Vilabu vinavyojulikana kwa kuwafukuza makocha mara kwa mara England

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika soka la kisasa, matokeo ya timu yamekuwa kigezo kikuu cha kuamua iwapo kocha ataendelea na kazi au atatimuliwa. Ingawa baadhi ya vilabu huwapa makocha muda wa kujenga timu, vingine havisiti kuachana nao pindi matokeo yanapoanza kuyumba.
Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, baadhi ya vilabu nchini England vimekuwa vikibadilisha makocha mara kwa mara kiasi cha kujijengea sifa ya kuwa sehemu ngumu kwa makocha kufanya kazi.
Wachambuzi wa soka wanasema kuwabadilisha makocha mara kwa mara si lazima kuboreshe matokeo ya timu. Wakati mwingine, hali hiyo huleta matatizo zaidi kwa sababu kila kocha mpya huja na mfumo wake wa uchezaji na anaweza kuhitaji muda na wachezaji wapya kujenga timu.
Hivi ndivyo baadhi ya vilabu vinavyoongoza kwa mabadiliko ya makocha.
Watford: Klabu inayojulikana zaidi kwa kuwafukuza makocha
Linapokuja suala la vilabu vinavyofahamika kwa kuwafukuza makocha, Watford ni miongoni mwa vinavyoongoza kwa sifa hiyo.
Tangu familia ya Pozzo ilipochukua umiliki wa klabu hiyo mwaka 2012, Watford imekuwa ikifanya mabadiliko mengi ya makocha katika kipindi kifupi. Baadhi ya makocha wameondoka kabla hata ya msimu kumalizika.
Miongoni mwa makocha walioiongoza timu hiyo ni Sean Dyche, Gianfranco Zola, Giuseppe Sannino, Oscar Garcia, Billy McKinlay, Slavisa Jokanovic, Quique Sanchez Flores, Walter Mazzarri, Marco Silva, Javi Gracia, Nigel Pearson na Claudio Ranieri.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotajwa, Watford imebadilisha makocha zaidi ya 25 kati ya mwaka 2012 na Oktoba 2026. Kocha wa mwisho kuondoka alikuwa Alessio Dionisi, aliyeiongoza timu hiyo katika mechi 12 pekee kabla ya pande hizo kuachana Oktoba.
Hali hiyo imeifanya Watford kuonekana kuwa miongoni mwa vilabu vinavyofanya mabadiliko ya makocha kwa kasi zaidi nchini England.
Nottingham Forest yaweka rekodi ya mabadiliko ya makocha
Miongoni mwa vilabu vya Ligi Kuu ya England katika kipindi hiki, Nottingham Forest ndiyo iliyofanya mabadiliko mengi zaidi ya makocha tangu mwaka 2000.
Ripoti zinaonyesha kuwa klabu hiyo imefanya mabadiliko 22 ya makocha, matano kati yake yakitokana na makocha kujiuzulu kwa hiari.
Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vilabu vingi vya ligi hiyo na inaonyesha namna viongozi wa Forest walivyokuwa wakitafuta suluhisho la matokeo yasiyoridhisha kwa kubadilisha makocha.
Leeds United na Sunderland
Leeds United na Sunderland zote zimekuwa na zaidi ya makocha 20 tangu mwaka 2000, wakiwemo waliojiuzulu.
Vilabu hivyo vimekabiliwa na changamoto za kushuka daraja kutoka Ligi Kuu na kushindwa kurejea kwa urahisi katika ligi hiyo. Hali hiyo imechangia viongozi wake kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha.
Katika hali nyingi, kocha huajiriwa kwa lengo la kuinusuru timu isishuke daraja au kuiongoza kurejea Ligi Kuu. Matokeo yanapokosekana kwa haraka, viongozi huamua kumtafuta kocha mwingine.
Chelsea na utamaduni wa kukosa subira
Miongoni mwa vilabu vikubwa barani Ulaya, Chelsea ni mojawapo ya vilabu vinavyojulikana kwa kuwabadilisha makocha mara kwa mara.
Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, klabu hiyo ya London imekuwa na makocha wengi, licha ya baadhi yao kuipa mafanikio makubwa.
Hata kutwaa taji hakujamhakikishia kocha kuendelea na kazi Stamford Bridge. Makocha mashuhuri kama Jose Mourinho, Carlo Ancelotti, Thomas Tuchel na Maurizio Sarri wameondoka licha ya kupata mafanikio katika vipindi vyao.
Ripoti zinaonyesha kuwa Chelsea imefanya mabadiliko ya makocha angalau 20 katika kipindi cha Ligi Kuu ya England, yakiwemo yaliyotokana na makubaliano ya pande zote mbili. Hali hiyo inaiweka miongoni mwa vilabu vilivyobadilisha makocha mara nyingi nchini England.
Tottenham na mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha
Licha ya kuwa miongoni mwa vilabu vikubwa nchini England, Tottenham pia imekuwa ikifanya mabadiliko kadhaa ya makocha.
