Viongozi wa Afrika waliobadili katiba ili kubaki madarakani

Chanzo cha picha, Getty Images
Demokrasia katika mataifa kadhaa ya Afrika imeendelea kukabiliwa na changamoto ya viongozi wanaotumia mabadiliko ya katiba kuondoa vikwazo vinavyowazuia kuendelea kushikilia madaraka ama kusalia madarakani. Baadhi wameondoa kabisa ukomo wa mihula ya urais, wengine wamebadili idadi ya mihula inayoruhusiwa, huku wengine wakipitisha katiba mpya na kutumia tafsiri yake kuanza upya hesabu ya muda wao wa uongozi.
Hivi karibuni, mjadala huo umeibuka tena baada ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi kusaini sheria ya kura ya maoni kuhusu masuala ya kikatiba Novemba 9, 2026. Serikali inasema hatua hiyo inalenga mageuzi ya kitaasisi, lakini upinzani unahofia kuwa huenda ikawa njia ya kumwezesha kugombea muhula wa tatu, ambao haujaruhusiwa chini ya masharti ya sasa ya katiba.
Historia ya Afrika ina mifano kadhaa ya viongozi waliofanikiwa kubadili masharti hayo na kuendelea kutawala zaidi ya muda uliokuwa umeruhusiwa awali. Katika baadhi ya nchi, katiba zilikuwa zikiweka ukomo wa mihula miwili, lakini mabadiliko yaliyofanywa yaliwaondolea viongozi vizuizi hivyo kabla ya muda wao kumalizika au kuwapa nafasi ya kuanza upya hesabu ya mihula.
Hata hivyo, si kila jaribio limefanikiwa. Baadhi ya viongozi walikabiliwa na upinzani wa wananchi, bunge, vyama vyao wenyewe au mahakama, na kushindwa kupata mabadiliko waliyokuwa wakiyahitaji. Hii ni mifano ya viongozi waliofanikiwa na wale ambao majaribio yao hayakufanikiwa.
Hapa ni baadhi ya viongozi waliofanikiwa kubadili katiba na kuendelea kutawala Afrika
Yoweri Museveni – Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Yoweri Museveni amekuwa madarakani Uganda tangu mwaka 1986. Katiba ya mwaka 1995 iliweka ukomo wa mihula miwili ya urais, kila mmoja ukiwa wa miaka mitano. Kwa masharti hayo, baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka 1996 na 2001, muhula wake wa pili ungeisha mwaka 2006, na asingeruhusiwa kugombea tena.
Hata hivyo, mwaka 2005, wakati akiwa katika muhula wake wa pili, bunge lilipitisha mabadiliko ya katiba yaliyoondoa kabisa ukomo wa idadi ya mihula ya urais. Mabadiliko hayo yalimfungulia njia Museveni kugombea tena uchaguzi wa mwaka 2006, ambao alishinda, na kuendelea kushiriki chaguzi zilizofuata na kushinda kila mara licha ya malalamiko ya wapinzani.
Mwaka 2017, serikali yake ilifanya mabadiliko mengine yaliyoondoa ukomo wa umri wa miaka 75 uliokuwa umewekwa na katiba kwa mgombea urais. Hatua hiyo ilimruhusu Museveni kuendelea kugombea licha ya kuvuka umri huo. Kwa mabadiliko hayo mawili, vikwazo vikuu vya idadi ya mihula na umri viliondolewa, na kumwezesha kuendelea kutawala hadi sasa akiwa miongoni mwa marais waliokaa madarakani muda mrefu zaidi Afrika.
Paul Biya – Cameroon

Chanzo cha picha, Paul Biya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Paul Biya aliingia madarakani Cameroon mwaka 1982. Katiba ya mwaka 1996 iliweka ukomo wa mihula miwili ya urais, kila mmoja ukiwa wa miaka saba. Kwa kuwa Biya alikuwa tayari ameshinda uchaguzi wa mwaka 1997 na 2004, muhula wake wa pili ulitarajiwa kumalizika mwaka 2011, ambao ungekuwa mwisho wa uongozi wake kwa mujibu wa masharti hayo.
Lakini Desemba 2007, Biya alitangaza nia ya kuondoa ukomo huo, na mwaka 2008 bunge lilipitisha mabadiliko ya katiba yaliyoondoa kipengele kilichomzuia rais kuhudumu zaidi ya mihula miwili. Mabadiliko hayo yaliondoa kizuizi kilichokuwa kinatarajiwa kumaliza uongozi wake mwaka 2011.
Baada ya mabadiliko hayo, Biya aliendelea kugombea na kushinda uchaguzi wa mwaka 2011, 2018 na 2025. Hivyo, badala ya kuondoka madarakani mwaka 2011 kama ilivyotarajiwa chini ya katiba ya awali, aliendelea kuongoza Cameroon kwa mihula mingine. Mabadiliko hayo yalizua upinzani kutoka kwa makundi ya kisiasa na wananchi waliodai kuwa yalilenga kumlinda rais dhidi ya ukomo wa madaraka.
Paul Kagame – Rwanda

Chanzo cha picha, Getty Images
Katiba ya Rwanda ya mwaka 2003 iliweka ukomo wa mihula miwili ya urais, kila mmoja ukiwa wa miaka saba. Paul Kagame alichaguliwa mwaka 2003 na kushinda tena mwaka 2010. Kwa masharti ya katiba hiyo, muhula wake wa pili ulitarajiwa kuwa wa mwisho na angehitajika kuondoka madarakani mwaka 2017.
Lakini mwaka 2015, Rwanda ilifanya kura ya maoni na kupitisha mabadiliko ya katiba yaliyobadilisha mfumo wa mihula ya urais. Mabadiliko hayo yaliruhusu Kagame kugombea muhula mwingine wa miaka saba kuanzia mwaka 2017, na baadaye mihula miwili zaidi ya miaka mitano kila mmoja.
Kwa utaratibu huo, badala ya kuondoka mwaka 2017, Kagame aliendelea na uongozi baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka huo kwa takribani asilimia 98.8. Mwaka 2024 alishinda tena uchaguzi wa urais, akiingia katika muhula mwingine wa miaka mitano. Mabadiliko hayo yanampa nafasi ya kuendelea kutawala hadi sasa.
Alassane Ouattara – Ivory Coast

