Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Hukumu ya kuuawa kwa risasi kwa afisa wa zamani wa jeshi la Marekani itarushwa mubashara, Pentagon yasema

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amesema umma utaweza kutazama mubashara kupitia mtandao, hukumu ya kifo kwa kupigwa risasi kwa mtu aliyepatikana na hatia ya mauaji ya watu wengi katika kambi ya kijeshi ya Fort Hood mwaka 2009.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Dinah Gahamanyi

  1. Watu 28 wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi na lori Tanzania

    Watu 28 wamepoteza maisha usiku wa kuamkia leo baada ya basi la abiria kugongana uso kwa uso na gari la mizigo aina ya Scania na kuwaka moto.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, ajali hiyo imetokea usiku wa kuamikia Ijumaa, Oktoba 9,2026 eneo la Mkambarani,mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania.

    Basi lilikuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Mbeya na Lori lilikua limepakia miti.

    ''Ajali hiyo imetokea baada ya lori aina ya Scania kugongana na basi hili na kusababisha vifo na majeruhi na uharibifu wa magari, chanzo ni dereva wa lori kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari eneo lisiloruhusiwa.'' Alisema ACP Kantimbo

    Majeruhi wanatibiwa katika hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

    Katika ajali nyingine iliyotokea eneo la Mvomero, watu wanne, wakiwemo akari polisi watatu, wamefariki dunia baada ya gari la polisi kugongana na lori.

  2. Magari yachomwa moto na maduka kuporwa huku vurugu dhidi ya wahamiaji zikizuka Afrika Kusini

    Takribani magari 24 yamechomwa moto na maduka yanayomilikiwa na raia wa kigeni kuporwa nchini Afrika Kusini baada ya maandamano ya kupinga uhamiaji kugeuka vurugu katika miji miwili mikubwa, polisi wamesema.

    Mapigano yalizuka Alhamisi katika eneo la Soweto, kitongoji kikubwa nje ya Johannesburg, jiji kubwa zaidi nchini humo, na pia katika mji wa bandari wa Durban ulioko pwani ya mashariki.

    Vurugu hizo zimekuja wakati kukiwa na ongezeko la hasira kufuatia uamuzi wa mahakama ulioitaka serikali kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinawazuia baadhi ya wahamiaji kuwasilisha maombi ya hifadhi ya ukimbizi.

    Afrika Kusini imekumbwa mara kadhaa na matukio ya vurugu dhidi ya wageni, ambapo wahamiaji kutoka nchi jirani wamekuwa walengwa wakuu wa mashambulizi hayo.

    Katika mji wa Durban, ulioko katika jimbo la KwaZulu-Natal mashariki mwa Afrika Kusini, waandamanaji walikusanyika nje ya kituo cha serikali cha kupokea wakimbizi wakidai kisitishe kupokea maombi mapya ya hifadhi kutoka kwa raia wa kigeni.

    Maandamano hayo ya Alhamisi yaligeuka kuwa ya vurugu baada ya madai kwamba raia mmoja wa kigeni alimshambulia mmoja wa waandamanaji.

    Polisi walisema raia watatu wa kigeni walikamatwa kuhusiana na tukio hilo la madai ya shambulio.

    Waandamanaji walieleza wasiwasi wao kuhusu idadi ya wahamiaji na waomba hifadhi wanaoingia nchini, huku wakitaka mamlaka kuchukua hatua kali zaidi kuhusu mfumo wa kupokea wakimbizi na waomba hifadhi.

    Mamlaka zimeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo, huku zikitoa wito wa utulivu na kuheshimu sheria wakati wa kushughulikia masuala yanayohusiana na uhamiaji na wakimbizi.

    Unaweza kusoma;

  3. Kiongozi wa zamani wa Venezuela Nicolás Maduro ashtakiwa kwa kula njama za kutekeleza mateso

    Waendesha mashtaka nchini Marekani wamemshtaki aliyekuwa kiongozi wa Venezuela, Nicolás Maduro, na mkewe, Cilia Flores, kwa kosa la kula njama za kutekeleza mateso dhidi ya watu waliokuwa wakizuiliwa nchini Venezuela.