Klabu hiyo imekuwa na zaidi ya makocha 20 katika kipindi cha Ligi Kuu ya England, huku ikiendelea kukabiliwa na changamoto ya kumaliza ukame wa miongo kadhaa bila kutwaa mataji makubwa.
Harry Redknapp, Andre Villas-Boas, Mauricio Pochettino, Jose Mourinho na Antonio Conte ni miongoni mwa makocha walioiongoza timu hiyo katika vipindi tofauti.
Manchester United: Haibadilishi makocha mara nyingi kama inavyodhaniwa
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ingawa mashabiki wa Manchester United mara nyingi hulalamikia mabadiliko ya makocha katika klabu hiyo, takwimu zinaonyesha kuwa haiko miongoni mwa vilabu vinavyofanya hivyo mara nyingi zaidi.
Tangu mwaka 2000, United imefanya mabadiliko saba ya makocha, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na Chelsea, Leeds United, Sunderland na Nottingham Forest.
Hata hivyo, mabadiliko mengi ya makocha katika klabu hiyo yalifanyika baada ya Sir Alex Ferguson kustaafu mwaka 2013.
Makocha walioondoka Manchester United baada ya Ferguson kustaafu
Manchester United imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kurejea katika kiwango chake cha zamani tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson. Katika jitihada za kurejesha mafanikio, klabu hiyo imeachana na makocha kadhaa.
David Moyes (2013 hadi 2014)
Moyes alichaguliwa kuwa mrithi wa Ferguson, lakini alishindwa kuiongoza timu hiyo kufikia malengo yaliyotarajiwa. Alitimuliwa kabla ya kumalizika kwa msimu wake wa kwanza.
Louis van Gaal (2014 hadi 2016)
Van Gaal aliipa United Kombe la FA, lakini mfumo wake wa uchezaji ulikosolewa kwa kutokuwa na mvuto. Hatimaye, klabu iliamua kuachana naye.
Jose Mourinho (2016 hadi 2018)
Mourinho aliipa United mataji ya Europa League na Kombe la Ligi. Hata hivyo, kutokuelewana kwake na viongozi wa klabu pamoja na baadhi ya wachezaji kulisababisha kuondoka kwake.
Ole Gunnar Solskjaer (2018 hadi 2021)
Solskjaer aliiongoza United kufika katika hatua mbalimbali za mashindano ya Ulaya na kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu. Hata hivyo, kushindwa kutwaa taji na matokeo yasiyoridhisha kulisababisha atimuliwe.
Ralf Rangnick (2021 hadi 2022)
Rangnick aliteuliwa kuwa kocha wa muda baada ya Solskjaer kuondoka.
Erik ten Hag
Ten Hag alitwaa mataji akiwa na United, lakini matokeo yasiyokuwa na uthabiti na kukosekana kwa maendeleo yaliyotarajiwa kulizua mjadala kuhusu mustakabali wake kabla ya kuondoka.
Ruben Amorim (2024 hadi 2026)
Amorim aliongoza United katika kipindi hicho kabla ya kuondoka katika klabu hiyo.
Darren Fletcher (5 hadi 12 Januari 2026)
Fletcher aliongoza timu hiyo kwa muda wa siku saba.
Michael Carrick (13 Januari hadi 12 Novemba 2026)
Carrick alichukua jukumu la kuiongoza timu hiyo kuanzia Januari hadi Novemba 2026.
Je, kumfukuza kocha ndiyo suluhisho?

Chanzo cha picha, Getty Images
Historia ya vilabu vingi inaonyesha kuwa kumfukuza kocha si mara zote suluhisho la matatizo ya timu.
Kwa mfano, Arsenal ilimpa Mikel Arteta muda wa kujenga timu licha ya kukabiliwa na matokeo yasiyoridhisha katika miaka yake ya mwanzo. Baadaye, timu hiyo ikawa miongoni mwa zinazowania ubingwa wa Ligi Kuu.
Liverpool nayo ilimpa Jurgen Klopp muda wa kujenga kikosi kilichofanikiwa kutwaa mataji ya Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Ulaya na mashindano mengine makubwa.
Kwa upande mwingine, vilabu vinavyowafukuza makocha mara kwa mara mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya kupata mafanikio ya kudumu. Hii ni kwa sababu kila kocha mpya huja na mfumo wake wa uchezaji na huenda akahitaji wachezaji wapya ili kutekeleza mipango yake.
Watford inaongoza kwa idadi ya mabadiliko ya makocha, huku Chelsea, Nottingham Forest, Leeds United na Sunderland nazo zikiwa na historia ya kufanya mabadiliko ya mara kwa mara.
Licha ya changamoto za Manchester United tangu kustaafu kwa Sir Alex Ferguson, klabu hiyo haimo miongoni mwa vilabu vikubwa vya England vilivyobadilisha makocha mara nyingi zaidi.
Historia inaonyesha kuwa mafanikio ya kudumu hayatokani tu na kumfukuza kocha. Yanahitaji mipango mizuri, uongozi wenye msimamo na uvumilivu wa kumpa kocha muda wa kujenga timu yenye uwezo wa kutwaa mataji.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid































