Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nchi 10 bora za kutembelea kabla hazijafurika watalii 2027
Si lazima tukushawishi kutembelea New York au Venice.Lakini vipi unafahamu kuwa mojawapo ya visiwa vilivyoko mbali zaidi duniani sasa vinaalika watalii wenye hamasa ya ugunduzi ili kutembelea fukwe zake?
Mnamo mwaka 2027, wasafiri nchini Japan wataweza kushuhudia ibada ya kale inayofanyika mara moja tu katika kila kizazi?
Tunaangazia maeneo bora ya kutembelea 2027. Ni yale yanayopendwa kuliko yaliyozoeleka kila mara, tukilenga sehemu zenye upekee katika mwaka ujao.
Kila eneo linakupa uzoefu usiosahaulika pamoja na fursa za kuleta mabadiliko chanya kwa watu na mazingira yanayofanya maeneo hayo kuwa ya kipekee.
1. Madagascar
Kwa nini utembelee?
Utapata fursa ya kushuhudia wanyamapori wa kipekee walio hatarini kutoweka huku ukichangia juhudi za uhifadhi wao.
Ikiwa na asilimia 92 ya mamalia wake wasiopatikana sehemu nyingine yoyote duniani, Madagascar ni moja ya maeneo bora zaidi kwa utalii wa wanyamapori.
Kinyonga aina ya Panther Chameleon na lemur anayejulikana kwa jina la Verreaux's sifaka, ni miongoni mwa viumbe wa kipekee wanaopatikana katika misitu ya mvua, korongo za mawe ya mchanga na mandhari zinazofanana na ulimwengu mwingine.
Wakati nchi hiyo ikitarajia kuongeza idadi ya watalii mara tatu ndani ya miaka miwili ijayo, utalii unaowajibika unaweza kusaidia kulinda maeneo yake ya asili pamoja na karibu spishi 10,000 za mimea na wanyama wanaopatikana Madagascar pekee.
Mwaka 2027, Hifadhi ya Mitsinjo itakamilisha mradi wake mkubwa wa kupanda miti katika eneo la hekta 150, hatua itakayosaidia kurejesha makazi ya lemur, fossa na aina mbalimbali za reptilia.
Katika Hifadhi ya Jamii ya Anja, mapato yatokanayo na ada za wageni hutumika kufadhili huduma za afya na miradi ya elimu. Sarah Faith wa kampuni ya Responsible Travel anasema: "Hifadhi hii ina mkusanyiko mkubwa zaidi duniani wa lemur wenye mikia ya mistari (ring-tailed lemurs), na ni rahisi sana kuwaona."
Wageni wanaweza kukaa katika Anja Reserve Lodge, ambako watapata vyumba vya kisasa pamoja na chakula kinachotayarishwa kwa kutumia mazao ya eneo hilo, huku wakifurahia mwonekano wa kuvutia wa milima ya Three Sisters.
2. Jiji la Quebec, Canada
Quebec, mji mkuu wa Canada unaozungumza Kifaransa, unajulikana kwa barabara zake za mawe na mandhari ya kuvutia kandokando ya Mto St. Lawrence.
Wageni huvutiwa na haiba yake ya kihistoria, lakini pia hupata fursa ya kufanya shughuli za nje kama vile kuteleza kwenye theluji katika bustani ya Plains of Abraham.
Juhudi zake katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu zimeifanya Quebec kuwa mji wa kwanza duniani kutambuliwa kwa ujumla wake kama Hifadhi ya Bayosfia ya UNESCO (UNESCO Biosphere Reserve).
Eneo la ufukweni limefanyiwa maboresho makubwa, likijumuisha L'Oasis du Port de Quebec, eneo la kwanza la kuogelea bandarini katikati ya jiji huko Amerika Kaskazini.
Pia, kuanzia Desemba 2026, wageni wataweza kufurahia sauna ya kisasa inayoelea majini.
