Uturuki yaweka Halk TV chini ya usimamizi, mmiliki alalamika

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka za Uturuki "zimedhibiti" moja ya vituo vya habari vinavyotazamwa zaidi nchini humo, mmiliki wake anayeishi London ameiambia BBC.
Akizungumza na kipindi cha Newshour cha BBC, Cafer Mahiroğlu alisema watu tisa wanaohusishwa na Halk TV walikamatwa wiki hii wakikabiliwa na mashtaka yakiwemo utakatishaji fedha, rushwa na kusambaza taarifa za kupotosha.
Mahiroğlu alisema baadhi ya jamaa wa familia yake ni miongoni mwa waliokamatwa wakati kituo hicho kinachounga mkono upinzani kilipowekwa chini ya usimamizi wa serikali mwezi uliopita. Aliongeza kuwa madai dhidi yake na Halk TV ni "ya uongo kabisa".
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Istanbul ilisema watangazaji wawili wa zamani wa habari wa kituo hicho walikuwa miongoni mwa kundi la hivi karibuni la watu waliowekwa kizuizini.
Katika taarifa, waendesha mashtaka waliwashutumu watangazaji hao kwa kutengeneza "taarifa za uongo" kwa malipo ya fedha.
Mamlaka pia zimetoa hati ya kukamatwa kwa mratibu wa habari wa kituo hicho, Kürşad Oğuz, ambaye "yuko nje ya nchi", taarifa hiyo ilisema bila kubainisha alipo.
Mahiroğlu aliiambia BBC kuwa anaweza kufungwa jela iwapo atajaribu kurejea Uturuki.
"Serikali inataka kudhibiti vyombo vyote vya habari... Nina wasiwasi zaidi kuhusu nchi yangu na demokrasia yangu kuliko kuhusu kituo changu," alisema.
Makao makuu ya Halk TV yalivamiwa na mamlaka za Uturuki mwezi uliopita, jambo lililosimamisha matangazo ya moja kwa moja ya kituo hicho. Hili ni tukio la hivi karibuni katika mfululizo wa hatua dhidi ya vyombo vya habari vinavyoonekana kuikosoa serikali ya Rais Tayyip Erdoğan.
Baadaye serikali ilimteua msimamizi mpya kuendesha kituo hicho.
Serikali ya Erdoğan inadhibiti sehemu kubwa ya vyombo vya habari nchini humo, ambayo imeorodheshwa miongoni mwa nchi zenye viwango duni zaidi vya uhuru wa vyombo vya habari duniani, ingawa serikali inasisitiza kuwa haiwakamati wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa kutekeleza shughuli za uandishi wa habari.
Hata hivyo, rais huyo ameongeza hatua dhidi ya sauti za upinzani tangu ushindi wake mwembamba katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2023.




