Jinsi mwanamume alivyomeza mswaki alipokuwa akisafisha meno

Buraash
    • Author, Omkar Karmbelkar
    • Nafasi, BBC Marathi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Ni jambo la kushangaza kusikia kwamba mswaki unaweza kumponyoka mtu mkononi wakati akisafisha meno na kuishia kuumeza. Hata hivyo, tukio la aina hiyo lilimtokea mwanamume mmoja nchini India na kumpelekea kulazwa hospitalini.

Tukio hilo lilimhusu Rajendra Malusare, mkazi wa kijiji cha Sherawali, katika wilaya ya Raigad, jimbo la Maharashtra nchini India.

Malusare, mwenye umri wa miaka 50, ni dereva wa pikipiki za kampuni ya Bajaj.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na madaktari haukuweza kubaini mahali ulipokuwa mswaki huo. Hata hivyo, uchunguzi wa baadaye kwa kutumia teknolojia ya endoskopi ulionyesha kuwa mswaki ulikuwa umekwama ndani ya tumbo lake.

Madaktari walifanikiwa kuutoa mswaki huo wenye urefu wa sentimita 19 bila kumfanyia mgonjwa upasuaji. Malusare aliruhusiwa kurejea nyumbani saa chache baada ya matibabu kukamilika.

Endoskopi ni utaratibu wa kitabibu unaotumia mrija mwembamba na unaopinda, wenye kamera kwenye ncha yake. Mrija huo huingizwa kupitia mdomoni ili kuwawezesha madaktari kuchunguza sehemu za ndani za koo, tumbo na mfumo wa chakula. Teknolojia hiyo pia inaweza kutumika kuondoa vitu vilivyokwama katika sehemu hizo za mwili.

Malusare, ambaye ana ulemavu na anaishi katika kijiji cha Sherawali, alikuwa akisafisha meno yake kama kawaida asubuhi ya siku hiyo, wakati mswaki ulipokwama ghafla kooni mwake.

Mara moja alikimbilia kupata matibabu kwa daktari wa eneo hilo.

Hata hivyo, mswaki huo haukuonekana kwenye picha za eksirei, hali iliyosababisha apelekwe katika hospitali moja mjini Navi Mumbai kwa uchunguzi zaidi.

Uchunguzi wa endoskopi ulithibitisha kuwa mswaki mzima ulikuwa umeingia ndani ya mwili wake.

Timu ya madaktari ikiongozwa na Dkt Raosaheb Rathod, bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na mtaalamu wa endoskopi katika Hospitali ya Medicover, ilifanikiwa kuuondoa mswaki huo kupitia utaratibu maalumu wa kitabibu uliokuwa na changamoto kadhaa.

Brashi hiyo ina urefu wa sentimita 19

d
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Takribani saa tatu hadi nne baada ya kumeza mswaki huo, Malusare alianza kuhisi maumivu tumboni.

Madaktari walipomfanyia uchunguzi wa endoskopi, waligundua kuwa mswaki huo wenye urefu wa sentimita 19 ulikuwa ndani ya tumbo lake.

Kwa mujibu wa madaktari, kuna uwezekano mdogo sana wa vitu virefu na vigumu kama miswaki kupita kwenye mfumo wa chakula na kutoka mwilini vyenyewe.

Vitu vya aina hiyo vinaweza kukwama kooni au katika sehemu nyingine nyembamba za mfumo wa chakula na kusababisha madhara makubwa, yakiwemo majeraha tumboni, kuziba kwa mfumo wa chakula au kutoboka kwa kuta za baadhi ya viungo vya ndani.

Uchunguzi wa endoskopi kwa Malusare ulichukua takribani dakika 30.

Kwa kuwa mswaki ulikuwa umefika tumboni, ilikuwa vigumu kuuondoa salama kupitia njia nyembamba ya koo.

Wakati wa utaratibu huo, mswaki ulikwama katika sehemu inayounganisha koo na tumbo.

Madaktari walilazimika kuwa waangalifu sana walipokuwa wakijaribu kuupitisha katika njia hiyo nyembamba.

Baada ya majaribio kadhaa, hatimaye walifanikiwa kuutoa mswaki mzima kupitia mdomoni bila kumfanyia mgonjwa upasuaji.

Dakika chache baada ya kuuondoa, madaktari walifanya uchunguzi mwingine kuhakikisha kuwa mswaki huo haukusababisha majeraha kwenye koo au sehemu nyingine yoyote ya mfumo wa chakula.

Iliwalazimu kufuatilia hali yake kwa muda, madaktari walithibitisha kuwa afya yake ilikuwa imetengamaa na kumruhusu kurejea nyumbani siku hiyo hiyo.

Katika matukio mengi, husikika taarifa za watu kumeza mifupa ya samaki, watoto wadogo kumeza vitu mbalimbali au sarafu na betri kuingia tumboni mwao.

Hata hivyo, kumeza mswaki mzima ni tukio lisilo la kawaida.

BBC ilimuuliza Dkt Rathod kwa nini picha za eksirei zilizopigwa awali kwa Malusare hazikuonyesha kuwa alikuwa amemeza mswaki.

