VAR, kupoteza muda na uingizaji wa wachezaji wa akiba - Sheria mpya kwa msimu mpya

Chanzo cha picha, Getty Images
Msimu wa 2026-27 utashuhudia idadi kubwa ya sheria mpya, ambazo nyingi zinalenga kushughulikia suala la kuvurugwa kwa kasi ya mchezo na kuufanya mchezo huo uwe wa kasi zaidi.
Sheria hizi zote zilianza kutumika katika Kombe la Dunia, lakini bado zilisababisha mkanganyiko katika raundi ya kwanza ya Kombe la Carabao wikendi iliyopita.
Mabadiliko haya yalianza kutatekelezwa katika nyanja zote za soka la Uingereza kuanzia ligi ya EFL na mechi ya Community Shield ya Jumapili iliopita kati ya Arsenal na Manchester City, hadi Ligi Kuu (Premier League) na ligi za ngazi za chini, bila shaka isipokuwa mfumo wa mwamuzi msaidizi wa video (VAR).
Lengo ni kuondoa matukio yanayowakera sana mashabiki na kuongeza muda wa mchezo kuendelea bila kuhitaji kuongeza muda mwingi wa nyongeza (stoppage time).
Mbinu hii ilifanya kazi vizuri katika Kombe la Dunia. Nchini Qatar mwaka 2022, mpira ulichezwa kwa wastani wa dakika 58 na sekunde 3, sawa na asilimia 56.86 ya muda wote wa mechi. Katika msimu huu wa joto, muda huo ulikuwa dakika 58 na sekunde 16, lakini muda wa nyongeza ulikuwa mfupi zaidi, ikimaanisha kuwa mpira ulichezwa kwa asilimia 60.43 ya muda wa mechi.
Mabadiliko haya yanalenga kubadili tabia za wachezaji, badala ya kutumika kama adhabu kali.
Hata hivyo, yanaweza kuonekana kuwa na athari hasi kwa timu zilizokuwa zikitumia mbinu za hila kupoteza muda ili kulinda matokeo.
Hapa kuna mambo unayopaswa kufuatilia na jinsi sheria hizo mpya zitakavyofanya kazi.
Hesabu za muda kwa ajili ya mikwaju ya goli na kurusha mpira

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hii inawahusu wachezaji wanaochelewesha makusudi kuanza tena kwa mchezo, ili muda wa kuhesabu usianze mara tu mpira unapotoka nje.
Mbinu yoyote inayoweza kuonekana kuvuruga mchezo ikiwemo kuacha mpira juu ya koni na kuudondosha ili mwenza wa timu auchukue—inaweza kusababisha kuanza kwa muda wa kuhesabu.
Mwamuzi atapuliza filimbi kumtaka mchezaji aharakishe na kuashiria kuanza kwa sekunde hizo tano, huku akionyesha waziwazi hesabu hiyo kwa kusogeza mkono juu na chini.
Muda huo ukimalizika, mwamuzi atapuliza filimbi tena na kuipa timu pinzani haki ya kurusha mpira.
Kanuni hiyo mpya haitahusu maandalizi ya kurusha mipira mirefu, kwani hayo huchukuliwa kuwa ni mipango maalum ya uchezaji (set-pieces).
Hata hivyo, muda wa kuhesabu unaweza kuanza mara tu wachezaji wanapokuwa katika nafasi zao.
Na kama njia ya kuwazuia makipa wanaotumia muda mrefu kupiga mipira ya goli (goal-kicks) kuelekea mwisho wa mchezo, sasa mwamuzi anaweza kuipa timu pinzani kona badala yake iwapo kipa atachelewa kupiga mpira mbele.
Uingizaji wa wachezaji na kutoka kwao uwanjani
Wachezaji wanaotolewa uwanjani wana sekunde 10 za kuondoka kupitia sehemu iliyo karibu zaidi.
Wakishindwa kufanya hivyo, mchezaji anayepaswa kuingia kuchukua nafasi yao haruhusiwi kuingia uwanjani kwa angalau dakika moja, na timu hulazimika kuendelea kucheza ikiwa na wachezaji 10.
Will Lankshear wa Middlesbrough ndiye aliyekuwa wa kwanza kuadhibiwa kwa utaratibu huu katika mchezo wa Kombe la Carabao dhidi ya Wrexham.