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast alitumia katiba mpya iliyopitishwa mwaka 2016 kuendelea kugombea urais licha ya kuwa tayari alikuwa amehudumu mihula miwili. Katiba ya awali ya mwaka 2000 ilikuwa imeweka ukomo wa mihula miwili ya miaka mitano kwa rais.
Ouattara alichaguliwa mwaka 2010 na kushinda tena mwaka 2015. Kwa mujibu wa masharti ya katiba ya zamani, muhula wake wa pili ulitarajiwa kumalizika mwaka 2020, na asingepaswa kugombea tena. Hata hivyo, mwaka 2016 serikali yake ilipitisha katiba mpya.
Mabadiliko hayo yalizua mjadala kuhusu namna mihula ya urais ilivyopaswa kuhesabiwa. Serikali ilitetea msimamo kuwa mihula aliyohudumu chini ya katiba ya zamani isihesabiwe katika ukomo wa katiba mpya. Tafsiri hiyo ilimruhusu Ouattara kugombea tena mwaka 2020, uchaguzi ambao alishinda licha ya upinzani kupinga uamuzi wake.
Mwaka 2025 aliendelea tena kugombea na kushinda uchaguzi wa urais. Kwa kutumia katiba mpya na tafsiri ya kuanza upya kwa hesabu ya mihula, Ouattara aliweza kuendelea madarakani zaidi ya mihula miwili iliyokuwa imewekwa na katiba ya awali.
Ismail Omar Guelleh – Djibouti

Chanzo cha picha, Getty Images
Ismail Omar Guelleh amekuwa rais wa Djibouti tangu mwaka 1999. Katiba ya nchi hiyo ya mwaka 1992 ilikuwa imeweka ukomo wa mihula miwili ya urais, kila mmoja ukiwa wa miaka sita. Baada ya kuchaguliwa mwaka 1999 na 2005, muhula wake wa pili ulitarajiwa kumalizika mwaka 2011, na asingepaswa kugombea tena.
Hata hivyo, mwaka 2010, wakati akiwa karibu kumaliza muhula wake wa pili, bunge lilipitisha mabadiliko ya katiba yaliyoondoa ukomo wa mihula ya urais. Hatua hiyo ilimfungulia njia ya kugombea tena uchaguzi wa mwaka 2011, ambao alishinda.
Baada ya hapo, Guelleh aliendelea kushinda chaguzi za mwaka 2016 na 2021. Kwa hiyo, badala ya kuondoka madarakani mwaka 2011, aliendelea kuongoza kwa mihula mingine kutokana na kuondolewa kwa kizuizi cha mihula miwili. Hatua hiyo imekuwa ikikosolewa na wapinzani wanaodai kuwa imeimarisha mkusanyiko wa madaraka mikononi mwa mtu mmoja.
Nchini Zimbabwe nako, bunge lilipitisha mabadiliko ya katiba mwaka 2026 ya kuongeza mihula ya urais na bunge kutoka miaka mitano hadi saba chini ya Rais Emmerson Mnangagwa, hatua inayotetewa kwa hoja ya mwendelezo wa sera lakini ikipingwa na wakosoaji kama mbinu ya kuongeza muda wa utawala.
Viongozi waliojaribu kubadili katiba lakini wakashindwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Si viongozi wote walioweza kutumia mabadiliko ya katiba kuendelea kutawala. Nchini Burkina Faso, Blaise Compaoré alijaribu mwaka 2014 kubadili katiba ili kugombea muhula mwingine baada ya kuwa madarakani tangu mwaka 1987. Jaribio hilo lilichochea maandamano makubwa yaliyomlazimisha kujiuzulu Oktoba 2014 na kuondoka nchini. Hata hivyo, huko nyuma Compaoré alifanikiwa kuondoa ukomo wa mihula mwaka 1997, kabla ya masharti ya mihula miwili kurejeshwa mwaka 2000/2003.
Nchini Nigeria, Olusegun Obasanjo alijaribu kati ya mwaka 2005 na 2006 kupata mabadiliko ya katiba kumruhusu kugombea muhula wa tatu baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka 1999 na 2003. Pendekezo hilo lilikataliwa na bunge mwaka 2006, hata baadhi ya wabunge wa chama chake walilipinga. Nchini Zambia, Frederick Chiluba naye alijaribu mwaka 2001 kubadili katiba ili agombee muhula wa tatu, lakini alikosa uungwaji mkono wa kutosha ndani ya chama chake na bunge, licha ya chama chake kuwa na wabunge wengi.
Nchini Malawi, Bakili Muluzi alijaribu mwaka 2002 kubadili katiba ili aongeze muhula wa tatu baada ya kuhudumu mihula miwili, lakini alilazimika kuachana na mpango huo kutokana na upinzani mkubwa na kukosa uungwaji mkono wa kutosha. Senegal, Abdoulaye Wade aliruhusiwa na mahakama kugombea tena mwaka 2012 baada ya kutetea kuwa katiba mpya ya mwaka 2001 ilianza upya hesabu ya mihula yake. Hata hivyo, alishindwa katika duru ya pili ya uchaguzi dhidi ya Macky Sall, hivyo juhudi zake za kuendelea kubaki madarakani zikashindwa kupitia sanduku la kura.


































