Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi akaunti za roboti zinavyotumika kueneza propaganda mitandaoni
Unapoingia kwenye mitandao ya kijamii na kujiunga na mjadala kuhusu serikali za Afrika Mashariki huenda ukakutana na akaunti nyingi zinazotetea msimamo mmoja, kutumia ujumbe unaofanana au kushambulia wanaokosoa mamlaka.
Baadhi ya akaunti hizo zinaweza kuonekana kuwa za watu wa kawaida. Zina majina, picha na hata historia ya machapisho.
Kwa mtumiaji wa kawaida, inaweza kuwa vigumu kujua kama ni wananchi wanaotoa maoni yao binafsi au kuna juhudi zilizoratibiwa za kushawishi mjadala huo.
Je, kile tunachokiona mitandaoni kinaakisi mitazamo halisi ya wananchi au baadhi yake yanategenezwa ili kuunda taswira fulani?
Nyuma ya baadhi ya kampeni hizo kunaweza kuwa na programu za kompyuta zinazochapisha ujumbe kiotomatiki, pamoja na watu wanaolipwa kuendesha akaunti na kusambaza ujumbe wenye malengo maalumu ya kisiasa.
Hizi ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa katika kile kinachojulikana kama propaganda za kimtandao.
Akaunti za roboti ni nini?
Akaunti za roboti, zinazojulikana kwa Kiingereza kama bots, ni akaunti zinazotumia programu za kompyuta kutekeleza shughuli mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo kuchapisha jumbe, kutoa maoni na kushiriki machapisho bila mtu kufanya kila hatua mwenyewe.
Baadhi huendeshwa kikamilifu na programu, huku nyingine zikidhibitiwa kwa sehemu na binadamu.
Pia kuna akaunti bandia zinazoendeshwa na watu halisi. Hizi zinaweza kuwa na tabia zinazofanana na bots, kwa mfano kuchapisha jumbe zilezile mara kwa mara au kushiriki katika mijadala kwa wakati uliopangwa.
Tofauti hii ni muhimu kwa sababu si kila akaunti yenye wafuasi wachache, jina lisiloeleweka au picha isiyo ya kawaida ni bot.
Hata hivyo, akaunti nyingi zinapochapisha ujumbe unaofanana kwa wakati mmoja, kutumia alama zilezile za reli au kujibu kwa namna inayofanana, inaweza kuwa ishara ya shughuli iliyoratibiwa.
Tanzania: Mijadala ya kisiasa chini ya ushawishi wa akaunti bandia
Wasiwasi kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii kushawishi maoni ya umma nchini Tanzania uliongezeka wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Uchunguzi uliofanywa na maabara ya utafiti wa kidijitali ya Code for Africa, iLab, ulibaini kuwepo kwa kampeni za mitandaoni zilizolenga kueneza simulizi fulani kuhusu ghasia na vifo vilivyotokea wakati wa uchaguzi nchini Tanzania.
Katika kipindi cha Novemba 20 hadi Desemba 5, 2025, watafiti walifuatilia takribani alama 30 za reli na maneno muhimu yaliyokuwa yakisambaza ujumbe wenye simulizi zinazofanana.
Ujumbe huo uliwalaumu waandamanaji kwa ghasia zilizosababisha vifo vya watu, huku taarifa kuhusu mauaji hayo zikikanushwa na kutajwa kuwa za uongo au zilizofadhiliwa na wageni. Kwa njia hiyo, kampeni hizo zilionekana kuhamisha lawama kutoka kwa polisi na kuzielekeza kwa waandamanaji.
Uchunguzi huo pia ulibaini matumizi ya video, picha na michoro iliyohaririwa ili kuunga mkono simulizi hilo. Baadhi ya maudhui yalilenga kukanusha madai ya mauaji ya watu wengi na kuyahusisha mashirika ya kiraia na ghasia hizo.
Lakini kampeni hizo ziliendeshwaje?
Katika uchunguzi huo, mtu aliyekuwa na ufahamu wa shughuli za kampeni za mitandaoni alieleza jinsi washiriki walivyoongezwa kwenye makundi ya WhatsApp na kupewa jumbe, picha na alama za reli za kutumia kwa nyakati maalumu.
Hii inaonyesha namna kampeni za kisiasa zinavyoweza kuratibiwa hata bila kutumia roboti zinazofanya kazi zenyewe.
Hata hivyo, chunguzi huo haukuthibitisha kwamba kila akaunti iliyoshiriki kampeni hizo ilikuwa roboti. Baadhi zilikuwa akaunti zinazoendeshwa na watu halisi walioshiriki katika shughuli zilizoratibiwa.