Wakati Boro ikiongoza kwa bao 1-0 katika dakika ya 80 kupitia kwa Lankshear, mshambuliaji huyo alitoka uwanjani kwa mwendo wa taratibu huku akiwapungia mikono na kuwashukuru mashabiki.
Kocha wa Boro, Kim Hellberg, alimtaka Lankshear kuharakisha, lakini alitumia muda mrefu sana, na hivyo mchezaji wa akiba Fin Cartwright akaambiwa hawezi kuingia uwanjani mara moja.
"Sikujua!" alisema mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham baada ya mchezo kumalizika.
Mchezaji wa akiba anapaswa kusubiri nje hadi mchezo utakapositishwa tena, jambo linaloweza kuifanya timu ibaki na wachezaji 10 kwa dakika kadhaa.
Kuna hali chache za kipekee, kama vile mchezaji anapokuwa ameumia au kuwepo kwa hofu ya kiusalama kuhusu sehemu anayopaswa kutokea.
Wachezaji waliojeruhiwa sasa lazima watoke nje ya uwanja kwa dakika moja
Mashabiki walikuwa wamezoea kuona wachezaji wakikaa nje ya uwanja kwa sekunde 30 baada ya mtaalamu wa tiba ya michezo kuingia uwanjani kuwapa huduma.
Sasa muda huo umeongezwa hadi dakika moja. Na utaratibu huo pia ni mkali zaidi.
Mchezaji lazima atoke nje ikiwa atasababisha mwamuzi kusimamisha mchezo, hata kama hataomba matibabu.
Hii ni ili kuzuia wachezaji kutumia mbinu hiyo kuvuruga kasi au mdundo wa mchezo wa timu pinzani.
Sheria hii haitatumika ikiwa mchezaji ameanguka na mpira ukatoka nje wenyewe, kwa mfano kwa ajili ya kurusha mpira au kupiga 'goal-kick'.
Kuna wasiwasi kwamba dakika moja ni muda mrefu sana, kwani inaweza kuwaadhibu wachezaji ambao wamejeruhiwa kweli.
Kuna hali chache za kipekee ambapo sheria hii haitatumika.
Ikiwa mchezaji aliyecheza rafu ataonyeshwa kadi ya njano au nyekundu, basi mchezaji aliyejeruhiwa hatalazimika kukaa nje katika hali zote.
Hii inapunguza uwezekano wa kutumia rafu za kimkakati ili kuifanya timu pinzani ibaki na wachezaji 10 uwanjani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, hakutakuwa tena na mapumziko ya kimkakati ya kipa?
'Mapumziko ya kimkakati ya kipa' yamekuwa mada moto katika misimu ya hivi karibuni.
Mbinu hii hutumiwa na kocha ili kuwapa wachezaji wake maelekezo mapya, au kuvuruga kasi ya mchezo ya timu pinzani.
Kipa hukaa chini uwanjani na kuashiria kuhitaji huduma ya matibabu, huku wachezaji wengine wakikimbilia eneo la benchi la ufundi kwa ajili ya mazungumzo ya timu.
Mara tu kocha anapomaliza kutoa maelekezo, kipa huinuka na kuendelea na mchezo.
Ligi na mashindano yote ya soka la kulipwa nchini Uingereza zitaanza majaribio mapya kwa lengo la kuondoa tabia hii.
Iwapo kipa ataomba huduma ya matibabu, mchezaji wa uwanjani (asiye kipa) atakayechaguliwa na kocha atalazimika kutoka nje ya uwanja kwa dakika moja.
Kuna muda wa sekunde 10 wa kumjulisha mwamuzi wa akiba ni nani anayetoka nje; vinginevyo, nahodha atalazimika kufanya hivyo.
Kuwakataza tu wachezaji kwenda kando ya uwanja (eneo la benchi la ufundi) hakutawazuia makocha kutumia mbinu hiyo ya mapumziko ya kipa kuvuruga kasi ya timu pinzani.
Nchi nyingine zinafanya majaribio tofauti kidogo ambapo nahodha wa timu ya kipa husika ndiye anayelazimika kutoka nje ya uwanja kila mara.
