Jinsi Donald Trump anavyoisaidia China kuimarika zaidi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Donald Trump aliingia madarakani akiahidi "kuifanya Marekani kuwa kubwa tena". Hata hivyo, wakati mjadala ukiendelea kuhusu kiwango ambacho ametimiza ahadi hiyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kuna taifa moja ambalo huenda limenufaika zaidi na mwelekeo wa sera zake za kigeni: China.

Beijing, ambayo kwa muda mrefu imekuwa mshindani mkuu wa Washington katika mbio za ushawishi wa kimataifa, imejikuta ikipata manufaa ambayo hayakutarajiwa kutokana na hatua mbalimbali za utawala wa Trump.

Mwanzoni, vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vilionekana kuiweka Beijing katika nafasi ya kujihami. Hata hivyo, kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi, China baadaye ilifanikiwa kutumia hali hiyo kuimarisha mahusiano yake ya kiuchumi na washirika wengine na kujionyesha kama mtetezi wa utulivu katika biashara ya kimataifa.

Kwa upande mwingine, mzozo wa kijeshi kati ya Marekani na Iran umefungua mazingira mapya ya kisiasa katika Mashariki ya Kati. Wakati Washington ikijikuta ikitumia rasilimali na umakini mkubwa katika eneo hilo, China imeendelea kupanua ushawishi wake wa kidiplomasia na kiuchumi, hasa kupitia uwekezaji, biashara ya nishati na ushirikiano wa kimkakati na mataifa ya Ghuba.

Matokeo yake, baadhi ya wataalamu wanaona kuwa ushindani kati ya Marekani na China haujaishia kwenye masuala ya biashara pekee, bali umehamia pia katika uwanja mpana wa diplomasia na ushawishi wa kimataifa, ambapo Beijing inaonekana kupata nafasi ya kuimarisha hadhi yake kama nguvu mbadala katika mfumo wa dunia unaobadilika.

Hili lilifanyika vipi?

China haishiriki katika mzozo wa sasa wa Ghuba, lakini wataalamu kadhaa wakuu wa Marekani wanaamini kuwa inajitokeza kama mshindi. Wachambuzi wa China kwa kawaida huwa waangalifu zaidi katika tathmini zao (maelezo zaidi hapa chini).

Wamarekani wanaeleza kuwa Donald Trump alianza mzozo huo bila tahadhari, akasababisha mgogoro mkubwa wa nishati na kuibua mashaka kuhusu utayari na uwezo wa Marekani wa kuwalinda washirika wake.

"Marafiki na wapinzani kwa pamoja wanakubali kwamba Marekani inazidi kufanana na taifa lisilofuata sheria za kimataifa (rogue state), likiwa tishio kwa utulivu na utaratibu wa dunia, na kuzidi kuwa chanzo cha dhihaka," anasema mwanasayansi wa siasa na mwanafalsafa wa Marekani, Francis Fukuyama, ambaye ni mmoja wa wataalamu wakuu wa Magharibi kuhusu demokrasia, utawala, na utaratibu wa dunia.

"Chini ya uongozi wa Trump, Marekani imekuwa ikijidhuru yenyewe mara kwa mara kiasi kwamba China haihitaji kufanya lolote," anaandika.

Shambulio dhidi ya Iran na vita vya kibiashara vya Trump vimeigeuza Marekani kuwa nguvu isiyotabirika na yenye kuharibu, na moja kwa moja kuifanya China ya kikomunisti, taifa la pili kwa nguvu ya kiuchumi na kijeshi duniani, kuwa nguzo ya utulivu na sera madhubuti.

"Kwa mtazamo wa Beijing, Washington inahujumu taratibu misingi ya nguvu zake yenyewe, ikigombana na washirika wake, na kuufanya ulimwengu mzima kugeuka dhidi yake," anabainisha Julian Gewirtz, aliyekuwa mshauri kuhusu masuala ya China katika Baraza la Usalama wa Taifa na Wizara ya Mambo ya Nje chini ya utawala wa Joe Biden.

"Matokeo yake, nchi nyingi zinaanza kuona kuwa ni rahisi na kuna uhakika zaidi kufanya mazungumzo na China kuliko na Marekani, ambayo inazidi kujali maslahi yake yenyewe pekee," anaandika Gewirtz, ambaye kwa sasa ni mtaalamu katika Chuo Kikuu cha Columbia.