Nani yuko nyuma ya akaunti hizi?
Tanzania si mfano wa pekee. Utafiti wa Taasisi ya Mtandao ya Chuo Kikuu cha Oxford, uliochapishwa mwaka 2021 chini ya jina Industrialized Disinformation, ulibaini ushahidi wa kampeni zilizoratibiwa za kushawishi maoni ya umma kupitia mitandao ya kijamii katika nchi 81.
Utafiti huo ulichunguza namna serikali, vyama vya kisiasa na kampuni binafsi zinavyotumia mitandao kusambaza ujumbe wa kisiasa na kuathiri mijadala ya umma.
Watafiti walibaini kuwa katika nchi 62, taasisi za serikali zilikuwa zikitumia mbinu za propaganda za kimtandao. Katika nchi 61, vyama vya kisiasa au wanasiasa pia walikuwa wakijihusisha na shughuli hizo.
Kampuni binafsi nazo zimekuwa sehemu ya shughuli hizi. Baadhi huajiriwa na serikali au wahusika wa kisiasa kuendesha kampeni kwa kutumia akaunti bandia, roboti na mbinu nyingine za kuongeza mwonekano wa ujumbe fulani ili uonekane kuwa maarufu zaidi.
Kwa mujibu wa utafiti huo, kampuni binafsi zilihusika katika kampeni za aina hiyo katika nchi 48.
Hii ina maana kwamba akaunti unayoiona ikitetea serikali au kushambulia wakosoaji huenda isiwe tu ya mtu anayetoa maoni yake binafsi. Inaweza kuwa sehemu ya kampeni pana inayoratibiwa na taasisi au kampuni yenye maslahi ya kisiasa.
Mtandao wa roboti uliounganishwa na Urusi
Mwaka 2024, Marekani ilifichua mfano wa operesheni kama hiyo iliyohusishwa na serikali ya Urusi.
Tarehe 9 Julai mwaka huo, Wizara ya Sheria ya Marekani ilitangaza kuvuruga mtandao wa akaunti 968 kwenye mtandao wa X, uliodaiwa kutumiwa kueneza ujumbe unaounga mkono malengo ya serikali ya Urusi.
Kwa mujibu wa nyaraka za uchunguzi, mtandao huo ulitumia teknolojia ya akili bandia kuunda akaunti bandia zilizojifanya kuwa za watu wa kawaida, wakiwemo raia wa Marekani.
Uchunguzi wa Marekani ulidai kuwa mpango wa kuunda mfumo huo uliongozwa na mtu aliyekuwa na nafasi ya juu katika shirika la habari la serikali ya Urusi, RT.
Nyaraka hizo pia zilieleza kuwa afisa wa Shirika la Usalama wa Shirikisho la Urusi, FSB, alihusika katika kuanzisha na kuongoza taasisi binafsi ya kijasusi iliyosaidia kuendesha operesheni hiyo, kwa idhini na ufadhili kutoka kwa uongozi wa Urusi.
Akaunti hizo zilitumiwa kusambaza ujumbe unaoendana na maslahi ya serikali ya Urusi, ikiwemo maudhui kuhusu vita vya Ukraine.
Mfano huo unaonyesha kuwa nyuma ya akaunti zinazoonekana kuwa za watu binafsi kunaweza kuwa na mtandao wa watu na taasisi wenye uwezo wa kuratibu kampeni katika majukwaa ya kimataifa.
Nani anapaswa kuwajibika?
Kutambua na kudhibiti matumizi ya akaunti za roboti si jukumu la watumiaji pekee na pia sio rahisi.
Kampuni zinazoendesha mitandao ya kijamii zina wajibu wa kubaini na kuchukua hatua dhidi ya akaunti zinazokiuka sera zao kwa kushiriki katika kampeni zilizoratibiwa za udanganyifu.
Taasisi za serikali na mamlaka za udhibiti nazo zinapaswa kuweka wazi hatua zinazochukuliwa kushughulikia matumizi mabaya ya majukwaa hayo, huku zikilinda haki ya wananchi kutoa maoni na kukosoa viongozi.
Kwa upande wa wananchi, ni muhimu kutokuchukulia idadi kubwa ya maoni yanayofanana kuwa ushahidi wa moja kwa moja kwamba watu wengi wanaunga mkono msimamo fulani.
Kwa mujibu wa mchangganuzi wa masuala ya usalama wa data mitandaoni anashauri watu kutofuata mkumbo kwa kuyaweka kifuani baada kuona wanaounga mkono hoja inayovuma mitandaoni, bali pia ni nani aliye nyuma ya akaunti hizo na je, maoni hayo yanaakisi sauti halisi za wananchi?