Alisema:"Vitu vilivyotengenezwa kwa plastiki havionekani vizuri kwenye picha za eksirei. Mifupa na vitu vya metali huonekana, lakini vitu kama mpira mara nyingi havionekani. Kwa hiyo, haiwezekani kuhitimisha kuwa hakuna kitu ndani ya mwili wa mtu kwa kutegemea picha ya eksirei pekee."

Aliongeza: "Ikiwa mgonjwa ana uhakika kuwa amemeza kitu fulani, au anahisi usumbufu mwilini baada ya tukio hilo, anahitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kitabibu. Katika kisa hiki, tulipofanya endoskopi, ambayo hutumia mrija wenye kamera kuchunguza sehemu za ndani za mwili, tuligundua kuwa mswaki ulikuwa umeingia mzima tumboni. Hii ndiyo sababu historia ya mgonjwa na dalili anazozieleza ni muhimu sana katika hali kama hizi.

Changamoto ambazo madaktari walikabiliana nazo kuuondoa mswaki

Buraash

Timu ya madaktari ilikabiliwa na changamoto kadhaa katika juhudi za kuutoa mswaki huo ndani ya mwili wa Malusare.

Madaktari waliweka kifaa maalumu kwenye ncha ya mrija wa endoskopi, ambacho walikitumia kuushika mwisho wa mswaki huo. Hata hivyo, mswaki ulikwama katika sehemu inayounganisha koo na tumbo.

Baada ya kubadilisha mkao wa mgonjwa na kufanya majaribio kadhaa, madaktari hatimaye walifanikiwa kuusogeza mswaki huo mbele.

Hata hivyo, mswaki huo ulikwama tena katika sehemu nyembamba ya koo. Kwa kuwa mswaki hauwezi kujikunja au kupinda kwa urahisi, utaratibu wa kuuondoa ulihitaji umakini na ustadi wa hali ya juu.

Dkt Rathod alisema:

"Baada ya kuutoa mswaki, tulifanya endoskopi nyingine. Safari hii tulichunguza sehemu za juu na chini za koo. Tulithibitisha kuwa hakukuwa na michubuko, kutokwa na damu au uharibifu wowote kwenye kuta za koo, licha ya changamoto tulizokabiliana nazo wakati wa kuutoa mswaki. Uchunguzi haukuonyesha madhara makubwa au majeraha ya hatari."

Aliongeza: "Baada ya hapo, tuliendelea kumfuatilia mgonjwa kwa muda. Tulipothibitisha kuwa hali yake ilikuwa imetengamaa, tulimruhusu kurejea nyumbani ndani ya saa tatu hadi nne."

BBC Marathi pia ilizungumza na Rajendra Malusare ili kufahamu jinsi tukio hilo lilivyotokea.

Alisema: ''Nilipomaliza kusafisha meno yangu, nilikuwa natumia mswaki huo pia kusafisha ulimi. Ndipo mswaki ulipokwama ghafla, kisha ukateleza na kuingia tumboni mwangu.Kwa kuwa koo langu lilikuwa limeumia, nilidhani mswaki ulikuwa umekwama humo. Lakini baadaye niligundua kuwa tayari ulikuwa umefika tumboni."

"Mwanzoni niliogopa kwa sababu nilidhani kuwa mswaki ukikwama ndani ya mwili wangu, huenda ningepata matatizo ya kupumua. Lakini nilikimbilia kwa daktari mara moja. Kwa kuwa sikuweza kupata matibabu Sherawali, nilielekea Kharghar, mjini Navi Mumbai. Nilidhani ningehitaji kufanyiwa upasuaji, lakini nilitibiwa kwa kutumia endoskopi na kuruhusiwa kurejea nyumbani siku hiyo hiyo," aliendelea kuiambia BBC:

Namna ya kuepuka kumeza mswaki

D

Mbali na namna tukio hilo lilivyokuwa la kushangaza, BBC ilimuuliza Dkt Rathod ni funzo gani muhimu ambalo umma unapaswa kujifunza kutokana na tukio hilo.

Alisema: "Jambo muhimu zaidi ni kutokuwa na haraka wakati wa kupiga mswaki. Epuka kuzungumza, kucheka au kufanya shughuli nyingine yoyote huku mswaki ukiwa mdomoni. Pia, kuwa mwangalifu usiingize mswaki ndani sana ya mdomo. Ikiwa mtu atameza mswaki au kitu kingine kikubwa kwa bahati mbaya, anapaswa kwenda hospitalini mara moja."

Dkt Rathod pia alitoa tahadhari muhimu kwa umma:

"Katika hali kama hizi, mtu hapaswi kujaribu kujitapisha au kula chakula kwa lengo la kusukuma kitu kilichokwama kirudi tumboni. Kufanya hivyo kunaweza kujeruhi umio, yaani njia inayopitisha chakula kutoka kooni kwenda tumboni, au kusababisha kitu hicho kukwama zaidi ndani."

Aliongeza:

"Hata kama maumivu yatapungua mwanzoni, bado kuna uwezekano wa kuwepo kwa majeraha ya ndani au matatizo mengine. Kwa hiyo, ni muhimu sana tatizo kutambuliwa mapema na mgonjwa kupata matibabu yanayofaa."