ambao pia wana azma ya kuwania urais.

Baadhi ya wafuasi wake wamemlinganisha na Barack Obama alipokuwa kijana, ambaye alivutia mamilioni ya watu kupitia ujumbe wake wa matumaini na mabadiliko wakati wa kampeni zake za kihistoria za kuwania urais wa Marekani mwaka 2008.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa msisimko unaomzunguka Sifuna huenda umetangulia uwezo wake halisi wa kisiasa. Wanasema kuwa umaarufu wake mkubwa unatokana zaidi na mitandao ya kijamii kuliko kuwa na mtandao imara wa wafuasi katika ngazi za mashinani.

Sifuna mwenyewe amekuwa akisita kuzungumzia azma yake ya kuwania urais, akisisitiza kuwa kipaumbele chake kwa sasa ni kujenga upinzani wenye umoja ambao unaweza kumshinda Ruto.

"Subirini kwanza, mazungumzo hayo yatafanyika baadaye sana," aliwaambia hivi karibuni waandishi wa habari jijini Nairobi alipoulizwa kuhusu azma yake ya urais na jinsi anavyokusudia kubadilisha umaarufu wake unaoongezeka kuwa kura.

Umaarufu wake unaongezeka katika kipindi muhimu cha siasa za Kenya, kufuatia kifo cha kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga, ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za taifa hilo kwa miongo kadhaa.

Odinga, ambaye aligombea urais mara tano bila mafanikio, alikuwa mshauri wa kisiasa wa Sifuna. Mwaka 2018, alimteua kuwa katibu mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), mojawapo ya vyama vikubwa vya kisiasa nchini Kenya.

.
Maelezo ya picha, Sifuna amekuwa akiwavutia vijana wengi katika mikutano yake
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa miaka mingi, Sifuna alikuwa miongoni mwa watetezi wakuu wa Odinga, akiwakabili wapinzani wake wa kisiasa katika mijadala ya televisheni, mikutano ya hadhara na bungeni.

Hata hivyo, baada ya kifo cha Odinga, mgawanyiko ndani ya chama cha ODM uliongezeka kuhusu iwapo chama hicho kinapaswa kuendelea kushirikiana na serikali ya Rais William Ruto.

Wakati baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho waliunga mkono ushirikiano wa karibu zaidi na rais, Sifuna alipinga vikali mpangilio huo, akisema kuwa upinzani unapaswa kuiwajibisha serikali badala ya kusaidia kuendeleza utawala wake.

Msimamo huo ulimgharimu nafasi yake ya katibu mkuu wa ODM pamoja na wadhifa wa uongozi katika Seneti, bunge la juu la Kenya.

Hata hivyo, kile ambacho huenda kingemaliza taaluma ya kisiasa ya mwanasiasa mwingine kinaonekana kumpa Sifuna msukumo mpya wa kisiasa.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Davis Ngemu anasema Sifuna amejitokeza kuwa miongoni mwa sauti kuu katika vuguvugu la Linda Mwananchi, jina ambalo kwa tafsiri ya jumla linamaanisha "mtetee mwananchi".

Vuguvugu hilo limejikita katika kuelezea hisia za kutoridhika zinazozidi kuongezeka miongoni mwa wananchi kuhusu kupanda kwa gharama za maisha, kodi kubwa, ukosefu wa ajira na kile ambacho wafuasi wake wanakiona kuwa ni tabaka la viongozi wa kisiasa ambalo linazidi kujitenga na maisha na mahitaji ya Wakenya wa kawaida.

Mikutano yake ya kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa ikivutia umati mkubwa wa watu, huku Sifuna akijitokeza kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa hasa miongoni mwa vijana.

Ujumbe wake pia unagusia baadhi ya malalamiko yaliyochochea maandamano yaliyoongozwa na vijana nchini Kenya mwaka 2024, wakati maelfu ya watu walipojitokeza barabarani kupinga mapendekezo ya kuongeza kodi na kudai serikali iwajibike zaidi kwa wananchi.

Maandamano hayo, ambayo kwa kiasi kikubwa yaliandaliwa kupitia mitandao ya kijamii, yalidhihirisha kutoridhika kwa wananchi kwa kiwango kikubwa na viongozi wa kisiasa kutoka vyama mbalimbali.

Ingawa maandamano hayo kwa kiasi kikubwa hayakuwa na kiongozi maalumu na hakuna ushahidi kwamba vuguvugu hilo kwa ujumla limeungana kumuunga mkono Sifuna, seneta huyo amejaribu kujitambulisha kama sauti ya kizazi kinachotaka aina tofauti ya uongozi.

Sifuna alizaliwa mwaka 1982 magharibi mwa Kenya na kusomea sheria kabla ya kuingia katika siasa.

Jaribio lake la kwanza la kuwania kiti cha useneta wa Nairobi mwaka 2017 liliishia kwa kushindwa. Hata hivyo, alirejea baada ya miaka mitano na kushinda kwa kishindo.