Mbali na urithi wa kikoloni, wageni wanaweza kutembelea jamii ya asili ya Huron-Wendat huko Wendake, ambako hupata fursa ya kujifunza historia na simulizi za mababu kupitia njia ya msituni ya Onhwa' Lumina, yenye maonesho ya picha na mwanga yanayoelezea tamaduni zao.
3. Rasi ya Ise-Shima, Japan
Ise-Shima ni eneo la pwani ya vijijini nchini Japan ambapo utapata uzoefu wa kipekee wa utamaduni wa baharini uliofungamana na zaidi ya miaka 2,000 ya imani ya Kishinto.
Tofauti na miji maarufu ya Tokyo, Kyoto na Osaka, eneo hili huwapa wageni nafasi ya kuona maisha ya jadi ya Kijapani.
Rasi hiyo ina ghuba za asili, misitu minene, hekalu takatifu zaidi la dini ya Shinto nchini Japan.
Mwaka 2027, wageni watapata fursa adimu ya kushuhudia sherehe ya kale ya Okihiki, inayofanyika mara moja kila baada ya miaka 20.
Katika sherehe hiyo yenye historia ya zaidi ya miaka 1,300, wakazi hubeba magogo makubwa kwa mikono ili kujenga upya majengo ya hekalu.
Maelfu ya washiriki waliovalia mavazi meupe ya jadi huandamana mitaani huku wakiimba, wakisherehekea urithi, ustadi wa kazi na matumizi endelevu ya rasilimali.
4. St Helena
Kisiwa cha St Helena, kilichopo katikati ya bahari ya Atlantiki, ni moja ya maeneo ya mbali zaidi duniani.
Licha ya uzuri wake wa asili, hakina idadi kubwa ya hoteli za kimataifa wala migahawa maarufu ya vyakula vya haraka.
Kwa miaka mingi, wageni wengi walifika kwa njia ya bahari, lakini tangu mwaka 2017 safari za ndege kutoka Johannesburg zimeanza kurahisisha usafiri.
Wageni huvutiwa na mandhari ya volkano, historia ya Napoleon Bonaparte na mji mkuu wa Jamestown, uliojazwa majengo ya mtindo wa Georgia ndani ya bonde la volkano.
Mwaka 2027, kisiwa hicho kitakuwa mwenyeji wa St Helena Adventure Week, tukio litakalowakutanisha wapenda matembezi ya milimani na kuogelea baharini.
Tamasha hilo litahitimishwa kwa mbio za riadha za vijijini zitakazofanyika Februari 28.
Kwa wakazi wapatao 4,000, utalii si tu chanzo cha mapato bali pia njia ya kusaidia uchumi wa eneo hilo na kuzuia vijana kuhama ili kutafuta ajira.
Serikali inakuza utalii kwa tahadhari ili kulinda mazingira na maisha ya jamii ya kisiwa hicho.
5. Salvador, Brazil
Salvador ni mji wa pwani uliopo kati ya Ghuba ya All Saints na Bahari ya Atlantiki, unaojulikana kwa mandhari yake ya kuvutia, ukarimu wa wakazi na utamaduni wenye mizizi mikubwa ya Kiafrika.
Mji huu uliwahi kuwa mji mkuu wa kwanza wa Brazil na kituo muhimu cha biashara ya watumwa kupitia Bahari ya Atlantiki.
Urithi wa Waafrika unaonekana wazi katika muziki, dini, sanaa na tamaduni za mji huo.
Wageni wanaweza kushuhudia mchezo wa jadi wa capoeira au kuonja acarajé, chakula maarufu cha mitaani chenye asili katika ibada za dini ya Candomblé.
Mwaka 2027, Salvador itakuwa moja ya miji mwenyeji wa Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA, mashindano yatakayofanyika kwa mara ya kwanza kabisa Amerika Kusini.
Tukio hilo linatarajiwa kuongeza umaarufu wa mji huo duniani.
