Mataifa saba yanayolipa mshahara mkubwa zaidi Afrika

- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Ripoti ya hivi karibuni ya LiveGDP imebainisha tofauti kubwa za viwango vya mishahara miongoni mwa mataifa ya Afrika, huku Djibouti ikiongoza kwa wastani wa juu zaidi wa mshahara wa kila mwezi unaobaki mikononi mwa mfanyakazi baada ya makato ya kodi na michango mingine ya lazima.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, viwango vya mishahara hutofautiana kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo kiwango cha maendeleo ya uchumi, uzalishaji wa wafanyakazi, nguvu ya sekta muhimu kama mafuta, madini, utalii na huduma za kifedha, pamoja na mahitaji ya soko la ajira. Mambo mengine yanayoathiri mapato ya wafanyakazi ni pamoja na viwango vya kodi, mfumuko wa bei, thamani ya sarafu na mazingira ya ajira katika kila nchi.
Katika ripoti hiyo, Kenya imeorodheshwa katika nafasi ya 10 kati ya mataifa 54 ya Afrika kwa wastani wa mshahara wa kila mwezi baada ya makato. Takwimu zinaonyesha kuwa mfanyakazi nchini Kenya hupokea wastani wa shilingi 44,553 (dola 344 za Marekani) kwa mwezi baada ya makato, kiwango kinachoiweka nchi katika nafasi ya 132 duniani.
"Kenya ina wastani wa mshahara wa dola 344 kwa mwezi baada ya makato na inashika nafasi ya 10 barani Afrika," ripoti hiyo ilisema.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kenya iliwapiku majirani zake Tanzania, Uganda na Rwanda, lakini ikabaki nyuma ya Djibouti, ambayo ndiyo iliyoongoza sio Afrika Mashariki pekee bali pia bara zima kwa wastani wa dola 2,836 kwa mwezi.
Hata hivyo, LiveGDP inaonya kuwa takwimu za mishahara pekee haziwezi kutumika kupima moja kwa moja ubora wa maisha au uwezo wa kununua bidhaa na huduma, kwani gharama za makazi, chakula, usafiri, afya, elimu na mfumuko wa bei hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.
Ifuatayo ni orodha ya mataifa saba bora ya Afrika yenye mishahara ya juu zaidi
1. Djibouti
Djibouti inaongoza Afrika kwa wastani wa mshahara wa kila mwezi unaobaki baada ya makato, ukiwa takriban KSh 367,311 (USD 2,836). Taifa hilo lipo katika lango la Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, karibu na moja ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za usafiri wa majini duniani. Hali hiyo imeifanya kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji wa mizigo na huduma za bandari.
Nafasi yake ya kimkakati katika njia za biashara za Bahari ya Shamu na uwepo wa kambi za kijeshi za kimataifa umechangia ukuaji wa uchumi wake.
2. Afrika Kusini
Afrika Kusini inashika nafasi ya pili kwa wastani wa mshahara wa KSh 164,486 (USD 1,270). Ikiwa ni moja ya uchumi mkubwa zaidi barani, taifa hilo lina sekta zilizoendelea za madini, fedha, viwanda na huduma.
3. Ushelisheli
Ushelisheli inafuatia kwa mshahara wa wastani wa KSh 102,318 (USD 790). Uchumi wake unategemea zaidi utalii, uvuvi na huduma za kifedha, huku idadi ndogo ya watu ikichangia kiwango cha juu cha mapato kwa kila mtu.
4. Mauritius
Mauritius ni miongoni mwa nchi zenye mishahara ya juu Afrika kutokana na uchumi wake uliotofautishwa unaojumuisha utalii, huduma za kifedha, teknolojia na viwanda vya nguo. Taifa hilo pia linajulikana kwa mazingira mazuri ya biashara.
5. Gabon
Gabon inanufaika na utajiri mkubwa wa mafuta na maliasili nyingine. Licha ya idadi ndogo ya watu, mapato yatokanayo na sekta ya mafuta yameifanya kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya mishahara barani.
6. Botswana
Botswana imejijengea sifa ya utulivu wa kisiasa na usimamizi mzuri wa mapato ya madini ya almasi. Sekta ya madini imekuwa nguzo muhimu inayosaidia viwango vya mishahara kubaki juu ikilinganishwa na mataifa mengi ya Afrika.
7. Namibia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Namibia inafunga orodha ya nchi saba bora kwa mishahara ya juu. Uchumi wake unategemea madini, uvuvi na utalii, huku viwango vya mishahara vikisaidiwa na idadi ndogo ya watu na sekta rasmi iliyoimarika.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, Kenya ilishika nafasi ya 10 Afrika, ikiwa na wastani wa mshahara wa KSh 44,553 (USD 344) kwa mwezi baada ya makato. Hii inaifanya kuwa juu ya nchi nyingi za Afrika Mashariki, zikiwemo Tanzania, Uganda na Rwanda.
Sudan Kusini ilirekodi kiwango cha chini zaidi kwa wastani wa shilingi 9,066 (dola 70), ikifuatiwa na Burundi kwa shilingi 9,713 (dola 75), Sierra Leone kwa shilingi 10,361 (dola 80), Gambia kwa shilingi 11,008 (dola 85), na Malawi pamoja na Sudan kwa shilingi 11,656 (dola 90) mtawalio.
Hata hivyo, LiveGDP ilionya kuwa takwimu za mishahara pekee haziwezi kutumika kupima moja kwa moja kiwango cha maisha. Gharama za makazi, chakula, usafiri, afya, elimu, mfumuko wa bei na thamani ya sarafu hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.
Kwa hivyo, orodha hiyo inaonyesha kiwango cha mapato yanayobaki mikononi mwa wafanyakazi baada ya makato, lakini sio kigezo kamili cha uwezo wa kununua bidhaa au ubora wa maisha katika kila nchi.


































