'Mwaka mmoja bila Polepole umekuwa mgumu sana'- Familia

Polepole
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Imetimia mwaka mmoja tangu aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba na mkosoaji wa serikali, Humphrey Polepole, kutoweka katika mazingira ambayo bado hayajafahamika. Familia yake inaamini alitekwa na watu wasiojulikana.

Kaka yake, Godfrey Polepole, ameiambia BBC kuwa familia imekuwa ikipitia kipindi kigumu tangu kutoweka kwa ndugu yao, huku juhudi za kumtafuta zikigonga mwamba.

Familia hiyo inasema haijapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa mamlaka za Tanzania na inaishutumu serikali kwa kuhusika na kutoweka kwake, madai ambayo serikali imekuwa ikiyakanusha mara kwa mara.

"Maisha bila ndugu yetu Humphrey yamekuwa magumu sana kwetu. Sisi ndugu zake, watoto wake na hasa mama yetu tumepitia kipindi cha maumivu makubwa," amesema Godfrey.

Anasema mama yao ameathirika zaidi na tukio hilo.

"Mama amekuwa akikesha usiku akihangaika kuwaza alipo mtoto wake. Hali hiyo imemsababishia msongo wa mawazo, na wakati mwingine hupoteza fahamu. Kwa umri alionao sasa, inakuwa vigumu kwake kuelewa kilichompata mwanawe au kwa nini hajarejea nyumbani."

Godfrey amesema kuwa katika kipindi chote cha mwaka mmoja tangu kutoweka kwa Humphrey Polepole, familia haijawahi kupewa taarifa yoyote rasmi kutoka kwa mamlaka kuhusu maendeleo ya uchunguzi.

"Nilijaribu mara kadhaa kuwasiliana na mamlaka mbalimbali, wakiwemo viongozi wa Jeshi la Polisi na maafisa wa wizara husika. Nilifanikiwa kuzungumza nao mara moja, lakini baadaye simu zangu hazikupokelewa tena," amesema.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ameeleza pia kuwa kutoweka kwa kaka yake kumeiacha familia katika maswali mengi yasiyo na majibu, huku baadhi ya masuala na misimamo aliyokuwa akiitetea akiendelea nayo kabla ya kutoweka kwake bado hayajapatiwa ufumbuzi.

Polepole alijiuzulu nafasi ya ubalozi na kuvuliwa rasmi hadhi ya ubalozi kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi wake na Rais Samia Suluhu Hassan.

Uamuzi wake ulifuatia kile alichoeleza kutoridhishwa na mwenendo wa mambo mbalimbali nchini Tanzania akidai hawezi kuwa sehemu ya serikali isiyojali misingi ya haki, sheria na katiba ya nchi.

Hata baada ya kujiuzulu na kuvuliwa hadhi ya ubalozi, Polepole aliendeleza harakati zake za ukosoaji wa serikali na chama tawala nchini Tanzania CCM.

Pamoja na masuala mengine Polepole alikosoa utaratibu uliotumika kumteua Samia na Dkt Emmanuel Nchimbi kuwa wagombea wa urais na Makamu wa rais katika uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Oktoba 29.

"Uchaguzi ule ulikiuka desturi ya CCM inayokifanya chama kuendelea kuwa imara" alisema Polepole.

Haikupita muda, Polepole akaendelea kuporomosha tuhuma moja baada ya nyingine huku akiwataja bayana watu mbalimbali, baadhi yao mashuhuri kwa tuhuma za ufisadi na kujinufaisha na fedha umma kinyume cha taratibu.

Kwa namna ya pekee alikuwa gumzo kwelikweli mtandaoni. Wapo waliompongeza kwa dhati kwa ujasiri wake, pia wapo waliomponda, kumbeza na kumbagaza wakidai hakuwa na hadhi ya kuzungumzia aliyoyaweka hadharani maana alikuwa sehemu ya CCM wakati wa rais Magufuli, na sehemu ya serikali wakati wa Rais Samia. Baadhi ya waliotuhumiwa walijibu pia.