Tangu wakati huo, amejijengea sifa ya kuwa mwanasiasa mwenye ufasaha wa kujieleza na anayekabiliana vikali na wapinzani wake, akitumia ucheshi, kejeli na maswali ya moja kwa moja kuwakabili maafisa wa serikali na wapinzani wa kisiasa.

Mtindo wake wa kukabiliana na wapinzani umemfanya kuwa sura inayofahamika kwenye televisheni na mitandao ya kijamii, ambako video za mijadala yake huvutia hisia na kupata umaarufu mara kwa mara.

Tofauti na wanasiasa wengi wakongwe wenye ushawishi nchini Kenya, Sifuna hahusishwi na tabaka la mabilionea nchini humo. Hali hiyo imeongeza mvuto wake miongoni mwa watu waliochoshwa na ushawishi wa fedha katika siasa na wanaotamani kuona sura mpya baada ya miaka mingi ya watu wale wale kuendelea kuzunguka katika ulingo wa kisiasa.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Macharia Gaitho, anamtaja kama "mtu wa wakati huu", akisema anawakilisha "nguvu na ubunifu wa kizazi kinachothubutu kuwazia mustakabali mpya na jasiri, usiofungwa na mfumo wa kawaida wa uongozi".

Hata hivyo, Gaitho anaonya kuwa mustakabali wa kisiasa wa Sifuna bado haujawa na uhakika.

"Sifuna yuko katika safari ambayo, akiongozwa ipasavyo, inaweza kumfikisha kileleni mwa uongozi wa Kenya; lakini pia anaweza kuanguka iwapo atashindwa kushindana katika ligi ya viongozi wakuu," Gaitho aliandika katika gazeti la Daily Nation nchini Kenya.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa, Barrack Muluka, anasema sasa Sifuna anapaswa kugeuza umaarufu alionao kuwa vuguvugu la kitaifa lenye uwezo wa kudumu.

"La sivyo, seneta huyo atakumbukwa tu kama mtu aliyeng'aa kwa muda mfupi, jambo ambalo wapinzani wake wanatamani litokee," anasema Muluka, akiongeza: "Historia haiwatendei haki viongozi wanaochukulia fursa ya wakati fulani kuwa ndiyo mwisho wa safari yao."

.
Maelezo ya picha, Rais William Ruto

Sifuna tayari amechukua hatua za kuunda chama chake cha kisiasa. Mwezi Oktoba, alizindua chama cha The Equitable Party (TEP), ambapo aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama hicho huku washirika wake wakimuunga mkono kuwa mgombea wao anayempendekeza kwa urais iwapo ataamua kuwania kiti hicho.

Tangu wakati huo, chama hicho kimeanza mchakato wa kubadilisha jina lake na kuwa Linda Mwananchi Movement, ingawa pendekezo hilo la kubadilisha jina bado linakabiliwa na vikwazo vya kiutawala.

Wakati wa uzinduzi huo, Sifuna aliwasilisha ajenda ya kiuchumi iliyolenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa Wakenya wa kawaida.

Aliahidi kufuta ushuru tata wa nyumba, kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mafuta na umeme, kupambana na ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za serikali, pamoja na kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana.

Pia amekosoa michango inayotolewa kwa mpango mpya wa serikali wa bima ya afya, akisema Wakenya wanakatwa fedha nyingi kupita kiasi.

Sifuna anasisitiza kuwa kupambana na ufisadi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya serikali kutatoa nafasi ya kupunguza ushuru.

Anasema wataalamu wanaandaa ilani ya kina zaidi itakayofafanua namna mapendekezo yake yatakavyotekelezwa.

Huku wasifu wake wa kisiasa ukiendelea kukua, amekuwa akikabiliwa na ukosoaji mkali zaidi kutoka kwa Rais William Ruto, ambaye amekuwa akimtaja mara kwa mara katika mikutano ya hadhara.

.

Rais Ruto amekuwa akimkejeli kwa kumtaja kama "Mtu bure" na huku akipuuza chama chake kipya cha kisiasa na kukiita "chama kitupu".

Ruto amemshutumu seneta huyo kwa kushindwa kutoa mapendekezo mbadala yanayoaminika kuhusu sera za serikali, na kuonya kuwa kufutilia mbali mpango wa nyumba za gharama nafuu kutahatarisha ajira.

Pia amedai kuwa rais wa zamani Uhuru Kenyatta ndiye anayemfadhili Sifuna ili kuidhoofisha serikali yake.

Kenyatta hajakanusha madai hayo hadharani. Badala yake, ameonekana kuukubali utani wa kuitwa "sponyo", neno la lugha ya mtaani linalomaanisha mfadhili.

Mabadilishano hayo ya maneno yanayozidi kuwa ya kibinafsi yanaonyesha jinsi kujitokeza kwa Sifuna katika siasa kunavyozidi kuwa sehemu ya mchuano mpana wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027