Mbali na michezo, wageni wanaweza kutembelea eneo la kihistoria la Pelourinho, lililotambuliwa na UNESCO kutokana na mitaa yake ya mawe, majengo ya kikoloni na makanisa ya mtindo wa Baroque.
Pia wanaweza kutembelea MUNCAB, makumbusho yenye moja ya makusanyo bora zaidi ya sanaa ya Waafrika walioko Brazil.
6. Okefenokee Swamp, Marekani
Okefenokee Swamp ni eneo linapatikana Amerika Kaskazini, likiwa na mazingira ya asili ambayo yamebakia karibu bila mabadiliko makubwa kwa zaidi ya miaka 6,500.
Eneo hilo, linalopakana na majimbo ya Georgia na Florida, lina njia za maji zinazopita katikati ya misitu ya mikaratusi, visiwa vidogo na mimea ya majini.
Eneo hilo lenye maji na miti ya asili ni makazi ya mamia ya mamba pamoja na ndege wa aina mbalimbali, hali inayovifanya kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi kwa utalii wa mazingira nchini Marekani.
Kusafiri kwa mtumbwi katika eneo hilo huonekana kama safari ya kurudi nyuma katika historia ya asili.
Mwaka 2026, sehemu ya Okefenokee ilitambuliwa na UNESCO kama Urithi wa Dunia, ikiwa ni eneo la kwanza la asili nchini Marekani kupata hadhi hiyo katika zaidi ya miaka 30.
Hatua hiyo imeimarisha ulinzi wa mazingira hayo dhidi ya miradi ya uchimbaji madini ambayo ilitishia mfumo wake wa ikolojia.
Wageni wanaweza kushiriki ziara zinazoongozwa na wataalamu wa mazingira au kutembea wenyewe kupitia njia maalumu za mbao.
Eneo hilo pia linafaa kwa shughuli za kutazama ndege, kupiga makasia na kujifunza kuhusu viumbe wa porini katika mazingira yao ya asili.
7. Burgundy, Ufaransa
Burgundy ni eneo maarufu la Ufaransa linalojulikana kwa mashamba yake ya mizabibu, vijiji vya kihistoria na haradali maarufu duniani.
Mwaka 2027, eneo hilo litapata umuhimu wa ziada kutokana na maadhimisho ya miaka 200 ya upigaji picha nchini Ufaransa, kwa kuwa linahusishwa na chimbuko la sanaa hiyo.
Wageni wanaweza kuanza safari yao katika jumba la makumbusho la Musée Nicéphore Niépce mjini Chalon-sur-Saône, ambako picha ya zamani zaidi duniani iliyohifadhiwa itaonyeshwa katika maonesho maalumu.
Karibu na hapo, Saint-Loup-de-Varennes ndiko Nicéphore Niépce alipotengeneza picha hiyo ya kihistoria miaka 200 iliyopita.
Mji wa Dijon unatoa fursa ya kutembelea mitaa ya kale, masoko ya kihistoria na vivutio vya kitamaduni.
Kutoka hapo, wasafiri wanaweza kufuata njia maarufu ya Route des Grands Crus, inayopita katika maeneo ya mashamba ya mizabibu yaliyotambuliwa na UNESCO.
Njiani, wageni watakutana na makanisa ya kale, migahawa ya jadi na wazalishaji wa familia wanaoendeleza urithi wa vyakula na mvinyo wa Burgundy.
8. Meghalaya, India
Meghalaya, jimbo la kaskazini mashariki mwa India, linajulikana kwa madaraja ya kipekee yaliyotengenezwa kwa mizizi hai ya miti, misitu mitakatifu na jamii za asili za Khasi na Jaintia ambazo zimeishi kwa maelewano na mazingira kwa karne nyingi.
Mwaka 2027, eneo hilo linatarajiwa kuwa moja ya vituo vinavyoongoza vya utalii wa kijamii nchini India.
Serikali inaunga mkono uanzishwaji na uboreshaji wa nyumba za wageni 1,000 ili kuhakikisha mapato ya utalii yanawanufaisha wenyeji moja kwa moja.