Humphrey Polepole ni nani?

Humphrey Polepole amekuwa mwanasiasa maarufu kwa takriban miaka 10 kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Malawi mwaka 2022. Baada ya kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu alifanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiseikali na kufanya kazi kwa karibu na taasi za vijana ukiwemo Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alianza kujulikana zaidi kwa umma mwaka 2012 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba mpya, iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba na kumaliza kazi yake mwaka 2014.

Mwaka 2016 Rais John Magufuli alimteua Polepole kuwa Mkuu wa wilaya ya Musoma, mkoani Mara, alikohudumu kwa miezi michache kisha kuhamishiwa Ubungo Dar es Salaam kwa nafasi hiyo hiyo ya ukuu wa wilaya na kuhudumu kwa miezi michache pia.

Umaarufu wake uliongezeka alipoteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, nafasi ambayo kimsingi ni ya kuwa msemaji wa chama hicho kinachotawala Tanzania.

Anafahamika kwa kutetea sera na utendaji wa CCM na serikali ya Rais Magufuli, hata pale kulipokuwa na utata mkubwa wa masuala kama vile tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji, kuwaweka watuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu na wengine kufunguliwa kesi nzito za uhujumu uchumi na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020.

Polepole

Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19, 2021, Polepole hakukaa kwa muda mrefu kwenye nafasi ya usemaji, kwani aliondolewa kisha kuteuliwa kuwa Mbunge kabla ya kuteuliwa balozi nchini Malawi.

Anajulikana pia kwa kauli tata au kuhusu ahadi za CCM na serikali ambazo hazikuwahi kutekelezwa, kama vile ujenzi wa barabara za juu (fly overs) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa barabara za juu zimejengwa nne pekee katika maeneo ya Ubungo, Tazara, Chang'ombe na makutano ya barabara za Mandela na Kilwa. Maeneo kama vile Mwenge na Morocco Barabara hizo bado hazipo.

Wakati fulani baada ya kuondolewa kwenye usemaji wa CCM aliwahi kunukuliwa kwenye mahojiano akisema CCM kumejaa watu wahuni wanaofanya matendo mabaya kama fitina, zengwe na uchawi, dhidi ya watu 'walionyooka' kama yeye na kudai hawezi kupatwa na uchawi hata shetani anamuogopa.

Tangu alipojiuzulu ubalozi na nyadhifa nyingine za umma barua aliyomwandikia Rais Samia Suluhu Hassan na kutaja sababu za kufanya hivyo, kumetokea masuala kadhaa.

Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Amos Makalla alizungumzia hatua hiyo siku ileile ya Julai 13 na kusema endapo Polepole angethibitisha iwapo barua ile ya kujiuzulu ni ya kwake maudhui ni ya kwake ni utashi wake lakini ambalo lilimfurahisha ni kwamba amemalizia kwa kusema atabaki kuwa mwanachama muadilifu wa CCM.

Pamoja na masuala mengine Polepole alikosoa utaratibu uliotumika kumteua Samia na Dkt Emmanuel Nchimbi kuwa wagombea wa urais na Makamu wa rais katika uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Oktoba 29.

"Uchaguzi ule ulikiuka desturi ya CCM inayokifanya chama kuendelea kuwa imara" alisema Polepole.

Haikupita muda, Polepole akaendelea kuporomosha tuhuma moja baada ya nyingine huku akiwataja bayana watu mbalimbali, baadhi yao mashuhuri kwa tuhuma za ufisadi na kujinufaisha na fedha umma kinyume cha taratibu.

Kabala ya kutoweka kwake katika njia ya kutatanisha Polepole kwa namna ya pekee alikuwa gumzo kwelikweli mtandaoni. Wapo waliompongeza kwa dhati kwa ujasiri wake, pia wapo waliomponda, kumbeza na kumbagaza wakidai hakuwa na hadhi ya kuzungumzia aliyoyaweka hadharani maana alikuwa sehemu ya CCM wakati wa rais Magufuli, na sehemu ya serikali wakati wa Rais Samia.