Waziri wa Ulinzi wa Ukraine aliyefukuzwa kazi aitisha uchaguzi wa urais

Chanzo cha picha, Reuters
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Mykhailo Fedorov, ametoa wito wa kufanyika kwa uchaguzi wakati wa vita, hatua ambayo wengi wanaiona kuwa changamoto kubwa zaidi kwa uongozi wa Rais Volodymyr Zelensky tangu vita dhidi ya Urusi vilipoanza mwezi Februari 2022.
"Demokrasia haiwezi kushikiliwa mateka na Urusi," alisema Fedorov, aliye na umri wa miaka 35, katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa YouTube siku ya Jumanne, akiongeza kuwa Ukraine inapigana "hasa kwa sababu tunataka kubaki kuwa taifa huru la Ulaya".
Tangu Urusi Iilipoanza uvamizi wake, Ukraine imekuwa chini ya sheria za kijeshi, hali iliyosababisha uchaguzi kusimamishwa.
Fedorov, ambaye hakumtaja Zelensky moja kwa moja katika video hiyo, aliondolewa ghafla katika wadhifa wake wa Waziri wa Ulinzi mwishoni mwa mwezi Julai, miezi sita tu baada ya kuteuliwa.
Zelensky bado hajatoa tamko lolote kuhusiana na video hiyo ya Fedorov, ambaye kufutwa kwake kazi kulichochea maandamano makubwa.
Fedorov alisifiwa kwa kuimarisha wizara hiyo, kuongoza juhudi za kupambana na ufisadi, na kutumia takwimu kuchambua na kujaribu kuboresha utendaji kaziwakati wa vita.
Inasadikiwa kuwa kufutwa kwake kulitokana na mvutano kati yake na kamanda mkuu wa jeshi, Oleksandr Syrskyi.
Katika video hiyo ya YouTube, Fedorov hakuelezea mipango yake ya kisiasa, badala yake alijikita katika umuhimu wa kuwepo kwa "utaratibu halali, salama na unaotekelezeka ambao utaiwezesha Ukraine kurejesha mchakato kamili wa kidemokrasia hata katikati ya vita vinavyoendelea kwa muda mrefu".
Fedorov ndiye mwanasiasa wa kwanza kigogo kuitisha uchaguzi mkuu ambapo kulingana na sheria za Ukraine,ni marufuku kuandaa uchaguzi wakati wa vita.
Pia unaweza kusoma:
























