Je, hii ndiyo ndege ya mwisho ya kivita kuendeshwa na binadamu Uingereza?

.
    • Author, Florence Freeman
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Ndege za kivita zisizo na rubani zinaweza kuwa sehemu kuu ya vita vya anga katika siku zijazo, kwa mujibu wa mkuu wa Jeshi la Anga la Uingereza (RAF), Marshal Sir Harv Smyth.

Kauli yake imeibua maswali kuhusu iwapo enzi ya marubani binadamu katika ndege za kivita inaelekea kufikia mwisho wake.

Sir Harv amesema maendeleo ya kasi ya teknolojia ya akili bandia (AI) na mifumo ya kiotomatiki yanabadilisha kwa kiasi kikubwa namna vita vya anga vitakavyopiganwa katika miongo ijayo.

Akizungumza kuhusu mpango wa Global Combat Air Programme (GCAP), ushirikiano wa Uingereza, Italia na Japan wa kutengeneza ndege mpya ya kivita ya kizazi cha sita, alisema ndege hiyo huenda ikawa ndege ya mwisho ya kivita kuendeshwa na binadamu ambayo Uingereza itawahi kutengeneza.

Ndege hiyo, inayojulikana kwa jina la Tempest, inatarajiwa kuanza kutumika mwaka 2035.

Mbali na kuwa na kasi kubwa na uwezo wa kujificha dhidi ya rada za adui, Tempest itakuwa na vihisi vya kisasa na mifumo ya akili bandia itakayosaidia rubani kufanya maamuzi katika mazingira yenye shinikizo kubwa.

Kwa mujibu wa Sir Harv, teknolojia mpya haimaanishi kwamba binadamu hawatahitajika tena vitani, bali baadhi ya majukumu hatari zaidi yatafanywa na mashine na mifumo ya AI.

Alisisitiza kuwa jukumu la mwisho la maamuzi muhimu linapaswa kubaki mikononi mwa binadamu.

"Majukumu hatari zaidi yatafanywa na mashine badala ya wanadamu," alisema, huku akiongeza kuwa ndege za kivita zisizo na rubani zinatarajiwa kuanza kupaa katika anga ya Uingereza kuanzia mwaka ujao.

Kauli hiyo inaashiria mabadiliko makubwa katika historia ya anga za kijeshi. Kwa miongo mingi, marubani wamekuwa kiini cha operesheni za kivita angani, lakini maendeleo ya teknolojia sasa yanaifanya dhana ya ndege za kivita zinazojiendesha yenyewe kuwa karibu zaidi na uhalisia.

Mpango wa GCAP ulitangazwa mwaka 2022 na unahusisha Uingereza, Italia na Japan. Mwezi Julai, mataifa hayo yalitia saini mkataba wa pauni bilioni 4.6 kwa ajili ya hatua inayofuata ya maendeleo ya mradi huo.

Serikali ya Uingereza inasema mradi huo tayari umezalisha ajira 3,500 na nafasi 1,000 za mafunzo ya ufundi.

Wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanaona kwamba ikiwa teknolojia ya AI itaendelea kukua kwa kasi ya sasa, ndege za kivita za siku zijazo zinaweza kutekeleza misheni nyingi bila uwepo wa rubani ndani ya chombo hicho.

Hata hivyo, mjadala bado unaendelea kuhusu kiwango ambacho mashine zinaweza kuaminiwa kufanya maamuzi katika mazingira ya vita, ambapo makosa yanaweza kugharimu maisha ya watu wengi.

Kwa sasa, Tempest inatarajiwa kubaki na rubani binadamu. Lakini kauli ya mkuu wa RAF inaonyesha wazi kuwa kizazi kinachofuata baada yake kinaweza kuwa mwanzo wa enzi mpya ya vita vya anga vinavyoendeshwa zaidi na akili bandia kuliko wanadamu.

Je, AI itachukua nafasi ya marubani wa kivita?

.

Kwa zaidi ya karne moja, marubani wamekuwa kiini cha nguvu za kijeshi za mataifa mengi duniani.

Historia ya vita vya anga, kuanzia Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia hadi migogoro ya kisasa ya Mashariki ya Kati na Ukraine, imejengwa juu ya uwezo wa marubani kusafiri katika mazingira hatari, kutambua malengo na kufanya maamuzi ya haraka wakati wa mapambano.

Hata hivyo, maendeleo ya haraka ya teknolojia katika miaka ya hivi karibuni yameanza kubadili mtazamo huo. Mataifa mengi sasa yanawekeza mabilioni ya dola katika mifumo ya kijeshi inayotegemea akili bandia, ndege zisizo na rubani na teknolojia za kiotomatiki ambazo zinaweza kutekeleza baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakifanywa na wanadamu hapo awali.

Katika miaka ya karibuni, matumizi ya ndege zisizo na rubani yameongezeka kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya vita. Migogoro ya Ukraine, Mashariki ya Kati na maeneo mengine imeonyesha jinsi teknolojia hiyo ilivyobadilika kutoka kuwa chombo cha kukusanya taarifa hadi kuwa silaha muhimu ya kushambulia malengo ya adui.

Wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanaeleza kuwa moja ya sababu zinazochochea mabadiliko hayo ni gharama kubwa ya mafunzo ya marubani wa kijeshi. Mafunzo ya rubani wa ndege ya kisasa ya kivita yanaweza kuchukua miaka kadhaa na kugharimu mamilioni ya dola kabla hajawa tayari kupelekwa vitani.

Mbali na gharama hizo, majeshi pia hukabiliwa na changamoto ya kupoteza vifaa vya gharama kubwa na wafanyakazi wenye ujuzi pale ndege inapopigwa au kupata hitilafu wakati wa operesheni.

Ndiyo maana baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa teknolojia za siku zijazo zitajengwa juu ya falsafa ya kupunguza hatari kwa wanadamu kadiri iwezekanavyo.

Katika mazingira hayo, ndege za kivita za kizazi kijacho zinatarajiwa kufanya kazi tofauti na zile zinazotumika sasa. Badala ya rubani kutegemea uwezo wake binafsi kufanya maamuzi yote akiwa angani, mifumo ya akili bandia itakuwa na uwezo wa kuchambua taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kwa sekunde chache na kumpa rubani mapendekezo ya hatua za kuchukua.

Mfumo huo unaweza kuchunguza rada za adui, kutambua vitisho vinavyokaribia, kutabiri hatari zinazowezekana na hata kusaidia kupanga mbinu za kujilinda au kushambulia. Hali hiyo inaweza kumpunguzia rubani mzigo mkubwa wa kufanya maamuzi wakati wa vita.

Kwa mujibu wa watengenezaji wa mpango wa GCAP, ndege ya Tempest imekusudiwa kuwa zaidi ya ndege ya kawaida ya kivita. Inatarajiwa kuwa sehemu ya mtandao mkubwa wa mifumo ya kijeshi inayoweza kushirikiana kwa wakati mmoja.

Katika mfumo huo, ndege yenye rubani inaweza kuongoza kundi la ndege ndogo zisizo na rubani zinazoweza kutumwa mbele kutekeleza kazi hatari zaidi. Ndege hizo zinaweza kufanya uchunguzi, kukusanya taarifa za kijasusi, kuvuruga rada za adui au hata kufanya mashambulizi bila kumweka rubani katika hatari ya moja kwa moja.

Baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa katika siku zijazo, ndege zinazotumia akili bandia zinaweza kuwa na uwezo wa kufanya baadhi ya kazi hizo bila kuhitaji maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa binadamu kila wakati.

Nani atawajibika AI ikikosea vitani?

Hata hivyo, maendeleo hayo yameibua mjadala mkubwa wa kimaadili na kisiasa duniani.

Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu pamoja na watafiti wa teknolojia wamekuwa wakionya kuhusu hatari za kuipa mifumo ya akili bandia uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi katika mazingira ya vita.

Wakosoaji wa teknolojia hiyo wanauliza iwapo mashine zinaweza kutofautisha kwa usahihi kati ya walengwa wa kijeshi na raia wasiokuwa na hatia katika mazingira changamano ya vita.

Pia kuna hofu kuhusu nani atakayewajibika endapo mfumo wa akili bandia utafanya kosa na kusababisha vifo vya raia au uharibifu mkubwa.

Kwa sasa, mataifa mengi makubwa yanayowekeza katika teknolojia hizo bado yanasisitiza kwamba maamuzi ya mwisho kuhusu matumizi ya nguvu za kijeshi yanapaswa kubaki mikononi mwa binadamu.

Hiyo ndiyo sababu Marshal Sir Harv Smyth amesisitiza kuwa licha ya mchango unaokua wa teknolojia, jukumu la uwajibikaji wa mwisho haliwezi kuhamishiwa kwa mashine.

Wakati huo huo, ushindani wa kimataifa katika teknolojia za kijeshi unaendelea kuongezeka. Marekani, China, Urusi na nchi kadhaa za Ulaya zinaendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa inayoweza kuunganisha akili bandia, uchambuzi wa data kwa kasi kubwa na ndege zisizo na rubani.

Kwa upande wa Uingereza, Tempest inaonekana kuwa jibu lake kwa ushindani huo wa kimataifa. Mradi huo unaonekana kuwa sio tu uwekezaji wa kijeshi bali pia mkakati wa kuhakikisha taifa hilo linaendelea kuwa miongoni mwa viongozi wa teknolojia za anga katika miongo ijayo.

Lakini swali linalobaki ni ikiwa ndege za kivita zinazoendeshwa na marubani wa binadamu zitakuwa sehemu ya historia katika siku zijazo.

Kwa sasa, Tempest bado itakuwa na rubani ndani ya chumba cha uongozi wa ndege. Hata hivyo, kauli ya mkuu wa Jeshi la Anga la Uingereza inaonyesha jinsi wataalamu wengi wa ulinzi wanavyoanza kufikiria kuhusu dunia ambayo akili bandia itakuwa mshirika mkuu, au pengine mrithi, wa rubani wa kivita.

Iwapo mwelekeo huo utaendelea, Tempest inaweza kukumbukwa si tu kama ndege mpya ya kisasa ya Uingereza, bali kama moja ya ndege za mwisho za kivita ambazo bado zilimtegemea binadamu kukaa kwenye chumba cha rubani

Imefasiriwa na Asha Juma