    Mashtaka hayo mapya yalitangazwa hadharani siku ya Alhamisi.

    Yanakuja baada ya mashtaka ya awali yanayohusiana na biashara ya dawa za kulevya na makosa ya silaha, ambayo wote wameyakanusha.

    Maduro, mwenye umri wa miaka 63, na Flores, mwenye miaka 69, wanashikiliwa tangu Januari katika kituo cha mahabusu cha Brooklyn, mjini New York.

    Walipelekwa huko baada ya vikosi vya Marekani kuwakamata katika uvamizi wa alfajiri kwenye makazi yao mjini Caracas, mji mkuu wa Venezuela.

    Wakili wa Maduro, Barry J. Pollack, amesema mteja wake anayakana mashtaka hayo mapya na anasubiri kwa shauku kupata fursa ya kujitetea mahakamani.

    Waendesha mashtaka wa Marekani pia walitangaza kuwa Flores ameongezewa kwenye shtaka la awali la ugaidi unaohusishwa na biashara ya dawa za kulevya.

    Kesi dhidi ya Maduro na Flores imepangwa kuanza kusikilizwa mwezi Juni 2027.

    Wote wawili wanaendelea kushikiliwa katika kituo cha mahabusu cha Brooklyn, baada ya ombi la Flores la kuhamishiwa kifungo cha nyumbani kukataliwa na jaji siku ya Alhamisi.

    Mashtaka hayo mapya yanahusiana na madai ya kuwatesa raia wa Marekani waliokuwa wanazuiliwa nchini Venezuela wakati Nicolás Maduro alipokuwa madarakani.

    Unaweza kusoma;

  4. Wanadiplomasia wengi wa Uingereza kuondoka ubalozi mdogo wa Jerusalem Mashariki, Israel yasema

    Israel imesema wanadiplomasia wengi wataondoka katika ubalozi mdogo wa Uingereza ulioko Mashariki mwa Jerusalem inayokaliwa, lakini Uingereza imesisitiza kuwa jengo hilo "halitafungwa" na litaendelea kufanya kazi kama "Ujumbe wa Uingereza".

    "Tusingependa mambo yafikie hatua hii," aliandika Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, kwenye mitandao ya kijamii. Alisema wanadiplomasia 20 pamoja na balozi mkuu wataondoka, huku kikosi kazi cha watu saba kikiruhusiwa kubaki ndani ya jengo hilo kwa shughuli zenye mipaka maalum.

    Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband, alisema baadhi ya wafanyakazi wameondolewa kwa muda kutokana na sababu za kiusalama, na kusisitiza kwamba ujumbe huo utaendelea na "kazi yetu na watu wa Palestina".

    Mnamo Septemba, Israel ilitangaza kuwa ingeufunga ubalozi huo mdogo kama hatua ya kulipiza kisasi baada ya Uingereza kuweka vikwazo dhidi ya makazi ya walowezi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, ambayo yanachukuliwa kuwa kinyume cha sheria za kimataifa.

    Hatua hizi mpya zinaonekana kupunguza hatari ya mgogoro wa kidiplomasia kati ya washirika hao wawili kuongezeka zaidi.

    Ubalozi mdogo wa Uingereza, ulioanzishwa mwaka 1838, unasimamia mahusiano ya Uingereza na Wapalestina wa Jerusalem, pamoja na wale wa Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

    Ubalozi huo ni tofauti na Ubalozi wa Uingereza mjini Tel Aviv, ambao ndio kituo kikuu cha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Uingereza na Israel na haujaathiriwa na hatua hizo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel alisema agizo la kufunga ubalozi huo lilipaswa kutekelezwa ndani ya siku 30, likiwa moja ya hatua kadhaa zilizotangazwa tarehe 8 Septemba kujibu vikwazo vya Uingereza dhidi ya makazi ya walowezi wa Israel katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa.