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vimesababisha uharibifu wa kijeshi na kiuchumi kwa washirika wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi na kote duniani. Wakati huo huo, China imeibuka kama nguvu inayochangia utulivu.

Wataalamu kutoka mpango wa Mashariki ya Kati wa taasisi ya Carnegie Endowment (ambayo nchini Urusi imeorodheshwa kama "wakala wa kigeni") wanaona kuwa faida kuu ya China ni kutokuwa na maadui wa wazi katika eneo hilo. "Tofauti na Marekani, Beijing inadumisha uhusiano wa kirafiki na kila upande, ikiwemo Israel, ambayo ni mshirika mkuu wa Washington," wanaandika.

"Pengo la ushawishi wa kidiplomasia kati ya Marekani na China linazidi kupungua. China inaendelea kujenga nguvu yake ya ushawishi wa kidiplomasia na kiutamaduni (soft power), huku Marekani ikidhoofisha nafasi yake yenyewe, ikitumia migogoro ya kijeshi mara kwa mara, na kuifanya diplomasia kuwa na nafasi ndogo zaidi katika siasa za Mashariki ya Kati," wanaamini.

Jinsi Marekani inavyopoteza nafasi yake kwa China

"Hii ni sura mpya katika siasa za kimataifa. Hapo awali, matatizo yalipojitokeza katika soko la mafuta, hatua ya kwanza ambayo rais wa Marekani angechukua ilikuwa kupiga simu Riyadh na kuiomba Saudi Arabia kuongeza mauzo ya mafuta nje ya nchi," alisema mtaalamu mkuu wa masuala ya mafuta wa Bloomberg, Javier Blas.

"Sasa inawezekana wakapiga simu Beijing kwanza na kuwaomba kupunguza uagizaji wa mafuta," alisema. "Hii ni mabadiliko ya kuvutia sana. Inavutia sana kuona ni athari gani za kisiasa jambo hili litakalokuwa nazo kwa Marekani."

Kulingana na Blas, China ilionyesha nguvu yake katika sekta ya mafuta kwa sababu mbili.

China haihitaji mgogoro wa kimataifa kwa sababu uchumi wake unategemea sana mauzo ya bidhaa nje ya nchi, na mgogoro ungewanyima fedha wanunuzi wa bidhaa hizo za Kichina.

Mtazamo kutoka China

Licha ya kufaidika na mabadiliko ya sasa ya kisiasa katika Mashariki ya Kati, China inaonekana kuchukua tahadhari na kuepuka kusherehekea mapema kile ambacho baadhi ya wachambuzi wanakitafsiri kama kupungua kwa ushawishi wa Marekani katika eneo hilo.

Profesa Wang Jin, mmoja wa wataalamu mashuhuri wa masuala ya Mashariki ya Kati nchini China kutoka Chuo Kikuu cha Northwest mjini Xi'an, anaonya dhidi ya hitimisho la haraka kwamba China imeibuka mshindi huku Marekani ikionekana kupoteza nafasi yake.

Katika makala aliyoiandika kwenye jarida la The Diplomat, Wang anasema hali ya sasa ni ngumu zaidi kuliko inavyoonekana.

"Hali hii haipaswi kurahisishwa kwa hitimisho kwamba Marekani imeshindwa na China imeshinda," anaandika. "Badala yake, Mashariki ya Kati inaingia katika kipindi kipya cha mabadiliko ambacho kinaweza kuleta changamoto mpya kwa China, huku Marekani ikipata fursa mpya za kimkakati."

Licha ya kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Beijing na nchi kadhaa za Ghuba, ushawishi wa kijeshi wa Washington bado una uzito mkubwa katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Wang, mataifa tajiri ya Mashariki ya Kati yanaendelea kutegemea teknolojia na mifumo ya ulinzi ya Marekani, hasa wakati ambapo hofu kuhusu makombora na ndege zisizo na rubani za Iran imeongeza mahitaji ya silaha za kisasa.

Anasema kuwa nchi kama Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain bado hazina mbadala wa kweli wa Marekani kama mshirika wao mkuu wa masuala ya usalama na ulinzi, jambo linaloonyesha kuwa ushawishi wa Washington katika eneo hilo unaendelea kuwa muhimu licha ya ushindani unaoongezeka kutoka China.

Imetafsiriwa na Abdalla Dzungu na kuhaririwana Ambia Hirsi