Kwa nini Marekani iliziondoa kwa ghafla ndege zake za kurusha mabomu kutoka Uingereza?

Chanzo cha picha, Reuters
Hatua ya ghafla na ya kina ya kuondolewa kwa ndege nzito za Marekani zenye uwezo wa kubeba mabomu siku ya Jumapili ilikuja kwa kasi kiasi cha kuacha kila mtu akijiuliza ni nini kilichosababisha hatua hiyo.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alisema kuwa kuondolewa kwa ndege hizo kulifanywa kwa kuzingatia "tahadhari kubwa," akiongeza kuwa Washington inaamini Iran inaendelea kufanya yale yale ambayo imekuwa ikifanya kwa "miaka 49: kutekeleza vitendo vya ugaidi dhidi ya Marekani na watu wengine wengi."
Hata hivyo, baadhi ya watu wameitafsiri hatua hiyo si kama "tahadhari kubwa," bali kama "hofu kubwa."
Kwa miezi saba iliyopita, ndege za Marekani aina ya B-1 Lancer na ndege nyingine zimekuwa zikiruka kutoka Farford ili kushambulia maeneo ya Iran yanayotumika kurushia makombora.
Mwezi Julai, Iran ilitoa tishio kwamba nchi yoyote itakayoipatia Marekani uwezo huo ingechukuliwa kuwa "shabaha halali" ya kushambuliwa.
Kisha, mnamo Septemba 27, hali ya hatari ilitangazwa baada ya wanaume watano wa Uingereza kukamatwa na baadaye kuachiliwa kwa dhamana baada ya kuonekana wakifanya tabia ya kutiliwa shaka katika magari yao matatu meupe katikati ya usiku karibu na uzio wa kambi ya anga.
Wikendi iliyopita, raia wa Uingereza na Iran mwenye uraia pacha alikamatwa kwa tuhuma za kuandaa vitendo vya kigaidi. Baadaye aliachiliwa kwa dhamana.
Sasa, ndege 12 muhimu za kimkakati za B-1 zimeondoka kwenye kambi hiyo kwa wingi, inaonekana kwa haraka sana kiasi kwamba ndege za angani za kujaza mafuta ambazo zilitakiwa kuzirudisha kwenye kambi zao kwenye bara la Marekani ziliripotiwa bado zikijaza mafuta juu ya Bahari ya Atlantiki, huku wanajeshi i wa ndege za B-1 Lancer wakiamriwa kujiandaa kwa kupaa mara moja.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa hivyo, inaonekana suala hilo limeonekana kuwa la dharura na hatari kiasi kwamba hatua kama hiyo imekuwa muhimu.
Ni karibu hakika kwamba uamuzi huu ulifanywa baada ya kupokea taarifa mpya za kiusalama, bila kujali kama taarifa hizo zilikuwa sahihi au la.
Maafisa wa Uingereza walikataa kutoa maelezo zaidi, lakini walisema: "Iran inaendelea kuwa tishio kubwa na endelevu kwa Uingereza, na ni jambo la kimantiki kwamba vituo vya anga vya Marekani vingekuwa mstari wa mbele katika orodha ya shabaha zinazoweza kushambuliwa."
Iran imekanusha kuhusika na matukio yaliyotokea katika Kituo cha Jeshi la Anga la Uingereza (Royal Air Force Base), na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amepunguza uzito wa madai yoyote yanayohusisha ule uokoaji wa haraka na ukamataji uliofanyika tarehe 27 Septemba.
Hali halisi ni kwamba, ingawa Uingereza haiko vitani na Iran, Marekani iko vitani nayo tofauti ambayo Tehran imepinga waziwazi. Kwa mtazamo wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Uingereza tayari imekuwa upande mmoja katika vita vya Marekani dhidi ya Iran.
Wakati huo huo, masuala ya kifedha pia yamekuwa na mchango wake katika uamuzi huo.
Ndege za kivita aina ya B-1 Lancer ambazo sasa zimeondoka kituoni hapo zina thamani ya takriban dola milioni 330 kila moja.
Marekani imewahi kupata hasara kubwa ya kifedha hapo awali kufuatia mashambulizi ya Iran dhidi ya vituo vyake katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mwishoni mwa mwezi wa Machi, Iran ilishambulia Kituo cha Jeshi la Anga cha Prince Sultan nchini Saudi Arabia na kuharibu ndege ya mfumo wa onyo la mapema na udhibiti wa angani (AWACS) aina ya A-3 Sentry.
Ndege hiyo pekee ilikuwa na thamani ya zaidi ya nusu bilioni ya dola.
"Sasa tunaishi katika ulimwengu ambapo ndege isiyo na rubani (drone) yenye thamani ya dola 1,000 inaweza kuharibu mojawapo ya ndege hizi," alisema Jenerali Richard Barons, ambaye aliwahi kuhudumu katika ngazi za juu kabisa za jeshi la Uingereza.
"Kwa hivyo, sijui tishio hilo lilikuwa lipi, lakini kwa kuzingatia kuwa ndege hizi hazikuwa na shughuli nyingi wakati huo, hatua ya busara zaidi ilikuwa kuzihamishia Texas," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Lakini je, hatua ya Marekani kuamuru ndege zake za kivita aina ya 'bomber' kuondoka katika Kituo cha Jeshi la Anga la Uingereza (RAF) cha Fairford inaashiria nini kuhusu imani ya Washington katika uwezo wa Uingereza wa kulinda kituo hicho?
Uingereza bado ni mmoja wa washirika wa karibu zaidi wa Marekani, na mamia ya wanajeshi wa Marekani bado wapo katika vituo vya RAF Fairford, pamoja na vile vya Mildenhall na Claxton.
Inawezekana kwamba, bila kuonekana hadharani, ukaguzi wa kiusalama unaendelea pande zote mbili za uzio unaozunguka kituo hicho.
Hata hivyo, ni vigumu kutohitimisha kuwa, licha ya jitihada za kupunguza uzito wa tukio hilo, lilikuwa ni jambo la aibu kwa Uingereza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema Marekani "ina imani na usalama wa vituo vyetu vyote" na kuongeza kuwa serikali ya Marekani inashirikiana "kwa karibu sana" na mamlaka za Uingereza, ambazo alisema zimeonyesha "ushirikiano mkubwa sana".
Polisi wa Uingereza wanaoshughulikia masuala ya kukabiliana na ugaidi bado wanachunguza matukio hayo katika kituo cha RAF Fairford na bado hawajatupilia mbali nadharia yoyote kuhusu chanzo cha matukio hayo.
Nimeambiwa kuwa wakati watu hao wakiwa huru kwa dhamana, maafisa bado wanachunguza kiasi kikubwa cha data, picha za CCTV na taarifa nyingine.
Wakati huo huo, Marekani inasisitiza kuwa sasa, baada ya ndege hizo kuondoka katika ardhi ya Uingereza, inaweza kuzipeleka kutoka katika vituo vyake vilivyo ndani ya Marekani hadi sehemu yoyote duniani.
Lakini kauli hizi zinaweza kuonekana kama jaribio la kupunguza uzito wa hali ambayo, kwa mtazamo wa Iran, imefanikiwa kurudisha nguvu kubwa ya mashambulizi ya Marekani kwenye vituo vyake vilivyo katika ardhi kuu ya Marekani.

