    Unaweza kusoma;

  5. Takribani watu 30 wauawa kwa shambulio la Urusi dhidi ya mabasi Ukraine

    Maafisa wa uokoaji wamesema kuwa watu wasiopungua 30 wameuawa baada ya mabomu ya kurushwa kutoka anga ya Urusi kushambulia mabasi mawili ya kiraia katika mji wa mstari wa mbele wa Kramatorsk mashariki mwa Ukraine.

    Mamlaka pia zimeripoti kuwa watu watatu waliuawa katika kijiji cha Bilenke, ambacho ni sehemu ya jamii ya Kramatorsk.

    Watu wengine 18 walijeruhiwa, kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Donetsk, Vadym Filashkin, ambaye aliishutumu Urusi kwa kulenga mabasi yaliyokuwa yakisafirisha abiria kwa nia ya kuua raia wengi iwezekanavyo.

    Miji ya Kramatorsk na jirani yake Slovyansk ni sehemu ya eneo linalojulikana kama ukanda wa ngome ("fortress belt"), ambao Urusi inajaribu kuuteka kama sehemu ya madai ya Rais Vladimir Putin ya kuyadhibiti maeneo yote ya viwanda ya Donbas nchini Ukraine.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema:

    "Shambulio hili halitapita bila jibu letu."

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye Telegram, Zelensky alisema:

    "Urusi inajaribu kuharibu maisha yote katika Donbas, na dunia inapaswa kuchukua hatua kuhusu hili. Ichukue hatua kali, sawa na kile ambacho Warusi wanastahili kutokana na vifo vyote walivyosababisha."

    Picha zilizochapishwa na waendesha mashtaka wa eneo hilo zilionyesha mabaki ya basi lililokuwa likiwaka moto, vipande vya mabaki ya mlipuko na baadhi ya waathirika barabarani.

    Hadi sasa, Urusi haijatoa maoni kuhusu shambulio hilo la karibuni. Tukio hilo linafuatia ongezeko kubwa la mashambulizi ya Urusi katika maeneo mbalimbali ya Ukraine pamoja na kuongezeka kwa idadi ya raia wanaouawa na kujeruhiwa.

    Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), kufikia mwezi Agosti mwaka huu, idadi ya raia waliouawa nchini Ukraine ilikuwa tayari imezidi jumla ya waliouawa katika mwaka mzima wa 2025.

    Katika shambulio moja lililotokea mapema Jumatano katika mji wa Pryluky, mashariki mwa Kyiv, jengo la ghorofa tano liliharibiwa na watu 22 kuuawa, wakiwemo watoto watano. Watatu kati ya watoto hao walikuwa na umri wa mwaka mmoja tu.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Ed Miliband, ambaye pamoja na Volodymyr Zelensky walitembelea eneo la shambulio hilo la Urusi mjini Pryluky, alisema tukio hilo linaonesha "nia ovu na mkakati ovu" wa Vladimir Putin.

    Miliband alitangaza kuwa Uingereza itaweka vikwazo zaidi dhidi ya Urusi, vikilenga meli zinazotumika kukwepa vikwazo , kampuni za mafuta, miamala ya sarafu za kidijitali (crypto) na vyanzo vya ufadhili wa vita.

    Pia alimwambia Zelensky kuwa Uingereza itaendelea kusimama pamoja na Ukraine:

    "Kwa muda wowote utakaohitajika hadi mtakaposhinda katika mzozo huu."

    Kauli hiyo inaonesha kuendelea kwa uungwaji mkono wa Uingereza kwa Ukraine wakati vita kati ya Ukraine na Urusi vikiendelea na idadi ya vifo vya raia kuongezeka.

    Unaweza kusoma;

  6. Adidas yaishtaki White Fox kuhusu mtindo wa mistari minne kwenye bidhaa zake

    Kampuni ya mavazi ya michezo ya Adidas imefungua kesi dhidi ya kampuni ya mitindo ya Australia, White Fox, kwa madai ya kuuza na kutangaza nguo zenye mistari minne ambayo inadai inafanana kwa namna inayoweza kuchanganya na nembo yake maarufu ya mistari mitatu.