Kuna vighairi sawa na vile vinavyotumika kwa wachezaji wa uwanjani, ikiwa ni pamoja na hali ambapo kipa amefanyiwa madhambi au anavuja damu.
Jambo la kuzingatia - kugusa mpira kwa mkono ndani ya eneo hatari
Katika soka la kisasa, kuna mwelekeo wa kuanzisha mpira wa goli kwa pasi fupi ndani ya eneo la hatari badala ya kuupiga mbali.
Mara nyingi utaratibu huu huhusisha beki mmoja au wawili ndani ya eneo la penalti, pamoja na kipa.
Kumekuwa na matukio machache ya utata ambapo haikuwa wazi kama mpira wa goli ulikuwa tayari umepigwa, na kisha beki akaugusa mpira huo kwa mkono.
Tyrone Mings wa Aston Villa alijikuta katika matatizo wakati wa mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Club Brugge mnamo Novemba 2024, ambapo timu yake iliadhibiwa kwa penalti baada ya yeye kuugusa mpira kwa mkono kufuatia pasi fupi kutoka kwa kipa Emiliano Martinez.
Hata hivyo, Gabriel wa Arsenal hakuadhibiwa alipougusa mpira kwa mkono katika mechi dhidi ya Bayern Munich mapema mwaka huo, baada ya David Raya kumpasia mpira huo.
Kuanzia msimu huu, kutakuwa na utaratibu mmoja thabiti unaotumika katika mashindano yote.
Sasa, iwapo mpira utapigwa na kipa au beki, mpira huo wa goli utachukuliwa kuwa tayari umepigwa.
Mguso wowote wa mpira kwa mkono au mkono wa juu (arm) unaofanywa na beki utahesabiwa kuwa ni penalti, au mpira wa adhabu usio wa moja kwa moja (indirect free-kick) iwapo mguso huo utafanywa na kipa kufuatia pasi ya kurudishiwa mpira (backpass).
Mambo zaidi kuhusu VAR!
Kuna maeneo mapya kadhaa ya matumizi ya VAR ambayo mashabiki wanapaswa kuyafahamu - ingawa si mengi kama ilivyokuwa kwenye Kombe la Dunia.
Wachezaji kutolewa uwanjani kwa kadi mbili za njano: VAR itaweza kupitia upya tukio la kadi ya pili ya njano kwa wachezaji walioonyeshwa kadi nyekundu.
Hakutakuwa na mapitio ya matukio yanayoweza kusababisha kadi ya pili ya njano kwa wachezaji ambao tayari wana kadi ya njano.
Lazima kuwe na makosa ya wazi ili kutoa uamuzi wa faulo, na siyo tu tofauti ya maoni binafsi kuhusu kadi husika.
Faulo ya upande wa mashambulizi kabla ya mpira kuanza kuchezwa: Kama sehemu ya majaribio, VAR inaweza kupitia upya tukio iwapo kutatokea faulo kabla ya mpira uliokufa (kama vile kona au faulo) na tukio hilo likasababisha moja kwa moja bao, penalti au adhabu ya kinidhamu.
Mchezo utaanza upya kwa kurudiwa kwa kona hiyo. Mantiki ni kwamba faulo haiwezi kutolewa ikiwa mpira hauko katika hali ya kuchezwa.
VAR haitaweza kupitia upya faulo za upande wa ulinzi kabla ya mpira kuanza kuchezwa kwa sababu haiwezekani kutoa penalti katika hali hiyo.
Kukosea utambulisho wa mchezaji: Wakati wa Kombe la Dunia, VAR iliingilia kati matukio ya kujidondosha (simulation). Hata hivyo, bodi ya sheria za soka (IFAB) imesisitiza kuwa hiyo sio tafsiri sahihi ya mabadiliko ya sheria.
Sheria hiyo inapaswa kutumika tu pale mwamuzi anapoiadhibu Timu A kwa kosa la mpira kugusa mkono, ilhali kosa hilo lilifanywa na mchezaji wa Timu B.
Mambo yasiyobadilika: Tofauti na ilivyokuwa kwenye Kombe la Dunia, hakutakuwa na uingiliaji kati wa VAR katika maamuzi yasiyo sahihi ya kona au kadi nyekundu kwa wachezaji wanaofunika midomo yao wakati wa mabishano au makabiliano.