Wageni wanaweza kushiriki matembezi ya asili, kujifunza ufumaji na utengenezaji wa kazi za mikono, pamoja na kuonja vyakula vya kienyeji vinavyotegemea mazao ya ndani na mimea inayokusanywa kutoka porini, ikiwemo manjano maarufu ya Lakadong.
Vivutio vingine ni pamoja na Hifadhi ya Nokrek Biosphere Reserve inayotambuliwa na UNESCO, misitu mitakatifu ya Mawphlang, na Tamasha la Cherry Blossom la Shillong.
Wageni pia wanaweza kufurahia muziki maarufu wa roki wa Meghalaya na kukutana na mafundi wanaoendeleza sanaa ya ufinyanzi mweusi wa Lyrnai yenye historia ya zaidi ya miaka 1,000.
9. Ghana, Africa
Ghana ilipojipatia uhuru mwaka 1957, ikawa nchi ya kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kujikomboa kutoka utawala wa kikoloni wa Ulaya, hatua iliyochochea harakati za uhuru katika mataifa mengi ya Afrika.
Mwaka 2027, nchi hiyo itaadhimisha miaka 70 ya uhuru sambamba na mpango wa Beyond the Return, unaolenga kuunganisha tena Waafrika wa diaspora na bara lao kupitia historia, utamaduni na urithi.
Katika pwani ya Ghana, wageni wanaweza kutembelea majumba ya kihistoria ya Cape Coast na Elmina, yaliyotambuliwa na UNESCO.
Maeneo hayo yana historia muhimu kuhusu biashara ya watumwa kupitia Bahari ya Atlantiki, na mwaka 2027 yatakuwa mwenyeji wa tamasha la sanaa na utamaduni la Panafest.
Mji mkuu Accra unatoa taswira ya Ghana ya kisasa kupitia majumba ya sanaa, wabunifu wa mitindo, muziki wa Afrobeats na migahawa inayochanganya ubunifu na vyakula vya kienyeji.
Huu ni upande wa nchi unaoonesha maendeleo ya kisasa sambamba na kuhifadhi urithi wake wa kitamaduni.
Katika pwani ya Volta, Meet Me There Eco Lodge huwapa wageni mazingira tulivu kando ya ziwa la maji ya chumvi huku mapato ya wageni yakifadhili miradi ya elimu na usafi katika vijiji jirani.
Wageni hupata mapumziko ya ufukweni pamoja na fursa ya kujionea maisha halisi ya jamii za vijijini nchini Ghana.
10. Daintree Rainforest, Australia
Daintree Rainforest nchini Australia ni msitu wa kale zaidi wa kitropiki duniani, ambako misitu minene hukutana na mwamba wa matumbawe, mojawapo ya maajabu makubwa ya bahari duniani.
Eneo hili linajulikana kwa fukwe za mchanga mweupe na wanyamapori wa kipekee kama ndege mkubwa aina ya cassowary na kangaroo.
Mwaka 2027, wageni watapata fursa ya kufahamu kwa kina utamaduni wa wenyeji wa Kuku Yalanji kupitia programu na vivutio vinavyoendeshwa na jamii za asili.
Kituo kipya cha wageni katika Kulki/Cape Tribulation kitaonesha historia, sanaa na simulizi za jamii hiyo ambazo zimekuwepo kwa maelfu ya miaka.
Ziara maalumu zinazoongozwa na wenyeji huwapeleka wageni ndani ya msitu wa mvua, ambapo hujifunza hadithi za kitamaduni, kushiriki shughuli za kijamii na kutembelea maeneo matakatifu yenye umuhimu mkubwa wa kiutamaduni.
Kuanzia mwisho wa 2026, hoteli ya kifahari ya mazingira Ever Bloomfield Eco-Lodge itatoa makazi mapya kwa watalii wanaotaka kuchunguza msitu na miamba ya matumbawe kwa karibu.