    Adidas imesema kuwa imekuwa ikiiomba mara kwa mara White Fox tangu mwezi Machi kusitisha uuzaji na matangazo ya bidhaa hizo, lakini kampuni hiyo yenye makao yake mjini Sydney imekataa kufanya hivyo.

    Muuzaji huyo wa mtandaoni wa bidhaa za mitindo ya haraka anapendwa sana na vijana nchini Australia, Uingereza na Marekani.

    Umaarufu wake umeongezeka kupitia mabango ya matangazo, matangazo kwenye mabasi na matumizi ya washawishi wa mitandao ya kijamii, wengi wao wakiwa katika umri wa vyuo vikuu.

    Katika Mahakama ya Shirikisho ya Australia siku ya Ijumaa, mawakili wa White Fox walikanusha madai yoyote ya ukiukaji wa alama ya biashara.

    Ingawa kampuni hiyo bado haijawasilisha utetezi wake rasmi, mawakili wake waliiambia mahakama mbele ya Jaji Ian Jackman kwamba wanakusudia kuhoji madai ya Adidas kwa kueleza kuwa kampuni nyingine maarufu za Australia kama Cotton On, Sportscraft na Glassons pia huuza nguo zenye mistari ya mapambo inayofanana.

    Kwa upande wake, mawakili wa Adidas waliiambia mahakama kuwa White Fox, kupitia matangazo na mauzo ya nguo zake zenye mistari minne, imekuwa na "nia ya kunufaika na sifa na umaarufu wa chapa yetu".

    Mahakama ilielezwa kuwa usikilizwaji wa kesi hiyo unatarajiwa kudumu kati ya siku tatu na nne mwanzoni mwa mwaka ujao.

    Katika hati yake ya madai, Adidas imesema kuwa muundo wake wa mistari mitatu una "sifa kubwa na thamani kubwa ya kibiashara" nchini Australia, ambako umesajiliwa kama alama ya biashara tangu mwaka 1957.

    Kampuni hiyo inadai kuwa tangu angalau mwezi Machi, White Fox imekuwa ikiuza na kutangaza nguo zenye mistari minne sambamba yenye upana sawa, jambo ambalo Adidas inasema ni ukiukaji wa alama yake ya biashara.

    Kwa mujibu wa madai ya Adidas, miundo ya White Fox ni "karibu kufanana kabisa au inafanana kwa kiwango kinachoweza kuwapotosha watumiaji" wakadhani kuwa bidhaa hizo zina uhusiano na chapa ya Adidas.

    Adidas inasisitiza kuwa muundo wake wa mistari mitatu ni alama ya biashara iliyo na sifa kubwa na inayotambulika kwa muda mrefu, hivyo matumizi ya mistari minne na White Fox inaweza kusababisha mkanganyiko miongoni mwa wateja na kunufaika isivyo halali kutokana na umaarufu wa chapa hiyo.

  7. Tetesi za soka Ijumaa: Real Madrid wanamuwania McTominay

    Real Madrid wanafuatilia kwa karibu mazungumzo ya kuongeza mkataba wa kiungo wa Scotland mwenye umri wa miaka 29, Scott McTominay, wa Napoli. Klabu hiyo ya Uhispania inaonesha nia ya kumsajili mwishoni mwa msimu.

    Manchester United hawana uwezekano mkubwa wa kumrudisha McTominay katika uwanja wa Old Trafford kwani wanalenga kusajili wachezaji wenye umri mdogo zaidi.

    Bayern Munich wanataka kuongeza mkataba wa winga wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 24, Michael Olise, ambao kwa sasa unaendelea hadi mwaka 2029. Inaaminika ataendelea kubaki Ujerumani isipokuwa Real Madrid watatoa ofa rasmi.

    Manchester United wamempa kiungo mshambuliaji mwenye miaka 16, JJ Gabriel, ofa rasmi ya mkataba wa udhamini. Hata hivyo, klabu hiyo inaweza kupata fidia ya pauni 350,000 pekee endapo mchezaji huyo ataamua kuondoka na kujiunga na klabu ya nje ya England.

    Chelsea wanavutiwa na huduma za kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi, Frenkie de Jong (29), kama mbadala wa muda mrefu wa Enzo Fernandez, ambaye alihamia Manchester City siku ya mwisho ya dirisha la usajili.

    Liverpool wana kipengele cha kumrejesha beki wa Bayer Leverkusen, Jarell Quansah (23), kwa pauni milioni 59.5. Hata hivyo, mchezaji huyo wa England, anayehusishwa pia na Real Madrid na Chelsea, anaripotiwa kutokuwa na mapango wa kurejea Anfield.

    Juventus wana mashaka kuhusu mshambuliaji wa Ujerumani mwenye miaka 24, Nick Woltemade, ambaye yuko kwa mkopo Newcastle United. Kutokana na hali hiyo, mabingwa hao wa Italia wanatazama mbadala wake, akiwemo mshambuliaji wa Monaco na timu ya taifa ya Marekani, Folarin Balogun (25).

    Newcastle United na Everton zote zinamuwania kiungo wa Galatasaray, Gabriel Sara. Mbrazil huyo mwenye miaka 27 aliwahi kuitumikia Norwich City kwa misimu miwili kabla ya kuhamia Uturuki.

    Hull City wako karibu kukamilisha usajili wa mlinda lango mwenye miaka 18, Deniz Donmezer, kutoka Kayserispor ya Uturuki kwa ada inayokadiriwa kuwa pauni milioni 1.5.

    Unaweza kusoma;

  8. Hukumu ya kuuawa kwa risasi kwa afisa wa zamani wa jeshi la Marekani itarushwa mubashara, Pentagon yasema

    Umma utaweza kushuhudia utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa njia ya kikosi cha risasi dhidi ya aliyekuwa meja wa Jeshi la Marekani, amesema Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth.

    Afisa wa Idara ya Ulinzi ya Marekani ameiambia BBC kuwa utekelezaji wa hukumu dhidi ya Nidal Hasan, ambaye aliwaua wanajeshi 13 wasio na silaha katika shambulio la Fort Hood mwaka 2009, utarushwa mubashara.

    Inaaminika kuwa huu unaweza kuwa utekelezaji wa kwanza wa hukumu ya kifo unaorushwa hadharani nchini Marekani katika karibu karne moja.

    Mwanasheria John Mills, ambaye hufanya kazi na wafungwa waliohukumiwa kifo, amesema uamuzi wa kurusha mubashara tukio hilo ni "wa kipekee katika enzi za kisasa" na unafanyika katika mazingira yenye maswali ya kisheria.

    "Tutahakikisha watu wanaweza kushuhudia, na kwamba utekelezaji huo unakuwa wa wazi kwa umma," alisema Pete Hegseth.

    "Pia watu wanapaswa kuelewa kuwa matendo ya aina hii yana madhara na adhabu kubwa."

    Mapema wiki hii, Pentagon ilitangaza kuwa itamtekelezea Nidal Hasan hukumu ya kifo, utekelezaji wa kwanza wa kijeshi nchini Marekani kwa zaidi ya miaka 60.

    Pete Hegseth alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha kihafidhina cha Real America's Voice kwamba Nidal Hasan "atapokea adhabu ya kifo kwa kupigwa risasi na kikosi cha wanajeshi. Ndivyo inavyopaswa kuwa."

    Alipoulizwa iwapo Nidal Hasan alikuwa ametoa ombi lolote la mwisho au kuwasiliana na Rais Donald Trump, Pete Hegseth alijibu:

    "Sijali. Tutakutana naye tarehe 3 Desemba."

    Msemaji wa Pentagon, Sean Parnell, alisema siku ya Jumatatu kwamba Pete Hegseth alikuwa ametoa pendekezo la utekelezaji wa hukumu hiyo kwa njia ya kikosi cha risasi, na kwamba Rais Donald Trump aliidhinisha uamuzi huo

  9. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo